Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Marco Polo Asafiri Hadi China

Marco Polo Asafiri Hadi China

Marco Polo Asafiri Hadi China

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

Watu watatu washuka kutoka mashuani kwenye gati huko Venice. Hakuna anayekimbia kuwakaribisha. Isingalikuwa sura yao ya ajabu, hakuna yeyote angalitambua kurudi kwao nyumbani baada ya kuwa ng’ambo kwa miaka 24. Walikuwa wamevaa kanzu zilizochakaa za Kimongolia ambazo awali zilikuwa za hariri bora. Kitabu kimoja kinasema kwamba “walifanana sana na Watarta kwa tabia na matamshi ingawa walikuwa wamesahau karibu lugha yao yote ya huko Venice.” Wasafiri hao ni Marco Polo, baba yake, na ndugu ya baba yake. Huo ulikuwa mwaka wa 1295.

WATU walioishi wakati huo waliziona hadithi za safari ndefu ya akina Polo hadi Cathay, ambayo ni China ya leo, kuwa za ajabu sana. Kitabu chenye habari za Marco ambacho hapo awali kiliitwa Description of the World na baadaye kikaitwa Travels of Marco Polo, kilizungumzia maeneo ambayo hayakuwa yamejulikana yenye ustaarabu, utajiri mwingi, na mali nyingi ambazo zilitafutwa sana na wafanyabiashara wa nchi za Magharibi. Kitabu chake kilichochea sana maoni ya watu waliokisoma. Miaka 25 baada ya Marco kurudi, maandishi yake yalikuwa yameandikwa katika Kifaransa cha Italia, Kifaransa, Kilatini, Kituskani, Kivenisi, na labda Kijerumani. Hayo yalikuwa mafanikio yasiyo na kifani katika Zama za Kati. Kitabu chake kilinakiliwa kwa mkono kwa karne mbili, na tangu mwaka wa 1477 kimeendelea kuchapishwa katika lugha nyingi. Huenda Marco Polo ndiye Mzungu maarufu zaidi kuwahi kusafiri hadi China. Kwa nini akafunga safari hiyo? Na je, mambo yote aliyodai kuyaona na kuyafanya ni ya kweli?

Wafanyabiashara wa Venice

Katika karne ya 13, wafanyabiashara wengi wa Venice walihamia Constantinople, ambayo sasa ni Istanbul, na kutajirika sana huko. Miongoni mwao ni Niccolò Polo baba ya Marco na Maffeo Polo ndugu ya baba yake. Wapata mwaka wa 1260, waliuza mali yao katika eneo hilo, wakaanzisha biashara ya vito na kusafiri hadi Sarai kwenye Mto Volga, jiji kuu la jimbo la magharibi la Milki ya Mongolia. Biashara yao ilitia fora, wakaongeza bidhaa zao maradufu. Kwa sababu ya vita hawakurudi nyumbani, bali walielekea mashariki, labda kwa kutumia farasi, kwenye jiji kubwa la kibiashara la Bukhara, ambalo ni Uzbekistan leo.

Vurugu iliyokuwapo iliwafanya wakae huko kwa miaka mitatu hadi wajumbe walipopitia Bukhara wakielekea kumwona Kublai, Mfalme wa Wamongolia wote aliyetawala kuanzia Korea hadi Poland. Wajumbe hao waliwaomba Niccolò na Maffeo waandamane nao kwa kuwa, kama Marco alivyosimulia, Mfalme huyo hakuwa amekutana na “Walatini” wowote—labda akimaanisha Wazungu wa kusini—na angefurahi kuongea nao. Baada ya kutembea kwa mwaka mmoja, akina Polo walifika kwenye jumba la Mfalme Kublai, mjukuu wa Mfalme Genghis, aliyeanzisha Milki ya Mongolia.

Mfalme huyo aliwakaribisha Niccolò na Maffeo na kuwauliza maswali mengi kuhusu Ulaya. Aliwapa bamba la dhahabu ambalo lingewalinda walipokuwa wakirudi Ulaya na vilevile barua ya kumwomba papa awatume “watu mia moja wenye hekima, wanaojua sheria ya Kristo, na wenye elimu ya kutosha kuwahubiria watu [wa Kublai].”

