Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hifadhi ya Nyumba za Mbao

Hifadhi ya Nyumba za Mbao

Hifadhi ya Nyumba za Mbao

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Slovakia

KATIKA nchi fulani, historia na umaridadi wa nyumba za zamani umehifadhiwa. Nyumba za kale zimekusanywa na kuhifadhiwa katika sehemu moja ili kizazi cha sasa kijue maisha na sanaa za mababu zao.

Hebu tutembelee hifadhi moja ya nyumba hizo katikati ya Ulaya, katika eneo la Orava ambalo liko kaskazini mwa Slovakia.

Hifadhi ya Kijiji cha Orava

Hifadhi ya Orava huko Zuberec inaonyesha historia ya eneo hilo waziwazi. Ilianzishwa katika mwaka wa 1967 na ina nyumba zilizokusanywa kutoka vijiji na mashamba 74 ya karibu na pia kutoka mitaa ya mbali. Nyumba hizo zote zilibomolewa, zikabebwa na kuunganishwa vizuri kwenye hifadhi hiyo.

Tunaweza kuona nyumba na mashamba 11 ya watu mashuhuri na wa kawaida wa Orava, kama vile mameya, matajiri, wakulima, vibarua wa mashamba, na mafundi. Kwa kuwa kwa karne nyingi wakazi wa Orava walijishughulisha hasa na kilimo na ufugaji wa ng’ombe na kondoo, kuna vibanda vingi vya kilimo katika hifadhi hiyo. Vibanda hivyo ni kama vile maghala ya nyasi kavu, sakafu ya kupuria, maboma ya ng’ombe, nyumba ya mchungaji, zizi la kondoo, na maghala mengine yaliyojengwa kwa magogo. Pia tunaona mzinga wa nyuki, vifaa vilivyoundwa kwa mikono, mnara wa kengele, kanisa la mbao, na hata makaburi ya mfano!

Tunapotazama ndani, tunatambua kwamba nyumba za kale za Orava zilikuwa na vyumba vinne—chumba cha mbele, chumba cha kuingilia, jikoni, na chumba cha nyuma. Pia huenda zilikuwa na chumba cha chini ya ardhi kilichotandazwa mawe bapa. Nyumba zilijengwa kwa mbao zilizochongwa ambazo kwa kawaida zilipakwa rangi nyeupe kwenye madirisha na milango. Paa zilizoundwa kwa ustadi zilifunikwa kwa mbao au vigae. Ingawa wakati mwingine sebule ilikuwa na sakafu ya udongo, kuta zilipakwa chokaa nyeupe au kufunikwa kwa mbao laini. Watu walitumia kuni kupika na kulikuwa na bomba la moshi jikoni. Moto wa jiko ulipasha joto sebule.

Kufanya Kazi na Kucheza Pamoja

Muundo wa nyumba hizo za mbao huonyesha kwamba kulikuwa na uhusiano wa karibu kati ya vizazi mbalimbali na katika jamii. Watu wa familia na wenyeji wa vijiji mbalimbali walishirikiana. Kwa kweli, watu hawangeweza kuendelea kuishi katika hali ngumu za eneo hilo la milimani bila ushirikiano mzuri. Watu wa familia na majirani walifanya kazi pamoja, kama vile kuwapeleka ng’ombe, kondoo, na bata-bukini malishoni, na wote kijijini waliungana kufyeka mashamba na kupeleka mavuno sokoni. Pia walitunza malisho na barabara za vumbi.

Licha ya kazi ngumu, maisha kijijini yalifurahisha, hasa wakati wa mavuno. Watu walifurahi walipopata maziwa mengi na wakati ng’ombe na kondoo walipozaa. Wakati huo, muziki na nyimbo za kitamaduni ziliimbwa milimani na kuchezwa kwa filimbi, vinanda, au kodiani. Katika majira ya baridi kali, wasichana na wanawake walioolewa waliungana kukusanya manyoya ya bata-bukini ili kutengeneza mito na mablanketi. Wanaume walipiga hadithi wakifanya kazi, na jioni watu wote walikusanyika kucheza dansi. Katika sehemu fulani za eneo hilo, desturi hiyo bado inaendelea hata leo.

Kukumbuka Mambo ya Kale

Mafundi stadi waliojenga nyumba hizo nzuri za kale za mbao walitumia mbinu za ujenzi na michoro iliyopitishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Walitumia vifaa vilivyopatikana katika eneo hilo. Isitoshe, majengo hayo yalijengwa kwa hekima na ni maridadi kwani yanafaana na mandhari. Ni wazi kwamba wajenzi walijitoa mhanga na kutumia bongo zao kufanya kazi yao.

Msanifu wa majengo anayejulikana ulimwenguni pote, Ludwig Mies van der Rohe, alisema hivi: “Kila pigo la shoka lilitimiza jambo muhimu na kila chimbo la patasi lilidhihirisha hisia fulani. . . . Ustadi wa vizazi vizima umehifadhiwa hapa. Ama kweli, vifaa vya pekee vilitumiwa, na majengo haya yanaonyesha hisia na mawazo chungu nzima ya wasanii! Jinsi yanavyochangamsha moyo na kuvutia! Ni kana kwamba yanaeleza hisia za nyimbo za kale!”

Tunapotua na kutazama majengo hayo, tunafikiria pia watu walioishi humo wakiendesha shughuli zao za kila siku. Laiti maisha yetu ya kisasa yenye hekaheka nyingi yangekuwa matulivu hivyo.

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Zuberec

[Picha katika ukurasa wa 15]

(1) Nyumba za mbao; (2) ndani; (3) wakazi wakipiga muziki na kucheza dansi wakiwa wamevalia nguo za kitamaduni