Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ugonjwa Unaporudi Mara ya Pili

Ugonjwa Unaporudi Mara ya Pili

Ugonjwa Unaporudi Mara ya Pili

SIMULIZI LA JACK MEINTSMA

Kutokana na chanjo zenye mafanikio na miradi ya kuwachanja watu, sayansi imefanya maendeleo makubwa katika jitihada za kukomesha polio, ugonjwa mbaya sana unaowapoozesha watoto. Hata hivyo, watu fulani huugua tena ugonjwa huo miaka mingi baada ya kupona.

HUENDA hujasikia kwamba ugonjwa wa polio unaweza kurudi tena. Hata mimi sikujua jambo hilo hadi ugonjwa huo uliponipata tena. Lakini ili uelewe jinsi ugonjwa huo ulivyoniathiri, acha niwaeleze juu ya jambo lililonipata siku moja katika mwaka wa 1941, nilipokuwa na umri wa mwaka mmoja hivi.

Mama yangu aligundua kwamba nilikuwa nimejikunja kwenye kiti changu kirefu. Alinipeleka kwa daktari mara moja. Baada ya kunichunguza, daktari alimwambia mama yangu hivi: “Mwana wako anaugua polio.” Muda si muda nilikuwa nimepooza kuanzia kiunoni hadi chini.

Baada ya kungojea kwa miezi sita, hatimaye nililazwa hospitalini. Kwa miaka mingi ugonjwa huo ulirudi mara kwa mara. Baada ya kufanyishwa mazoezi mengi ya viungo, niliweza kutumia miguu yangu tena. Nilipokuwa na umri wa miaka 14, nilianza kutembea tena. Lakini matatizo mengine kama vile kushindwa kuzuia mkojo yaliendelea. Kwa miaka mingi, nilifanyiwa upasuaji mara nyingi, nikatumia kiti cha magurudumu, na kufanyishwa mazoezi ya viungo. Bado saizi ya kiatu changu cha kulia ni mara tatu ya kiatu cha kushoto, na mguu wangu wa kulia ni mrefu kuliko mguu wa kushoto kwa sentimeta 3 hivi. Mapema katika miaka yangu ya 20, tatizo langu lenye kuaibisha la kushindwa kuzuia mkojo lilikwisha. Hatimaye, nikadhani kwamba ugonjwa wangu wa polio umekwisha!

Kisha nilipofikia umri wa miaka 45, nilianza kuhisi maumivu miguuni na uchovu. Pia, ilikuwa vigumu sana kulala kwa sababu misuli ya miguu yangu ilikuwa ikishtuka-shtuka usiku. Hali hizo zilizidi. Unaweza kuwazia jinsi nilivyoshtuka ilipogunduliwa kwamba ninaugua tena polio miaka 44 tangu mama yangu alipogundua kwamba ninaugua mara ya kwanza.

Polio Ni Nini?

Polio ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vinavyoingia mwilini kupitia mdomoni na virusi hivyo huzaana matumboni. Baada ya kushambulia mfumo wa neva, virusi hivyo vinaweza kumfanya mtu apooze kabisa haraka. Virusi hivyo vinapofika ubongoni kisha kwenye uti wa mgongo, dalili za kwanza huwa homa, uchovu, maumivu ya kichwa, kutapika, kukakamaa kwa shingo, na maumivu ya miguu na mikono. Neva nyingi huacha kufanya kazi na kusababisha misuli fulani ya mikono, miguu, na kifua kupooza.

Lakini mwili una nguvu za kustaajabisha za kujiponya. Neva ambazo hazikuathiriwa na virusi hufanyiza sehemu mpya ili kuunganisha chembe za misuli ambazo zilitenganishwa wakati baadhi ya neva zilipoharibika. Chembe moja ya neva katika uti wa mgongo inaweza pia kufanyiza nyuzi kwenye mwisho wake ambazo zinaweza kuungana na chembe zaidi za misuli kuliko awali na hivyo kuongeza sana uwezo wake. Chembe ya neva ambayo mwanzoni ilichochea chembe 1,000 za misuli, hatimaye inaweza kuunganisha kati ya chembe 5,000 hadi 10,000. Yaelekea hivyo ndivyo nilivyoweza kutembea tena.

