Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mambo Tunayoweza Kujifunza Kutokana na Makaburi ya Peru

Mambo Tunayoweza Kujifunza Kutokana na Makaburi ya Peru

Mambo Tunayoweza Kujifunza Kutokana na Makaburi ya Peru

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI PERU

UNAWEZA kujifunza mambo mengi kuhusu jamii fulani ya watu kutokana na jinsi wanavyowatendea wafu wao. Hiyo ni kweli kabisa nchini Peru ambapo kuna mabaki ya tamaduni nyingi kama vile tamaduni chache za kabila la Moche, Chimu, Nazca, Chachapoya, Colla, na Inca. Kila utamaduni ulikuwa na desturi zake za maziko zilizoonyesha imani tofauti-tofauti kuhusu ulimwengu wa wafu.

Wanasayansi na vilevile wezi wa makaburi wamefukua maelfu ya makaburi na kugundua maiti zilizohifadhiwa vizuri zilizofungwa kwa vitambaa virefu vya pamba iliyofumwa au isiyofumwa. Baadhi ya vitambaa hivyo vimefumwa vizuri kwa mitindo mbalimbali. Maelfu ya miili iliyohifadhiwa vizuri imepatikana katika mchanga wenye joto wa jangwani katika Pwani ya Bahari ya Pasifiki, nchini Peru.

Makaburi ya Wakuu

Maiti za watu wa familia za kifalme waliozikwa pamoja na mali nyingi na panga na vitu vingine vya mfalme zimefukuliwa katika makaburi ya kabila la Moche. Watu wengine walizikwa na vitu hivyo pia. Inaonekana watumishi walitolewa dhabihu ili wawafuate wakuu wao katika ulimwengu wa wafu. Wengine hata walikatwa miguu. Kwa nini? Dhana moja inasema kwamba walikatwa miguu ili wasitoroke wajibu wao katika ulimwengu wa wafu.

Karibu na Ziwa Titicaca kwenye urefu wa meta 3,827 kuna makaburi makubwa yanayoitwa chullpas, ambayo ni minara ya mawe yenye urefu wa meta 12 hivi na ni mipana juu kuliko chini. Inaonekana hapo ndipo wakuu wa kabila la Colla, walioshindwa na kabila la Inca, walipozikwa. Baadhi ya makaburi hayo yana michongo ya nyoka, paka, na tumbili. Wanyama hao waliabudiwa kwa kuwa walionwa kuwa walinzi wa ulimwengu wa wafu.

Huko Karajia, karibu na mji wa Chachapoyas, kuna makaburi ya kustaajabisha. Kwenye miamba, kuna majeneza yenye urefu wa meta 2 yaliyotengenezwa kwa udongo mgumu, na baadhi yake yana mabaki ya rangi iliyotumiwa karne nyingi zilizopita. Nyuso zilizochongwa kwenye majeneza hayo zinakodolea macho vikali bonde lenye majani kana kwamba zinatawala eneo hilo lote.

Uthibitisho wa Ukatili

Hivi majuzi katika kitongoji kimoja cha Lima, wanaakiolojia wamefukua makaburi yenye kina kirefu yenye miili karibu 2,200 iliyohifadhiwa na kufungwa kwa vitambaa katika vifurushi. Inaonekana ni ya watu wa Inca na ilihifadhiwa vizuri sana. Kifurushi kimoja kilikuwa kikubwa sana na kilikuwa na uzito wa kilogramu 240 na urefu wa meta 1.8. Kilikuwa na maiti mbili—maiti ya mtu mmoja mashuhuri wa kabila la Inca ambayo ilikuwa imefungwa kwa kilogramu 140 za pamba na karibu na kifurushi hicho, maiti ya mtoto ambaye huenda alikuwa wa ukoo mmoja na mtu huyo. Mtu hubaki akijiuliza vifo hivyo vilisababishwa na nini.

Maiti nyingine ni za watoto waliotolewa dhabihu kwa miungu ya milima ya Andes. Yaelekea wazazi wao waliona ni pendeleo kuwatuma watoto wao kwenye “ule ulimwengu mwingine,” labda ili wakawawakilishe kwa miungu. Kwa kawaida watoto walizikwa kwenye kilele cha mlima au karibu nacho. Maiti ya msichana mmoja iliyofichwa kwa karne nyingi, ilipatikana kwenye theluji ya Sara Sara huko Ayacucho kwenye urefu wa meta 5,000 hivi. Watoto hao waliotolewa dhabihu walifungwa kwa vitambaa, na nyakati nyingine walizikwa pamoja na zawadi na vitu vingine kama vile michongo midogo ya dhahabu au fedha ya mnyama anayeitwa lama.

Ni Nini Uliokuwa Msingi wa Matumaini ya Wafu?

Si makabila hayo ya kale ya Peru tu yaliyokuwa na desturi za maziko zilizotegemea imani ya maisha baada ya kifo. Hata leo watu wanaonyesha kwa njia mbalimbali kwamba wanaamini kuna maisha baada ya kifo.

Kuna imani mbalimbali kuhusu maisha baada ya kifo. Kwa mfano, watu wengi wanaamini kuzaliwa upya katika mwili mwingine, uhamaji wa nafsi, toharani (purgatory), moto wa mateso, na kuwasiliana na wafu. Dhana kama hizo zinategemea fundisho moja, kwamba mtu anapokufa, mwili pekee ndio unaokufa na kitu fulani kisichoweza kufa huendelea kuishi. Biblia haiungi mkono dhana hizo.—Mhubiri 3:18-20; 9:5, 10; Ezekieli 18:4.

Badala yake, Biblia inafundisha kwamba mtu mwenyewe ni nafsi, kiumbe anayeweza kufa. (Mwanzo 2:7) Hata hivyo, Neno la Mungu pia linatoa tumaini zuri kwa ajili ya wafu. Biblia inafundisha kwamba kutakuwa na “ufufuo wa waadilifu na wasio waadilifu pia.” (Matendo 24:15) Biblia haisemi tu kuhusu tumaini hilo. Ina masimulizi ya watu waliojionea wafu wakifufuliwa. (Yohana 11:17-47; 1 Wakorintho 15:3-6) Basi mamilioni ya watu ambao wameishi na kufa wana taraja zuri kama nini!

[Picha katika ukurasa wa 13]

Majeneza huko Karajia (juu)

[Hisani]

© Mylene D’Auriol/PromPerú

[Picha katika ukurasa wa 13]

Minara ya makaburi yenye urefu wa meta 12, karibu na Ziwa Titicaca

[Hisani]

© Carlos Sala/PromPerú

[Picha katika ukurasa wa 14]

Maiti iliyoganda ya msichana mdogo ilipatikana juu ya Mlima wa Andes

Wanaakiolojia wamefukua maiti 2,200 hivi karibu na Lima

[Hisani]

Top left: © Alejandro Balaguer/PromPerú; inset: Ira Block/NGS Image Collection