Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vinu vya Upepo Vyatukumbusha Zama za Kale

Vinu vya Upepo Vyatukumbusha Zama za Kale

Vinu vya Upepo Vyatukumbusha Zama za Kale

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UHOLANZI

SI AJABU kwamba picha nyingi za mandhari zilizochorwa na Jacob van Ruisdael, Meindert Hobbema, Rembrandt van Rijn, na wachoraji wengine stadi wa Uholanzi katika karne ya 17 huonyesha vinu vya upepo! Zamani hizo kulikuwa na vinu vya upepo 10,000 hivi nchini Uholanzi. Hata hivyo, mbali na kuwavutia wasanii, vinu hivyo maridadi vilitumiwa kwa njia nyingine. Kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1400 hadi mwishoni mwa miaka ya 1800, vilifanya kazi ambayo injini za dizeli na za umeme hufanya leo. Vilitumiwa kuvuta maji, kusaga nafaka, kupasua mbao, na kufanya kazi nyingine nyingi viwandani. Hata hivyo, vinu vya upepo havikuchafua hewa kama injini za kisasa.

Kutia Matanga

Ukienda Uholanzi leo, unaweza kuona vifaa hivyo vya tangu jadi, ingawa idadi yake imepungua hadi 1,000 hivi. Je, ungependa kujifunza mengi kuvihusu? Jiunge nasi tunapotembelea kinu kimoja cha upepo ambacho kimekuwapo kwa miaka 350 kwenye kingo maridadi za Mto Vechte, katikati mwa Uholanzi.

Ni asubuhi nyangavu katika majira ya kuchipua. Mwendeshaji wa kinu cha upepo, Jan van Bergeijk anatukaribisha kwa kahawa motomoto na anatueleza kwamba hali ya hewa inafaa kabisa kuendesha kinu. Hata hivyo, kwanza kabisa lazima paa ya kinu igeuzwe kukabili upepo. Jan anaeleza jinsi inavyogeuzwa huku akikanyaga tindi za gurudumu la mbao ambalo linamzidi urefu mara mbili. Gurudumu hilo limeunganishwa na paa ya kinu. Jan anapozungusha gurudumu, paa hiyo inazunguka hadi mishale yake yote ambayo ina urefu wa meta 13 inapopigwa na upepo mwingi. Kisha, gurudumu linafungwa ardhini kwa mnyororo ili lisisonge. Halafu Jan anachukua tanga la turubali na kulifunga kwenye kila mshale. Baada ya kutia mnyororo, Jan anaachilia breki, kisha matanga yanasukumwa na upepo na mishale yote minne inaanza kuzunguka polepole. Kwa muda fulani, twatazama kwa mshangao mishale hiyo inayozunguka kwa mvumo. Halafu Jan anatuita ili tuone jinsi injini ya kinu inavyofanya kazi.

Kuchunguza Kinu cha Upepo

Tunapanda ngazi iliyoinuka na kufika kwenye paa ya kinu ambapo twaona mhimili wa mbao uliolala ambao umeunganishwa na ile mishale. Mhimili huo huendesha mtaimbo ulio wima kwa kutumia magurudumu ya mbao yaliyo na meno na fito. Twaona mafuta meupe karibu na hapo. Jan anasema kwamba yanatumiwa kulainisha beringi za mawe ambamo mhimili wa mbao unazunguka. Lakini yeye hutumia nta ya nyuki kulainisha meno ya magurudumu ya mbao za mialoni. Twaona pia jinsi mwendo wa mishale unavyoweza kupunguzwa. Gurudumu moja lina vipande kadhaa vya mbao. Vipande hivyo vinapokazwa, vinasimamisha magurudumu; na vinapoinuliwa, mishale huzunguka.

Tunapoteremka ngazi kwa uangalifu, tunatazama mtaimbo mkuu ambao umeanzia juu hadi chini ya kinu. Twanusa harufu ya mbao kuukuu na kusikia mlio wa gia ambazo zinazunguka. Chini ya mtaimbo ulio wima, kuna magurudumu mengine ya mbao yenye meno na fito. Magurudumu hayo huendesha gurudumu la maji. Twasimama karibu na gurudumu hilo linalozunguka na kusikiliza mshindo wa maji yanayopita haraka na mvumo wa matanga yanayozunguka. Ni kana kwamba tumerudi zama za kale. Tunashangaa na kufurahia yale tunayoona.

