Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Njia Sita za Kutunza Afya

Njia Sita za Kutunza Afya

 Njia Sita za Kutunza Afya

Changamoto Katika Nchi Zinazoendelea

NI VIGUMU kudumisha usafi hasa katika nchi ambazo hazina maji safi ya kutosha wala huduma za kuondoa maji machafu na takataka. Hata hivyo, kuna faida za kudumisha usafi. Inakadiriwa kwamba zaidi ya nusu ya magonjwa na vifo vya watoto wachanga husababishwa na viini vya magonjwa vinavyoingia mwilini kupitia mikono michafu, au wanapokula chakula chenye viini au kunywa maji machafu. Magonjwa mengi, hasa ya kuharisha, yanaweza kuzuiwa kwa kutumia mapendekezo yafuatayo yaliyo katika kitabu Ukweli Kuhusu Maisha, kilichochapishwa na Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa.

1 Ondoa kinyesi kabisa

Kuna viini vingi katika kinyesi. Viini vinavyoingia majini au katika chakula, au ambavyo viko mikononi, mezani, au kwenye vyombo vya chakula na sehemu za kutayarishia chakula, vinaweza kuingia mdomoni na kumezwa, na hivyo kusababisha magonjwa. Njia bora ya kuvizuia viini hivyo visienee ni kuondoa kinyesi kabisa. Kinyesi cha wanadamu kinapaswa kutupwa chooni. Hakikisha kwamba hakuna mavi ya wanyama karibu na nyumba za watu, kwenye vijia, au mahali ambapo watoto hucheza.

Mahali ambapo vyoo havipatikani, kifukie kinyesi ardhini mara moja. Kumbuka kwamba vinyesi vyote vina viini vya magonjwa, hata vinyesi vya watoto wachanga. Hata vinyesi vya watoto vinapaswa kutupwa chooni au kufukiwa ardhini.

Safisha vyoo mara nyingi. Mashimo ya vyoo yafunikwe na maji yavutwe kwenye vyoo vya maji.

2 Nawa mikono

Unapaswa kunawa mikono kwa ukawaida. Viini huondolewa kwa kunawa mikono kwa maji na sabuni au kwa maji na majivu. Kunawa kwa maji peke yake hakutoshi, mikono yote miwili inapaswa kusuguliwa vizuri kwa sabuni au majivu.

Ni muhimu sana kunawa mikono baada ya kutoka chooni, na baada ya kumsafisha mtoto mdogo aliyejisaidia. Ni muhimu pia kunawa mikono  baada ya kushika wanyama, kabla ya kuwalisha watoto au kugusa chakula.

Kunawa mikono huzuia watu wasiambukizwe minyoo wanaosababisha magonjwa. Minyoo hao ni wadogo hivi kwamba hawaonekani bila kutumia hadubini. Wao huishi katika kinyesi na mkojo, katika maji ya mito na maziwa, ardhini, na katika nyama mbichi au nyama ambazo hazijapikwa vizuri. Njia moja muhimu ya kuzuia minyoo wasiingie mwilini mwako ni kunawa mikono. Pia, ukivalia viatu unapokuwa karibu na vyoo unaweza kuwazuia minyoo wasiingie mwilini mwako kupitia ngozi ya miguu.

Mara nyingi watoto huweka mikono mdomoni. Kwa hiyo, ni muhimu kuwanawisha mikono mara kwa mara, hasa baada ya wao kujisaidia na kabla ya kula. Wafundishe kunawa mikono yao na kutocheza karibu na vyoo au karibu na sehemu ambazo watu hujisaidia.

3 Nawa uso kila siku

Ili kuzuia usiambukizwe magonjwa ya macho, nawa uso kwa maji na sabuni kila siku. Nyuso za watoto zinawishwe pia kila siku. Uso mchafu unavutia inzi walio na viini kwenye mwili wao. Viini hivyo vinaweza kusababisha magonjwa ya macho na hata upofu.

Yachunguze macho ya watoto wako kwa ukawaida. Macho yasiyo na ugonjwa huwa yenye unyevunyevu na yanang’aa. Ikiwa macho ya mtoto ni makavu, mekundu, yanauma, au kutoa usaha, mtoto anapaswa kuchunguzwa na mtaalamu wa afya au daktari.

