Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Kodi Hulipwa ili Kuwe na “Maendeleo”?

Je, Kodi Hulipwa ili Kuwe na “Maendeleo”?

Je, Kodi Hulipwa ili Kuwe na “Maendeleo”?

“Sisi hulipa kodi ili kuwe na maendeleo.”—Maandishi kwenye jengo la Huduma za Malipo ya Kodi, Washington, D.C.

SERIKALI husema kwamba kodi ni muhimu ingawa zinawalemea watu—zinalipwa ili kuwe na “maendeleo.” Iwe unakubaliana na taarifa hiyo au la, ni wazi kwamba kwa kawaida watu hutumia pesa nyingi kulipa kodi.

Kodi zinaweza kugawanywa katika makundi mawili: kodi zinazotozwa moja kwa moja na zisizotozwa moja kwa moja. Kodi ya mapato, kodi ya shirika, na kodi ya rasilimali ni baadhi ya kodi zinazotozwa moja kwa moja. Kati ya hizo, kodi ya mapato ndiyo inayochukiwa zaidi. Ni hivyo hasa katika nchi ambako kodi ya mapato hutozwa kulingana na mapato ya mtu—hivyo ikiwa mapato yako ni ya juu, utalipa kodi ya juu. Watu wanaopinga ulipaji wa kodi fulani wanasema kwamba kodi inapotozwa hivyo, hilo huwaadhibu watu wanaofanya kazi kwa bidii na waliofanikiwa.

Kitabu OECD Observer cha Shirika la Ushirikiano na Maendeleo ya Kiuchumi kinasema kwamba “huenda wafanyakazi wakatozwa kodi ya mapato na serikali za mtaa, za wilaya, au za majimbo kuongezea kodi ya mapato inayotozwa na serikali kuu. Ndivyo ilivyo huko Hispania, Iceland, Japan, Kanada, Korea, Marekani, katika nchi za Skandinavia, Ubelgiji, na Uswisi.”

Kodi zisizotozwa moja kwa moja zinatia ndani kodi ya mauzo, kodi inayotozwa vileo na sigara, na ushuru wa forodhani. Tofauti na kodi zinazotozwa moja kwa moja, watu hawatambui kuwa wanatozwa kodi hizo waziwazi, lakini zinaweza kuwalemea watu, hasa maskini. Katika gazeti Frontline la India, mwandishi Jayali Ghosh anasema kwamba si kweli kuwa matajiri na watu wanaochuma mapato ya kadiri hulipa sehemu kubwa ya kodi nchini India. Ghosh anasema: “Kodi zisizotozwa moja kwa moja ni zaidi ya asilimia 95 ya kodi zote zinazokusanywa na serikali za Majimbo. . . . Huenda watu maskini zaidi ndio hutumia sehemu kubwa ya mapato yao kulipa kodi kuliko matajiri.” Huenda tofauti hiyo husababishwa na kodi za juu zinazotozwa bidhaa zinazonunuliwa na watu wengi kama vile sabuni na chakula.

Serikali hutumiaje pesa zinazokusanywa?

Pesa Hutumiwaje?

Ni kweli kwamba serikali hutumia pesa nyingi kutoa huduma muhimu. Kwa mfano, nchini Ufaransa, mtu 1 kati ya 4 ameajiriwa na serikali. Hiyo inatia ndani walimu, wafanyakazi wa posta, wafanyakazi wa majumba ya makumbusho na hospitali, polisi, na wengineo. Kodi zinahitajiwa ili kuwalipa mishahara. Kodi pia hutumiwa kutengeneza barabara, shule, na hospitali na vilevile kulipia gharama za kukusanya takataka na kutuma barua.