Wakati huohuo, Marco alizaliwa. Alikutana na baba yake mara ya kwanza alipokuwa na umri wa miaka 15, mnamo mwaka wa 1269. Walipoingia maeneo ya “Wakristo,” Niccolò na Maffeo wakapata habari kwamba Papa Clement wa Nne amekufa. Walisubiri mtu achukue mahali pake, lakini kipindi hicho cha miaka mitatu kabla ya kuchaguliwa kwa papa atakayefuata ndicho kilichokuwa kirefu zaidi katika historia. Baada ya miaka miwili, katika mwaka wa 1271, wakarudi kwa Mfalme huyo wakiwa na Marco, aliyekuwa na umri wa miaka 17.

Safari ya Marco

Huko Acre, Palestina, mwanasiasa maarufu wa kanisa, Teobaldo Visconti, aliwapa akina Polo barua kadhaa wampelekee Mfalme ili kumjulisha ni kwa nini hawakuweza kutekeleza ombi lake la kupelekewa watu mia moja wenye hekima. Walipofika Asia Ndogo, walipata habari kwamba Visconti mwenyewe alikuwa ameteuliwa kuwa papa, kwa hiyo wakarudi kwake huko Acre. Badala ya kuwatuma watu mia moja wenye hekima, papa huyo mpya, Gregory wa Kumi, alituma wanaume wawili watawa wenye mamlaka ya kutawaza makasisi na maaskofu na kuwapa vyeti rasmi na zawadi kwa ajili ya Mfalme. Kikundi hicho kikafunga safari tena, lakini watawa hao wakaamua kurudi kwa sababu waliogopa vita vilivyozuka katika maeneo hayo. Akina Polo wakasonga mbele.

Watu hao watatu walisafiri katika maeneo ambayo leo yanaitwa Uturuki na Iran na kushuka Ghuba ya Uajemi wakitaka kupita baharini. Hata hivyo, walipoona kwamba meli ni mbovu, “zimezeeka . . . na kuunganishwa kwa kamba,” wakaamua kupitia nchi kavu. Walienda kaskazini na mashariki, wakapita maeneo makubwa yasiyokalika, milima mikubwa, nyanda zenye majani, na maeneo ya malisho ya Afghanistan na Pamirs kabla ya kufika Kashgar, katika eneo ambalo sasa linaitwa Xinjiang Uygur huko China. Kisha wakapitia njia za zamani kusini mwa Bonde la Tarim na Jangwa la Gobi, na kufika Cambaluc, ambayo sasa ni Beijing. Safari yote ilichukua miaka mitatu na nusu, ambayo ilihusisha kupambana na hali mbaya ya hewa na ugonjwa usiojulikana wa Marco.

Marco anaandika mambo yenye kupendeza aliyoona njiani kama vile, mlima ambapo safina ya Noa inasemekana ilitua huko Armenia, mahali ambapo inasemekana wale Mamajusi walizikwa huko Uajemi, maeneo ya baridi kali na yenye giza lisilokoma huko kaskazini ya mbali. Marco ndiye mwandishi wa kwanza wa Ulaya anayetaja petroli. Anataja kwamba “salamanda” si sufu ya mnyama asiyeweza kushika moto kama watu wengi walivyodhani, bali ni madini ya asbestosi yanayopatikana katika eneo la Xinjiang Uygur. Anasema kwamba makaa ya mawe yanapatikana kwa wingi huko China hivi kwamba watu wanaweza kuoga kwa maji ya moto kila siku. Anaandika pia kuhusu mapambo, vyakula, vinywaji—hasa maziwa ya farasi ya Wamongolia—desturi za kidini na za kimizungu, biashara, na bidhaa zilizouzwa katika maeneo aliyotembelea. Hakuwa amewahi kuona pesa za noti zilizotumiwa katika milki za Mfalme.

Marco haelezi kamwe maoni yake bali anaeleza mambo aliyoona au kusikia bila hisia zozote. Tunaweza tu kukisia jinsi alivyohisi aliposhambuliwa na waporaji ambao waliwateka nyara na kuwaua baadhi ya watu aliokuwa nao.

Je, Alimtumikia Mfalme Kublai?

Marco anadai kwamba akina Polo walimtumikia Mfalme Kublai kwa miaka 17. Anadai kwamba wakati huo Mfalme alimtuma mara nyingi kwenda sehemu za mbali za milki yake ili kukusanya habari, na hata akawa gavana wa eneo ambalo leo ni jiji la Yang-chou, Mkoa wa Jiangsu.

