Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuwatembelea Ndege Waliokuwa Hatarini

Kuwatembelea Ndege Waliokuwa Hatarini

Kuwatembelea Ndege Waliokuwa Hatarini

SIKUZOTE nimependezwa na unamna-namna na umaridadi wa ndege. Nilipokuwa nikipanga kutembelea Bermuda, nilipata kitabu chenye habari kuhusu ndege anayeitwa cahow. Kitabu kimoja kuhusu ndege kilisema: “Idadi ndogo ya ndege hao inapatikana kwenye visiwa vya Bandari ya Castle, vilivyo katika eneo la mbali zaidi la Bermuda. Wakiwa huko wanachunguzwa na wako chini ya ulinzi mkali wa mtunzaji.”

Hamu yangu iliamshwa! Nilitamani sana kujionea ndege hao, hivyo nikawasiliana na Dakt. David Wingate, aliyekuwa afisa wa hifadhi huko Bermuda. Sasa amestaafu, lakini wakati huo alikuwa pia mtunzaji kwenye visiwa vya Bandari ya Castle. Dakt. Wingate aliniruhusu niambatane naye kutembelea sehemu iliyolindwa ambapo ndege hao hutagia.

Makao ya Viumbe

Hifadhi ya Viumbe ya Bandari ya Castle iko karibu na visiwa vikuu vya Bermuda, vilivyo katika Bahari ya Atlantiki, kilometa 900 hivi mashariki mwa North Carolina, Marekani. Kisiwa cha Nonsuch ndicho kikubwa zaidi kati ya visiwa tisa vidogo ambavyo ni sehemu ya hifadhi hiyo. Kisiwa cha Nonsuch kina ukubwa wa ekari 15 na kiko mashariki kabisa mwa Bermuda. Chini ya usimamizi wa Dakt. Wingate, kisiwa hicho kilifanywa kuwa makao ya viumbe ili hatimaye mimea na wanyama wa asili waliosalia wa Bermuda wahifadhiwe.

Siku moja nyangavu na yenye kupendeza tunaanza safari katika mashua ya Dakt. Wingate kutoka Nonsuch kuelekea kisiwa kidogo cha karibu. Furukombe anaruka juu ya maji ya bahari, huku manyoya meupe ya mabawa yake yakionyesha rangi ya bluu ya maji. Ndege maridadi wa tropiki wanaoitwa mikia-mirefu huko Bermuda, wanaruka kwa furaha kana kwamba wanachumbiana huku manyoya ya mkia wao mkubwa yakipepea juu na chini. Kwa kawaida ndege hao wangenivutia, hata hivyo leo ninafikiria tu kuhusu ndege wa cahow.

Ndege Huyo Atokea Tena

Dakt. Wingate anaeleza: “Walowezi walioishi huko zamani walisema kwamba ndege fulani wa baharini walirudi kwenye nchi kavu usiku na walipokuwa wakitaga tu kama ndege wa cahow. Wakati huo idadi ya cahow ilikuwa kubwa sana, lakini mambo yakabadilika. Karibu na mwaka wa 1560, Wahispania walipeleka nguruwe huko Bermuda. Hiyo ilikuwa hatari sana kwa ndege hao kwa sababu nguruwe walikula mayai yao, vifaranga wao, na huenda hata ndege wakubwa. Watu walioishi huko pia walikula sana ndege hao. Panya walipopelekwa Bermuda bila kukusudia mwaka wa 1614, cahow zaidi walikufa. Panya hao waliogelea mpaka kwenye visiwa vidogo ambako cahow walitaga mayai na kula mayai na vifaranga wao. Hivyo, kufikia mwaka wa 1630, ndege wa cahow walikuwa wamepungua sana hivi kwamba walifikiriwa kuwa wametoweka kabisa.”

Niliuliza hivi huku mashua ikivuma: “Ndege wa cahow waligunduliwaje tena?”

