Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Uvamizi Wakomeshwa na Internet

Mtu mmoja anayeitwa Mauricio huko Uruguay alikuwa akiwasiliana na rafiki yake nchini Brazili akitumia mtandao wa Internet unaoonyesha picha ya mtu anayezungumza, wakati rafiki yake alipokatisha mazungumzo ili amfungulie mtu fulani mlango. Muda si muda, Mauricio akawaona wanaume wawili kupitia mtandao, mmoja wao akiwa na bunduki. Mauricio aliwatazama huku akiwa na wasiwasi. Bila kufahamu kwamba wanaonekana, walianza kumwibia rafiki yake. Mauricio alimpigia simu mtu wa ukoo huko São Paulo, naye akawapigia simu polisi. Polisi waliizingira nyumba hiyo. Baada ya kuteka nyumba hiyo kwa saa tatu, wakora hao walijisalimisha kwa polisi bila kumuumiza mtu yeyote.

Tofauti Kati ya Mwanadamu na Nyani

Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi kuhusu DNA ya sokwe, tumbili na nyani wa aina fulani, umeonyesha kwamba chembe zao za urithi zinatofautiana na za wanadamu kuliko wanasayansi walivyofikiri. Gazeti New Scientist la Uingereza linasema kwamba “kuna tofauti kubwa kati ya DNA ya nyani na ya wanadamu na kati ya DNA ya sokwe na tumbili.” Kelly Frazer wa kampuni ya Perlegen Sciences, ya California, Marekani, ambayo ilifanya uchunguzi huo, anasema kwamba “chembe hizo za urithi zilipolinganishwa, ilionekana kwamba zinatofautiana sana.” Gazeti New Scientist lilisema kuna “tofauti kubwa sana kati yetu na nyani.”

Watu wa Ukoo Waliopotea

Familia nyingi duniani kote huwa hazijui mahali watu wao wa ukoo walipo baada ya vita au misukosuko ya kisiasa. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung la Ujerumani, kongamano la hivi majuzi huko Geneva, Uswisi, lenye kichwa, “Waliopotea,” lilizungumzia matatizo ya familia za watu waliopotea. Kulingana na Sophie Martin, msimamizi wa Mradi Kuhusu Watu Waliopotea wa Halmashauri ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, “[familia] hubaki na wasiwasi miaka mingi baada ya vita kumalizika.” Mara nyingi, familia zilizoathiriwa “hushindwa kuishi maisha ya kawaida au kukabiliana na hali hiyo.” Mara nyingi vikundi vilivyohusika katika vita hukataa kushirikiana kuwatafuta watu waliopotea. Si kwamba hawawezi, lakini hawataki. Mtaalamu mmoja alisema kwamba kufunua ukweli kuhusu vifo vya watu waliopotea kwaweza kufunua makosa yaliyofanywa wakati wa vita.

Watoto Walionyonyeshwa Wana Akili Nyingi na Afya Bora

Gazeti The Daily Telegraph la Sydney, Australia, linasema kwamba “watafiti huko Queensland waliwachunguza watoto wapatao 4000 huko Brisbane na kugundua kwamba wale walionyonyeshwa wana akili nyingi zaidi.” Profesa Jake Najman wa Chuo Kikuu cha Queensland alisema: “Kadiri mama anavyomnyonyesha mtoto kwa muda mrefu ndivyo anavyokuwa na akili nyingi. Tofauti kati ya wale wanaonyonyeshwa na wasionyonyeshwa ni kubwa sana, karibu pointi nane. Hiyo huamua ikiwa mtoto atakuwa na akili ya wastani au mwerevu.” Gazeti Sunday Telegraph la Sydney linaripoti kuwa faida nyingine ya kunyonyesha ni kwamba kunapunguza uwezekano wa watoto kunenepa kupita kiasi kwa asilimia 30. Kulingana na mtaalamu wa kunyonyesha Joy Heads, “karibu vitu vyote katika maziwa ya mama hufaidi mtoto. Hakuna ubaya wowote mtoto akiwa mnene kwa sababu ya kunyonya. Lakini mtoto anapokuwa mnene kwa sababu ya kunywa maziwa ya chupa, anaweza kuwa mnene baadaye maishani.”