Kodi hutumiwa pia kugharimia matumizi ya kijeshi. Katika mwaka wa 1799, Waingereza matajiri walitozwa kodi ya kwanza ya mapato ili kugharimia vita dhidi ya Wafaransa. Lakini wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, serikali ya Uingereza ilianza kuwatoza wafanyakazi kodi ya mapato. Leo, pesa nyingi hutumiwa kugharimia shughuli za kijeshi hata wakati wa amani. Shirika la Stockholm la Utafiti wa Amani ya Kimataifa lilikadiria kwamba gharama za kijeshi ulimwenguni pote katika mwaka wa 2000, zilikuwa dola bilioni 798 hivi za Marekani.

Kutoza Kodi Ili Kubadili Mazoea ya Watu

Kodi hutozwa pia ili kuwachochea watu waache mazoea mabaya au wafanye mema. Kwa mfano, kodi ya vileo hutozwa ili kupunguza unywaji wa kupita kiasi. Kwa hiyo, katika nchi nyingi, asilimia 35 hivi ya bei ya kileo huwa kodi.

Sigara pia hutozwa kodi za juu sana. Nchini Afrika Kusini, asilimia 45 hadi 50 ya bei ya sigara huwa kodi. Hata hivyo, nyakati nyingine serikali hutoza kodi hizo kwa sababu tofauti mbali na kufaidi jamii. Kama mwandishi Kenneth Warner anavyosema katika gazeti Foreign Policy, sigara “huleta mamia ya mabilioni ya dola kila mwaka kupitia mauzo, na mabilioni zaidi kupitia kodi.”

Mfano mmoja wa jinsi kodi inavyoweza kubadili mazoea ulitukia mapema katika karne ya 20. Wabunge wa Marekani walitaka kupunguza familia za matajiri. Jinsi gani? Kwa kuanzisha kodi ya mali. Tajiri anapokufa, kodi ya juu hutozwa ili kupunguza sana mali alizokusanya. Watetezi wa kodi hiyo wanasema kwamba “inaondoa mali kutoka kwa familia na watu wachache na kuzielekeza kwa umma na serikali.” Labda hilo ni kweli, lakini matajiri wamebuni mbinu nyingi za kuhepa kodi hiyo.

Kodi huendelea kutumiwa kuendeleza mipango ya kijamii, kama vile kuhifadhi mazingira. Gazeti The Environmental Magazine linaripoti: “Hivi majuzi, nchi tisa za Ulaya Magharibi zimeanzisha kodi fulani ili kuhifadhi mazingira, hasa kwa kupunguza vichafuzi vya hewa.” Kodi inayotozwa kwa kutegemea kiasi cha mapato, ambayo ilitajwa mwanzoni, pia ni mfano wa kodi inayokusudiwa kubadili mazoea. Inakusudiwa kupunguza tofauti kati ya matajiri na maskini. Serikali fulani pia huwapunguzia kodi watu wanaotoa misaada au wenzi walio na watoto.

Kwa Nini Sheria za Kodi Zinatatanisha?

Wabunge wanapopendekeza kodi mpya, wao hujaribu kuwazuia watu wasiihepe kwa vyovyote kwani pesa nyingi zinaweza kupotea. Tokeo ni nini? Sheria za kodi huwa tata sana. Makala moja katika gazeti Time ilieleza kwamba matatizo mengi yanayofanya sheria za kodi za Marekani ziwe tata “hutokana na kubainisha mapato,” yaani, kujua kiasi kinachopaswa kutozwa. Magumu mengine yanatokana na kanuni nyingi “zinazowaruhusu watu kupunguziwa na kutolipa kodi fulani.” Hata hivyo, si Marekani tu yenye sheria tata za kodi. Sheria ya kodi iliyotungwa hivi majuzi nchini Uingereza ilichukua kurasa 9,521 zilizojaza mabuku kumi.

