Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unaweza Kupata Wapi Kanuni za Maadili?

Unaweza Kupata Wapi Kanuni za Maadili?

Unaweza Kupata Wapi Kanuni za Maadili?

TUNAISHI katika ulimwengu ambamo maadili yanabadilika. Matendo ya udanganyifu yaliyoshutumiwa zamani, yanakubaliwa leo. Mara nyingi wezi na matapeli hutukuzwa na kusifiwa katika vyombo vya habari. Hivyo, watu wengi wana maoni kama haya yanayotajwa katika Biblia: “Wakati wowote ulipomwona mwizi, naam, ulipendezwa naye.”—Zaburi 50:18.

Hata hivyo, matapeli hawapaswi kusifiwa. Mwandishi mmoja alisema: “Sifa moja ya matapeli ni uwezo wao wa kiasili wa kuwatumia watu vibaya, na mara nyingi uwezo huo huanza kuonekana wakiwa wachanga sana. Isitoshe, hawajuti wala kuhisi hatia wanapowatumia watu vibaya. Badala yake, wao hujihisi vizuri sana, na hilo huwachochea kuendelea kuwatumia wengine vibaya ili kupata chochote wanachotaka, licha ya wengine kuumia.”

Bila shaka, watu humwonea huruma mjane anayepoteza pesa zake zote kupitia ulaghai, lakini watu wengi hawajali wakati mtu anapoiba pesa nyingi katika shirika kubwa la biashara au kulaghai kampuni ya bima. Wengi husema kwamba mashirika hayo yana pesa nyingi. Lakini ulaghai huo hauathiri tu mashirika hayo, kwani wateja pia hulipia hasara hiyo. Kwa mfano, huko Marekani, familia za kawaida hutozwa zaidi ya dola 1,000 kwa ajili ya bima ili kulipia hasara inayosababishwa na ulaghai.

Pia, watu wengi hujifaidi kwa kununua bidhaa bandia za bei ya chini zenye vibandiko vya mashirika makubwa, kama vile nguo, saa, marashi, vipodozi, na mikoba. Huenda wakatambua kwamba bidhaa hizo bandia husababishia makampuni hasara ya mamia ya mabilioni ya dola kila mwaka, huku wakifikiri kwamba hawaathiriwi. Hata hivyo, hatimaye wateja hulazimika kulipa zaidi kwa ajili ya bidhaa na huduma halali. Isitoshe, kununua bidhaa bandia huwatajirisha wahalifu.

Mwandishi mmoja anayefanya kazi ya kupambana na ulaghai aliandika: “Ninasadiki kwamba kuna ulaghai mwingi sana leo hasa kwa sababu tunaishi katika jamii isiyo na maadili. Maadili yamezorota sana hivi kwamba yamesababisha ulaghai. . . . Katika jamii yetu, maadili hayafundishwi nyumbani. Katika jamii yetu, maadili hayafundishwi shuleni, kwa sababu walimu watashtakiwa wakiyafundisha.”

Tofauti na hilo, Mashahidi wa Yehova hufundisha na kujitahidi kuishi kulingana na kanuni za maadili za Neno la Mungu. Wanaongozwa na kanuni kama hizi:

● “Mpende jirani yako kama wewe mwenyewe.”—Mathayo 22:39.

● “Usipunje.”—Marko 10:19.

● “Mwizi asiibe tena, bali afanye kazi ya bidii, akifanya kwa mikono yake kazi iliyo njema, ili awe na kitu cha kumgawia mtu aliye na uhitaji.”—Waefeso 4:28.

● “Tunataka kujiendesha kwa unyoofu katika mambo yote.”—Waebrania 13:18.

Ingawa Mashahidi hawajivuni wala kujiona kuwa wakamilifu, wanaamini kwamba ikiwa watu wote wangefuata kanuni hizo, ulimwengu ungekuwa mahali pazuri zaidi pa kuishi. Wanaamini pia katika ahadi ya Mungu kwamba siku moja ulimwengu utakuwa hivyo.—2 Petro 3:13.

[Blabu katika ukurasa wa 11]

Ikiwa watu wote wangefuata kanuni za maadili za Neno la Mungu, ulimwengu ungekuwa mahali pazuri zaidi pa kuishi

[Picha katika ukurasa wa 10]

Wakristo wa kweli hufuata kanuni za Biblia kama vile, “Mpende jirani yako kama wewe mwenyewe”