Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Prague Jiji Lenye Historia ya Kuvutia

Prague Jiji Lenye Historia ya Kuvutia

Prague Jiji Lenye Historia ya Kuvutia

NA MWANDISHI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA CHEKI

JE, UNGEPENDA kutembelea jiji lililodumu kwa zaidi ya miaka elfu moja, lenye majengo ya Kiroma ya karne ya 10, majengo ya Kigothi, majengo ya kipindi cha Mwamko wa Sanaa, majengo ya karne ya 17, 18, majengo ya Wagiriki na Waroma ya karne ya 19, na yenye mtindo maridadi wa sanaa ya karne ya 20? Basi jiunge nasi tunapotembelea Prague, jiji lenye kuvutia la Ulaya ya Kati. Kicheki si rahisi, lakini ukibeba kitabu cha matamshi kitakusaidia sana. Lakini kwanza, jiji la Prague liko wapi?

Tazama ramani ya Ulaya. Tafuta Berlin, jiji kuu la Ujerumani, upande wa mashariki. Teremka kusini umbali wa kilometa 300 hivi bila kupinda, na jiji kubwa la kwanza utakaloona katika Jamhuri ya Cheki ni jiji kuu la Prague. Ukiteremka kusini zaidi kisha mashariki utaona Vienna, Austria, kisha Budapest, Hungaria. Unaweza kufika katika majiji hayo yote ukisafiri saa kadhaa kwa gari.

Mto Vltava hupita katikati ya Prague. Tutagawanya Prague katika maeneo matano kwa madhumuni ya safari yetu. (Ona ramani kwenye ukurasa wa 23.) Eneo la kwanza liko juu ya kilima, kwenye ukingo wa magharibi. Hapo utaona Kasri la Prague na Hradc̆any, mji uliojengwa karibu na kasri hilo yapata mwaka wa 1320. Ndani ya eneo la kasri mna Kanisa Kubwa la Kigothi la St. Vitus, ambalo lilianza kujengwa mnamo mwaka wa 1344 lakini lilikamilishwa mwaka wa 1929. Vito vya kifalme na kaburi la Mwana-Mfalme Wenceslas vinapatikana humo. Ili ufike kwenye eneo hilo la kasri, unaweza kutembea au kutumia usafiri wa umma. Pana mwinuko mkali, kwa hiyo usisahau kuvaa viatu vyepesi vya matembezi! Unapokuwa katika eneo la kasri, usikose kutazama vijumba vidogo na maduka ya vito kwenye Barabara ya Dhahabu (Zlatá Ulic̆ka katika Kicheki). Majengo hayo yalijengwa mwishoni mwa miaka ya 1500 kwa ajili ya walinzi wa mfalme. Baadaye katika karne ya 17, wafua-dhahabu waliishi humo. Ndiyo maana barabara hiyo inaitwa Barabara ya Dhahabu.

Mtaa Mdogo, Malá Strana, uko kusini mwa eneo la kasri. Kitabu kimoja cha mwongozo kinasema: “Mtaa huo una kasri nyingi maridadi za karne ya 17 na nyumba za kale zenye ishara za kuvutia.” Prague huitwa Jiji la Minara Mia Moja ya Pia ingawa kuna minara mingi zaidi, na hilo linatukumbusha wakati ambapo Wacheki wengi walipenda dini. Katika Mtaa Mdogo, tunaona baadhi ya makanisa hayo, ambayo sasa yana watu wachache baada ya Ukomunisti kuisha. Mojawapo ya makanisa maarufu zaidi ni Kanisa la St. Nicholas. Lilianza kujengwa mwaka wa 1703 na kukamilika mwaka wa 1761. Lilichorwa na baba na mwanaye lakini ujenzi ulichukua muda mrefu sana hivi kwamba wote walikufa kabla halijakamilika.

Kuvuka Mto Vltava

Kuna angalau madaraja saba yanayovuka Mto Vltava upande wa mashariki wa Prague. Daraja linalojulikana zaidi ni Daraja la Charles (Karlu̇v Most), linalotumiwa na watembeaji. Huwezi kuthamini Prague iwapo hujawahi kutembea kwenye daraja hilo lenye urefu wa meta 520. Jaribu kutembea kwenye daraja hilo mapema asubuhi na jioni. Utafurahi kuona daraja hilo na mazingira yake kukiwa na nuru nyingi au kidogo.

Daraja hilo linaunganisha Mtaa Mdogo kwenye ukingo wa kushoto na Mji wa Kale ulio mashariki, kwenye ukingo wa kulia. Kwa kawaida Daraja la Charles, huwa limejaa watalii, wanasarakasi, na wachuuzi, wote wakiwa wamesisimuka. Huenda ukasikia kikundi cha jazi cha Kicheki kikicheza kwa ustadi muziki unaopendwa wa New Orleans. Hata wanauza CD na kaseti za muziki mtamu. Katika sehemu nyingine huenda ukawaona wanafunzi wakijaribu kuchuma pesa kwa kuuza sanamu ndogo maridadi za kauri za majengo maarufu zaidi katika Mji wa Kale. Unaweza kujenga mfano wa mji wa kale nyumbani mwako, kutia ndani saa ya falaki!