Kuishi Ndani ya Kinu cha Upepo

Baadhi ya vinu, kama vile vya kusaga nafaka havikuwa na vyumba vya kuishi. Injini ilikuwa kubwa sana. Kwa kawaida, mwendeshaji wa kinu aliishi katika chumba kingine karibu na kinu pamoja na familia yake. Hata hivyo, kinu kama hiki tunachotembelea kina vyumba vya kuishi.

Leo huenda watu wakafikiri kwamba kuishi ndani ya kinu ni jambo la kustarehesha, lakini haikuwa hivyo zamani. Chumba cha chini kilitumiwa kama sebule na mahali pa kulala. Kilikuwa na kitanda cha watu wawili, mahali pa kupikia, na pa kuweka vitu. Kabla ya katikati ya karne ya 20, choo kidogo kilijengwa nje juu ya mtaro. Jan anaeleza kwamba waendeshaji wa vinu wenye familia kubwa, baadhi yao wakiwa na zaidi ya watoto kumi, walilazimika kutafuta mahali pa ziada pa kulala. Nyakati nyingine, kitinda-mimba alilala chini ya kitanda cha wazazi huku watoto wengine wakilala ama sebuleni au kwenye orofa ya pili au ya tatu chini ya magurudumu yenye kelele!

Vinu fulani vya upepo vilitumiwa kukausha maji kwenye mashamba ambayo hapo awali yalikuwa sehemu ya maziwa au bahari. Vinu hivyo vilifanya kazi mchana na usiku. Vyumba vilivyokuwa ndani ya vinu vilikuwa na upepo na baridi kwa sababu vilijengwa sehemu zilizo wazi ili vipate upepo mwingi. Watu walioishi ndani ya vinu walikuwa na maisha magumu sana kwa sababu walikabili pia hatari ya kupigwa na dhoruba na radi. Kwa sasa, bado watu wanaishi ndani ya vinu vya upepo 150 hivi nchini Uholanzi, hasa waendeshaji stadi.

Vinu vya Upepo Vyenye Matumizi Mbalimbali

Kinu kinapoendelea kuvuta maji, tunaenda nje na kukalia kiti cha mbao. Jan anatueleza matumizi mbalimbali ya vinu vya upepo, kama vile kusaga nafaka, kupeleka maji kwenye mto au bwawa, kusindika mafuta, kutengeneza karatasi, kupasua mbao, na kadhalika. Anasema pia kwamba kinu cha kwanza cha kuvuta maji kilijengwa mwanzoni mwa karne ya 15. Baadaye, vinu kama hivyo vilitumiwa kukausha maziwa kadhaa kama vile Ziwa Schermer, Beemster, na Wormer, karibu na Amsterdam.

Leo mamia ya maelfu ya Waholanzi huishi na kufanya kazi katika maeneo ambayo yalikuwa maziwa hapo awali. Hata uwanja mkuu wa ndege wa Uholanzi ulio karibu na Amsterdam umejengwa mahali ambapo palikuwa na ziwa. Wasafiri walio uwanjani huwa meta nne chini ya usawa wa bahari! Lakini usiogope kwamba uwanja utafunikwa na maji. Injini za dizeli au za umeme (zinazotumiwa badala ya vinu vya upepo) huvuta maji uwanjani usiku na mchana.

Je, Vinu vya Upepo Vinazungumza?