Hata hivyo, sasa inadhaniwa kwamba baada ya miaka 15 hadi 40, mifumo hiyo ya chembe za neva na misuli huenda ikaanza kulemewa na uchovu kwa sababu ya kutumiwa kupita kiasi. Watu wengine waliopona polio miaka mingi iliyopita hupata tena dalili za ugonjwa huo. Watu wengi wenye hali hiyo huhisi udhaifu wa misuli, uchovu, maumivu ya viungo na misuli, hushindwa kustahimili baridi, na kushindwa kupumua. Ijapokuwa ni vigumu kupata idadi sahihi, Shirika la Afya Ulimwenguni linakadiria kwamba kuna watu milioni 20 ulimwenguni ambao waliugua polio zamani. Uthibitisho wa sasa unaonyesha kwamba kati ya asilimia 25 hadi 50 ya watu hao wanaugua polio tena.

Wanaweza Kupata Msaada Gani?

Watafiti wanasema kwamba chembe nzee ya neva iliyotumiwa kupita kiasi huchoka sana hivi kwamba sehemu zake za mwisho huacha kufanya kazi na kutengana tena na nyuzi nyingi za misuli. Ili kupunguza hali hiyo, mtu aliyepona polio hapaswi kutumia sana misuli iliyoathiriwa. Baadhi ya madaktari wa viungo wanapendekeza kutumia vifaa vya kujitegemeza kama vile bakora, vifaa vya kutegemeza viungo, magongo, viti vya magurudumu, na vigari maalum. Nililazimika kutumia vifaa vya kutegemeza miguu. Pia, nina viatu vya pekee vinavyotegemeza viwiko vya miguu na kunizuia nisianguke.

Huenda mtu akahitaji pia kufanya mazoezi kwa kiasi na kunyoosha misuli ikitegemea hali yake. Kuogelea au kutumia vidimbwi vya maji ya moto ni njia nzuri za kuboresha utendaji wa moyo bila kuumiza misuli. Ni muhimu kwa mgonjwa kushirikiana na daktari anapofanya mazoezi yoyote.

Watu waliopona ugonjwa wa polio wanapotumia sana chembe za neva, nyuzi fulani za misuli huacha kufanya kazi vizuri. Hivyo, wanaweza kupoteza nguvu au hata kuchoka kupita kiasi. Wanaweza pia kupoteza nguvu kwa sababu ya mfadhaiko unaotokana na kuhisi maumivu nyakati zote au kukabiliana na hali hiyo yenye kudhoofisha. Nimetambua kwamba kupumzika mchana hunisaidia kupunguza uchovu. Madaktari wengi huwatahadharisha wagonjwa wafanye mambo kwa kiasi badala ya kujikaza sana na kujichosha.

Tatizo kubwa zaidi ambalo nimekabili ni kuhisi maumivu ya viungo na misuli nyakati zote. Wengine wanaweza kuhisi maumivu hasa kwenye misuli ambayo imetumiwa kupita kiasi wanapofanya shughuli zao. Wengine huchoka na kuhisi maumivu kwenye misuli kama mtu aliye na mafua.

Maumivu yanaweza kupungua kwa kutumia dawa za kupunguza mwasho au dawa nyingine. Licha ya kupata matibabu, watu wengi waliougua polio zamani hupata maumivu yenye kudhoofisha na yanayodumu. Matibabu ya kuzoeza viungo na vilevile joto na kujinyoosha kunaweza kusaidia. Mwanamke mmoja aliyeacha kazi ya utaalamu wa unusukaputi aliniambia, “Ninaweza kujikakamua nijiondoe kwenye kiti hiki cha magurudumu na kutembea chumbani, lakini nitahisi maumivu mengi sana hivi kwamba hakuna haja ya kufanya hivyo.” Hata ninapotumia dawa zinazonisaidia, inanibidi nitumie kiti cha magurudumu mara nyingi.

