Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Eneo la Ireland Lenye Kuvutia

Eneo la Ireland Lenye Kuvutia

Eneo la Ireland Lenye Kuvutia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI IRELAND

SI KILA mtu aliyevutiwa na eneo hilo. Wengine waliliona kuwa jangwa kame lenye miamba. Luteni-Jenerali Mwingereza Edmund Ludlow alisema hivi baada ya kutembelea eneo hilo katika mwaka wa 1651: “Hakuna maji ya kutosha kumzamisha mtu, hakuna mti unaoweza kumtundika mtu, wala udongo wa kutosha kumzika.”

Hata hivyo, wageni wengi huvutiwa nalo. Wataalamu wa viumbe, wa mimea, wanaakiolojia, wanahistoria, na maelfu ya watu wengine ambao hutembelea eneo hilo kwa ukawaida huliona kuwa “lenye kuvutia na lenye kustaajabisha sana.” Ni eneo gani hilo? Kwa nini linawavutia watu wengi?

“Eneo Lenye Miamba”

Liko kwenye pembe moja ya Ulaya kwenye pwani ya magharibi ya Ireland kati ya majabali maarufu ya Moher upande wa kusini na Ghuba ya Galway upande wa kaskazini. Eneo hilo linaitwa Burren, jina linalotokana na neno boireann la Ireland linalomaanisha “eneo lenye miamba.”

Eneo hilo lina miamba mingi. Kitabu kimoja cha mwongozo kinasema kwamba katika maeneo mengi “miamba mikubwa ya chokaa ya kijivu na majabali yaliyotokezwa na tukio lisilo la kawaida yako kila mahali.” Eneo zima la Burren limekalia miamba ya chokaa ambayo iko kwenye eneo la kilometa 1,300 hivi za mraba. Ni kana kwamba sehemu kubwa ya eneo hilo “la ajabu linalofanana na mwezi” haina udongo wowote.

Ni Kama “Kifaa Kikubwa cha Kuhifadhi Joto”

Upepo na mvua vimechonga miamba hiyo ya chokaa na kufanyiza maumbo ya kupendeza, yanayofanya eneo la Burren kuwa lenye kuvutia kwa njia ya pekee. Lakini si umaridadi wake uliowavutia watu walioishi huko maelfu ya miaka iliyopita. Walipendezwa hasa na uwezo wa ajabu wa Burren wa kutokeza majani ya kutosha kulisha ng’ombe mwaka mzima.

Eneo kubwa la miamba ya chokaa lenye kina cha zaidi ya meta 900 katika sehemu fulani ni kama “kifaa kikubwa cha kuhifadhi joto, kinachofyonza joto wakati wa kiangazi na kuliondoa polepole wakati wa baridi kali.” Zaidi ya hilo, hali ya joto ya wastani ya bahari ilifanya eneo hilo kuwa eneo linalofaa kilimo, lililotumiwa na wakazi hao wa mapema.

Wajenzi wa Zamani

Kuna mambo mengi yanayoonyesha kwamba kulikuwa na watu walioishi katika eneo la Burren, kama wale wakulima wa mapema. Kuna mawe mengi makubwa ya makaburi. Jiwe linalojulikana sana ni la Poulnabrone, lililojengwa muda mrefu kabla ya wakati wa Kristo. Tunachoweza kuona leo ni mabaki ya kaburi la kale—mawe makubwa ya chokaa yaliyotumiwa na wajenzi wa kale kujenga kaburi hilo ili kuwakumbuka “watu wao maarufu waliokufa.” Wataalamu wanasema kwamba wakati kaburi hilo lilipojengwa, lilifunikwa kwa rundo kubwa la mawe na udongo.

Kabla ya Waselti kuwasili nchini Ireland, wakazi wa Burren walikuwa wamejenga makaburi mengi ya umbo la kabari. Katika mwaka wa 1934, huko Gleninsheen, kijana mmoja aliona “kitu cha ajabu.” Kilikuwa mkufu maridadi wa dhahabu, ambao sasa unaonwa kuwa “mojawapo ya maendeleo makubwa ya masonara wakati Zama za Shaba Nyekundu zilipokaribia kwisha nchini Ireland.”

Mambo mengi hayajulikani kuwahusu watu hao wa kale. Walikuwa watu wa aina gani? Waliamini nini? Kwa nini walijenga majengo kama yale yaliyo katika kilele cha Kilima cha Turlough? Je, eneo hilo la kiajabu ni ngome ya kale iliyojengwa kilimani, au ilitengwa kuwa sehemu takatifu kwa ajili ya desturi za kidini? Hakuna anayejua.

Baadaye watu walijenga nyumba na kuzungusha maboma ya mawe au udongo. Kisha wengine wakajenga makanisa, makao ya watawa, na kasri.

