Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Viini Sugu Vinavyoibuka Tena

Jinsi Viini Sugu Vinavyoibuka Tena

Jinsi Viini Sugu Vinavyoibuka Tena

YAMKINI virusi, bakteria, protozoa, kuvu, na viini vingine vimekuwapo tangu uhai ulipoanza duniani. Kwa kuwa viini hivyo ambavyo ni viumbe sahili zaidi vinaweza kustahimili hali zozote, vimeishi mahali ambapo viumbe wengine hawawezi kuishi. Vinapatikana katika matundu ya maji ya moto katika sakafu ya bahari na vilevile katika maji ya barafu ya Aktiki. Sasa viini hivyo vinakinza hata dawa kali zaidi za kuua viini.

Miaka 100 iliyopita, ilijulikana kwamba viini fulani vilisababisha magonjwa, lakini watu walioishi wakati huo hawakuwa wamesikia kuhusu dawa yoyote ya kuua viini. Kwa hiyo endapo mtu aliambukizwa ugonjwa mbaya, madaktari wengi hawakuwa na lolote la kufanya ila tu kumfariji. Alitegemea tu mfumo wake wa kinga upigane na ambukizo hilo. Iwapo alikuwa na mfumo dhaifu, kwa kawaida matokeo yalikuwa mabaya sana. Mara nyingi hata mkwaruzo mdogo ulioambukizwa viini ulisababisha kifo.

Hivyo, uvumbuzi wa dawa ya kwanza ya kuua viini ulileta mabadiliko makubwa ya kitiba. Matumizi ya dawa za sulfa katika miaka ya 1930 na dawa kama vile penisilini na streptomycin katika miaka ya 1940 yalichangia uvumbuzi mwingi katika miaka iliyofuata. Kufikia miaka ya 1990, kulikuwa na viuavijasumu vipatavyo 150 katika makundi 15.

Mataraja Yaambulia Patupu

Kufikia miaka ya 1950 na 1960, watu fulani walifikiria kwamba magonjwa ya kuambukiza yamekwisha. Hata wataalamu fulani wa viini waliamini kwamba muda si muda magonjwa hayo yangetokomea. Mnamo 1969, daktari mkuu wa Marekani aliliambia bunge kwamba baada ya muda huenda wanadamu “hawatahangaishwa tena na magonjwa ya kuambukiza.” Mnamo mwaka wa 1972, mshindi wa tuzo ya Nobeli Macfarlane Burnet na David White waliandika hivi: “Inaelekea sana kwamba wakati ujao hakutakuwa na jambo lolote la kuripoti kuhusu magonjwa ya kuambukiza kwa sababu hayatakuwepo.” Kwa kweli, wengine walidhani kwamba magonjwa hayo yangekomeshwa kabisa.

Maoni ya kwamba magonjwa ya kuambukiza yangekomeshwa yaliwafanya wengi wawe na uhakika kupita kiasi. Muuguzi mmoja aliyefahamu madhara yaliyosababishwa na viini kabla viuavijasumu havijavumbuliwa, alisema kwamba wauguzi fulani vijana walianza kupuuza usafi. Alipowakumbusha wanawe mikono, walimjibu hivi: “Usijali, sasa tuna viuavijasumu.”

Hata hivyo, kutegemea viuavijasumu na kuvitumia kupita kiasi kumetokeza madhara. Magonjwa ya kuambukiza yamesitawi. Isitoshe, yameibuka tena na kuwa kisababishi kikuu cha kifo ulimwenguni! Mambo mengine ambayo yamechangia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza ni vita, kuenea kwa utapiamlo katika nchi zinazoendelea, ukosefu wa maji safi, uchafu, usafiri wa haraka, na mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni.

Bakteria Sugu

Viini vya kawaida vimekuwa sugu na hivyo kusababisha tatizo kubwa ambalo halikutarajiwa na wengi. Hata hivyo, kwa kuzingatia matukio ya zamani, watu walipaswa kutarajia kwamba viini vingekinza dawa. Kwa nini? Kwa mfano, hebu fikiria ilivyokuwa wakati dawa ya kuua wadudu ya DDT ilipoanza kutumiwa katikati ya miaka ya 1940. * Wafugaji walifurahi sana wakati nzi walipotoweka baada ya dawa hiyo kuanza kutumiwa. Lakini nzi wachache hawakufa, na watoto wao wakarithi uwezo wa kukinza dawa hiyo. Muda si muda, nzi hao waliongezeka sana kwa kuwa hawangeweza kuangamizwa na dawa ya DDT.

Hata kabla ya dawa ya DDT kutumiwa, na kabla ya penisilini kutumiwa katika matibabu mwaka wa 1944, tayari ilikuwa imegunduliwa kwamba bakteria hatari zinaweza kuwa sugu. Dakt. Alexander Fleming, aliyevumbua penisilini, alijua hivyo. Alipokuwa katika maabara yake, aliona vizazi mbalimbali vya bakteria ya Staphylococcus aureus vikifanyiza kuta za chembe ambazo hazingeweza kupenywa na dawa aliyokuwa amegundua.