Haijulikani ikiwa Marco anasema ukweli mtupu. Wamongolia waliwashuku Wachina, kwani walikuwa wamewashinda vitani, na waliwaajiri wageni wasimamie milki yao. Lakini linaonekana kuwa jambo lisilowezekana kwamba Marco, ambaye hakuwa na elimu, angeweza kuwa gavana. Huenda Marco alitilia chumvi cheo chake. Hata hivyo, wasomi wanakubali kwamba huenda alikuwa “mjumbe aliyetegemeka mwenye cheo fulani.”

Hata hivyo, Marco Polo alieleza kinaganaga kuhusu majiji yenye utajiri mwingi na desturi za kipagani zisizo za kawaida za nchi ambazo zilipuuzwa kabisa na Wazungu au zilizojulikana tu kupitia hadithi na uvumi. Je, kweli maeneo hayo yenye watu wengi na utajiri mwingi kuliko Ulaya yalikuwapo? Lilionekana kuwa jambo lisilowezekana.

Marco alisema kwamba jumba la Mfalme Kublai ndilo “Jumba bora kuliko yote. Ni jengo kubwa sana, lenye vitu vingi sana, na lenye kupendeza sana hivi kwamba hakuna mtu awaye yote duniani angeweza kujenga makao mengine bora zaidi.” Kuta zake zilikuwa zimefunikwa kwa dhahabu na fedha na kwa michongo ya dhahabu ya majoka, wanyama, ndege, wanajeshi, na sanamu. Paa yake ndefu yenye rangi nyekundu sana, manjano, kijani, na bluu, iling’aa kama fuwele. Bustani zake zenye kupendeza zilijaa wanyama wa kila aina.

Tofauti na njia zilizojipinda za Ulaya katika Zama za Kati, njia za Cambaluc zilikuwa pana na zilinyooka sana hivi kwamba mtu angeweza kuona kutoka ukuta mmoja wa jiji hadi mwingine. Jiji hilo lilipokea “bidhaa nyingi adimu na za thamani kubwa . . . , kuliko jiji lingine lolote ulimwenguni,” anasema mwanamume huyo wa Venice. “Kila siku mikokoteni 1000 iliyobeba hariri iliingia jiji hilo.”

Idadi ya meli zilizokuwa zikiabiri Mto Yangtze, mojawapo ya mito mikubwa zaidi ulimwenguni, ilikuwa yenye kushangaza. Marco anakadiria kwamba bandari ya Sinju ilikuwa na meli zipatazo 15,000.

Miongoni mwa desturi za Kimongolia ambazo Marco anataja ni ile ya kufanya harusi ya watoto waliokufa. Ikiwa mwana wa familia fulani alikufa akiwa na umri wa miaka minne au zaidi na binti wa familia nyingine mwenye umri huohuo akafa, huenda baba zao wakaamua watoto hao waliokufa waoane kwa kufanya makubaliano na kuandaa karamu kubwa. Chakula kiliandaliwa, na sanamu zilizotengenezwa kwa karatasi za watumwa, pesa, na vitu vya nyumba ziliteketezwa kwa kuwa iliaminika kwamba “wenzi” hao wangemiliki vitu hivyo katika ule uliodhaniwa kuwa ulimwengu mwingine.

Marco anavutiwa sana na ujuzi wa jeshi la Wamongolia, mbinu zao za kuongoza, na uhuru wa ibada. Maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi yalitia ndani kutoa msaada kwa ajili ya maskini na wagonjwa, askari wa doria wa kuzuia moto na ghasia, maghala ya chakula kwa ajili ya nyakati za mafuriko, na mfumo wa kutuma barua uliowezesha mawasiliano ya haraka.

Ijapokuwa alijua kwamba Wamongolia walikuwa wamejaribu kushambulia Japani, Marco hakudai kwamba aliwahi kufika huko. Hata hivyo, anasema kwamba kulikuwa na dhahabu nyingi sana Japani hivi kwamba ilitandazwa kotekote kwenye dari na sakafu ya jumba la maliki. Kati ya vitabu vyote vya Ulaya, kitabu cha Marco tu ndicho kilichotaja kuhusu Japani kabla ya karne ya 16.

Kitabu cha Marco kilisifiwa na kuchambuliwa vikali kwa karne nyingi. Baada ya kuchunguza makosa yote ya kitabu hicho, wasomi wa leo wanakifafanua kuwa “maelezo yasiyo na kifani” kuhusu upeo wa utawala wa Kublai.