Lakini sasa tazama sanamu nyingi za “watakatifu” Wakatoliki zilizo kila upande wa daraja. Sanamu hizo zinawakilisha matukio mengi ya historia ya dini huko Cheki. Zilianza kutengenezwa wakati wa John Nepomuk (1683) hadi wakati wa Cyril na Methodius (1938). Hata hivyo, sanamu inayowavutia wanafunzi wengi wa Biblia ni ile ya Kristo, iliyotengenezwa mwaka wa 1629. Kwa nini ni ya pekee?

Kando yake kuna maandishi ya Kiebrania ya dhahabu kutia ndani Tetragramatoni, zile herufi nne zinazowakilisha jina la Mungu, Yehova, ambalo linapatikana karibu mara 7,000 katika Maandiko ya Kiebrania.

Mji wa Kale Utakushangaza Sana

Unapovuka Daraja la Charles na kupita chini ya Mnara wa Daraja la Mji wa Kale (tafuta sanamu ya ndege wa mdiria upande wa mashariki, ambayo ni alama iliyopendwa na Wenceslas), utakuwa umeingia katika Mji wa Kale, ambako utapiga picha mpaka uchoke! Utafurahia majengo mengi maridadi. Ukisonga mbele bila kupinda unapotoka kwenye daraja, utajikuta kwenye Barabara ya Charles (Karlova), ambayo inaungana na vijia vingi vyembamba vinavyopindapinda vyenye maduka mengi madogo na wateja wengi. Lakini chunguza majengo mbalimbali ya kipindi cha Mwamko wa Sanaa na ya karne ya 17.

Unapotembea huku na huku na kustaajabia mandhari, utafika kwa ghafula kwenye Eneo la Kati la Mji wa Kale, na utaona kwanza umati ukikodolea macho saa fulani, hasa inapokaribia kugonga. Hiyo ndiyo Saa ya Baraza la Mji, saa ya falaki yenye kuvutia. Lakini usitarajie ionyeshe mizunguko ya sayari kwa usahihi. Ilitengenezwa wakati watu walipoamini kwamba dunia ilikuwa katikati ya ulimwengu na kwamba jua na nyota ziliizunguka. Hata hivyo, saa hiyo imeundwa kwa njia maridadi na kwa uhandisi wa hali ya juu. *—Ona sanduku kwenye ukurasa unaofuata.

Sasa tunaelekea kwenye Eneo la Kati la Mji wa Kale, ambalo linavutia kwa sababu ya majengo maridadi ya aina mbalimbali. Eneo hilo ni kubwa sana hivi kwamba umati mkubwa wa watu unaonekana mdogo sana. Kuna mengi ya kuona. Usiwe na haraka, na usome kitabu chako cha mwongozo ili ujue kile unachoona. Lile kanisa kubwa unaloona kwa mbali lenye minara pacha na minara mingi ya pia linaitwa Kanisa la Týn na lilijengwa mwaka wa 1365. Hatuwezi kuandika kuhusu majengo yote maridadi tunayoona katika eneo hili kubwa, kama vile Kasri la Golz-Kinský la karne ya 18.

Katikati ya eneo hilo, kuna sanamu kubwa ya ukumbusho ya John Hus (1372-1415), Mcheki aliyekuwa Mwanageuzi wa kidini. Ingawa alikuwa kasisi Mkatoliki, aliwakasirisha viongozi wa kanisa kwa sababu alifichua kwa ujasiri maadili mapotovu ya makasisi na kushutumu matumizi ya pesa za msamaha. Ijapokuwa aliahidiwa ulinzi ikiwa angehudhuria Mkutano wa Constance ili kueleza maoni yake, Hus alihukumiwa kifo kwa kuwa mwasi na akateketezwa mtini.

Historia ya Wayahudi Huko Prague

Eneo la nne, ambalo hupaswi kukosa ni Mtaa wa Wayahudi. Uliitwa Josefov katika Kicheki baada ya Joseph wa Pili wakati ubaguzi dhidi ya Wayahudi ulipopungua mwaka wa 1784. Mojawapo ya majengo maarufu katika mtaa huo ni Sinagogi la Old-New. Lilijengwa wapata mwaka wa 1270 na ndilo sinagogi la zamani zaidi Ulaya ambalo linatumiwa hata leo. Pia ni mojawapo ya majengo ya zamani zaidi ya Kigothi huko Prague. Unaweza kuingia kwenye sinagogi hilo, na ukitazama kwa uangalifu utaona jina la Mungu katika Kiebrania, lakini usithubutu kupiga picha. Usipotii onyo la kutopiga picha, utatupwa nje na mlinzi.

