Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Ndege Wana Uwezo wa Ajabu wa Kujisawazisha

Ndege wana kiungo fulani ndani ya sikio kinachowawezesha kudumisha usawaziko wanaporuka. Lakini kiungo hicho hakiwasaidii kusimama wima wala kutembea, “kwa kuwa tofauti na wanadamu, hawasimami wima na mikia yao si mizito kuweza kusawazisha mwili,” lasema gazeti la Ujerumani Leipziger Volkszeitung. Gazeti hilo laeleza hivi: “Baada ya kufanya utafiti kwa miaka minne, mchunguzi wa wanyama Reinhold Necker amegundua kiungo kingine kinachowasaidia njiwa wadumishe usawaziko.” Necker aligundua kwamba ndege wana chembe za hisia na kijishimo chenye umajimaji karibu na nyonga, ambacho inaonekana huwasaidia kudumisha usawaziko. Ripoti hiyo inasema kwamba “umajimaji huo ulipotolewa, njiwa hawakuweza kuketi au kutembea macho yao yalipofunikwa. Walianguka kutoka mahali walipotua, ingawa bado waliweza kuruka.”

Kutoa Sadaka kwa Kutumia Kadi za Mikopo

“Makanisa mengi zaidi nchini Kanada” yameanza kutumia “mbinu za kisasa za benki, kama vile kadi za benki na za mkopo ambazo waumini wanaweza kutumia kutoa sadaka,” lasema gazeti Vancouver Sun. Mashine za kutoa pesa zimewekwa ndani ya makanisa pamoja na “bahasha za kuweka sadaka na mtu anaweza kutoa sadaka kupitia mashine hiyo au kutumia kadi za mikopo.” Watu huingiza kadi zao katika mashine halafu wanaibonyeza kuonyesha kiasi wanachotaka kuchanga, kisha wanaweka risiti katika sahani ya sadaka. Padri mmoja alisema hivi: “Tunaishi katika ulimwengu ambapo hatutatumia pesa taslimu tena na kanisa pia linapaswa kubadilika kupatana na hali hizo.” Mweka-hazina mmoja wa kanisa alisema hivi kwa utani: “Tukitumia kadi za mikopo tunapewa nafasi ya kusafiri bure kwa ndege, na pia kwenda mbinguni kwa kutoa sadaka. Hebu wazia, tunaweza kupata faida maradufu.”

Tunza Sauti Yako

“Matatizo ya sauti ni kati ya matatizo ambayo hayashughulikiwi kikamilifu,” lasema gazeti Natal Witness la Afrika Kusini. Kulingana na Julie Barkmeier, profesa msaidizi wa sayansi ya usemi na kusikia, matatizo hayo husababishwa mara nyingi na vinundu au uvimbe kwenye viungo vya usemi vinavyotokea sauti inapotumiwa vibaya. Kitabu kimoja maarufu cha tiba kinasema kwamba kutumia sauti vibaya kunaweza kutia ndani kupaaza sauti, kusema kwa sauti ya chini isivyo kawaida, au kupumua hewa chafu kama moshi wa sigara au mvuke kutoka viwandani. “[Viungo vya usemi] vinapotikisika sana, vinaweza kukwaruzana na kusababisha uvimbe mwororo ambao unaweza kuzidi na kuwa vinundu,” lasema gazeti Natal Witness. Jambo hilo humfanya mtu atoe sauti yenye mkwaruzo. Makala hiyo inatoa ushauri huu: “Iwapo sauti yako imebadilika kwa majuma mawili au zaidi, unapaswa kumwona daktari. Ili kutunza sauti yako, . . . usipige mayowe au kuzungumza kwa sauti ya juu sana, usikohoe au kusafisha koo mara nyingi, unywe maji mengi, usinywe vinywaji vyenye kafeini sana, usivute sigara na, kabla ya kuzungumza, vuta pumzi nyingi. . . . Halafu, usiongee sana.”

“Mtoto Asiyejulikana” Ametambulishwa

Miaka 90 baada ya meli ya Titanic kuzama katika Aprili 1912, mtoto mmoja aliyekufa katika mkasa huo ametambulishwa kulingana na gazeti The Times la London. Mwili wake pamoja na miili ya watu wengine 43 ambao hawajatambuliwa, ilipatikana ikielea majini na ilizikwa huko Nova Scotia, Kanada. Jiwe la kaburi lake limeandikwa hivi: “Mtoto Asiyejulikana.” Kundi la watu 50 wakiwemo wanasayansi, wanahistoria, wataalamu wa nasaba, na madaktari wa meno walitumia chembe za urithi kumtambua mtoto huyo kuwa Eino Panula kutoka Finland, mwenye umri wa miezi 13, aliyekufa pamoja na mama yake na ndugu zake wanne. Familia hiyo ilinuia kuanza maisha mapya nchini Marekani, ambapo baba ya Eino aliyekuwa amesafiri mapema, aliwangojea lakini hawakufika. Kwa kuwa hakuna mtu aliyejitokeza kumdai mtoto huyo, wafanyakazi wa meli ya kuokoa ya Kanada walilipia kaburi lake na kulitunza. Huenda hata wale wengine ambao hawajulikani kwa sasa wakatambuliwa kwa kutumia chembe za urithi. Ili kusaidia katika uchunguzi huo, “mtu wa ukoo wa upande wa mama [wa mmoja wa watu waliokufa] alitoa damu wakati ambapo huyo mtu aliyekufa angekuwa na umri wa miaka 100,” lasema gazeti The Times.

