Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ulaghai Ni Tatizo la Ulimwenguni Pote

Ulaghai Ni Tatizo la Ulimwenguni Pote

Ulaghai Ni Tatizo la Ulimwenguni Pote

WAYNE alionekana kuwa mtu mwenye kuvutia na mwenye sauti nyororo, na Karen alikuwa akitafuta mume mwenye sifa hizo. Karen alisema: “Nilikuwa nimesali na kutumaini kumpata mwanamume wa aina hiyo. Mtu yeyote aliyetutazama aliona kwamba tunafaana kabisa. Alinifanya niamini kwamba mimi ndiye penzi la moyo wake.”

Hata hivyo, kulikuwa na tatizo. Wayne alimwambia Karen kwamba ndiye aliyekuwa wa tatu kwa cheo katika Shirika la Ujasusi la Australia. Alitaka kustaafu, lakini shirika hilo halingekubali. Alijua siri nyingi sana kuhusu shirika hilo. Hivyo, wangemwua! Wayne na Karen wakafanya mpango kuoana, kukusanya mali zao, kuondoka Australia, na kukimbilia Kanada. Karen aliuza nyumba yake na mali zake zote na kumpa Wayne pesa hizo.

Walifunga ndoa kama walivyokuwa wamepanga. Kisha Wayne akatoroka nchini, lakini Karen akaachwa huku akiwa tu na dola nne za Marekani katika benki. Muda si muda akagundua kwamba alikuwa amenaswa na mtego wa tapeli aliyetumia udanganyifu mwingi ili kumlaghai. Wayne alijifanya kuwa mtu mzuri ili amvutie. Alikuwa amemdanganya kuhusu malezi yake, mapendezi yake, utu wake, na upendo wake kwake ili amwamini, na hivyo kumsababishia hasara ya zaidi ya dola 200,000. Ofisa mmoja wa polisi alisema hivi: “Karen ameumizwa sana kihisia. Hata bila kufikiria kiasi cha pesa alichopoteza, ni jambo la kusikitisha sana jinsi watu wanavyoweza kuwaumiza wengine.”

Karen alisema: “Nimechanganyikiwa sana. Alijifanya kuwa mtu tofauti kabisa.”

Karen ni mmoja tu kati ya watu wengi sana ulimwenguni ambao wametumbukia katika mitego ya walaghai. Haijulikani watu hupoteza pesa ngapi kupitia ulaghai, lakini inakadiriwa kwamba wao hupoteza mamia ya mabilioni ya dola, na kiasi hicho huongezeka kila mwaka. Mbali na kupoteza pesa, watu wanaolaghaiwa kama Karen huumia sana kihisia wanapotambua kwamba mtu wanayemwamini amewatumia vibaya.

Kuzuia Ni Bora

Ulaghai hufafanuliwa kuwa “mbinu ya udanganyifu ya kupata pesa kwa kutumia unafiki, habari za uwongo, na ahadi zisizo za kweli.” Kwa kusikitisha, walaghai wengi hawaadhibiwi kwa sababu mara nyingi ni vigumu kuthibitisha kwamba udanganyifu ulitumiwa kimakusudi. Isitoshe, matapeli wengi hujua na hutumia kasoro za sheria, hivyo wao huwalaghai watu wakitumia njia zitakazowaepusha na mashtaka. Zaidi ya hilo, kumshtaki tapeli mahakamani huchukua muda na pesa nyingi. Kwa kawaida, wale wanaoshtakiwa kwa ulaghai huwa wameiba mamilioni ya dola au wamefanya mambo makubwa yanayowashtua watu wengi. Hata tapeli akikamatwa na kuadhibiwa, yaelekea tayari atakuwa ametumia au kuficha pesa hizo. Hivyo, mara nyingi watu ambao wamepoteza pesa kupitia ulaghai hawapati pesa hizo.

Kwa ufupi, ukilaghaiwa, huenda usiwe na la kufanya. Ni afadhali kuepuka kulaghaiwa kuliko kujaribu kupata pesa ulizopoteza. Mwanamume mmoja mwenye hekima aliandika hivi zamani: “Mtu mwerevu ni yule ambaye ameona msiba na kujificha, lakini wasio na uzoefu wameendelea mbele nao lazima waumie.” (Methali 22:3) Makala inayofuata itaeleza jinsi unavyoweza kujilinda dhidi ya ulaghai.