Hivyo miaka 60 hivi iliyopita, Dakt. Fleming alionya kwamba bakteria hatari ndani ya mwili wa mgonjwa zinaweza kupata uwezo wa kukinza penisilini. Kwa hiyo ikiwa penisilini haikuua bakteria nyingi hatari, bakteria sugu ziliongezeka. Basi ugonjwa huo ambao haungeweza kutibiwa na penisilini ungerudi tena na kuwa sugu zaidi.

Kitabu The Antibiotic Paradox kinaeleza hivi: “Utabiri wa Fleming ulitimia kwa kadiri kubwa zaidi kuliko alivyokuwa amesema.” Jinsi gani? Iligunduliwa kwamba chembe za urithi za aina fulani za bakteria zilitokeza vimeng’enya vinavyopunguza nguvu za penisilini. Hivyo, mara nyingi hata kumeza tembe nyingi za penisilini hakukusaidia. Hilo lilikuwa jambo lenye kusikitisha sana!

Ili kupambana na magonjwa ya kuambukiza, dawa mpya za kuua viini zilianza kutumiwa kuanzia miaka ya 1940 hadi miaka ya 1970, na nyingine chache zikavumbuliwa katika miaka ya 1980 na 1990. Dawa hizo zingeweza kuua bakteria ambazo zilikinza dawa za awali. Lakini miaka michache baadaye, kukaibuka aina fulani za bakteria ambazo zilikinza dawa hizo mpya.

Wanadamu wametambua kwamba bakteria hukinza dawa kwa njia ya ajabu sana. Bakteria zinaweza kubadili ukuta wa chembe ili kuzuia dawa isipenye au kubadili mfumo wake ili zisife. Pia bakteria inaweza kuondoa dawa mara tu inapoingia, au inaweza kuiharibu.

Kadiri watu wanavyozidi kutumia dawa za kuua viini, ndivyo aina mbalimbali za bakteria sugu zimeongezeka na kuenea. Je, hiyo ni balaa tupu? La, nyakati nyingine haiwi hivyo. Dawa moja inaposhindwa kutibu ambukizo fulani, kwa kawaida dawa nyingine hufaulu. Ingawa tatizo la bakteria sugu limekuwa baya, mara nyingi kumekuwa na suluhisho.

Kukinza Dawa za Aina Mbalimbali

Wanasayansi wa kitiba wamesikitika kugundua kwamba bakteria hubadilishana chembe za urithi. Mwanzoni ilidhaniwa kwamba bakteria za aina moja tu ndizo hubadilishana chembe za urithi. Lakini baadaye chembe zilezile sugu ziligunduliwa katika bakteria tofauti. Kutokana na utaratibu huo wa kubadilishana chembe za urithi, bakteria za aina mbalimbali zimeweza kukinza dawa nyingi za kawaida.

Isitoshe, uchunguzi uliofanywa katika miaka ya 1990 ulionyesha kwamba bakteria fulani zimekuwa sugu bila kusaidiwa na bakteria nyingine. Hata dawa moja inapotumiwa, bakteria fulani hupata uwezo wa kukinza dawa nyingi, za kiasili na zisizo za kiasili.

Utabiri Wenye Kuhuzunisha

Ingawa dawa nyingi za kuua viini hufaulu kutibu wagonjwa wengi, je, dawa hizo zitafaulu wakati ujao? Kitabu The Antibiotic Paradox kinasema hivi: “Hatuwezi kutarajia kwamba ambukizo lolote lile litakomeshwa na dawa ya kwanza inayotumiwa.” Kitabu hicho kinaendelea kusema: “Katika sehemu fulani za ulimwengu kuna dawa chache za kuua viini, hivyo hakuna dawa inayoweza kutibu ugonjwa kabisa . . . . Watu wanaugua na kufa kutokana na magonjwa ambayo miaka 50 iliyopita ilitabiriwa kwamba yangekomeshwa kabisa.”

Mbali na bakteria, kuna viini vingine pia ambavyo vimepata uwezo wa kukinza dawa. Virusi, kuvu, na vimelea vingine vidogo vina uwezo huo wa ajabu. Hivyo kuna viini vingi sugu ambavyo vitafanya jitihada zote za kuvumbua na kutengeneza dawa ziambulie patupu.

Basi, ni nini kinachoweza kufanywa? Je, inawezekana kukomesha au angalau kudhibiti viini sugu? Ni nini kinachoweza kufanywa ili dawa za kuua viini ziendelee kushinda magonjwa katika ulimwengu unaoendelea kukumbwa na magonjwa ya kuambukiza?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Dawa za kuua wadudu ni sumu kama dawa za matibabu. Dawa hizo zote zimesaidia na vilevile zimesababisha madhara. Ijapokuwa dawa zinaweza kuua viini hatari, zinaweza pia kuua bakteria muhimu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

Dawa za Kuua Viini

Viuavijasumu ni aina moja ya dawa ambazo hutumiwa kuua viini mbalimbali. Kwa kawaida, matumizi ya dawa hizo huitwa tiba ya kemikali. Ingawa tiba ya kemikali hutumiwa kutibu kansa, hapo awali ilitumiwa, na bado inatumiwa kutibu magonjwa ya kuambukiza.

