Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Chakula Kutoka Shamba Lako

Chakula Kutoka Shamba Lako

Chakula Kutoka Shamba Lako

NA MWANDISHI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

KATIKA nchi nyingi, kila siku watu huhangaikia jinsi watakavyolisha familia zao. Mara nyingi jambo hilo huwa gumu kwa sababu mboga huwa bei ghali. Hata hivyo, wengine wamesuluhisha jambo hilo kwa urahisi kwa kuzalisha chakula chao wenyewe!

Labda hata wewe unataka kuwa na shamba dogo. Huenda kusiwe na shamba karibu na mahali unapoishi, lakini unaweza kutafuta shamba lisilo mbali sana. Unaweza kuokoa pesa kwa kuzalisha chakula kitamu chenye afya! Kulima kunaweza kuwa njia bora ya kufanya mazoezi. Ni jambo unaloweza kufanya pamoja na familia na hata watoto watafurahia. Pia shamba litakupa nafasi ya kujifunza mambo mengi. Utajifunza sifa kama vile subira. (Yakobo 5:7) Isitoshe, unaweza kuboresha uhusiano wako na Muumba wa vitu vyote vyema unapoona mimea ikikua.—Zaburi 104:14.

Usidhani kwamba ni kazi rahisi kuzalisha chakula chako mwenyewe au kwamba utapata matokeo haraka. Hata hivyo, ukiwa na bidii na ujuzi kiasi fulani, unaweza kufanikiwa!

Familia Yafanikiwa

Wafikirie Timothée na Lucie, wenzi Wakristo wenye watoto wawili, wanaoishi Bangui, jiji kuu la Jamhuri ya Afrika ya Kati. Waligundua kwamba kuwa na shamba ni njia bora na yenye kufurahisha ya kuongeza mapato yao.

Lucie, alipokuwa na umri wa miaka 13, alilima shamba lililokuwa karibu na nyumba yao alipotoka shuleni na mwishoni mwa juma. Alifurahi kuona mimea ikikua. Hata hivyo, hakufikiria kuzalisha chakula kwa ajili ya familia hadi miaka mingi baadaye. Aliamua kulima shamba lililokuwa karibu ambapo watu walitupa takataka. Lucie aliona lingetokeza mazao bora. Ingawa lilikuwa limeachwa kwa miaka mingi, takataka ziliozea hapo na kufanya udongo uwe na rutuba. Lucie na Timothée waliamua kulima shamba hilo.

Jinsi Walivyoanza

Kwanza walihitaji kufanya utafiti. Waliomba mashauri kutoka kwa wengine wanaojua kukuza mboga na kuwasikiliza kwa makini. Kwa kuwa shamba hilo lilihitaji maji, hata walijifunza kuchimba kisima. Pia walisoma vitabu.

Walijifunza pia kuhusu mimea inayopaswa kukuzwa pamoja, na kwamba mimea fulani husaidia au kuzuia ukuzi wa mimea mingine. Watu wengine husema kwamba karoti na nyanya hufanya vizuri zinapopandwa pamoja. Vivyo hivyo, figili na koliflawa hunawiri vizuri pamoja. Mmea wa dili hunawiri unapopandwa na njegere, matango, saladi, na vitunguu. Lakini saladi za kijani na kitimiri hazinawiri vizuri zinapopandwa pamoja. Vitunguu hudhuru maharagwe machanga na njegere. Mimea isiyopatana hudhoofika na kuvamiwa kwa urahisi na wadudu inapopandwa pamoja.

Timothée na Lucie walijifunza pia kwamba haifai kukuza mmea wa aina moja, kwa kuwa ukishambuliwa na wadudu au ugonjwa, wanaweza kupoteza zao lote. Kukuza mimea inayofaana kuliwasaidia wasipoteze zao lao. Mimea na maua hurembesha shamba na kuvutia nyuki na wadudu wengine wanaofaidi shamba.

Wenzi hao pia waligundua njia za kuzuia wadudu bila kuwapulizia dawa zenye sumu. Waligundua kwamba kupanda vitunguu saumu kunaweza kuua wadudu fulani. *

Timothée na Lucie walikuwa na subira na walifanya kazi kwa bidii na sasa wana shamba linalonawiri. Wanakuza kabeji, kitimiri, nyanya, karoti, matango, na biringanya. Wakati mwingine wao huvuna zaidi ya chakula wanachohitaji!

Lima Shamba Lako!

Hata hivyo, si Afrika tu ambapo watu wamegundua umuhimu wa kulima mashamba madogo. Kwa mfano, nchini Ujerumani, kuna zaidi ya maeneo milioni moja yenye mashamba madogo-madogo mijini. Wakati mwingine yanaitwa Schrebergaerten (kwa heshima ya daktari Mjerumani Daniel Schreber), na yamegawanywa katika mashamba (yenye ukubwa wa meta 200 mpaka meta 400 za mraba). Mashamba hayo hukodiwa na wakazi wa mijini. Kulingana na mtafiti mmoja, mashamba hayo “yanachangia sana utoaji wa matunda na mboga.” Pia wenye mashamba huyaona kuwa “paradiso” ambapo wanaweza kufanya kazi na kustarehe.

Biblia inaahidi kwamba hivi karibuni, dunia nzima itakuwa bustani, yaani paradiso halisi. (Luka 23:43) Lakini kwa sasa huenda ukapata shamba dogo na ufurahie kuzalisha chakula chako mwenyewe.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Kwa madokezo zaidi kuhusu kuua wadudu bila dawa, ona makala “Kilimo cha Kutumia Mbolea ya Kimaumbile,” katika toleo la Amkeni! la Machi 22, 2002.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Timothée na Lucie wakichota maji kwa ajili ya shamba lao

[Picha katika ukurasa wa 24]

Shamba dogo huko Munich, Ujerumani