4 Tumia maji safi tu

Watu hawashikwi sana na magonjwa wanapotumia maji safi ya kunywa na kuyahifadhi vizuri ili yasichafuliwe kwa viini. Ingawa inaaminika kuwa maji ya bomba ni salama na machoni yanaonekana safi, bado yanaweza kuwa na viini vya magonjwa. Maji ya mabwawa, mito, matanki yasiyofunikwa au visima yana uwezekano wa kuwa na viini vingi zaidi. Kuchemsha maji huua viini vya magonjwa.

Visima vya maji vinapaswa kufunikwa. Ndoo, kamba, na vyombo vingine vinavyotumika kuchota na kuhifadhi maji vinapaswa kuoshwa kwa ukawaida na kuwekwa mahali safi, lakini visiwekwe chini. Wachunge  wanyama ili wasikaribie visima wala wasiingie ndani ya nyumba. Usitumie dawa za kuwaua wadudu waharibifu au kemikali karibu na maji.

Nyumbani, maji ya kunywa yawekwe katika chombo safi kilichofunikwa. Ni bora kuwa na chombo cha kuhifadhia maji chenye mfereji. Ikiwa chombo hakina mfereji, kikombe safi au kifaa safi kitumiwe kuchota maji kutoka katika chombo cha kuhifadhia. Mikono michafu haipaswi kamwe kutumbukizwa katika chombo cha kuhifadhia maji ya kunywa.

5 Zuia chakula kisichafuliwe kwa viini

Kwa kupika chakula kikaiva vizuri, unaweza kuua viini vya magonjwa. Ni muhimu nyama ya jamii za kuku na nyama nyingine zipikwe na kuiva barabara. Viini vya magonjwa huongezeka sana katika chakula chenye uvuguvugu. Kwa hiyo, chakula kiliwe mara moja baada ya kupikwa. Ikiwa itakubidi kuhifadhi chakula kwa zaidi ya saa mbili, hakikisha kinahifadhiwa katika hali ya joto au kuwekwa mahali penye baridi. Kifunike chakula kilichopikwa ambacho kitaliwa baadaye. Jambo hilo litawazuia inzi na wadudu. Kipashe moto chakula hicho kabla ya kukila.

Maziwa ya mama ndiyo maziwa bora zaidi kwa watoto. Maziwa ya wanyama ambayo yamechemshwa au kutayarishwa kiwandani ni salama kuliko maziwa ambayo hayajachemshwa. Usitumie chupa za kunyonyesha, isipokuwa umeziosha kwa maji ya moto kabisa kabla ya kuzitumia. Mara nyingi chupa za kunyonyesha huwa na viini vya ugonjwa wa kuharisha. Ni bora kuwanyonyesha watoto au kuwalisha kwa kutumia kikombe safi kisicho na chuchu.

Safisha matunda na mboga katika maji safi. Jambo hilo ni muhimu hasa ikiwa watoto watapewa vyakula hivyo bila kupikwa.

6 Ondoa takataka zote za nyumbani

Inzi, mende, na panya hueneza viini vya magonjwa. Viumbe hao huzaana sana katika takataka. Ikiwa sehemu unayoishi haina huduma ya kuondoa takataka, tupa takataka katika shimo ambamo zinaweza kufukiwa au kuteketezwa kila siku. Ondoa takataka zote na maji machafu nyumbani kwako.

Ukitumia mapendekezo hayo kwa ukawaida, utazoea haraka kuyafuata kila siku maishani mwako. Si vigumu kuyafuata na hayagharimu pesa nyingi, na kwa kuyafuata utatunza afya yako na afya ya familia yako.

[Picha katika ukurasa wa 11]

Mahali ambapo vyoo havipatikani, kifukie kinyesi ardhini mara moja

[Picha katika ukurasa wa 11]

Nawa mikono kwa ukawaida

[Picha katika ukurasa wa 12, 13]

Nawa uso kwa maji na sabuni kila siku

[Picha katika ukurasa wa 12]

Watu wanaotumia maji safi ya kunywa na kuyahifadhi vizuri ili yasichafuliwe kwa viini hawashikwi sana na magonjwa

[Picha katika ukurasa wa 13]

Kifunike chakula kilichopikwa ambacho kitaliwa baadaye

[Picha katika ukurasa wa 13]

Takataka zifukiwe au ziteketezwe kila siku