Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kiapo cha Kale Ambacho Ni Muhimu Leo

Kiapo cha Kale Ambacho Ni Muhimu Leo

Kiapo cha Kale Ambacho Ni Muhimu Leo

KARIBU mwaka wa 400 K.W.K., Hippocrates, daktari Mgiriki anayejulikana kuwa mwanzilishi wa tiba aliandika kiapo cha Hippocrates. Kiapo hicho chenye kanuni zenye kuheshimika bado huwaongoza wanatiba. Je, hivyo ndivyo umefundishwa? Ikiwa ndivyo, si wewe peke yako. Lakini je, jambo hilo ni kweli kabisa?

Mambo ya hakika yanaonyesha kwamba huenda si Hippocrates aliyeandika kiapo hicho chenye jina lake. Isitoshe, leo wanatiba hawakubaliani nyakati zote na maandishi ya awali ya kiapo hicho.

Je, kweli tunajua mwandishi wa kiapo hicho cha kale? Na hata tukijua, je, kina umuhimu kwetu leo?

Je, Hippocrates Ndiye Aliyeandika Kiapo Hicho?

Kuna sababu nyingi zinazotilia shaka kwamba Hippocrates ndiye aliyeandika kiapo hicho. Sababu moja ni kwamba kiapo hicho kinaanza kwa kusihi miungu kadhaa. Hata hivyo, Hippocrates anaonwa kuwa mtu wa kwanza kutofautisha tiba na dini na kusema kwamba magonjwa yanasababishwa na mambo ya asili badala ya mambo yanayozidi uwezo wa wanadamu.

Isitoshe, mambo mengi yanayokatazwa katika kiapo hicho yalipatana na tiba ya wakati wa Hippocrates. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 21.) Kwa mfano, sheria na kanuni nyingi za kidini za wakati wa Hippocrates hazikukataza kutoa mimba na kujiua. Pia mtu anayeapa kwa kiapo hicho huahidi kutofanya upasuaji. Lakini vitabu vya kitiba vinavyodaiwa kuwa viliandikwa na Hippocrates na waandishi wengine wa kale, vinazungumzia mbinu za upasuaji.

Kwa hiyo, ijapokuwa bado kuna mjadala kuhusu mwandishi wa kiapo hicho, inawezekana hakikuandikwa na Hippocrates. Inaonekana falsafa ya kiapo hicho inapatana na maoni ya Wapaithagorea wa karne ya nne K.W.K., ambao walitetea kanuni zilizohusiana na utakatifu wa uhai na kupinga upasuaji.

Chatoweka na Kurudi

Haidhuru ni nani aliyeandika kiapo hicho, hakuna shaka kwamba kimekuwa muhimu sana katika nyanja ya tiba katika nchi zilizoendelea, na hasa, katika kutetea maadili. Kiapo hicho kimeitwa “kanuni bora zaidi kati ya maadili ya tiba,” “msingi wa uhusiano wa mgonjwa na daktari katika nchi zilizoendelea,” na “maadili ya juu zaidi yanayoongoza wataalamu.” Katika mwaka wa 1913, daktari maarufu wa Kanada Sir William Osler alisema: “Kiwe kiliandikwa au hakikuandikwa wakati wa Hippocrates, hilo si muhimu . . . Kwa karne 25 kiapo hicho kimetumiwa na wanatiba, na katika vyuo vikuu vingi maneno yake hutumiwa kuwaidhinisha watu kuwa madaktari.”

Hata hivyo, kiapo hicho kilipingwa mwanzoni mwa karne ya 20, labda kwa sababu ya maendeleo ya kisayansi wakati huo. Kwa kuwa watu waliamini kwamba wanapaswa kutumia akili ili wapate ujuzi na ukweli, kiapo hicho kilionwa kuwa kimepitwa na wakati na kwamba hakikufaa. Lakini licha ya maendeleo ya kisayansi, bado kanuni za maadili zinahitajiwa. Labda ndiyo sababu kiapo hicho kimekubaliwa tena katika miaka ya karibuni.

Katika nyakati za karibuni, madaktari wengi wanaoanza au kuhitimu masomo ya tiba wamekuwa wakiapishwa. Katika mwaka wa 1993, uchunguzi uliofanywa kuhusu shule za tiba za Marekani na Kanada, ulionyesha kwamba asilimia 98 ya shule hizo zilitumia kiapo fulani. Ni asilimia 24 tu ya shule zilizofanya hivyo mwaka wa 1928. Huko Uingereza, uchunguzi kama huo ulionyesha kwamba asilimia 50 hivi za shule hutumia kiapo au azimio fulani. Huko Australia na New Zealand, asilimia 50 hivi za shule hufanya hivyo pia.

Kubadilika na Wakati

Lakini kiapo cha Hippocrates kinaweza kubadilishwa. Kadiri miaka ilivyopita, kilibadilishwa kipatane na mafundisho ya Jumuiya ya Wakristo. Wakati mwingine mabadiliko yalifanywa ili kushughulikia mambo mengine kama vile watu wanaokumbwa na tauni. Hivi majuzi kimebadilishwa kipatane na maoni ya kisasa.

