Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mambo Tuliyojifunza Kutoka kwa Mbilikimo

Mambo Tuliyojifunza Kutoka kwa Mbilikimo

Mambo Tuliyojifunza Kutoka kwa Mbilikimo

NA MWANDISHI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

“Vueni viatu vyenu. Tutatembea ndani ya maji na kupitia kijia cha tembo. Fuateni maagizo yangu kwa makini. Tukikutana na sokwe, inameni chini na msimtazame uso kwa uso. Tukikutana na tembo, simameni tuli.”

TUNAPUMZIKA barazani kwenye mkahawa mmoja, na kutafakari mambo yote ambayo tumeona. Mto Sangha unatiririka mbele yetu; na kwenye upande ule mwingine, twaona msitu mkubwa wenye kuvutia. Tuko Bayanga, kwenye ncha ya kusini ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, katikati ya Kamerun na Jamhuri ya Kongo.—Ona ramani katika ukurasa wa 19.

Baada tu ya kuwasili katika sehemu ya mapokezi ya Mbuga ya Kitaifa ya Dzanga-Ndoki, hatukukumbuka tena safari yetu yenye kuchosha. Mbuga hiyo iko umbali wa kilometa 480 kutoka Bangui, jiji kuu la Jamhuri ya Afrika ya Kati, na tulisafiri kwa muda wa karibu saa 11 kupitia kijia chembamba ili kufika huko. Katika sehemu fulani tuliona mianzi kando ya barabara. Huko Ngoto, ilitubidi tutumie feri kuvuka mto. Ilikuwa feri ya kipekee kwani haikuendeshwa na injini bali ilisukumwa na mkondo. Feri hiyo hushikiliwa na kapi inayopitia kwenye kebo kubwa, na vijana kadhaa waliiongoza ipitie njia ifaayo.

Mbele zaidi kwenye Mto Bambio, kuna daraja linaloning’inia ambalo linafaa sana kwani linaweza kushushwa au kuinuliwa ikitegemea kiwango cha maji mtoni wakati wa kiangazi na wakati wa mvua. Eneo hilo linapendeza sana, na twaona wanyama katika makao yao ya asili na twawaona Mbilikimo wa Aka, * ambao bado wanafuata utamaduni wao.

Je, ungependa kujiunga nasi katika safari hii yenye kupendeza? Tunatembezwa na Mbilikimo anayeitwa Benoît. Kwanza tunaenda kwenye kijiji chao kukutana na Germaine na Valérie, Mbilikimo wawili ambao ni madaktari wa mitishamba. Na tunastaajabu sana wanapotuonyesha mimea mbalimbali msituni ambayo inatumiwa katika matibabu.

Mimea Inayoponya

Baada ya kuendesha gari kwa dakika kadhaa msituni, Mbilikimo hao wanatuomba tutoke ndani ya gari na kuwafuata msituni. Wanatengeneza kijia kwa mapanga yao, nasi tunawafuata kwa karibu. Tunashangazwa na mmea unaotambaa unaoitwa mo nzambu nzambu. Mbilikimo hao wanakata vipande vya sentimeta 50 vya mimea hiyo, halafu tunakunywa maji yake. Ni safi, yanaburudisha, na yanazima kiu.

Tunaposonga mbele zaidi, tunaonyeshwa jani la mpera. Mbilikimo huchemsha majani hayo na kutengeneza chai inayotibu kikohozi. Mti mwingine unaoitwa ofuruma, hutoa utomvu mweupe ambao ni dawa bora ya kutibu uvimbe wa mboni ya jicho. “Je, kuna dawa ya sumu ya nyoka?” twauliza. “Bila shaka ipo. Sisi huponda majani ya bolo, [jina la Kiaka la mmea wa Kitropiki unaotambaa] na kuyatia kwenye jeraha,” wanajibu mbilikimo. Baada ya kila hatua, tunaonyeshwa mimea ambayo inatumiwa katika matibabu. Mimea hiyo hutumiwa kuponya vidonda, minyoo ya tumboni, maambukizo ya sikio, matundu ya meno, na utasa.

Tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa watu hawa ambao nyakati nyingine huonwa kuwa wajinga. Tunapoendelea kutembea msituni, madaktari hao wawili wa mitishamba wanakusanya chakula chao—uyoga, maboga ya mwituni, na mizizi inayotumiwa badala ya vitunguu-saumu. Haikosi baadhi ya majani ni matamu sana kwa sababu wanayala papo hapo! Itafurahisha sana kuendelea kujifunza mengi katika ulimwengu mpya ambao Mungu ameahidi!—Isaya 65:17; 2 Petro 3:13; Ufunuo 21:1-4.

Wote Wanakusanyika Kwenye Mwamba wa Chumvi

Alasiri twaenda kuwaona tembo kwenye mwamba wa chumvi. Tunapoelekea huko ndipo Mbilikimo anayetutembeza anapotupatia maagizo yaliyo kwenye utangulizi wa makala hii. Lakini mwamba wa chumvi ni nini? Ni eneo kubwa lililojaa madini ya chumvi yanayopendwa na wanyama fulani. Kwa hiyo, kila siku tembo, nyati, paa, nguruwe-mwitu wakubwa, na wanyama wengine wa mwitu hukusanyika hapo.

Jukwaa limejengwa mbugani karibu na mwamba wa chumvi kwa sababu msitu ni mkubwa sana na hivyo wanyama hawaonekani kwa urahisi. Hata hivyo, ili kufika kwenye jukwaa hilo, inatubidi tupitie eneo lenye maji yanayotufika kwenye mapaja. Mbilikimo anayetutembeza anasikiliza kwa makini kelele mbalimbali na anahakikisha kwamba tuko karibu naye nyakati zote. Kwa nini? Kwa sababu tembo hutumia kijia hiki wakati mwingine!

