Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hesabu Huwafaidi Watu Wote

Hesabu Huwafaidi Watu Wote

Hesabu Huwafaidi Watu Wote

HESABU haziwasaidii tu wanasayansi bali zinawafaidi watu wote. Wewe hutumia hesabu unaponunua vitu, unaporekebisha nyumba yako, au unaposikiliza utabiri wa hali ya hewa.

Watu wengi huona kwamba hesabu zinawachosha na kwamba haziwasaidii maishani. Je, hayo ndiyo maoni yako? Acheni tuone jinsi hesabu zinavyoweza kutusaidia, jinsi zilivyo rahisi kuelewa, na jinsi tunavyoweza kuzifurahia.

Unaponunua Vitu

Hebu wazia kwamba umeenda dukani kisha ukaona bidhaa iliyopunguzwa bei. Tuseme bidhaa hiyo ilikuwa ikiuzwa kwa dola 35 lakini sasa bei yake imepunguzwa kwa asilimia 25. Lo! Hiyo yaonekana kuwa bei nzuri. Lakini je, unajua bei mpya ya bidhaa hiyo? Utahitaji kutumia hesabu ya arithimetiki. *

Utaanza kwa kuondoa asilimia iliyopunguzwa kutoka kwa asilimia 100, na utapata asilimia 75 (asilimia 100 − asilimia 25 = asilimia 75). Kisha utazidisha bei ya awali kwa asilimia 75 (0.75). Basi, bei ya sasa itakuwa dola 26.25 (35 × 0.75 = 26.25). Kwa kuwa sasa unajua kiasi unachohitaji kulipa, unaweza kuamua ikiwa bei hiyo ni nafuu.

Lakini vipi ikiwa hukubeba kifaa cha kupigia hesabu? Unaweza kufanya hesabu akilini. Kwa mfano, tuseme bidhaa fulani ilikuwa ikiuzwa kwa dola 45 lakini sasa bei yake imepunguzwa kwa asilimia 15. Unaweza kutumia dokezo linalofuata kufanya hesabu akilini. Unapofanya hesabu hiyo anza kwa kutumia asilimia 10. Ili ujue asilimia 10 ya namba yoyote ile, unahitaji kugawanya namba hiyo mara 10. Hilo si jambo gumu. Kisha, kwa kuwa unajua kwamba ukijumlisha 10 na 5 utapata 15, na kwamba nusu ya 10 ni 5, unaweza kujua bei ya bidhaa hiyo haraka kwa kujumlisha na kuondoa. Hebu tujaribu kufanya hivyo.

Kwa kuwa asilimia 10 ya 45 ni 4.50, basi asilimia 5 ya 45 itakuwa nusu ya idadi hiyo, yaani, 2.25. Isitoshe, ili ujue asilimia 15 ya 45 utahitaji kujumlisha namba hizo, na utapata 6.75 (4.50 + 2.25 = 6.75). Mwishowe, utaondoa 6.75 kutoka kwa 45 na utapata bei iliyopunguzwa, yaani dola 38.25 (45 − 6.75 = 38.25). Unaweza kutumia mbinu hiyohiyo kujua ushuru ambao umetozwa kwa ajili ya bidhaa au bakshishi unayohitaji kutoa baada ya kula mkahawani. Lakini wakati huu hutaondoa kiasi ulichopata bali utajumlisha kiasi ulichopata kwa bei ya awali.

Hata hivyo, uwe mwangalifu usije ukakata kauli haraka-haraka unapofanya hesabu akilini. Kwa mfano tuseme kwamba bei ya nguo au ya suruali imepunguzwa kwa asilimia 40 kisha ikapunguzwa tena kwa asilimia 40. Hiyo haimaanishi kwamba bei yake imepunguzwa kwa asilimia 80, bali inamaanisha kwamba imepunguzwa kwa asilimia 64. Asilimia ya pili imekatwa kwenye bei iliyopunguzwa, wala haijaondolewa kwenye bei ya awali. Naam, bado bei imepunguzwa, lakini ni vizuri kujua imepunguzwa kwa kiasi gani.

Hata hivyo, kuna mambo mengine ambayo hayawezi kutatuliwa kwa arithimetiki tu. Lakini, uzuri ni kwamba fani nyingine za hesabu zinaweza kutumiwa.

Kurekebisha Nyumba

Tuseme unahitaji kurekebisha sakafu nyumbani mwako na una kiasi kidogo tu cha pesa. Kabla hujaenda dukani, unapiga hesabu kwanza ili ujue unachohitaji. Unahitaji hasa kuzingatia idadi ya vifaa utakavyohitaji kurekebisha sakafu. Jiometria yaweza kukusaidia.