Katika tafsiri nyingi za kiapo hicho, dhana ambazo hazizungumzii tiba ya kisasa zimeondolewa huku dhana zilizo muhimu kwa jamii ya kisasa zikiongezwa. Kwa mfano, kanuni inayomwezesha mgonjwa ajiamulie mambo ni muhimu katika tiba ya leo, lakini haikuwapo katika tiba ya Ugiriki ya kale wala haikuwa sehemu ya kiapo cha Hippocrates. Viapo vingi vinavyotumiwa leo vinakazia sana haki za mgonjwa.

Isitoshe, uhusiano kati ya daktari na mgonjwa umebadilika kwani imekuwa muhimu sana kwa mgonjwa kupewa habari kamili kabla ya kukubali tiba. Kwa hiyo inaeleweka ni kwa nini shule chache tu za tiba zinatumia kiapo cha Hippocrates cha awali.

Labda mabadiliko mengine ya kiapo hicho ni ya kushangaza. Katika mwaka wa 1993, ni asilimia 43 tu ya viapo vilivyofanywa huko Marekani na Kanada vilivyosema kwamba madaktari wanawajibika kwa matendo yao. Tafsiri nyingi za kisasa za kiapo hicho hazihusishi adhabu ya kukiuka matakwa yake. Viapo vingi havikushutumu kumwua mgonjwa akiteseka sana, kutoa mimba, wala havikuhusisha uwezekano wa kuomba msaada wa miungu. Na asilimia 3 tu ya viapo vilivyotumiwa na shule zilizochunguzwa vilihusisha kiapo cha kutofanya ngono na wagonjwa.

Umuhimu wa Kiapo

Licha ya mabadiliko mengi katika kiapo cha Hippocrates, kwa kawaida viapo huonwa kuwa muhimu kwa wataalamu walioamua kufuata kanuni za maadili zenye kuheshimika. Uchunguzi uliofanywa mwaka wa 1993 ambao umetajwa juu, ulionyesha kwamba viapo vingi vinakazia ahadi ambazo madaktari huwapa wagonjwa wao zinazowawajibisha watu wanaotazamia kuwa madaktari kujitahidi kuwatunza wagonjwa kadiri wanavyoweza. Viapo hivyo hukazia kanuni nzuri za maadili zinazoongoza wanatiba.

Katika makala moja iliyochapishwa katika jarida The Medical Journal of Australia, Profesa Edmund Pellegrino aliandika: “Huenda watu wengi wanakiona kiapo cha tiba kuwa kitu cha zamani kisicho na umuhimu wowote. Lakini kanuni nyingi za kiapo hicho hazijasahauliwa na wataalamu na zikisahauliwa kabisa, tiba itakuwa biashara inayofanywa tu ili kupata faida.”

Huenda wataalamu wataendelea kubishania umuhimu wa kiapo cha Hippocrates au viapo vya kisasa vinavyokitegemea. Hata hivyo, madaktari wanapaswa kuthaminiwa kwa sababu ya kujitoa mhanga kuwatunza wagonjwa.

[Sanduku katika ukurasa wa 21]

KIAPO CHA HIPPOCRATES

TAFSIRI YA LUDWIG EDELSTEIN

Naapa kwa jina la Tabibu Apollo, Asclepius, na Hygieia na Panaceia na miungu wote, nikiwafanya kuwa mashahidi wangu kwamba nitatimiza kiapo hiki na agano hili kulingana na uwezo na utambuzi wangu:

Kumwona yule aliyenifunza kazi hii kama mzazi wangu na kushirikiana naye maishani, na ikiwa anahitaji pesa nitamgawia zangu, na nitawaona watoto wake kuwa sawa na ndugu zangu wa kiume na ikiwa wanataka, nitawafundisha kazi hii bila malipo wala agano; kuwafundisha kwa mdomo watoto wangu na watoto wa yule aliyenifunza na wanafunzi waliotia sahihi agano na ambao wameapa kulingana na sheria ya tiba wala si mwingine yeyote.

Nitatumia kanuni za lishe kwa faida ya wagonjwa kulingana na uwezo na utambuzi wangu; nitawalinda wasipatwe na madhara na dhuluma.

Sitampa mtu yeyote dawa inayoweza kumuua hata akiiomba wala sitaipendekeza kwa kusudi hilo. Vilevile sitamsaidia mwanamke kutoa mimba. Nitalinda uhai wangu na kazi yangu kwa usafi na utakatifu.

Sitafanya upasuaji hata kwa watu wanaougua kijiwe, lakini nitawaachia watu wanaofanya kazi hiyo.

Nyumba yoyote nitakayoitembelea, ni kwa faida ya mgonjwa, na sitataka kumdhulumu yeyote kimakusudi, kutumia ujanja wala kufanya ngono na watu wa kike na wa kiume, wawe huru au watumwa.

Chochote nitakachoona au kusikia, niwe ninamtibu mgonjwa au la, kinachohusiana na maisha ya watu, ambacho hakipaswi kutangazwa, nitakiweka kikiwa siri nikiona kuwa ni aibu kukisema.

Nikitimiza kiapo hiki bila kukivunja, acha niruhusiwe kufurahia maisha na kazi, niwe mashuhuri kati ya watu wote watakaoishi; nisipokitimiza na kuapa kwa uwongo, acha nipatwe na kinyume cha mambo hayo.

[Picha katika ukurasa wa 20]

Ukurasa wa maandishi ya Hippocrates

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]

Hippocrates and page: Courtesy of the National Library of Medicine