Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Vidonda Vyenye Zipu

Gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung linaripoti kwamba kufunga vidonda kwa zipu ya tiba ni afadhali kuliko kuvishona. “Bendeji yenye zipu hunata kama bendeji za kawaida. Bendeji hiyo, ambayo ina meno ya zipu, hubandikwa pande zote za kidonda na kufungwa kama zipu ya nguo.” Uchunguzi uliofanywa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Göttingen, Ujerumani, ulilinganisha vikundi viwili vya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe ngozini. Sehemu iliyo chini ya ngozi yao ilishonwa kama kawaida. Lakini tabaka la juu la ngozi ya wagonjwa wa kikundi kimoja lilifungwa kwa zipu za tiba huku wale wa kikundi kile kingine walishonwa kama kawaida. Vidonda vilivyotiwa zipu havikuacha makovu makubwa na alama nyingi za mishono kama vidonda vilivyoshonwa.

Chungu Wanaotengeneza Dawa ya Kuua Magugu

Shirika la habari la Bloomberg linaripoti hivi: “Chungu fulani wanaokuza kuvu kwa ajili ya chakula hutengeneza pia dawa ya kuua magugu.” Chungu fulani hawawezi kumeng’enya majani na vitu wanavyoingiza kwenye vichuguu vyao. Wao huhifadhi majani yaliyooza ambayo wamekusanya katika vyumba vyao na huyatumia kukuza kuvu. Hata hivyo, kuvu hizo hushambuliwa na kimelea kidogo sana ambacho hupunguza au kuharibu chakula chao. Ili kulinda kuvu, chungu hutengeneza bakteria juu ya miili yao. Ripoti hiyo inasema: “Wakati kimelea kinaposhambulia, chungu hao hukisugua kwa miili yao na kukipaka dawa hiyo ya kuua magugu.”

Waumini Wanapungua Nchini Kanada

Katika mahojiano yaliyofanywa na gazeti Publishers Weekly, mwandishi Yann Martel wa Kanada ambaye ana asili ya Kifaransa alisema kwamba “waumini wanapungua sana nchini Kanada.” Isitoshe, ripoti moja ya gazeti The New York Times inasema kwamba huko Montreal “idadi ya watu wanaoenda kanisani inapungua haraka sana hivi kwamba katika miaka mitatu iliyopita makanisa 18 yamefungwa, yakaachwa, na kugeuzwa kuwa nyumba, na hata moja liligeuzwa kuwa duka la kuuza piza.” Marguerite Van Die, profesa wa theolojia kwenye Chuo Kikuu cha Queen’s huko Kingston, Ontario, anasema kwamba “katika jamii hii, dini haina nguvu yoyote.”

Radi ya Venezuela Husaidia Tabaka la Ozoni

Ingawa asilimia 90 ya tabaka la ozoni limefanyizwa kwa mnururisho wa urujuanimno kutoka kwa jua, asilimia 10 iliyosalia hufanyizwa na radi. Na radi hutukia mara nyingi katika maeneo yenye majimaji ya Mbuga ya Kitaifa ya Catatumbo, katika Jimbo la Zulia, nchini Venezuela. Gazeti The Daily Journal la Caracas linaripoti kwamba “radi hutukia kwa siku 140 hadi 160” kila mwaka katika eneo la Mto Catatumbo. Inasemekana kwamba radi hiyo hutokezwa na methani, ambayo hufanyizwa kwa majani yanayooza na kwa vitu vingine vilivyo kando ya mto na kwenye mabwawa ya matope yaliyo karibu, pamoja na mawingu yaliyo chini na hali mbaya ya hewa. Jambo jingine la pekee kuhusu radi inayotukia Catatumbo ni kwamba inaanzia mbali sana hivi kwamba ngurumo zake hazisikiki. Kituo cha Internet cha Lost World Adventures kinasema kwamba hilo “ni tukio lisilo na kifani ulimwenguni.”

Majiji Yenye Gharama za Juu za Maisha

Tokyo, Moscow, na Osaka ndiyo majiji yenye gharama za juu zaidi za maisha ulimwenguni. Hiyo ndiyo kauli iliyofikiwa katika uchunguzi uliofanywa na shirika la Mercer Human Resource Consulting. Uchunguzi huo uliohusisha majiji 144, ulilinganisha bidhaa na huduma zaidi ya 200, kutia ndani gharama za nyumba, mavazi, usafiri, burudani, fanicha, na vyombo vya nyumbani. Nusu ya majiji 20 yenye gharama za juu zaidi za maisha yako Asia. Geneva, London, na Zurich ni miongoni mwa majiji yenye gharama za juu zaidi barani Ulaya, baada ya Moscow. New York City ndilo la kumi katika orodha hiyo, hali hakuna jiji lolote la Kanada lililoorodheshwa katika nafasi 100 za kwanza. Jiji la Asunción nchini Paraguay ndilo jiji lenye gharama za chini zaidi za maisha.

