Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Bidhaa Zinapungua

Gazeti Time linasema kwamba “bidhaa fulani zinapunguzwa licha ya kuwa tunaishi wakati ambapo watu wengi wanapenda bidhaa kubwakubwa na magari makubwa ya michezo. Watengenezaji wa bidhaa wanapunguza bidhaa zao za pakiti pole kwa pole—kama vile, maziwa ya mtindi, aiskrimu, sabuni za kufua, na nepi—lakini hawapunguzi bei yake.” Mbinu hiyo si mpya, lakini kwa kuwa uchumi unazorota na wateja ni waangalifu sana na hawataki kutumia pesa nyingi, watengenezaji wengi wa bidhaa wanapunguza bidhaa sana ili wapate faida. Wanunuzi wengi hawatambui kwamba uzito wa bidhaa umepungua kwa gramu chache au urefu wake umepungua kwa sentimeta kadhaa, hivyo wanatumia pesa nyingi kwa bidhaa chache. Edgar Dworsky, mwanzilishi wa mtandao wa kutetea wanunuzi, anasema hivi: “Wanunuzi hawajaona umuhimu wa kuchunguza uzito wa bidhaa au kuzihesabu kila wanapozinunua. Hiyo ni hila kwani wanunuzi hawana habari kwamba wanadanganywa.”

Sabuni Huokoa Uhai

Kulingana na Val Curtis, mhadhiri katika Chuo cha London cha Usafi na Tiba ya Kitropiki, maisha ya watu milioni moja yangeokolewa kila mwaka kwa kunawa mikono kwa sabuni kwa sababu watu hawangepata magonjwa ya kuharisha. Kulingana na gazeti The Daily Yomiuri, Curtis aliliambia Kongamano la Tatu la Ulimwengu Kuhusu Maji, huko Kyoto, Japan, kwamba viini vilivyo katika kinyesi cha wanadamu ni “adui mkubwa zaidi wa afya ya umma.” Gazeti hilo linasema kwamba “katika jamii fulani, ni kawaida kwa wanawake kuwaosha watoto wao wanapoenda chooni na baadaye kutayarisha chakula bila kunawa mikono.” Kunawa mikono kwa maji na sabuni kunaweza kuzuia kuenea kwa virusi na bakteria hatari. Kulingana na Curtis, katika nchi zinazoendelea, kunawa mikono kwa sabuni kunagharimu thuluthi moja tu ya pesa ambazo zingetumiwa kusafisha maji ili kuzuia magonjwa ya kuharisha.

Njia ya Alpine

Hivi majuzi, Njia ya Alpine (Via Alpina) yenye vijia vingi vya kutembea ilifunguliwa Ulaya mwaka wa 2002. Gazeti The Independent la London linasema kwamba “Njia ya Alpine yenye urefu wa kilometa 5,000, inayopitia katika sehemu za kale ni njia maridadi zaidi ya mashambani barani Ulaya.” Njia hiyo ambayo inaunganisha nchi nane za eneo la Alpine, inaanzia Trieste katika pwani ya kaskazini-mashariki ya Italia na kumalizikia eneo la pwani la Monte Carlo, Monaco. Njia hiyo imepanda polepole kwenye milima mpaka kufikia urefu wa meta 3,000 huku ikizunguka vilele virefu sana. Kulingana na shirika la utalii la Ufaransa, La Grande Traversée des Alpes, njia hiyo imepita “karibu na mandhari zenye kuvutia zaidi za kimaumbile na kijamii.” Haitarajiwi kwamba watu wengi watamaliza kutembea njia hiyo yote. Gazeti hilo linasema kwamba badala yake, “unaweza kutembea kilometa chache pamoja na familia yako kisha urudi nyumbani. Hata hivyo, Njia ya Alpine inatoa nafasi nzuri kwa wale wanaotaka kufurahia likizo kwa amani na utulivu karibu na nyumbani.” Watembeaji wanaweza kukaa katika mojawapo ya hoteli 300 zilizoko katika njia hiyo.