Miili ya watu fulani waliougua polio zamani haiwezi kuondoa damu kwenye ngozi, jambo ambalo mwili hufanya kwa kawaida ili kuhifadhi joto katika chembe za misuli. Bila uwezo huo, kiungo kilichoathiriwa hupoteza joto jingi na kupoa. Misuli inapopoa, chembe ya neva haiwasiliani vizuri na misuli, na hivyo misuli huacha kufanya kazi vizuri. Kwa hivyo, ni muhimu kupasha joto misuli iliyoathiriwa kwa kuvaa nguo nyingi. Watu wengine hutumia blanketi ya umeme au chupa ya maji ya moto kunapokuwa baridi usiku. Ni muhimu kujiepusha na baridi. Nililazimika kuhamia eneo lenye joto.

Kwa kawaida watu waliowahi kuugua polio inayoathiri uti wa mgongo kwenye sehemu ya juu ya shingo hupata matatizo ya kupumua kwani ugonjwa huo hudhoofisha misuli ya kupumua. Miaka mingi iliyopita, ugonjwa huo uliwafanya watu wengi wawekwe katika mashine za kuwasaidia kupumua. Leo, mashine inayoingiza na kuondoa hewa kwenye mapafu ya mgonjwa inaweza kutumiwa kusaidia misuli ya mapafu iliyodhoofika. Huwa vigumu kwangu kupumua ninapofanya kazi nyingi. Kwa hiyo, kila siku mimi hutumia kifaa kidogo cha kuzoeza misuli ya mapafu.

Watu waliougua polio zamani wanapaswa kutambua hatari nyingine. Si vizuri kufanyiwa upasuaji na kurudi nyumbani siku hiyohiyo. Dakt. Richard L. Bruno wa Taasisi ya Kessler ya Tiba ya Viungo anasema: “MTU YEYOTE ALIYEUGUA POLIO ZAMANI HAPASWI KUFANYIWA UPASUAJI NA KURUDI NYUMBANI SIKU HIYOHIYO isipokuwa awe amefanyiwa upasuaji usiohusisha mambo mengi unaohitaji tu kutiwa ganzi kwenye sehemu inayopasuliwa.” Anaongeza kwamba watu waliougua polio zamani wanahitaji mara mbili ya wakati wa kawaida ili kupona kutokana na athari za nusukaputi na huenda wakahitaji dawa za kutuliza maumivu. Kwa kawaida wao hukaa hospitalini muda mrefu zaidi ya wagonjwa wengine. Kama ningejua hilo, singepata nimonia baada ya kufanyiwa upasuaji mdogo hivi majuzi. Ni jambo la hekima kuzungumzia mambo hayo pamoja na daktari-mpasuaji na mtaalamu wa unusukaputi kabla ya upasuaji.

Maisha Yangu Leo

Nilikuwa na umri wa miaka 14 nilipoweza kutembea, na nilifikiri kwamba matatizo yangu mengi yalikuwa yamekwisha. Hata hivyo, baada ya miaka mingi bado ninapatwa na matatizo yaleyale. Bila shaka, ni jambo la kawaida kuvunjika moyo nyakati nyingine. Hata hivyo, bado ninaweza kutembea na kujifanyia mambo. Nimetambua kwamba dawa bora ni kuwa na maoni yanayofaa, kubadilika kulingana na hali, na kufurahia yale ambayo bado ninaweza kufanya.

