Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Hali ya Hewa Imebadilika?

Kwa Nini Hali ya Hewa Imebadilika?

Kwa Nini Hali ya Hewa Imebadilika?

“Mafuriko makubwa na dhoruba kali zinazotukia sasa zitatokea mara nyingi zaidi.” —THOMAS LOSTER, MTAALAMU WA KUKADIRIA MADHARA YA HALI YA HEWA.

JE, NI kweli kwamba hali ya hewa imebadilika? Watu wengi wanaonelea hivyo. Dakt. Peter Werner, ambaye ni mtaalamu wa hali ya hewa katika Taasisi ya Potsdam ya Uchunguzi wa Athari za Hali ya Hewa, anasema hivi: “Tunapochunguza hali ya hewa ulimwenguni, kama vile kiasi cha mvua kisicho cha kawaida, mafuriko, ukame, dhoruba, na kuona mabadiliko yake, tunaweza kusema kwa hakika kwamba hali hizo zisizo za kawaida zimeongezeka mara nne katika miaka 50 iliyopita.”

Wengi wanaonelea kwamba hali ya hewa isiyo ya kawaida inaonyesha kwamba joto la dunia linaongezeka kupita kiasi. Shirika la Kuhifadhi Mazingira la Marekani linasema: “Ongezeko la joto duniani linasababishwa na gesi fulani hewani (kama vile mvuke, kaboni dioksidi, oksidi-nitrasi, na methani) zinazonasa joto la jua. Kama gesi hizo hazingekuwepo, joto lingerudi angani na halijoto ya wastani duniani ingepungua kwa nyuzi 33 Selsiasi.”

Hata hivyo, wengi wanasema kwamba mwanadamu ameharibu mfumo huo wa asili bila kujua. Makala moja ya chapisho la Shirika la Marekani la NASA linaloitwa Earth Observatory, ambalo linapatikana kwenye Internet, inasema hivi: “Kwa makumi ya miaka, viwanda na magari yamechafua anga kwa mabilioni ya tani za gesi zinazosababisha ongezeko la joto . . . Wanasayansi wengi wanahofu kwamba ongezeko la gesi hizo limezuia joto la ziada lisitoke duniani. Hivyo, gesi hizo zinanasa joto la ziada katika anga ya Dunia kama vile kioo cha mbele cha gari kinavyonasa joto linaloingia ndani ya gari.”

Watu fulani wanadai kwamba wanadamu hawajasababisha ongezeko kubwa la gesi hizo. Hata hivyo, Kamati ya Serikali Mbalimbali Kuhusu Badiliko la Hali ya Hewa (IPCC) ambayo inadhaminiwa na Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Ulimwenguni na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa inaripoti hivi: “Kuna uthibitisho mpya na wenye nguvu zaidi unaoonyesha kwamba katika miaka 50 iliyopita joto la dunia limeongezeka hasa kwa sababu ya shughuli za wanadamu.”

Pieter Tans, ambaye ni mtaalamu wa hali ya hewa kwenye Shirika la Kitaifa la Usimamizi wa Bahari na Anga, anasema hivi: “Kwa maoni yangu, sisi wanadamu tumesababisha asilimia 60 ya tatizo hilo . . . Hali za kiasili zimesababisha asilimia 40.”

Mambo Yanayoweza Kusababishwa na Ongezeko la Joto

Ongezeko la gesi hizo ambalo limetokana na shughuli za wanadamu limesababisha nini? Wanasayansi wengi sasa wanakubali kwamba joto la dunia limeongezeka. Limeongezeka kiasi gani? Ripoti ya kamati ya IPCC ya mwaka wa 2001 inasema hivi: “Joto la uso wa dunia limeongezeka kwa nyuzi 0.4 Selsiasi hadi 0.8 Selsiasi tangu mwishoni mwa karne ya 19.” Watafiti wengi wanaonelea kwamba huenda ongezeko hilo dogo ndilo linalosababisha mabadiliko makubwa ya hali ya hewa.

Ama kwa hakika, mfumo wa hali ya hewa duniani ni tata sana, na wanasayansi hawawezi kueleza kwa uhakika athari za ongezeko la joto duniani. Hata hivyo, wengi wanaamini kwamba kumekuwa na ongezeko la mvua upande wa kaskazini wa dunia, ukame huko Asia na Afrika, na kwamba El Niño imetukia mara nyingi zaidi katika Pasifiki.

Suluhisho la Ulimwenguni Pote Lahitajika

Kwa kuwa wengi wanaonelea kwamba mwanadamu ndiye aliyesababisha tatizo hilo, je, mwanadamu anaweza kulitatua? Jamii kadhaa zimetunga sheria ili kupunguza uchafuzi unaosababishwa na magari na viwanda. Hata hivyo, ijapokuwa jitihada hizo ni nzuri, hazijafua dafu. Uchafuzi upo ulimwenguni pote, kwa hiyo suluhisho linapaswa kuwa la ulimwenguni pote! Mnamo mwaka wa 1992, Kongamano la Dunia lilifanywa huko Rio de Janeiro. Miaka kumi baadaye, Kongamano la Ulimwengu la Maendeleo Yasiyoharibu Mazingira lilifanywa huko Johannesburg, Afrika Kusini. Wajumbe 40,000 kutia ndani viongozi wa nchi wapatao 100, walihudhuria kongamano hilo katika mwaka wa 2002.