Dakt. Wingate anajibu: “Mwaka wa 1906, Louis Mowbray, mtaalamu wa vitu vya asili, alimpata ndege wa ajabu akiwa hai kwenye kisiwa kimoja kwenye Bandari ya Castle. Hatimaye alitambuliwa kuwa ndege wa cahow. Baadaye, mwaka wa 1935, kifaranga wa cahow alipatikana akiwa amekufa baada ya kugonga mnara wa taa. Na mwaka wa 1945, cahow mkubwa alipatikana akiwa amekufa kwenye ufuo wa Kisiwa cha Cooper, Bermuda. Huo ulikuwa uthibitisho uliotosha kuwafanya watafiti kutafuta ndege wengine. Kikundi cha watafiti kiliongozwa na Dakt. Robert Cushman Murphy wa Hifadhi ya Marekani ya Vitu vya Asili, na Louis S. Mowbray, msimamizi wa Hifadhi ya Serikali ya Viumbe wa Baharini ya Bermuda, ambaye ni mwana wa Louis Mowbray aliyempata yule cahow mwaka wa 1906.”

Dakt. Wingate anatabasamu anapoeleza: “Lilikuwa pendeleo kubwa kuombwa nijiunge na kikundi hicho, hasa kwa sababu nilikuwa mwanafunzi tu mwenye umri wa miaka 15 na nilipendezwa sana na ndege! Jumapili hiyo ya Januari 28, 1951, ilikuwa siku ambayo ilibadili maisha yangu. Sitasahau kamwe furaha ya Dakt. Murphy wakati yeye na Mowbray walipofanikiwa kumshika cahow akiwa hai katika nyufa yenye kina kirefu! Punde baadaye, serikali ikafanya visiwa vidogo vya Bandari ya Castle kuwa hifadhi ya cahow. Kisiwa cha Nonsuch kikawa sehemu ya hifadhi hiyo mwaka wa 1961, na mwaka uliofuata, mimi na mke wangu tulihamia huko ili niwe mtunzaji wa hifadhi hiyo.”

Tulipokaribia hifadhi hiyo niliuliza: “Mlipata cahow wangapi wakati wa utafiti huo wa kwanza?”

Alijibu: “Vikundi vinane vya ndege wawili-wawili vilipatikana mwaka wa kwanza. Ilikuwa vigumu sana kupata viota vyao hivi kwamba ilichukua miaka kumi kupata idadi yote ya ndege hao ambayo wakati huo ilitia ndani vikundi 18 vya ndege wawili-wawili wanaotaga. Baada ya miaka mingine 35 ya kuwahifadhi, waliongezeka na kufikia idadi ya vikundi 52 vya ndege wawili-wawili.”

Msaada wa Wanadamu

Dakt. Wingate anaongeza hivi: “Ndege wa cahow huishi katika mashimo yenye kina cha meta 2 mpaka 3.5, ambayo yamejipinda ili kuzuia mwangaza usifike kwenye kiota. Ili kuongeza sehemu za kutagia mayai, tulichimba mashimo. Tuliyatengeneza kwa kuchimba mitaro na kuifunika kwa saruji. Mwishoni mwa shimo kuna kifuniko kinachoweza kutolewa. Hiyo inatuwezesha kuona viota ili kutambua ikiwa kuna yai lililotagwa au kuanguliwa au yai ambalo halikuanguliwa. Wakati yai ambalo halikuanguliwa linapoachwa, tunaweza kulichukua ili kulichunguza kuona kwa nini halikuanguliwa. Katikati ya miaka ya 1960, mabaki ya dawa ya kuua wadudu ya DDT yalisababisha gamba la yai kuwa nyembamba na kuvunjika. Sasa tuna wasiwasi kwamba kemikali kama PCB [polychlorinated biphenyl] inaweza kusababisha madhara kama hayo. Ingawa Amerika Kaskazini na Ulaya imepiga marufuku matumizi ya kemikali hizo, nchi nyingi zinazoendelea hazijafanya hivyo.”

Kuna matatizo mengine. Dakt. Wingate anasema: “Ndege wa cahow na ndege wakali zaidi wa tropiki wamekuwa wakipigania mahali pa kutagia mayai. Huenda ndege wa cahow akachagua mahali pa kutagia ndani ya shimo lenye kina kifupi, kisha ndege wa tropiki akajenga kiota chake mlangoni! Ndege huyo mchokozi huharibu mayai au hushambulia na kuua vifaranga wa cahow. Kwa kuwa kila wakati ndege hao wawili hurudi mahali pao pa kutagia, tatizo hilo huendelea mwaka baada ya mwingine. Ili kuwaokoa ndege wa cahow, tuliweka vizibo vya mbao kwenye milango ya mashimo yao. Vizibo hivyo vina umbo la yai linalotosha ndege wa cahow kuingia bila kumruhusu ndege mkubwa wa tropiki kuingia. Hivyo, ukubwa wa milimeta 3 huokoa maisha ya ndege wa cahow.”