Kwa mfano, nilipoanza huduma ya wakati wote ya Kikristo miaka kumi hivi iliyopita, ilikuwa rahisi kutembea kuliko ilivyo sasa. Nilikuwa nikitembea mbali bila kuchoka wala kuhisi maumivu. Hata hivyo, siku hizi siwezi kwenda mbali. Ili nisitumie nguvu nyingi, mimi huepuka kupanda ngazi na milima. Mimi hutumia kiti changu cha magurudumu wakati wowote inapowezekana. Kwa kushiriki katika huduma kwa njia mbalimbali, mimi huifurahia na inanifaidi.

Naam, ugonjwa huo huathiri maisha yangu. Huenda afya yangu itazorota. Lakini ninafarijiwa na ahadi ya Biblia ya ulimwengu mpya ambamo watu wote watakuwa vijana tena, wakiwa na afya na nguvu kamili. Kwa miaka mingi, nimekuwa nikifikiria maneno yenye kutia moyo ya Isaya 41:10: “Usiogope, kwa maana mimi nipo pamoja nawe. Usitazame huku na huku, kwa maana mimi ni Mungu wako. Nitakutia nguvu. Nitakusaidia kwelikweli.” Kwa msaada wa Mungu, nimeazimia kusonga mbele hadi wakati ambapo ugonjwa huo utakoma.

[Maelezo ya chini]

[Sanduku katika ukurasa wa 20]

‘Je, Nimepata Polio Tena?’

Wataalamu wengi hujumlisha baadhi ya kanuni zifuatazo ili kutambua kwamba mtu amepata polio tena:

▪ Uthibitisho wa kwamba mtu alikuwa ameugua polio zamani

▪ Kipindi cha kupona kwa kadiri fulani au kabisa kisha kipindi ambacho kinahusisha mfumo wa neva kurudia hali yake ya kawaida (angalau kwa miaka 15)

▪ Kudhoofika kwa misuli, kuchoka, kuharibika kwa misuli, au maumivu ya misuli na viungo yanayoanza hatua kwa hatua au ghafula

▪ Matatizo ya kupumua au kumeza

▪ Dalili zinazoendelea kwa angalau mwaka mmoja

▪ Kutopata matatizo mengine ya mfumo wa neva, ya kitiba, au ya viungo

Si watu wote waliougua polio zamani wanaopata ugonjwa huo tena, ingawa wanapoendelea kuzeeka huenda chembe za neva na misuli yao iliyotumiwa kupita kiasi zikachoka na kuzeeka kabla ya wakati wake. Isitoshe, zaidi ya nusu ya watu waliougua polio zamani wanaoenda hospitalini kwa sababu wana dalili mpya hawana ugonjwa huo. Mtaalamu mmoja anasema: “Asilimia 60 ya watu waliougua polio zamani ambao wana dalili mpya wana tatizo la kitiba au la mfumo wa neva ambalo halihusiani na polio, na tatizo hilo linaweza kutibiwa. Asilimia 20 ya watu hao wana matatizo ya viungo yanayosababishwa na athari zilizosalia.”

[Sanduku katika ukurasa wa 21]

Je, Kuna Tiba?

Kwa kuwa chanzo cha ugonjwa huo hakijathibitishwa na majaribio kamili hayawezi kufanywa kwenye maabara, kwa sasa hakuna tiba ya ugonjwa huo. Hata hivyo, matibabu yanahusisha njia tatu. Mtaalamu mmoja anasema: “Zaidi ya asilimia 80 ya watu wanaougua polio tena watafaidika kwa matibabu ya viungo.”

Njia hizo tatu ni:

1. Kufanya mabadiliko maishani

▪ kuhifadhi nishati

▪ kutumia vifaa vya kutegemeza mwili

▪ kufanya mazoezi yasiyochosha

▪ kujipasha joto

2. Dawa mbalimbali

Ingawa dawa nyingi zimetumiwa, iwe ni zile zilizopendekezwa na daktari au za kiasili, hakuna iliyofaulu. Kuna ripoti zisizothibitishwa zinazoonyesha kwamba wagonjwa wamepata nafuu, lakini uchunguzi zaidi unahitajiwa. Kumbuka kwamba mitishamba inaweza kuathiri utendaji wa dawa zilizopendekezwa na daktari, kwa hiyo sikuzote mweleze daktari mitishamba ambayo unataka kutumia.