Tunapopanda jukwaani, tunawatazama wanyama kwa muda—zaidi ya tembo 80, nyati na paa kadhaa. Mwanasayansi mmoja aliyechunguza tembo hao kwa muda wa miaka 11 yupo hapa pia. Anatuambia hivi: “Kila tembo ni tofauti. Nimeorodhesha tembo 3,000, na ninajua majina ya tembo 700 kati yao.” Kwa kusikitisha, pembe za tembo hao zinapendwa sana kwa sababu hutumiwa kutengeneza mihuri inayotumiwa katika nchi fulani za Mashariki kuwatambulisha waandishi na wachoraji. *

Kuwinda kwa Kutumia Nyavu

Mapema asubuhi inayofuata, tunaandamana na kundi la wawindaji kumi ili tujionee jinsi ya kuwinda kwa kutumia nyavu. Wanaume na wanawake huja na nyavu zao zilizotengenezwa kwa mimea inayotambaa. Kila wavu una urefu wa meta 20 na upana wa sentimeta 120. Kadiri tunavyopenya ndani zaidi msituni, wawindaji hao wanatawanyika na kuvuta nyavu hizo walizounganisha, ili zifike umbali wa meta 200 hivi. Wanazingira nyavu hizo huku wakisonga mbele na nyuma, kisha wanatikisa matawi na kupaaza sauti ili wanyama waingie nyavuni. Wakati huu hakuna mnyama anayenaswa. Wawindaji wanafungua nyavu hizo na kupenya ndani zaidi msituni, na kurudia utaratibu huo. Wanaweza kufanya hivyo mara moja, mara mbili, hata mara kumi.

Tumechoka adhuhuri inapofika. Mbilikimo wameona ndimba watatu na paa mdogo, lakini walitoroka. Kusudi letu si kumwona mnyama akinaswa kwenye nyavu. Badala yake, tunataka kujua jinsi watu hao wanavyoishi kwa vifaa vichache visivyo vya kisasa. Kwa hiyo, hatukati tamaa hata kidogo kwa sababu tumeona mambo ya kustaajabisha.

Kuabiri Katika Mto Sangha kwa Mtumbwi

Ni nani asingependa kuabiri taratibu juu ya maji? Ukitumia mtumbwi, utafurahia hata zaidi kwa kuwa unayaona maji kwa karibu. Tunapoabiri kwa mtumbwi wakati wa jioni twaona korongo-visiwa na ndege wengine wengi wenye rangi mbalimbali zenye kuvutia sana. Baadhi ya ndege hao huruka kutoka tawi moja hadi jingine kwenye ukingo wa mto kana kwamba wanatufuata.

Kwingineko, twaona masokwe-mtu wakiruka kutoka mti mmoja hadi mwingine wakijifurahisha, au labda wakitaka kutufurahisha! Alain Patrick, mwendeshaji wa mtumbwi huo, anafanya juu chini kutupeleka mbali zaidi kwa kuwa jana aliona viboko hapo. Je, leo tutawaona? Hapana, wameondoka. Lakini twaona vijiji kadhaa kando ya mto na vilevile watoto wengi wanaoendesha mitumbwi yao midogo kwa ustadi mkubwa ajabu. Pasina shaka hatutasahau jinsi tulivyoabiri Mto Sangha kwa mtumbwi.

Mambo ya Kukumbuka Tunaporudi Nyumbani

Tunaporudi Bangui, tunakumbuka vitu vingi tulivyoona. Tumeshangazwa na kuduwazwa na mengi. Hasa hatutasahau jinsi Mbilikimo wanavyotumia hekima kuishi msituni na kufaidika kutokana na kila kitu kilichomo.

Isitoshe, ingawa hatukuwa na wakati wa kutosha kuona kila kitu, tulikuwa na fursa ya kutembelea sehemu ya pekee ya dunia ambako tembo, masokwe, masokwe-mtu, viboko, paa, chui-weusi, na ndege na vipepeo wa rangi mbalimbali wanapatikana. Tunaarifiwa kwamba misitu mikubwa ya Hifadhi ya Dzanga-Sangha na Mbuga ya Kitaifa ya Dzanga-Ndoki ina aina 7,000 hivi za mimea na aina 55 za wanyama.

Jamii hizo nyingi za viumbe hutukumbusha andiko hili la Biblia: “Jinsi kazi zako zilivyo nyingi, Ee Yehova! Zote umezifanya kwa hekima. Dunia imejaa vitu ulivyotokeza.” (Zaburi 104:24) Mambo tuliyojifunza yameimarisha azimio letu la kufanya vile zaburi hiyohiyo inavyosema: “Nitamwimbia Yehova katika maisha yangu yote; Nitampigia Mungu wangu muziki maadamu nipo. Kutafakari kwangu juu yake na kuwe kwenye kupendeza. Mimi nami nitashangilia katika Yehova.”—Zaburi 104:33, 34.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Mbilikimo wanaoishi katika eneo la ikweta la Afrika wanajulikana kwa sababu ni wafupi. Kimo chao hakizidi meta 1.27 (futi 5).

^ fu. 15 Mihuri hiyo hutengenezwa pia kwa vifaa vingine. Kwa habari zaidi, soma gazeti la Amkeni! la Mei 22, 1994, ukurasa wa 22-24.

[Ramani katika ukurasa wa 19]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

KAMERUN

JAM. YA KONGO

JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Bangui

Bayanga

Mbuga ya Kitaifa ya Dzanga-Ndoki

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

© Jerry Callow/Panos Pictures