Mapango ya Burren

Hata mapango ya Burren yanavutia. Maji yamepenya chini kwenye miamba ya chokaa na kutokeza “mojawapo ya mapango yenye kustaajabisha zaidi ya Ireland.” Kuna mapango mengi sana. Mengi yana vijito, mito, na maporomoko ya maji. Inasemekana kwamba pango linaloitwa Poll an Ionain, lina jiwe refu zaidi la chokaa linaloning’inia barani Ulaya lenye urefu unaozidi meta tisa!

Kwa kuwa mapango mengi ni hatari, watu wanaotembelea mapango hayo ambao hawataki kuhatarisha uhai wao hutembelea pango la Burren linaloitwa Aillwee, ambalo ndilo pango la umma. Huko unaweza kuona mabaki ya mnyama ambaye alitoweka nchini Ireland zaidi ya miaka elfu moja iliyopita, yaani dubu wa kahawia. Inaonekana dubu hao waliishi ndani ya mapango hayo wakati wa baridi, kwani hali ya joto ya mapango hayo huwa nyuzi 10 Selsiasi mwaka mzima. Ndani kabisa ya mapango ya chokaa, unaweza kuona mawe ya chokaa yenye maumbo ya ajabu, na miamba mingine isiyo ya kawaida. Unaweza pia kujaribu kuwazia kiasi cha maji kilichofanyiza mapango hayo ya ajabu.

“Mimea ya Aina Mbalimbali”

Jambo linalofanya eneo la Burren liwe tofauti ni mimea yake. Mwandishi mmoja anasema kwamba ni “mojawapo ya sehemu zenye kustaajabisha na zenye unamna-namna mwingi barani Ulaya.” Kuna fuo na milima, malisho na misitu. Kuna mamia ya mabonde yaliyozungukwa na miamba, yaliyofanyizwa maelfu ya miaka iliyopita wakati baadhi ya mapango ya Burren yalipoporomoka. Katika majira ya kiangazi maziwa fulani ya kiajabu hukauka na kuwa malisho. Kuta za mawe, nyingine zilizofanyizwa maelfu ya miaka iliyopita, ziko kila mahali kwenye miamba ya chokaa na huzunguka maeneo yenye mimea na nyasi.

Pia kuna mianya na nyufa kwenye miamba ya chokaa, zinazofanya eneo hilo liwe la kipekee. Nyufa hizo zinaweza kufikia kina cha meta mbili. Katika kila ufa, kuna udongo ambao umeota mimea ya aina mbalimbali.

Mtaalamu wa mimea Cilian Roden, anasema kotekote katika Burren, “mimea yenye kupendeza ambayo kwa kawaida haipatikani kwa urahisi inapatikana kwa wingi kama mibaruti au miti yenye miiba.” Ingawa kuna aina 600 tofauti za mimea, si wingi au unamna-namna wa mimea hiyo unaofanya eneo la Burren liwe tofauti. Ni jinsi ambavyo mimea hiyo imechangamana. Kwa miaka mingi, wataalamu wa mimea wameshangaa “jinsi mimea ya Aktiki, ya milima ya Alps, ya Mediterania, mimea inayonawiri kwenye udongo wenye asidi na wenye alkalini inavyokua pamoja katika sehemu hiyo ndogo iliyo magharibi mwa Ireland.”

Ua moja la buluu ambalo linadhaniwa kwamba humea katika milima ya Alps, humea hata kwenye usawa wa bahari wa Burren. Mimea fulani ya Aktiki na ya maeneo yaliyo karibu na tropiki yanapatikana karibu-karibu. Zaidi ya aina 20 za okidi husitawi katika eneo hilo. Pia kuna mimea ya wild thyme, wood sorrel, bloody cranesbill, bird’s-foot trefoil, thrift, na mingine mingi. Hivyo inafaa kusema kwamba eneo la Burren lina “mimea ya aina mbalimbali.”

Kweli, eneo hilo lina miamba mingi. Hata hivyo, Burren si jangwa lisilo na mimea. Linaonyesha umaridadi na unamna-namna wa uumbaji. Linasisimua, linafurahisha, linachochea, na linachangamsha moyo. Tembelea Ireland uone eneo la Burren lenye kuvutia!

[Ramani katika ukurasa wa 22]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

IRELAND KASKAZINI

IRELAND

Eneo la Burren

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mandhari ya Burren

[Picha katika ukurasa wa 23]

Majabali ya Moher yenye urefu wa meta 200 kutoka Bahari ya Atlantiki

[Picha katika ukurasa wa 22]

Ndani: Hata mapango ya Burren yanavutia

[Hisani]

Courtesy of Aillwee Caves

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]

Courtesy www.burrenbeo.com

[Picha katika ukurasa wa 24 zimeandaliwa na]

Flowers: Courtesy www.burrenbeo.com