Katika eneo hilo pia unaweza kuona eneo la kale la makaburi ukitazama kupitia malangoni. Lina maelfu ya makaburi yenye maandishi ya Kiebrania. Karibu na hapo kuna jengo la Baraza la Mji la Kiyahudi lenye saa mbili—moja yenye namba za Kiroma na nyingine ya herufi za Kiebrania.

Sinagogi la Pinkas lililo karibu “sasa linatumiwa kama kumbukumbu la Wayahudi 77,297 kutoka Bohemia na Moravia waliouawa kwenye vyumba vya Wanazi vya gesi ya sumu.” Majina yao, pamoja na ya wale Wayahudi 36,000 kutoka Prague yameandikwa kwenye kuta zake za ndani.—Prague Art and History.

“Mji Mpya” wa Kale

Eneo la mwisho tutakalotembelea ni Mji Mpya (Nové Mĕsto). Ingawa unaitwa mpya, ulijengwa na Charles wa Nne kama soko la farasi mwaka wa 1348. Sehemu maarufu zaidi ya mji huo ni Eneo la Wenceslas, linalosemwa kuwa “kituo cha kibiashara katika Prague ya kisasa.” Kuna majengo yenye mitindo ya kisasa ya kisanaa, kama vile Hotel Evropa yenye kuvutia, lakini kitu chenye kupendeza zaidi ni sanamu iliyotengenezwa mwaka wa 1912 inayoonyesha Wenceslas akiwa amepanda farasi.

Safari yetu ya Prague haiwezi kukamilika kabla ya kutembelea sehemu za utamaduni, hasa mahali muziki unapochezwa. Kwa hiyo usikose kutembelea Ukumbi wa Kitaifa wa Michezo ya Kuigiza na Jumba la Kitaifa la Muziki. Mamilioni ya wapenzi wa muziki wamesikiliza “Muziki wa Ala wa New World,” uliochezwa na Antonin Dvorak. Utaona Jumba la Makumbusho la Dvorak katika jengo kubwa jekundu la karne ya 17. Franz Liszt alisema kwamba Bedr̆ich Smetana anayeonwa kuwa “mwanzilishi wa muziki wa Wacheki” ni “mtungaji ambaye ni Mcheki damu.” Anajulikana hasa kwa sababu ya mashairi yenye upatano yanayoitwa “Má Vlast” (Nchi Yangu) na utenzi wa kimuziki unaoitwa Vltava ambao unaeleza kuhusu mto unaopita katikati ya Prague. Jumba la Makumbusho la Smetana liko kwenye kingo za mto katika Mji wa Kale.

Kuna mengi sana ya kuona na kufurahia jijini Prague! Karibu ujionee mwenyewe. Njoo ufurahie historia na utamaduni uliodumu kwa miaka elfu moja!

[Maelezo ya Chini]

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Saa ya Falaki

Saa hiyo ina sehemu tatu. Saa inapogonga, madirisha mawili yaliyo upande wa juu hufunguka na kumruhusu mtu aone mifano ya mitume 12 wakifuatana. Mahali pa Yuda Iskariote na Yakobo mwana wa Alfayo pamechukuliwa na Paulo na Barnaba ambao si kati ya wale mitume 12 wanaotajwa katika Biblia. Chini tu ya mitume kuna gofu la mtu, ambalo linawakilisha Kifo. Gofu linapita kwanza kisha linafuatwa na mitume. Gofu linainua na kuinamisha shisha kwa mkono wa kushoto. Mifano mingine inayofuata inatia ndani jogoo anayewika, Mturuki akitikisa kichwa, Ubatili akijitazama kwenye kioo, na Mchoyo ambaye ni mkopeshaji mwenye pupa.

Saa hiyo ya falaki inaonyesha pia aina tatu za wakati—wakati wa Wabohemia katika namba za Kiarabu, wakati wa kawaida katika namba za Kiroma, na wakati wa mchana wenye saa 12 kulingana na mfumo wa Kibabiloni. Sasa unaona umuhimu wa kuichunguza kwa makini saa hiyo maridadi!

[Ramani katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

ENEO LA KATI LA PRAGUE

Kasri la Prague na Hradc̆any

Mtaa Mdogo

Mto Vltava

Mtaa wa Wayahudi

Mji wa Kale

Mji Mpya

[Picha katika ukurasa wa 22]

Maandishi haya ya Kiebrania yanatia ndani Tetragramatoni

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kasri ya kisasa yenye miundo ya karne ya 17

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Daraja la Charles

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mnara wa saa wa Baraza la Mji wa Kale na Kanisa la St. Nicholas

[Picha katika ukurasa wa 25]

Ndani ya Kanisa Kubwa la St. Vitus

[Picha katika ukurasa wa 25]

Eneo la Wenceslas