Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mawasiliano Ni Muhimu kwa Viumbe na Mimea

Mawasiliano Ni Muhimu kwa Viumbe na Mimea

Mawasiliano Ni Muhimu kwa Viumbe na Mimea

JULIE alipokuwa mtoto mchanga, wazazi wake walitazamia kwa hamu kusikia maneno yake ya kwanza. Mama ya Julie alisema hivi: “Kila mzazi hufurahia sana kusikia mtoto wake akisema ‘Mama’ au ‘Baba.’ Julie aliponiita ‘Mama’ mara ya kwanza ilikuwa ni kana kwamba ananikumbatia kwa mikono yake midogo akisema: ‘Wewe ni mama yangu. Nakupenda, na ninataka kuongea nawe.’ Sitasahau kamwe tukio hilo la pekee.” Ama kweli, uwezo wa kuwasiliana ni zawadi yenye thamani sana!

Hata hivyo, si wanadamu peke yao wanaoweza kuwasiliana. Ijapokuwa wanyama huongozwa hasa na silika, wao pia wana njia za kustaajabisha za kuwasiliana. Kwa mfano, kila mwaka pengwini wa emperor wanaochumbiana katika eneo lenye theluji la Antaktika huwasiliana kwa kutoa milio kabla ya majira ya baridi kali. Pengwini hao hawatoi milio hiyo ili kuwafurahisha wenzao, bali wanafanya hivyo kwa sababu maisha ya kifaranga wao wa baadaye yanahusika. Jinsi gani?

Baada ya kutaga yai, pengwini wa kike humwachia pengwini wa kiume yai hilo ili aende baharini kutafuta chakula, naye pengwini wa kiume huliatamia kwa kuliweka katikati ya manyoya yake. Baada ya siku 65 hivi, pengwini wa kike hurudi akitembea na kuteleza kwa tumbo kwenye barafu kwa umbali wa kilometa 150. Yeye hukabili kibarua kigumu anapotafuta kikundi chake cha pengwini. Lakini atamjuaje mwenzi wake na kifaranga wake kati ya makumi ya maelfu ya pengwini wanaotoa milio? Wakati wa uchumba, kila ndege hujitahidi kukumbuka nyimbo za mwenzi wake kabisa hivi kwamba hata baada ya kutengana kwa miezi kadhaa wanaweza kutambuana!

Zaidi ya kuwasiliana kwa milio mbalimbali yenye kustaajabisha, viumbe huwasiliana pia kwa ishara, kwa rangi zenye kuvutia, kwa kumulika-mulika, na kwa harufu. Amini usiamini, kama vile tutakavyoona baadaye, hata mimea inaweza kuwasiliana na mimea mingine au na wanyama fulani. Naam, mawasiliano ni muhimu kwa mimea na viumbe wanaotegemeana sana.

Je, ungependa kujifunza zaidi kuhusu mbinu za ajabu za mawasiliano zinazotumiwa na viumbe na mimea? Je, ungependa kujua jinsi unavyoweza kuboresha uwezo wako wa kuwasiliana na kuuthamini zaidi? Makala zinazofuata zaweza kukusaidia.

[Picha katika ukurasa wa 3]

Pengwini wa kike aina ya “emperor” humtambuaje mwenzi wake?