Vifaa vya kurekebisha sakafu huuzwa hasa kulingana na meta za mraba zinazohitaji kufunikwa. Kwa mfano, eneo la meta moja ya mraba lina urefu wa meta moja na upana wa meta moja. Kabla hujabainisha idadi ya vifaa utakavyohitaji kwa ajili ya sakafu, unapaswa kwanza kujua ukubwa wa sakafu wa kila chumba na ushoroba nyumbani mwako. Ramani zinazoonyesha sakafu za nyumba nyingi huchorwa maumbo ya mraba na ya mstatili. Kwa hiyo, kanuni hii ya hesabu inaweza kukusaidia kufanya hesabu hiyo: ukubwa = urefu × upana (ukubwa unahesabiwa kwa kuzidisha urefu kwa upana). Hiyo ndiyo kanuni ya jiometria inayotumiwa kubainisha ukubwa wa mstatili au mraba.

Ili kuonyesha jinsi kanuni hiyo inavyotumiwa, tuseme unataka kurekebisha sakafu katika vyumba vyote isipokuwa tu jikoni na bafuni. Unapima kila chumba kisha unachora ramani kama ile inayoonyeshwa kwenye ukurasa wa 23. Miraba na mistatili iliyo kwenye ramani hiyo inaonyesha ukubwa wa vyumba na mahali vilipo. Sasa, ukitumia kanuni iliyotajwa juu hebu ona ikiwa unaweza kubainisha idadi ya vifaa utakavyohitaji kurekebisha sakafu. Unaweza kutumia madokezo yafuatayo: Unaweza kupiga hesabu ya ukubwa wa kila chumba kisha ujumlishe idadi ulizopata. Au, unaweza kutumia njia fupi kwa kupiga hesabu ukubwa wa sakafu ya nyumba yote kisha uondoe ukubwa wa sakafu ya jikoni na bafu. *

Neno “jiometria” lina asili ya Kigiriki, nalo linapotafsiriwa moja kwa moja linamaanisha “kupima ardhi.” Jiometria hutia ndani kuchunguza ukubwa, umbali, kiasi cha ujazo, na mambo mbalimbali kuhusu maumbo na mistari. Kanuni mbalimbali za hesabu hutumiwa ili kujua ukubwa wa maumbo mbalimbali. Kila siku, wanasayansi, wahandisi, na wapambaji wa nyumba hutumia kanuni hizo kujua vifaa wanavyohitaji ili kufanya kazi zao. Lakini mbali na arithimetiki na jiometria, kuna fani nyingine za hesabu.

Fanya Hesabu Kila Siku

Fani nyingine za hesabu ni aljebra na kalkulasi. Kwa karne nyingi, hesabu zimetumiwa ulimwenguni pote na wanaume na wanawake wa tamaduni zote na dini zote. Hesabu hujibu maswali magumu ambayo watu hukabili katika sayansi, biashara na shughuli nyinginezo. Iwe unajaribu kuchunguza vitu vilivyopo ulimwenguni au kupanga bajeti ya familia yako, unahitaji kujua kufanya hesabu ili ufanikiwe.

Kwa hiyo, hata ikiwa ulichukia hesabu ulipokuwa shuleni, mbona usijaribu kuzifanya tena? Kama vile watu wanavyojifunza lugha kwa kuizungumza, unahitaji kufanya hesabu ili uzijue. Jaribu kufanya hesabu chache kila siku. Jaribu kujibu maswali ya hesabu na kucheza michezo ya hesabu. Ukipata jibu sahihi, huenda maoni yako kuhusu hesabu yakabadilika. Ama kwa hakika, hilo litakusaidia kuthamini zaidi hekima ya yule Mwanahisabati Mkuu ambaye alibuni dhana hizo za ajabu, Muumba wetu, Yehova Mungu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Yasemekana kwamba arithimetiki (usemi unaotokana na neno la Kigiriki linalomaanisha “namba”) ndiyo fani ya hesabu ambayo imekuwepo kwa muda mrefu zaidi. Arithimetiki ilianza kutumiwa maelfu ya miaka iliyopita. Ilitumiwa na Wababiloni, Wachina, na Wamisri wa kale. Arithimetiki hutusaidia kila siku kuhesabu na kupima vitu vilivyopo duniani.

^ fu. 14 * Jibu = meta 54 za mraba.

[Mchoro katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

⇩ |⇦ meta 3 ⇨|⇦ meta 3 ⇨| |

| | | |

| | | |

| | | |

3 | Jikoni | Chumba cha kulia | Sebule |

meta | | | |

| | | |

| | | |

| | | |

⇧⇩ ------------ ------ ------- |

|

1.5 Ushoroba |

meta |

|

⇩⇧ ----------------------- ----- |

| | | |

| | | |

| | | |

3 | | Bafu | |

meta | Chumba cha kulala | | |

| | | |

| | | |

| | | |

⇧ |⇦ 5 meta ⇦|⇦ 1.5 m ⇨|⇦ 3 meta ⇦|

[Picha katika ukurasa wa 23]

Hesabu zinaweza kukusaidia katika shughuli zako za kila siku