Ndani ya Hifadhi

Mwishowe, tunafika kwenye kisiwa kidogo. Tunatoka kwenye mashua katikati ya mawimbi ya bahari na kukanyaga miamba iliyochongoka. Ili kufikia viota, inatubidi kupanda juu ya miamba mirefu yenye ncha kali. Kiota kimoja kinaweza kufikiwa tu kwa ngazi. Huenda hiyo ni kawaida kwa Dakt. Wingate, lakini kwangu mimi, ni jambo la kusisimua!

Dakt. Wingate anachunguza viota vyote. Je, bado makundi ya ndege yanatembelea viota vyao? Je, kuna alama za nyayo kuelekea mashimo hayo? Je, kuna mayai ambayo hayajaanguliwa? Tunapata yai moja ambalo halijaanguliwa, lakini kwa kuwa halikuachwa kabisa, Dakt. Wingate analiacha hapo. Mara nyingi, ndege wa cahow huendelea kukalia mayai ambayo hayajaanguliwa bila kukata tamaa. Dakt. Wingate anagundua jambo jingine asilotazamia. Anapata kifaranga mahali ambapo hakuwa ameona yai! Uvumbuzi huo unamfurahisha hivi kwamba anasahau lile yai ambalo halikuwa limeanguliwa.

Jitihada zote hizo haziambulii patupu kwani Dakt. Wingate anapoondoa kifuniko cha shimo ninaona kitu kidogo chenye rangi ya kijivu. Ni kifaranga wa cahow. Mara kwa mara, anasongasonga kwa sababu ya kusumbuliwa na mwangaza. Katika mashimo mengine, ninaona ndege mkubwa akiwa amekalia yai.

Dakt. Wingate amewasaidia vifaranga wengi waliokuwa hatarini. Ndege mmoja wa tropiki alimshambulia kifaranga na kuvunja mdomo wake. Kwa kufadhaika, Wingate aliunganisha mdomo huo. Alishangaa na kufurahi sana wakati kifaranga huyo alipopona! Wakati mwingine, alimwokoa kifaranga dhaifu ambaye alikuwa ameachwa akiwa mdogo sana na wazazi wake. Alimweka kwenye kisanduku, akamlisha uduvi, ngisi, mafuta ya chewa, na vitamini. Hatimaye, aliweza kuruka baharini. Kufikia sasa, jitihada za kuhifadhi ndege wa cahow zinafanikiwa. Ama kwa hakika, ndege huyo amekuwa ishara ya tumaini kwa wahifadhi ulimwenguni kote. Lengo la Dakt. Wingate ni kuona Kisiwa cha Nonsuch kikiwa na makundi 1,000 ya ndege wawili-wawili wa cahow hatimaye. Tutaona ikiwa lengo hilo litatimia.

Kuwatembelea ndege wa cahow waliokuwa karibu kutoweka hunifanya nifikiri. Ikiwa Muumba anatambua wakati shomoro anapoanguka chini, je, hatatambua wakati jamii nzima ya ndege inapokuwa hatarini? (Mathayo 10:29) Inafariji kama nini kujua kwamba siku moja wanadamu hawatahatarisha jamii yoyote ya viumbe duniani!—Isaya 11:6-9.—Tumetumiwa makala hii.

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BERMUDA

Kisiwa cha Nonsuch

[Picha katika ukurasa wa 18]

Ndege wa “cahow” akiwa ndani ya shimo

[Hisani]

Jeremy Madeiros, Conservation Officer, Bermuda

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mlango wa shimo la ndege huyo

[Picha katika ukurasa wa 18]

Dakt. Wingate anaonyesha kizibo kwenye mlango wa shimo la “cahow”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Jeremy Madeiros, Conservation Officer, Bermuda

Globe: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

© Brian Patteson

Jeremy Madeiros, Conservation Officer, Bermuda