Mishale inapoendelea kuzunguka, Jan anatuuliza kama tumewahi kusikia kuhusu vinu vinavyozungumza. “Eti vinu vinazungumza? Haiwezekani,” tunajibu. Anaeleza kwamba kwenye nyanda tambarare za Uholanzi, mara nyingi vinu vilionekana kutoka mbali na hivyo mwendeshaji wa kinu angeweza kutuma ujumbe kwa majirani waliokuwa mbali kwa kugeuza mishale ya kinu kwa njia mbalimbali. Kwa mfano, mwendeshaji alipoenda kupumzika, aliiweka mishale mingine ikiwa wima na mingine ikiwa imelala (A). Alipokuwa mapumzikoni aliiweka katika umbo la mshazari (B). Alifanya hivyo pia wakati wa hali mbaya ya hewa ili mishale isiinuke juu sana na kupigwa na radi. Alionyesha kwamba ana shangwe au anatarajia jambo fulani kwa kusimamisha mishale kabla haijafika juu kabisa (C). Alionyesha kwamba ana huzuni au anaomboleza kwa kuisimamisha mishale baada tu ya kupita sehemu ya juu (D).

Kulikuwa pia na desturi nyingi. Kaskazini ya Amsterdam, nyakati nyingine vinu vilipambwa wakati wa sherehe, kama vile harusi. Kisha mishale iliwekwa katika umbo la mshazari, kama wakati ambapo mwendeshaji alikuwa mapumzikoni, na ikatiwa madoido na matamvua. Wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, Uholanzi ilipomilikiwa na jeshi la Ujerumani, wenyeji walitumia mishale ya vinu kuwaonya watu waliojificha kwamba jeshi lilikuwa likija kuwavamia. Mambo hayo yote tuliyoelezwa kuhusu vinu vya upepo yalifanya matembezi yetu na Jan, mwendeshaji wa kinu, yawe yenye kufana sana.

Miaka kadhaa iliyopita, jitihada za kuhifadhi vinu vya upepo ziliimarishwa wakati Shirika la Elimu, Sayansi, na Utamaduni la Umoja wa Mataifa lilipoorodhesha vinu 19 kwenye Mirathi ya Ulimwengu. Vinu hivyo viko huko Kinderdijk karibu na jiji la bandari la Rotterdam. Kwa hiyo, vinu hivyo vilivyokuwa viwanda vya kawaida sasa vimekuwa nguzo za kitamaduni. Isitoshe, wafanyakazi wengi wa kujitolea hudumisha na kulinda vinu kotekote nchini. Kwa sababu ya jitihada zao, watalii kutoka sehemu zote ulimwenguni wanaweza kuona vinu vya upepo vilivyowavutia wachoraji mashuhuri wa kale.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Uuzaji wa Vinu vya Upepo Wapigwa Marufuku

Miaka 300 hivi iliyopita, mafundi wa vinu vya upepo walihitajika sana. Meli zilisafirisha sehemu mbalimbali za vinu kwa wingi kutoka Uholanzi. Zaidi ya hayo, wageni walikuja kutafuta mafundi wa vinu nchini na kuwashawishi waajiriwe katika nchi nyingine. Muda si muda, vinu vya upepo kama vya Uholanzi vilianza kuonekana katika Baltiki, Hispania, Ireland, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, na Ureno. Ama kweli, katikati ya karne ya 18, mafundi wa vinu vya upepo walikuwa wamepungua sana hivi kwamba serikali ya Uholanzi ilichukua hatua. Mnamo Februari 1752, serikali ilipiga marufuku uuzaji wa vinu vya upepo katika nchi nyingine. Mwanahistoria Mholanzi Karel Davids anasema kwamba tangu wakati huo, hakuna mtu aliyeruhusiwa kumsaidia mgeni kununua, kutengeneza, au kusafirisha “sehemu yoyote ya kinu cha upepo cha Uholanzi” au “kuuza kifaa cha kuvitengeneza katika nchi nyingine.” Kumbe upelelezi wa viwanda na vikwazo vya kibiashara vilianza zama za kale.

[Picha]

Chini: Jan anageuza paa ya kinu kukabili upepo; magurudumu ya mbao yenye meno; sebule

[Hisani]

All photos: Stichting De Utrechtse Molens

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 22]

(Ona kichapo)

A

B

C

D

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

De Saen painting by Peter Sterkenburg, 1850: Kooijman Souvenirs & Gifts (Zaanse Schans Holland)