Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Watu Wanavyolengwa

Jinsi Watu Wanavyolengwa

Jinsi Watu Wanavyolengwa

Mara tu baada ya kumaliza shule, Monika alianza kuzoezwa kuwa karani katika kampuni moja ya sheria. Monika alitazamia kufanya kazi baada ya kumaliza shule.

Horst alikuwa daktari akiwa na umri wa miaka 30 na kitu. Alikuwa na mke na watoto, na ilionekana wazi kwamba angepata sifa na mshahara mnono.

Monika na Horst walidhulumiwa kazini.

TUNAJIFUNZA jambo muhimu kutokana na visa vya Monika na Horst: Haijulikani ni nani atakayedhulumiwa kazini. Mfanyakazi yeyote anaweza kudhulumiwa. Basi unaweza kujilindaje? Njia moja ni kujifunza jinsi ya kuwa mwenye amani kazini hata kukiwa na wafanyakazi wagumu.

Kusikilizana na Wafanyakazi Wenzako

Watu wengi hulazimika kufanya kazi na watu kadhaa na kushirikiana ili wafanikishe kazi. Wafanyakazi wakielewana, wanafanya kazi vizuri. Wasipoelewana, hawafanyi kazi vizuri na kuna uwezekano mkubwa wa kudhulumiwa.

Ni nini kinachoweza kuwafanya watu washindwe kufanya kazi vizuri pamoja? Sababu moja ni kwamba huenda wafanyakazi wakabadilishwa mara nyingi. Katika hali kama hiyo, inakuwa vigumu kuwa na marafiki. Isitoshe, wafanyakazi wapya hawajui utaratibu wa kazi, na hilo huwazuia wafanyakazi wote kufanya kazi haraka. Kazi ikiongezeka, wanaweza kuwa na mfadhaiko kila wakati.

Isitoshe, wafanyakazi hao wasipokuwa na miradi hususa, hakutakuwa na umoja. Kwa mfano, hilo linaweza kutokea wakati msimamizi asiyejiamini anapotumia muda mwingi kutetea cheo chake badala ya kusimamia kazi. Hata huenda akajaribu kufanya hivyo kwa kuwagonganisha wafanyakazi. Pia, huenda wafanyakazi fulani wasijue majukumu yao kwa sababu hayajabainishwa waziwazi. Kwa mfano, wafanyakazi wawili wanaweza kugombana ikiwa kila mmoja wao anadhani kwamba yeye ndiye mwenye jukumu la kuidhinisha invoisi.

Katika hali hiyo, wafanyakazi hunyamaziana na mara nyingi hawasuluhishi mambo. Wivu huwafanya wasielewane na kuwachochea kushindana ili kupata kibali cha mkubwa. Makosa madogo huonwa kuwa makubwa. Basi, matatizo madogo yanakuwa matatizo makubwa. Hivyo, dhuluma inaweza kutokea.

Jinsi Dhuluma Inavyoanza

Baada ya kipindi fulani, huenda mfanyakazi mmoja akaanza kudhulumiwa. Huenda jambo hilo likampata mtu wa aina gani? Inaelekea ni mtu aliye tofauti na wengine. Kwa mfano, anaweza kuwa mwanamume anayefanya kazi na wanawake au mwanamke anayefanya kazi na wanaume. Huenda mtu anayejiamini akaonekana kuwa mchokozi, hali mtu mnyamavu akaonwa kuwa mdanganyifu. Huenda mtu anayeweza kudhulumiwa akawa mwenye umri mkubwa au kijana kuliko wengine au hata ndiye anayestahili zaidi kazi hiyo.

Haidhuru ni nani anayedhulumiwa, jarida la kitiba la mta la Ujerumani linasema kwamba wafanyakazi “huanza kumtesa na kumwonea mtu waliyechagua kudhulumu ili kujituliza kutokana na mfadhaiko wao.” Mtu anayedhulumiwa anapojaribu kusuluhisha hali hiyo huenda asifanikiwe sana na hata huenda mambo yakachacha. Kadiri dhuluma inavyozidi, ndivyo yule anayedhulumiwa anavyojihisi mpweke zaidi. Wakati huo, huenda anayedhulumiwa akashindwa kupambana na hali hiyo akiwa peke yake.

Bila shaka, watu wamekuwa wakidhulumiwa kazini sikuzote. Lakini huenda wengi wakakumbuka wakati ambapo wafanyakazi walishirikiana. Wafanyakazi hawakupanga kuwadhulumu wengine. Lakini kama vile daktari mmoja alivyosema, kwa miaka mingi “watu wameacha kuwa na umoja na hawajali.” Sasa watu hawajali hata wakipigana kazini.

Hivyo, wote walioajiriwa wangependa sana kupata majibu kwa maswali haya: Je, dhuluma inaweza kuzuiwa? Watu wanawezaje kufanya kazi pamoja kwa amani?

[Picha katika ukurasa wa 6]

Lengo la dhuluma ni kumfanya mtu ahisi kwamba hafai hata kidogo