Warudi Venice

Akina Polo waliondoka China wapata mwaka wa 1292. Marco anasema kwamba walisafiri kwa miezi 21 baharini kuanzia Quanzhou ya sasa, wakasimama kidogo huko Vietnam, Rasi ya Malay, Sumatra, na Sri Lanka, kisha wakafuata pwani ya India hadi Uajemi. Katika mkondo wa mwisho wa safari yao, walifika Constantinople na mwishowe Venice. Kwa kuwa walikuwa wameondoka kwa miaka 24, si ajabu kwamba watu wao wa ukoo hawangeweza kuwatambua. Wakati huo, Marco alikuwa na umri wa miaka 41 au 42.

Ni vigumu kukadiria umbali ambao Marco alisafiri. Mwandishi mmoja ambaye hivi majuzi alijaribu kufuata njia ambazo Marco alipitia, alisafiri zaidi ya kilometa 10,000 kati ya Iran na China peke yake. Hata kwa kutumia mbinu za sasa za usafiri, safari hiyo ilikuwa ngumu sana.

Inasemekana kwamba Marco alimtumia Rustichello kuandika kitabu chake katika gereza moja huko Genoa mwaka wa 1298. Kulingana na mapokeo, Marco alipokuwa akiongoza mashua moja ya kutoka Venice, alitekwa nyara wakati Wagenoa walipopigana na Venice baharini. Rustichello, ambaye alikuwa mfungwa mwenzake, alikuwa na ujuzi wa kuandika hadithi katika Kifaransa au Kifaransa cha Italia, na yaonekana alichochewa kuandika kwa sababu ya kushirikiana na Marco.

Huenda Marco aliachiliwa mwaka wa 1299 wakati Venice na Genoa zilipofanya amani. Alirudi Venice, akaoa, akapata binti watatu. Akafa katika jiji lao la nyumbani mwaka wa 1324 akiwa na umri wa miaka 69.

Watu fulani bado wanatilia shaka ikiwa Marco alifanya mambo yote anayosimulia au ikiwa anasimulia tu yale aliyokuwa amesikia kutoka kwa wasafiri wengine. Lakini hata iwe Marco Polo alipata habari zake wapi alipoandika kitabu chake Description of the World, bado wasomi wanakitambua. Mwanahistoria mmoja anasema hivi: “Kabla ya wakati huo na tangu wakati huo, hakuna mtu yeyote mwingine aliyewahi kuelimisha Ulaya kwa habari nyingi za kijiografia kadiri hiyo.” Kitabu cha Marco Polo kinaonyesha jinsi wanadamu wanavyopenda kusafiri, kuona maeneo mapya na nchi za mbali.

[Ramani katika ukurasa wa 24, 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Jinsi Marco alivyotembea hadi China (Ona kichapo)

Alipokuwa China (Ona kichapo)

Safari ya kurudi nyumbani (Ona kichapo)

ITALIA

Genoa

Venice

UTURUKI

Istanbul (Constantinople)

Trabzon

Acco (Acre)

(Sarai)

GEORGIA

Mlima Ararati

IRAN (UAJEMI)

Ghuba ya Uajemi

AFGHANISTAN

UZBEKISTAN

Bukhara

PAMIRS

Kashgar

BONDE LA TARIM

JANGWA LA GOBI

MONGOLIA

(KOREA)

CHINA (CATHAY)

Beijing (Cambaluc)

Yang-chou

Mto Yangtze

Quanzhou

MYANMAR

VIETNAM

RASI YA MALAY

SUMATRA

SRI LANKA

INDIA

[Hisani]

Map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Venice

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Mlima Ararati

[Hisani]

Robert Azzi/Saudi Aramco World/PADIA

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mwanamke Mmongolia

[Hisani]

C. Ursillo/Robertstock.com

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mpiga makasia, Myanmar

[Picha katika ukurasa wa 25]

Ukuta Mkubwa wa China

[Picha katika ukurasa wa 25]

Beijing

[Picha katika ukurasa wa 25]

Vietnam

[Picha katika ukurasa wa 25]

Viungo vya India

[Picha katika ukurasa wa 26]

Wapanda-farasi wa China, Mfalme Kublai, Mto Yangtze

[Credit Lines]

Horsemen: Tor Eigeland/Saudi Aramco World/PADIA; Kublai Khan: Collection of the National Palace Museum, Taiwan; Yangtze River: © Chris Stowers/Panos Pictures

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

© Michael S. Yamashita/CORBIS

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 27]

© 1996 Visual Language