Lugha Zinazotokomea

Uchunguzi mmoja ulioripotiwa katika gazeti The Independent la London unasema kwamba “idadi ya lugha zinazozungumzwa ulimwenguni zinapungua haraka kuliko jinsi wanyama wanavyopungua.” Wataalamu wa lugha wanakadiria kwamba ulimwenguni pote watu huzungumza lugha 6,809, na asilimia 90 huzungumzwa na watu wasiozidi 100,000. Lugha 357 zinazungumzwa na watu wasiozidi 50, hali 46 huzungumzwa na mwenyeji mmoja tu. Ukoloni umefanya lugha 52 kati ya 176 za makabila ya Amerika Kaskazini zitokomee, na vilevile lugha 31 kati ya lugha 235 za makabila ya Waaborijini wa Australia zimetokomea. Profesa Bill Sutherland wa Chuo Kikuu cha East Anglia, Uingereza, alisema kwamba ikiwa hatari inayokabili lugha italinganishwa na jinsi wanyama wanavyohatarishwa, idadi kubwa ya lugha zitasemwa kuwa “zinakabili hatari kubwa,” “zinakabili hatari,” au “ziko karibu kukabili hatari.” Anaongeza hivi: “Hatari zinazokabili ndege na wanyama zinajulikana wazi lakini inaonekana lugha zinahatarishwa hata zaidi.”

Kisababishi cha Mafua

Gazeti The New York Times linasema kwamba watu wengi husema “ukipigwa na baridi utapata mafua.” Hata hivyo, “kwa zaidi ya karne moja, wanasayansi wametumia wakati na nguvu nyingi wakijaribu kukanusha wazo hilo. Lakini licha ya jitihada zao, hakuna uthibitisho wa kutosha kuonyesha kwamba mafua hayasababishwi na hali ya hewa na hilo huwafanya wajitoe mhanga kufanya uchunguzi zaidi.” Tangu Louis Pasteur alipofanya uchunguzi mwaka wa 1878, uchunguzi mwingi umefanywa kutambua jinsi baridi inavyochangia mafua. Si ajabu kwamba watafiti hawana uhakika kuhusu jambo hilo. Dakt. Jack Gwaltney, Jr., mmoja wa wataalamu wakuu zaidi wa mafua ulimwenguni, anadokeza kwamba mafua husababishwa na kiasi cha unyevu hewani wala si joto. Kulingana na gazeti Times, “mafua si ugonjwa mmoja bali ni mchanganyiko wa magonjwa mengi yanayofanana, na yote hutokea kwa mfuatano kulingana na hali ya hewa na kwa njia zisizojulikana kwa sasa.”

Matatizo ya Akili Kazini

Gazeti Globe and Mail la Kanada linasema “siku hizi watu wanashindwa kufanya kazi kwa sababu ya matatizo ya akili wala si ya kimwili.” Zaidi ya makampuni 180 huko Kanada yalishiriki katika uchunguzi kuhusu kushughulikia matatizo ya kushindwa kufanya kazi. Kulingana na uchunguzi huo, “asilimia 79 ya washiriki walisema kwamba matatizo ya akili ndiyo huwafanya watu washindwe kufanya kazi kwa kipindi kifupi na asilimia 73 wakasema kwamba matatizo hayo ndiyo kisababishi kikuu cha kushindwa kufanya kazi kwa muda mrefu.” Baadhi ya sababu zilizotajwa kuwa zinachangia ongezeko la mfadhaiko kazini, mahangaiko, na kushuka moyo ni kwamba wafanyakazi wazee wanashindwa kufanya kazi nyingi, na teknolojia ya kisasa inawafanya waajiriwa “wafanye kazi kila wakati” hata wakiwa nyumbani. Kulingana na Dakt. Richard Earle, wa Taasisi ya Mfadhaiko ya Kanada huko Toronto, waajiri wanaweza kusaidia “kwa kuwaelimisha wasimamizi jinsi ya kutambua na kushughulikia matatizo ya akili na kutoa huduma za kuwasaidia wafanyakazi na huduma nyinginezo.”