Viini ni viumbe wadogo ambao wanaweza kuonekana tu kwa kutumia hadubini. Ingawa viuavijasumu huua viini vinavyosababisha magonjwa, vinaweza pia kuua viini vyenye faida.

Mnamo mwaka wa 1941, Selman Waksman, aliyeshiriki kuvumbua dawa ya streptomycin, alitumia neno la Kiingereza “antibiotic” (viuavijasumu) kumaanisha dawa zinazoua bakteria ambazo zimetengenezwa kutokana na vijidudu. Viuavijasumu na dawa nyingine za kuua viini zina faida kwa sababu zinaangamiza viini bila kumdhuru mgonjwa sana.

Hata hivyo, kihalisi viuavijasumu vyote vina kiasi fulani cha sumu. Wataalamu hutumia namba fulani kuonyesha tofauti kati ya kiwango ambacho dawa inaua viini na jinsi ambavyo inamdhuru anayeitumia. Ikiwa namba hiyo ni ya juu, inaonyesha kwamba dawa hiyo ni salama, na ikiwa ni ya chini, inaonyesha kwamba dawa ni hatari. Kwa kweli, maelfu ya dawa za kuua viini zimegunduliwa, lakini nyingi haziwezi kutumiwa katika matibabu kwa sababu zina sumu nyingi inayoweza kuwadhuru wanadamu au wanyama.

Penisilini ilikuwa dawa ya kwanza ya kiasili ya kuua viini kuwahi kutumiwa. Ilitokana na kuvu inayoitwa Penisillium notatum. Penisilini ilitiwa mishipani kwa mara ya kwanza mwaka wa 1941. Muda mfupi baadaye, mnamo mwaka wa 1943, dawa ya streptomycin ilitengenezwa kutokana na bakteria ya Streptomyces griseus, inayopatikana udongoni. Baadaye dawa nyingine za kuua viini zilitengenezwa kutokana na vitu vilivyo hai na vitu visivyo hai. Hata hivyo, bakteria zimebuni njia za kukinza dawa nyingi na kusababisha tatizo la kitiba ulimwenguni pote.

[Picha]

Kuvu ya penisilini inayoonekana chini ya chombo hiki huzuia ukuzi wa bakteria

[Hisani]

Christine L. Case/Skyline College

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Aina za Viini

Virusi ndivyo viini vidogo zaidi. Virusi husababisha magonjwa ya kawaida kama vile mafua na mwasho wa koo. Pia vinasababisha magonjwa hatari kama polio, Ebola, na UKIMWI.

Bakteria ni vijiumbe sahili vyenye chembe moja isiyokuwa na kiini na kwa kawaida vina kromosomu moja tu. Kuna trilioni nyingi za bakteria mwilini mwetu hasa katika mfumo wa kumeng’enya chakula. Zinatusaidia kumeng’enya chakula na ni chanzo kikuu cha vitamini K inayosaidia kugandisha damu penye jeraha.

Kati ya aina 4,600 hivi za bakteria, inasemekana kwamba ni aina 300 hivi tu zinazosababisha magonjwa. Hata hivyo, bakteria ndizo zinazosababisha magonjwa mengi ya mimea, wanyama, na wanadamu. Magonjwa yanayokumba wanadamu ni kama vile kifua-kikuu, kipindupindu, dondakoo, kimeta, kuoza kwa meno, aina fulani za nimonia, na magonjwa fulani ya zinaa.

Protozoa ni vijiumbe vyenye chembe moja kama bakteria, lakini vingine huwa na zaidi ya kiini kimoja. Aina za protozoa ni amiba, trypanosome, na kimelea kinachosababisha malaria. Ijapokuwa thuluthi moja ya viumbe ni vimelea, ni vichache tu vinavyosababisha magonjwa ya wanadamu. Kuna aina 10,000 hivi za vimelea.

Kuvu pia zinaweza kusababisha magonjwa. Vijiumbe hivyo vina kiini na hufanyiza nyuzi zilizojipinda-pinda. Magonjwa ya kawaida yanayosababishwa na kuvu ni kama vile mashilingi, ukungu kwenye vidole vya miguu, na Candida. Magonjwa hatari yanayosababishwa na kuvu huwapata hasa watu ambao mfumo wao wa kinga umedhoofishwa na utapiamlo, kansa, dawa, au maambukizo ya virusi.

[Picha]

Virusi vya Ebola

Bakteria ya “Staphylococcus aureus”

Protozoa ya “Giardia lamblia”

Kuvu ya mashilingi

[Hisani]

CDC/C. Goldsmith

CDC/Janice Carr

Courtesy Dr. Arturo Gonzáles Robles, CINVESTAV, I.P.N. México

© Bristol Biomedical Image Archive, University of Bristol

[Picha katika ukurasa wa 4]

Alexander Fleming, aliyevumbua penisilini