Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Amate—Mafunjo ya Mexico

Amate—Mafunjo ya Mexico

Amate—Mafunjo ya Mexico

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

WENYEJI wa Mexico wana historia ndefu yenye kupendeza. Vitabu vyenye picha zinazowakilisha maneno ni mojawapo ya vitu vya thamani vya kitamaduni ambavyo vimesalia. Mtu anaweza kuchunguza mambo mengi katika vitabu hivyo kama vile historia, sayansi, dini, utaratibu wa kupanga miaka na matukio, na hata maisha ya kila siku ya jamii zilizostaarabika za eneo la Marekani na Mexico kama vile Waazteki na Wamaya. Watu walioitwa tlacuilos au waandishi waliandika historia yao kwa njia ya kusisimua juu ya vifaa mbalimbali.

Ingawa vitabu fulani vilitengenezwa kwa vitambaa, ngozi za mbawala, au aina fulani ya mkonge-pori, karatasi za amate ndizo zilizotumiwa hasa. Neno amate linatokana na neno amatl la lugha ya Nahuatl, linalomaanisha karatasi. Karatasi za amate zilitokana na ganda la aina fulani ya mtini wa jamii ya Moraceae. Kulingana na kitabu Enciclopedia de México, ‘ni vigumu kutofautisha jamii nyingi za miti hiyo isipokuwa utazame shina, majani, maua, na matunda yake.’

Jinsi Karatasi Hizo Zinavyotengenezwa

Baada ya ushindi wa Wahispania katika karne ya 16, jitihada zilifanywa kuzuia karatasi hizo zisitengenezwe. Kwa nini? Washindi hao waliona kwamba utengenezaji wa karatasi hizo ulihusiana sana na desturi za kidini zilizokuwapo kabla ya ushindi wao, ambazo zilishutumiwa na Kanisa Katoliki. Katika kitabu chake Historia de las Indias de Nueva España e Islas de la Tierra Firme, mtawa Mhispania Diego Durán alisema kwamba wenyeji “waliandika historia ndefu sana kuhusu mababu zao. Maandishi hayo yangetuelimisha sana ikiwa watu hawangeyaharibu kwa sababu ya ujinga. Watu fulani wajinga walifikiri kwamba maandishi hayo yalikuwa sanamu, wakayachoma, ijapokuwa yalikuwa rekodi muhimu ya historia.”

Hata hivyo, jitihada za kukomesha desturi ya kutengeneza karatasi hazikufaulu, na ingali inaendelea hadi leo. Karatasi zingali zinatengenezwa katika sehemu mbalimbali za milima ya kaskazini ya Sierra katika jimbo la Puebla, kama vile huko San Pablito, katika manispaa ya Pahuatlán. Likinukuu habari zilizorekodiwa na daktari wa Mfalme Philip wa 2, Francisco Hernández, gazeti Arqueología Mexicana (Akiolojia ya Mexico) linasema kwamba “watengenezaji wa karatasi walikata tu matawi manene ya miti na kuacha miche. Kisha, wakati wa usiku, matawi hayo yalitiwa ndani ya mito au vijito vya karibu ili yawe laini. Siku iliyofuata, ganda lilitenganishwa na tawi, ganda la nje likatenganishwa na la ndani, kisha la nje likatupwa.” Ganda la ndani liliposafishwa, sehemu zake zilitandazwa na kupondwa-pondwa kwa nyundo ya mawe.

Siku hizi, sehemu hizo za mti huchemshwa katika mabirika makubwa na kutiwa jivu na chokaa ili kuzilainisha na kuondoa vitu fulani. Zinaweza kuchemshwa kwa saa sita hivi. Kisha zinasafishwa kwa maji na kuachwa ndani ya maji. Mafundi hutandaza sehemu mojamoja juu ya kipande bapa cha mbao huku nyingine zikitoka upande wa kushoto hadi kulia na nyingine zikitoka juu hadi chini. Baadaye, wao hugongagonga sehemu hizo hadi zinaposokotana na kutengeneza karatasi. Mwishowe, ncha za karatasi hukunjwa ndani ili ziwe ngumu, na karatasi huanikwa juani ili ikauke.

Karatasi hizo huwa na rangi mbalimbali. Kwa kawaida huwa za kahawia, lakini kuna nyeupe, za rangi ya pembe ya tembo, zenye madoadoa ya kahawia na meupe, na pia za manjano, buluu, waridi, na kijani.

Jinsi Zinavyotumiwa Leo

Vitu maridadi vya Mexico, ambavyo vimeundwa kwa mkono, hutengenezwa kwa karatasi hizo. Ijapokuwa picha fulani zilizochorwa kwenye karatasi hizo zinahusiana na dini, nyingine zinaonyesha wanyama, sherehe, na mandhari kuhusu maisha yenye furaha ya wenyeji wa Mexico. Mbali na picha maridadi, karatasi hizo zimetumiwa pia kutengeneza kadi, vifaa vya kutia alama katika kitabu, na vitu vingine. Ufundi huo huwavutia wenyeji na wageni ambao huvinunua ili wavitumie kama mapambo. Vifaa hivyo vinauzwa pia katika nchi nyingine. Vitabu vinavyofanana na vitabu vya kale vimetengenezwa. Hapana shaka Wahispania walivutiwa navyo walipoviona mara ya kwanza! Diego Durán, mtawa wa chama cha watawa cha Dominic aliyetajwa awali, alisema kwamba wenyeji “waliandika na kuchora mambo mengi katika vitabu na karatasi ndefu na kutia miaka, miezi, na siku ambazo mambo hayo yalitukia. Amri na sheria zao, orodha zao za sensa, n.k., ziliandikwa kwenye michoro hiyo kwa utaratibu na upatano mkubwa sana.”

Inapendeza kuona kwamba desturi ya kutengeneza karatasi za amate imeendelea hadi leo, na vilevile utamaduni wa wenyeji wa kale wa Mexico. Kama wale tlacuilos, au waandishi, wa kale, mafundi wa sasa hustaajabia karatasi hizo ambazo zinaweza kufafanuliwa kuwa mafunjo ya Mexico.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kupondaponda sehemu za mti