Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Madrid Jiji Kuu Lililojengwa kwa Ajili ya Mfalme

Madrid Jiji Kuu Lililojengwa kwa Ajili ya Mfalme

Madrid Jiji Kuu Lililojengwa kwa Ajili ya Mfalme

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

BAADHI ya majiji makuu ulimwenguni yalijengwa karibu na bandari za kiasili zenye shughuli nyingi ambazo zimetumiwa kwa miaka mingi. Mengine yalijengwa kwenye vivuko vya mito vinavyotumiwa sana na yakasitawi haraka. Majiji mengi makuu ya Ulaya yamekuwa maarufu tangu enzi za Waroma. Lakini Madrid, jiji kuu la Hispania, lilianza kwa njia tofauti. Jiji hilo lilikuwa na wakaaji wanaopungua 10,000 mnamo mwaka wa 1561, wakati ambapo lilipata umaarufu upesi.

Sababu ilikuwa wazi. Philip wa Pili, mfalme wa Hispania mwenye milki kubwa, alikuwa amechoka kuhamisha makao yake ya kifalme kutoka jiji moja hadi jingine katika ufalme wake wa Castile. Kwa kuwa alikuwa mwindaji hodari, alitaka makao yake makuu yawe karibu na maeneo aliyopenda kuwindia. Jiji la Madrid lilikuwa eneo linalofaa kabisa, na lilikuwa na maji safi, nafasi kubwa ya kupanuliwa, hata kulikuwa na mashamba yenye rutuba karibu.

Baada ya uamuzi huo, Philip alianzisha mradi wa ujenzi ili afanye Madrid liwe jiji kuu linalofaa. Baadaye, wafalme Wahispania walilipamba jiji hilo, na likahusianishwa sana na watawala hao. Kufikia karne ya 17, Madrid lilikuwa jiji kubwa zaidi nchini Hispania. Leo Madrid ni jiji la kisasa lililositawi na lina zaidi ya wakaaji milioni tatu.

Kwa kuwa wafalme wa Hispania walipenda sana Madrid, majengo mengi ya kale ya jiji hilo yanahusianishwa na nasaba mbili kuu za wafalme. Sehemu ya kale zaidi ya jiji hilo inaitwa Madrid ya Waaustria, na ilijengwa katika karne ya 16 na 17 wakati wa nasaba ya wafalme wa Austria, au Habsburg. Sehemu zilizojengwa baadaye zinaitwa Madrid ya Nasaba ya Bourbon, ambayo ilianza kutawala katika mwaka wa 1700 na inatawala hadi leo.

Kwa karne nyingi, wafalme wa Hispania waliunga mkono au kugharimia ujenzi wa majengo mengi ya kifahari ya jiji hilo kuu. Michoro mingi yenye thamani ambayo walikusanya ndiyo kivutio kikuu katika jumba la sanaa la kitaifa huko Madrid. Baadaye, shamba kubwa la kifalme lililo katika eneo la Madrid, liligeuzwa kuwa mbuga na bustani kuu za jiji hilo.

Jiji Lenye Bustani Nyingi

Kwa kuwa wafalme hao walipenda sana kuwinda na kupanda bustani, eneo kubwa la mbuga lilikuwa tayari limehifadhiwa wakati jiji la Madrid lilipoanza kupanuka. Ijapokuwa katika miaka ya karibuni kumekuwa na maendeleo ya haraka katika miji, bado kuna sehemu kubwa ya mbuga inayoanza milimani hadi kusini kwenye malango ya katikati ya jiji.

Hapo zamani wafalme waliwinda katika mbuga moja ya Madrid inayoitwa Casa de Campo, ambayo iko karibu na jumba la kifalme. Sasa kuna hifadhi ya wanyama katika mbuga hiyo. Kaskazini mwa Madrid kuna eneo kubwa lenye msitu wa mialoni ambalo linaitwa kilima cha El Pardo. Eneo hilo liko kilometa 10 tu kutoka katikati ya jiji.

Muda mfupi baada ya kufanya Madrid kuwa jiji kuu, Philip wa Pili aliweka mipaka ya hifadhi hiyo ya wanyama. Baba yake alijenga makao yaliyotumiwa wakati wa kuwinda, na bado yanapamba hifadhi hiyo hadi leo. Sasa hifadhi hiyo yenye misitu ndiyo makao ya ndege wawili walio katika hatari kubwa ya kutoweka huko Ulaya, yaani tai wa Hispania wa imperial na tumbusi mweusi wa Ulaya.