Ofisi ya Utafiti wa Sheria za Kodi katika Chuo Kikuu cha Michigan inaripoti hivi: “Kila mwaka walipa-kodi nchini Marekani hutumia zaidi ya saa bilioni tatu wakijaza fomu za malipo ya kodi. . . . Kwa ujumla, wakati na pesa ambazo walipa-kodi wa Marekani hutumia [kujaza fomu za malipo ya kodi] hugharimu dola bilioni 100 kila mwaka, au asilimia 10 hivi ya kodi zinazotozwa. Gharama hizo nyingi husababishwa na utata wa sheria za kodi ya mapato.” Reuben, aliyetajwa mwanzoni mwa makala ya kwanza anasema: “Hapo zamani, nilikuwa ninajaza fomu hizo mwenyewe, lakini ilinichukua wakati mwingi, na nilihisi kwamba ninalipa pesa nyingi kuliko inavyostahili. Kwa hiyo sasa nimemwajiri mhasibu afanye kazi hiyo.”—Ona sanduku “Kutii Sheria za Kodi,” kwenye ukurasa wa 8.

Watu Wanaolipa, Wanaoepuka, na Wanaohepa Kodi

Watu wengi wanaweza kukubali shingo upande kwamba kodi hufaidi jamii. Msimamizi wa Idara ya Kodi ya Uingereza alieleza hivi: “Hakuna mtu anayefurahia kulipa kodi ya mapato, lakini wengi wanakubali kwamba inatufaidi.” Wengine wanakadiria kwamba asilimia 90 ya watu nchini Marekani hulipa kodi. Shirika moja la kodi linakiri hivi: “Idadi kubwa ya watu ambao hawalipi kodi hufanya hivyo kwa sababu hawaelewi sheria na utaratibu, si kwamba wanahepa kimakusudi.”

Hata hivyo, watu wengi hutafuta njia za kuepuka kulipa kodi fulani. Kwa mfano, fikiria yale ambayo makala moja katika gazeti U.S.News & World Report ilisema hivi kuhusu kodi ya shirika: “Mashirika mengi hutumia sheria kuepuka kiasi kikubwa cha kodi—na wakati mwingine kodi yote—kwa kuomba wapunguziwe kodi na kwa kutumia ujanja.” Makala hiyo ilitoa mfano huu kuonyesha mbinu ya ujanja: “Shirika moja la Marekani linaweza kuanzisha ofisi katika nchi ya kigeni isiyotoza kodi nyingi. Halafu, linaweza kufanya shirika lililoko Marekani liwe tawi la ofisi hiyo.” Kwa hiyo shirika hilo huepuka kulipa kodi za Marekani, ambazo zinaweza kufikia asilimia 35, hata ingawa “huenda makao hayo makuu ni ofisi tu yenye kabati ya faili na sanduku la posta.”

Kisha kuna kuhepa kodi kabisa-kabisa. Inaripotiwa kwamba katika nchi moja ya Ulaya watu hupenda kuhepa kodi. Kulingana na uchunguzi uliofanywa nchini Marekani, asilimia 58 tu ya wanaume walio kati ya umri wa miaka 25 na 29 ndio wanaoamini kwamba haifai kudanganya kuhusu mapato yao. Waandishi wa ripoti hiyo wanakiri hivi: “Ripoti hiyo inaonyesha kwamba tabia na maadili ya jamii yetu yamezorota.” Nchini Mexico, inakadiriwa kwamba asilimia 35 hivi ya watu huhepa kodi.

Hata hivyo, kwa ujumla, watu hutambua umuhimu wa kulipa kodi, na hawaoni ubaya kuzilipa. Lakini, maneno haya yanayojulikana sana, ambayo huenda yalisemwa na Kaisari Tiberio, ni ya kweli: “Mchungaji mwema huwanyoa kondoo lakini hawachuni ngozi.” Iwapo unaona kwamba unakandamizwa na mfumo wa kodi unaolemea, usio wa haki, na unaotatanisha sana, unapaswa kuwa na maoni gani kuhusu kulipa kodi?

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

Fikiri Kabla ya Kuhama!