3. Kuwa na maisha bora

“Dawa bora ambayo daktari anaweza kumpa mtu anayeugua polio tena ni kumwelimisha na kumtia moyo. . . . Wagonjwa wanaoweza kuboresha maisha yao (wale wenye ustadi wa kutatua matatizo, wenye hali nzuri maishani, wanaoweza kupata habari na kutegemezwa, na wanaotaka kutumia vifaa vinavyotegemeza mwili) walifaulu zaidi katika shughuli zao za kila siku.”—Dakt. Susan Perlman.

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

Vipi Kufanya Mazoezi?

Mwanzoni, watu waliougua polio walitiwa moyo kufanya mazoezi hadi wahisi wamechoka sana. Kisha katika miaka ya 1980, walionywa kuhusu hatari za kufanya mazoezi, hasa kudhoofisha chembe za misuli yao.

Leo wataalamu wanapendekeza watu wafanye mazoezi kwa kiasi. Sasa wanasema, ‘Usifanye mazoezi kupita kiasi, lakini usikae tu.’ Kituo cha Kitaifa cha Mazoezi ya Mwili na Ulemavu kinasema: “Kulingana na ujuzi mpya ambao tumepata, hata ikiwa hatuwezi kutenda kwa kadiri gani, tunapaswa kutiwa moyo kufanya mazoezi, kupanga ratiba nzuri ya kufanya mazoezi na kushikamana nayo ili tuweze kufaidika.”

Kwa ufupi, ratiba ya kibinafsi ya mazoezi inapaswa

▪ Kupangwa kwa msaada wa daktari mwenye ujuzi au mtaalamu wa tiba ya viungo

▪ Kuhusisha kuanza kufanya mazoezi kwa kiasi na kuendelea hatua kwa hatua

▪ Kuhusisha kupasha misuli joto kabla ya mazoezi na kupumzika baada ya kufanya mazoezi

▪ Kuhusisha kufanya mazoezi ya kunyoosha viungo

▪ Kuhusisha mazoezi yanayofanywa kwenye vidimbwi vya maji ya moto, ikiwa vinapatikana

Katika jarida The Johns Hopkins Medical Letter, mtaalamu mmoja anasema hivi: “Uchovu na maumivu yanayoendelea kwa zaidi ya saa moja, yanaonyesha kwamba misuli imetumiwa kupita kiasi.” Kwa hiyo, tambua ishara za mwili wako na uepuke maumivu, uchovu, na kuwa mnyonge.

[Sanduku katika ukurasa wa 23]

Uwezekano wa Kupata Ugonjwa Huo

Ingawa kila kisa ni tofauti, mambo yafuatayo yanaweza kuzidisha uwezekano wa kupata tena ugonjwa wa polio:

Kiwango cha ugonjwa huo mara ya kwanza. Ikiwa ugonjwa huo ulikuwa mbaya sana mara ya kwanza, kuna uwezekano mkubwa wa kuupata tena

Umri wa mgonjwa alipougua polio mara ya kwanza. Waliougua polio wakiwa wachanga hawakabili uwezekano mkubwa wa kuupata tena

Kupona. Kwa kushangaza, ikiwa mgonjwa alipona kabisa au kwa kadiri kubwa mara ya kwanza, anakabili uwezekano mkubwa wa kupata polio tena

Mazoezi ya mwili. Ikiwa mtu aliyeugua polio zamani amezoea kufanya mazoezi kupita kiasi kwa miaka mingi, hilo linaweza kuongeza uwezekano wa kupata polio tena

[Picha katika ukurasa wa 19]

Muuguzi akinisaidia kupona baada ya upasuaji, nilipokuwa na umri wa miaka 11

[Picha katika ukurasa wa 23]

Leo, nikiwa na mke wangu katika huduma ya Kikristo ya wakati wote