Viumbe wa Baharini Wanatoweka

Kulingana na wanabiolojia wa bahari Dakt. Ransom Myers wa Chuo Kikuu cha Dalhousie huko Halifax na Dakt. Boris Worm wa Taasisi ya Sayansi ya Bahari huko Kiel, Ujerumani, bahari za ulimwengu zimevuliwa kupita kiasi. Wanasema kwamba viumbe wa baharini wanakaribia kutoweka, mmoja baada ya mwingine, kwa sababu ya utumizi wa teknolojia ya setilaiti na vyombo vya kuchunguza bahari ili kutafuta samaki. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti The Globe and Mail la Toronto, “aina zote za samaki wakubwa wamekamatwa hatua kwa hatua tangu miaka 50 iliyopita hivi kwamba asilimia 90 ya aina zote wametoweka.” Dakt. Myers anaamini kwamba kutoweka kwa samaki hao na wengine wanaoliwa sana, kama vile tuna, chewa, halibati, marlin, na chuchunge, kutaathiri sana hali ya bahari za ulimwengu. Dakt. Worm anaongezea hivi: “Tunaingilia maisha ya viumbe wa dunia na hilo si jambo la hekima hata kidogo.”

Ugonjwa wa Malaria Umelemea Afrika

Gazeti Le Figaro la Ufaransa linasema kwamba malaria huua “watoto 3,000 barani Afrika kila siku.” Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), zaidi ya watu milioni 300 huathiriwa vibaya na malaria barani Afrika kila mwaka na angalau milioni moja kati yao hufa. Katika mwaka wa 2000, Burundi ilipata janga kubwa zaidi la malaria. Katika muda wa miezi saba, nusu ya watu—karibu milioni 3.5—waliambukizwa. Tatizo hilo linasababishwa na vimelea sugu ambao hawauawi na dawa ya kwinini. Mataifa mengi ya Afrika yanaogopa kutumia pesa nyingi, hivyo hayataki kununua dawa za karibuni kama zile zinazotengenezwa kutokana na mmea wa Kichina unaoitwa Artemisia annua. Matokeo yanakuwa kama alivyosema afisa wa shirika la WHO, kwamba “ugonjwa wa malaria umelemea Afrika.”

Kuhifadhi Kilatini

Ingawa Kilatini huonwa kuwa lugha iliyokufa, Vatikani inajaribu kukifufua na kukifanya kiwe lugha ya kisasa. Kwa nini? Kwa sababu ingawa Kiitaliano hutumiwa kwa ukawaida huko Vatikani, Kilatini ndiyo lugha rasmi huko Vatikani na hutumiwa katika barua na maandishi mengine. Kilatini kilipata pigo kubwa miaka ya 1970 wakati ilipoamuliwa kwamba Misa inaweza kuongozwa katika lugha za kienyeji. Ndipo Papa Paul wa 6 akaanzisha Wakfu wa Kilatini ili kuendeleza lugha hiyo. Hatua moja iliyochukuliwa na wakfu huo ni kuchapisha kamusi ya kutafsiri Kilatini hadi Kiitaliano, iliyotolewa katika mabuku mawili ambayo yaliuzwa yote. Sasa kamusi hiyo imeunganishwa na kuwa buku moja, ambalo huuzwa kwa dola 115. Lina maneno 15,000 hivi ya Kilatini ambayo yamefanywa ya kisasa, kama vile “escariorum lavator” (mashine ya kuosha vyombo). Gazeti The New York Times linasema kwamba buku jipya “linatarajiwa baada ya miaka miwili au mitatu.” Maneno mengi ya buku hilo yatakuwa “yale yanayotumiwa katika nyanja ya kompyuta na habari.”

Maelezo Hayaeleweki

Likiripoti kuhusu uchunguzi uliofanywa katika nchi kadhaa, gazeti la sayansi wissenschaft.de lilisema kwamba “wagonjwa husahau asilimia 80 hivi ya mambo ambayo wameambiwa na daktari wanapokuwa hospitalini, na karibu nusu ya mambo wanayokumbuka si sahihi.” Kulingana na Roy Kessels, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Utrecht huko Uholanzi, sababu kuu za kusahau ni uzee, kukata kauli haraka, mfadhaiko, na maelezo ambayo hayaeleweki. Ili kuwasaidia wagonjwa wakumbuke mambo muhimu, madaktari wanashauriwa wazungumze waziwazi, wataje mambo muhimu zaidi kwanza, na watumie picha kama za eksirei.