Mifumo ya kodi hutofautiana katika nchi mbalimbali. Hata kodi za mapato zinaweza kutofautiana sana katika nchi ileile. Je, inafaa kuhamia eneo linalotoza kodi nafuu? Labda, lakini unapaswa kufikiri kabla ya kuhama.

Kwa mfano, makala moja katika gazeti OECD Observer inawakumbusha wasomaji kwamba hawapaswi kuangalia tu kiwango cha kodi ya mapato. Inasema hivi: “Kodi halisi huathiriwa na viwango mbalimbali vya kupunguza kodi.” Kwa mfano, nchi fulani hazitozi kodi kubwa ya mapato. Lakini “hazipunguzi kodi sana na haziwaruhusu watu wasilipe kodi fulani.” Kwa hiyo, mtu anaweza kulipa kodi zaidi huko kuliko katika nchi ambazo zinatoza kodi ya juu na ambazo zinawaruhusu watu wapunguziwe au wasilipe kodi fulani.

Nchini Marekani, watu fulani hufikiria kuhamia majimbo ambayo hayatozi kodi ya mapato. Lakini je, kufanya hivyo huokoa pesa? Sivyo kulingana na kitabu Kiplinger’s Personal Finance, kinachosema: “Katika visa fulani, uchunguzi wetu unaonyesha kwamba majimbo ambayo hayatozi kodi ya mapato hupata pesa kwa kutoza kodi za juu za mali, za mauzo, na kodi nyingine.”

[Sanduku katika ukurasa wa 8]

Kutii Sheria za Kodi

Kwa wengi wetu, kulipa kodi ni mzigo mzito na wenye kulemea. Kwa hiyo Amkeni! lilimwomba mtaalamu wa kodi atoe madokezo kadhaa.

“Omba mashauri yenye kutegemeka. Hilo ni muhimu kwa sababu sheria za kodi zinaweza kuwa tata, na mara nyingi kutojua sheria si udhuru wa kutolipa kodi. Ingawa huenda mlipa-kodi akawaona maafisa wa kodi kuwa maadui, wanaweza kumpa maelezo sahihi na sahili ambayo yanaweza kumsaidia kushughulikia masuala ya kodi. Mashirika ya kodi hutaka ujaze fomu za kulipa kodi kwa usahihi unapoanza kulipa kodi. Hawakusudii kukushtaki kwa kutolipa.

“Ikiwa unapata ugumu kufanya hesabu ya kodi yako, omba mashauri kutoka kwa mtaalamu wa kodi. Lakini jihadhari! Ingawa wataalamu wengi wa kodi ni wazuri, kuna wengi wanaotumia hila. Omba mashauri kutoka kwa rafiki au mfanyabishara anayeaminika ili akusaidie kujua sifa za mtaalamu huyo.

“Tenda haraka. Watu wanaochelewa kulipa kodi huadhibiwa vikali.

“Weka rekodi nadhifu. Hata iwe unatumia njia gani kuweka rekodi, hakikisha zina habari za karibuni zaidi. Hivyo, hutatumia wakati mwingi kufanya hesabu za kodi wakati wa kulipa unapofika. Pia hutatatanika iwapo rekodi zako zitakaguliwa.

“Uwe mnyofu. Huenda ukashawishiwa kudanganya au kuvunja sheria kidogo. Lakini maafisa wa kodi wana mbinu nyingi za kugundua udanganyifu. Kwa hiyo ni vizuri kuwa mnyofu nyakati zote.

“Jihusishe. Mtaalamu wa kodi akiwasilisha rekodi zisizo sahihi, wewe ndiwe unayewajibika. Kwa hiyo, hakikisha mtaalamu uliyeajiri anafuata matakwa yako.”

[Picha katika ukurasa wa 7]

Katika nchi nyingi bidhaa za tumbaku na vileo hutozwa kodi za juu

[Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Kodi hulipia huduma nyingi ambazo nyakati nyingine hatuzitilii maanani