Bustani ya Retiro ilikuwa bustani kubwa sana ya kifalme iliyopatikana katikati ya Madrid, ambako familia ya kifalme ilitazama mashindano ya kupigana na fahali na hata vita vya wanajeshi wa majini. Katika karne ya 18, watu wote waliruhusiwa kutembelea bustani hiyo, maadamu wangevalia nadhifu. Lakini sasa hakuna sheria kali kuhusu mavazi, na Madrileños (wakaaji wa Madrid) wengi hutembelea bustani hiyo kila mwisho wa juma. Jumba la kifalme lililojengwa kwa vyuma na vioo, na safu za nguzo zenye umbo la nusu-duara zilizo karibu na ziwa ni kati ya vivutio vya bustani hiyo.

Charles wa Tatu, mfalme aliyeishi katika karne ya 18 ambaye alipendezwa sana na sanaa na sayansi, alianzisha bustani za Royal Botanic Gardens karibu na Bustani ya Retiro. Kwa muda wa karne mbili na nusu zilizopita, mimea mingi ya Amerika ya Kati na ya Kusini imepandwa katika bustani hiyo.

Barabara ya Sanaa

Wafalme wa Hispania walifanya jiji la Madrid liwe pia na mojawapo ya majumba maarufu ya sanaa ulimwenguni. Charles wa Tatu, anayejulikana kuwa meya maarufu wa Madrid, aliamuru Jumba la Makumbusho la Prado lijengwe. Mingi ya michoro inayopatikana huko ni ya wafalme wa Hispania, ambao walianza kuikusanya zaidi ya karne nne zilizopita.

Katika karne ya 17, mchoraji wa mfalme aliyeitwa Velázquez alichora picha na vilevile alisafiri kotekote Ulaya ili anunue picha nyingine kwa ajili ya mfalme Philip wa Nne. Karne iliyofuata, Francisco de Goya akawa mchoraji wa mfalme. Basi haishangazi kwamba Jumba la Prado lina picha nyingi zilizochorwa na wachoraji hao wawili mashuhuri.

Majumba mengine ya sanaa ni kama vile Jumba la Thyssen-Bornemisza na Jumba la Kitaifa la Centro de Arte Reina Sofía, ambayo yako katika barabara moja na Jumba la Prado. Barabara hiyo ya kifahari yenye miti, inayoitwa Barabara ya Sanaa, pia imepambwa kwa sanamu nyingi maarufu za Madrid.

Jiji la Madrid pia limepata vipindi vya heri na shari, kama majiji mengi. Jiji hilo kuu lilizingirwa kwa muda mrefu wakati wa Vita vya Wenyewe kwa Wenyewe vya Hispania (1936-1939), na baadhi ya alama za risasi za vita hivyo zimeonyeshwa kwenye mnara wa ukumbusho wenye umbo la tao unaoitwa Puerta de Alcalá. Hata hivyo, tangu mwanzoni, waanzilishi wa jiji hilo walitaka Madrid liwe na watu wa matabaka mbalimbali ambao wangeishi pamoja kwa amani.

Mkataba wa Madrid, uliofanywa mwaka wa 1202, ulisema kwamba raia hawapaswi kupigana, wala kuwa na bunduki, wala kutumia lugha chafu au matusi. Walipaswa pia kudumisha usafi jijini, kuepuka kuwalaghai raia wenzao, na kutopanga arusi zenye gharama nyingi. Ama kwa hakika, malengo hayo yametimia kwani leo jiji la Madrid ni safi—ingawa siku hizi watu wanapanga arusi zenye gharama nyingi! Wageni wanaotaka vyakula vya bei nafuu wanaweza kula tapa, vidonge vidogo vyenye ladha tamu ambavyo huandaliwa pamoja na kinywaji baridi katika mikahawa mingi.

Katika miaka ya karibuni, jiji la Madrid limepanuka sana. Sasa kuna njia nzuri za usafiri zinazoweza kutumiwa na mamilioni ya watalii wanaotembea huku kila mwaka. Maelfu ya Mashahidi wa Yehova kutoka Hispania na nchi nyinginezo watatembelea jiji hilo katika mwezi wa Julai na Agosti. Mashahidi wanapanga kufanya kusanyiko la kimataifa katika uwanja mmoja mkubwa wa soka huko Madrid. Hivyo, wengi watakaohudhuria watapata nafasi ya kujionea jiji kuu lililojengwa kwa ajili ya mfalme.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24, 25]

MAKAO YA KIFALME

Jumba la Kifalme la Royal. Huenda hilo ndilo jengo lenye fahari zaidi huko Madrid. Jumba hilo lipo mahali ambapo ngome ya Waarabu wa kale ilipokuwa. Jiji la Madrid lilianza kujengwa kuzunguka ngome hiyo. Ingawa mnamo mwaka wa 1931 liliacha kuwa makao ya kifalme, sasa jumba hilo linatumiwa kwa ajili ya shughuli muhimu za serikali. Kuna bustani zilizopandwa kwa mpangilio maalumu kuanzia kwenye jumba hilo hadi kwenye mto ulio chini yake.