Kupiga Simu za Mbali Sana

Mtu mmoja anampigia opareta simu huko Philadelphia, Marekani. Ijapokuwa msichana anayeipokea simu hiyo anajiita Michelle, jina lake halisi ni Meghna. Yuko nchini India na ni usiku wa manane huko. Vituo vya kupigia simu nchini India vimewaajiri zaidi ya wafanyakazi 100,000 kutoa huduma kwa ajili ya kampuni za ng’ambo kama vile American Express, AT&T, British Airways, Citibank, na General Electric. Kulingana na gazeti India Today, makampuni hayo yamehamisha huduma zao hadi India kwa sababu ya bei nafuu za kupiga simu mbali na vilevile kuna wafanyakazi wengi wenye elimu wanaojua Kiingereza, “ambao hulipwa mishahara ya chini kwa asilimia 80 ikilinganishwa na wenzao katika nchi za magharibi.” Ili wawe na matamshi kama ya Wamarekani, opareta kama vile Meghna huchukua miezi wakijizoeza na “kutazama sinema za Hollywood.” Kompyuta ya Meghna hata huonyesha hali ya hewa huko Philadelphia, ili kumwezesha kutaja jambo hilo pia. Yeye humalizia kwa kusema, “Uwe na siku njema.”

Mfumo wa Maji Chini ya Bahari

Gazeti Canadian Geographic laripoti kwamba volkano mbili chini ya bahari ambazo zinafanyiza mfumo wa maji ziligunduliwa karibu na Kisiwa cha Vancouver huko Kanada. Kwa muda mrefu wanasayansi wamejua kwamba kuna mfumo wa maji chini ya sakafu ya bahari. Mtaalamu wa maji na miamba katika Chuo Kikuu cha California, huko Santa Cruz, Andrew Fisher, anasema “ugumu uliopo ni kwamba sehemu kubwa ya sakafu ya bahari haina miamba inayoweza kupenyeza maji.” Fisher na wenzake waligundua kwamba maji huingia ndani ya mlima uliomo baharini. Mlima huo umeibuka kutoka kwenye udongo wa sakafu ya bahari ambao haupenyezi maji. Kisha maji hayo hutokea kwenye mlima mwingine wa baharini ulio umbali wa zaidi ya kilometa 50. Fisher anatumaini kwamba uvumbuzi huo utafunua mengi zaidi kuhusu maji na vijiumbe wa baharini.

Masomo Hayajui Uzee

Nchini Nepal, ambako watu wengi hawajui kusoma wala kuandika, mzee mmoja mwenye zaidi ya wajukuu 12, amepata umaarufu kwa jitihada yake ya kupata elimu. Bal Bahadur Karki, anayejulikana kama Mwandishi Baje, alizaliwa katika mwaka wa 1917 na alishiriki katika Vita vya Pili vya Ulimwengu. Akiwa na umri wa miaka 84, alipata Cheti cha Kumaliza Shule baada ya kufanya mtihani mara nne. Sasa ana umri wa miaka 86, na anafanya kozi chuoni. Anasomea Kiingereza na hata kuwafundisha wengine lugha hiyo. Anasema kwamba anahisi akiwa kijana anapoketi darasani pamoja na vijana. Mara ya mwisho alipokuwa katika jiji kuu la Kathmandu, alipokea zawadi nyingi na kushangiliwa sana kwa sababu ya mafanikio yake. Aliwatia moyo wengine wasiache kujifunza kwa sababu tu ni wazee. Hata hivyo, Mwandishi Baje alilalamika kuhusu jambo moja. Alilazimika kutembea kwa siku tatu ili apande basi kwani hakupunguziwa nauli na hangeweza kugharimia nauli ya kawaida ya ndege. Aliliambia hivi gazeti The Kathmandu Post: “Kampuni za ndege zinapaswa kunipunguzia nauli kama wanafunzi wengine kwa sababu mimi pia ni mwanafunzi.”

Watoto Wenye Magonjwa ya Akili

Gazeti ABC la Hispania linaripoti kwamba “asilimia 22 ya watoto na vijana waliobalehe nchini Hispania wana ugonjwa fulani wa akili.” Mtaalamu wa magonjwa ya akili ya watoto, María Jesús Mardomingo, anasema watoto “hasa wana kasoro za tabia, mfadhaiko, mshuko wa moyo, na matatizo ya ulaji.” Wataalamu wameona kwamba hali hiyo imeongezeka sana katika miaka 30 iliyopita, hivyo wamekata kauli kwamba mara nyingi matatizo ya kihisia huletwa na maendeleo ya kiuchumi. Kwa mfano, wanasema kuna mabadiliko makubwa ya kijamii na kitamaduni, hasa kupuuzwa kwa mamlaka ya wazazi. Mardomingo anasema: “Ijapokuwa tunajua kwamba watoto huharibika wazazi wanapowawekea sheria kali na kudai mengi, inafaa kusawazisha upendo na mamlaka.”