Makongamano hayo yamewasaidia sana wanasayansi kufikia kauli moja. Gazeti Der Tagesspiegel la Ujerumani lasema hivi: “Ijapokuwa huko nyuma [katika mwaka wa 1992] wanasayansi walikuwa na mashaka kuhusu ongezeko la joto duniani, ni wachache tu wanaotilia shaka jambo hilo leo.” Hata hivyo, waziri wa mazingira wa Ujerumani, Jürgen Trittin anatukumbusha kwamba suluhisho la tatizo hilo halijapatikana bado. Alisema hivi kwa mkazo: “Ni lazima mambo yaliyojadiliwa katika kongamano la Johannesburg yasiwe maneno matupu tu bali yatekelezwe.”

Je, Uharibifu wa Mazingira Utakomeshwa?

Ongezeko la joto duniani ni mojawapo tu ya matatizo ya mazingira yanayowakumba wanadamu leo. Ni rahisi kutaja hatua ambazo zinapasa kuchukuliwa lakini ni vigumu sana kuzitekeleza. Mtaalamu wa tabia za wanyama wa Uingereza, Jane Goodall, aliandika hivi: “Sasa kwa kuwa hatimaye tumetambua kwamba tumeharibu sana mazingira, tunatumia stadi zetu zote kutafuta masuluhisho ya kitekinolojia.” Lakini anaonya hivi: “Tekinolojia haitoshi. Tunapaswa pia kuwa na nia ya kupata masuluhisho.”

Hebu fikiria tena tatizo la kuongezeka kwa joto duniani. Mbinu za kuzuia uchafuzi zinagharimu pesa nyingi na mara nyingi nchi maskini haziwezi kuzigharimia. Hivyo, wataalamu fulani wanahofu kwamba vizuizi vya matumizi ya umeme vinaweza kusababisha viwanda vingi vihamishwe kwenye nchi maskini ili vipate faida. Hata viongozi wenye nia nzuri wamo mashakani. Wanapojaribu kulinda uchumi wa nchi zao, mazingira yanaharibika. Wanapojaribu kulinda mazingira, wanahatarisha uchumi.

Severn Cullis-Suzuki wa jopo la ushauri la Kongamano la Dunia, alionyesha kwamba mabadiliko yanapaswa kuletwa na jitihada za mtu mmoja-mmoja aliposema hivi: “Sisi wenyewe ndio tunaoweza kurekebisha mazingira. Hatuwezi kuwategemea tu viongozi wetu. Tunapaswa kufahamu kabisa wajibu wetu na jinsi tunavyoweza kuleta mabadiliko hayo.”

Kwa kawaida tunatarajia watu watunze mazingira. Lakini si rahisi kuwafanya watu wabadili maisha yao. Kwa mfano: Watu wengi wanakubali kwamba magari yanachangia ongezeko la joto duniani. Hivyo, mtu anaweza kuamua kutotumia gari lake mara nyingi, au kutokuwa na gari. Lakini si rahisi kufanya hivyo. Hivi majuzi, Wolfgang Sachs wa Taasisi ya Wuppertal ya Hali ya Hewa, Mazingira, na Nishati alisema kwamba “sehemu mbalimbali ambazo huhusika katika shughuli za kila siku (kazini, shuleni, au dukani) ziko mbali sana hivi kwamba huwezi kufika huko bila kutumia gari. . . . Si kwamba tunataka tu kuwa na gari. Watu wengi hulazimika kuwa na gari.”

Wanasayansi fulani kama vile Profesa Robert Dickinson wa Chuo cha Sayansi ya Dunia na Anga cha Taasisi ya Tekinolojia ya Georgia, wanaona kwamba huenda haiwezekani kuzuia madhara ya ongezeko la joto duniani. Dickinson anaonelea kwamba hata uchafuzi ukikomeshwa leo, madhara ambayo tayari yapo yatabaki kwa angalau miaka 100!

Kwa kuwa serikali na watu binafsi hawawezi kurekebisha uharibifu wa mazingira, ni nani anayeweza? Tangu zamani, wanadamu wameomba miungu yao iwasaidie kudhibiti hali ya hewa. Ijapokuwa jitihada hizo hazingeweza kufua dafu, zinaonyesha jambo moja la hakika: Ili kutatua matatizo hayo, wanadamu wanahitaji msaada wa Mungu.

[Blabu katika ukurasa wa 7]

“Kuna uthibitisho mpya na wenye nguvu zaidi unaoonyesha kwamba katika miaka 50 iliyopita joto la dunia limeongezeka hasa kwa sababu ya shughuli za wanadamu”

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

“Je, Ongezeko la Joto Duniani Linadhuru Afya?”

Swali hilo lenye kuvuta fikira lilizushwa katika makala moja ya gazeti Scientific American. Makala hiyo ilitabiri kwamba ongezeko la joto duniani “litafanya magonjwa mengi hatari yaenee na kutokea mara nyingi zaidi.” Kwa mfano, katika maeneo fulani, “inakadiriwa kwamba idadi ya vifo vinavyosababishwa na joto kali itaongezeka maradufu kufikia mwaka wa 2020.”

Haijulikani waziwazi kama ongezeko la joto duniani linaweza kuleta magonjwa ya kuambukiza. “Inasemekana kwamba magonjwa yanayoletwa na mbu yataongezeka,” kwani mbu “huzaana kwa wingi na huuma zaidi joto linapoongezeka. . . . Hivyo, joto linapoongezeka katika maeneo mbalimbali, huenda mbu wakaingia hata mahali ambapo hawakuwepo zamani, na kueneza magonjwa.”

Mwishowe, mafuriko na ukame zinaweza kuchafua maji. Ama kweli, ongezeko la joto duniani ni jambo linalopaswa kutiliwa maanani.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Gesi zinazosababisha ongezeko la joto duniani hunasa joto hewani badala ya kuliachilia lirudi angani

[Hisani]

NASA photo

[Picha katika ukurasa wa 7]

Wanadamu wamechafua hewa kwa mabilioni ya tani za gesi na hivyo kusababisha ongezeko la joto duniani