Jumba la Kifalme la Aranjuez. Eneo la Aranjuez liko kilometa 50 hivi kusini mwa jiji kuu, karibu na Mto Tagus. Philip wa Pili, aliyeanzisha ujenzi wa jumba hilo la kifalme, alipenda eneo hilo kwa sababu lina udongo wenye rutuba na hali ya hewa ya wastani. Charles wa Tatu alikamilisha ujenzi wa jumba hilo na upandaji wa bustani zake maridadi katika karne ya 18.

El Escorial. Muda mfupi baada ya kufanya Madrid kuwa jiji kuu, Philip wa Pili alianzisha ujenzi wa makao hayo makubwa ya watawa wa kiume pamoja na maktaba, kaburi, na jumba la kifalme. Zaidi ya miaka 20 baada ya ujenzi kukamilika, jumba hilo likawa makao makuu ya milki ya Philip. Lilijengwa mahali patulivu ambapo angeweza kufanya kazi bila kusumbuliwa. Jumba hilo limehifadhi mojawapo ya hati muhimu za kale za Hispania, kutia ndani Biblia kadhaa za Kihispania za zama za kati.

Jumba la Kifalme la El Pardo. Makao hayo ya kifalme yanayotumiwa wakati wa kuwinda yako katika ile hifadhi iliyo karibu na Madrid. Baba ya Philip wa Pili ndiye aliyejenga jengo hilo mara ya kwanza, na ua wake wa ndani pia ulijengwa wakati huo.

Kuna jumba la kifalme la kifahari katika eneo la La Granja de San Ildefonso, lililoko kilometa 80 upande wa kaskazini. Jumba hilo lilijengwa na Philip wa Tano kwa kufuata muundo wa Jumba la Kifalme la Versailles, ambako alikulia. Bustani zake maridadi na mabubujiko ya maji yamezingirwa na milima yenye misitu mikubwa ya misindano.

[Hisani]

Foto: Cortesía del Patrimonio Nacional, Madrid, España

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]

BAADHI YA SEHEMU MAARUFU ZA UKUMBUSHO HUKO MADRID

Plaza Mayor (1). Kwa zaidi ya karne tatu, ua huo umetumiwa kama soko na vilevile kwa ajili ya shughuli mbalimbali za umma, kama vile mashindano ya kupigana na fahali, kutawazwa kwa wafalme, na kuhukumiwa kwa watu waliodhaniwa kuwa waasi. Kuna mchoro katika Jumba la Makumbusho la Prado (2) ambao unaonyesha vizuri ua wa Plaza Mayor wakati wa kesi kubwa ya kuwahukumu waasi, iliyofanywa huko Madrid mwaka wa 1680.

Ofisi za baraza la jiji zipo katika ua maridadi wa kale unaoitwa Plaza de la Villa, ambapo mikutano ya kwanza ya baraza la jiji ilifanyiwa. Ua huo umezungukwa na majengo ya kale, ukionyesha jinsi jiji la Madrid lilivyokuwa katika karne ya 16. Karibu na hapo, mgeni anaweza kuona ua wa Puerta del Sol, ambao ndio ua unaotumiwa zaidi katika jiji hilo. Barabara zote zinazotoka Madrid kuelekea mikoani huanzia kwenye ua huo. Sehemu hizo ziko katika eneo la kale zaidi la jiji hilo.

Madrid lilipopanuka, wafalme wa nasaba ya Bourbon—hasa Charles wa Tatu—walijenga au kufadhili miradi ya ujenzi wa sehemu nyingine za ukumbusho, na mara nyingi walifuata mitindo ya ujenzi ya Ufaransa, mahali walikotoka. Baadhi ya sehemu hizo zinatia ndani Jumba la Kifalme la Royal, Maktaba ya Kitaifa (3), Jumba la Makumbusho la Manispaa (4), Bubujiko la Cybele (5), Bubujiko la Neptune, na Puerta de Alcalá (6).

[Hisani]

Picture 2: MUSEO NACIONAL DEL PRADO; pictures 5 and 6: Godo-Foto