Kompyuta Inayoiga Hali za Dunia

Mnamo Machi 11, 2002, wahandisi Wajapani walianza kutumia kompyuta yenye uwezo mkubwa zaidi iliyowahi kuundwa. Lengo lao lilikuwa “kuunda kompyuta ambayo inaiga kabisa hali za dunia,” lasema gazeti Time. Kompyuta hiyo inayoitwa Earth Simulator, ina ukubwa wa viwanja vinne vya tenisi na imegharimu dola milioni 350 hivi za Marekani. Inaweza kufanya hesabu zaidi ya trilioni 35 kwa sekunde. Uwezo wake ni mara tano zaidi ya ule wa kompyuta ya jeshi la Marekani inayoweza kufanya hesabu trilioni 7.2 kwa sekunde, ambayo ndiyo ya pili kwa uwezo ulimwenguni. Gazeti Time linasema hivi: “Baada ya kuingiza habari kuhusu hali ya hewa ya dunia kutoka vituo vya angani na baharini kwenye kompyuta hiyo, watafiti wanaweza kuiga hali za dunia, na kuisongeza mbele na kujua kitakachotukia wakati ujao. Tayari wanasayansi wametabiri jinsi halijoto za bahari za ulimwengu zitakavyokuwa miaka 50 ijayo.”

Faida za Kusoma

“Watoto wanaofurahia kusoma wanapopata nafasi, wanafaulu katika masomo yao kuliko wale wanaozaliwa katika familia tajiri na mashuhuri,” lasema gazeti The Independent la London. Uchunguzi wa kimataifa kuhusu tabia za kusoma za watoto wenye umri wa miaka 15 ulionyesha kwamba “kupenda kusoma” na “kusoma mara nyingi” kuna faida kubwa kuliko kuwa na wazazi wenye elimu walio na kazi nzuri. Uchunguzi huo uligundua kwamba “watoto wenye umri wa miaka 15 kutoka familia maskini ambao wanapenda kusoma sana walipata alama nyingi zaidi katika mtihani wa kusoma (wastani wa 540) kuliko watoto wa wataalamu wa hali ya juu ambao hawapendi kusoma (491),” gazeti hilo lilisema. Uchunguzi huo uliohusisha watoto 1,000 ulionyesha kwamba “wasichana wengi husoma ili kujifurahisha kuliko wavulana.” Asilimia 75 ya wasichana walisema kwamba walisoma kitabu fulani katika mwezi uliopita ikilinganishwa na asilimia 55 ya wavulana.

Kimelea Mjanja

Watafiti nchini Brazili wamegundua mbinu ya ujanja ambayo vimelea wanaoambukiza mfumo wa kinga wa wanadamu hutumia kusababisha ugonjwa wa leishmaniasis, laripoti gazeti Folha de S. Paulo la Brazili. Vimelea hao hutumia utaratibu wa mwili ambapo chembe za mwili zisizohitajika au zinazoweza kudhuru humezwa na chembe nyingine zinazoitwa macrophages. Ili wamezwe, vimelea hao huiga ishara fulani ambazo chembe zinazomezwa hutoa mwanzoni mwa utaratibu huo. Wakiwa ndani ya chembe zinazowameza, vimelea hao huanza kuzaana na kuongezeka haraka na kuambukiza chembe nyingine. Matokeo huwa mwasho, kufura kwa wengu na maini, na mara nyingine kifo. Kulingana na gazeti Folha de S. Paulo, watafiti wanatumaini kwamba kugunduliwa kwa mbinu ya vimelea hao kutaleta tiba ya ugonjwa wa leishmaniasis.

Kujikinga na Mbu

“Kuna aina 2,500 za mbu na wanapatikana duniani kote,” lasema gazeti México Desconocido. Ijapokuwa mbu wa kiume na wa kike hunywa maji matamu ya maua, ni mbu wa kike tu ambao huwauma watu na kusababisha malaria, kidingapopo, na kupitisha virusi vya West Nile. Unawezaje kujikinga na mbu? Gazeti hilo linadokeza mambo kadhaa: (1) Epuka kutoka nje jioni na usiku, wakati ambapo kuna mbu wengi. (2) Tumia chandarua, hasa kile ambacho kimetiwa dawa ya mbu. (3) Valia mavazi yasiyobana, soksi, na ikiwezekana, vaa kofia yenye neti kufunika sehemu zote za kichwa. (4) Jipake mafuta yenye dawa ya kufukuza mbu katika sehemu za mwili ambazo hazijafunikwa. (5) Tumia miligramu 300 ya vitamini B1 kila siku. Hiyo hufanya harufu ya jasho la watu wengine kuwafukuza mbu. (6) Katika maeneo yenye majimaji, jipake matope kwenye ngozi yako kama kinga ya dharura. Ukiumwa na mbu, epuka kujikuna usije ukatokwa na damu na kueneza viini. Badala yake, jipake mafuta ya kalamini.