Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Safari Ndefu Zaidi kwa Basi la Umeme

Safari Ndefu Zaidi kwa Basi la Umeme

Safari Ndefu Zaidi kwa Basi la Umeme

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UKRAINIA

Je, waweza kufurahia safari yenye kuvutia sana kwa sarafu chache? Ndiyo, ukikata tikiti ya kusafiri kwa basi la umeme linaloenda masafa marefu zaidi kuliko mabasi mengine ya umeme ulimwenguni. Basi hilo husafiri umbali wa kilometa 95 hivi, kutoka Simferopol, katikati ya Rasi ya Krimea iliyo kusini mwa Ukrainia, hadi mji wa Yalta ulio kwenye ufuo wa kaskazini wenye joto wa Bahari Nyeusi. Mbona usijiunge nasi katika safari hiyo yenye kuvutia?

KWENYE ofisi za kampuni ya usafiri ya Simferopol tunakutana na Slavny Giorgi Mihailovich, ama Bwana Slavnyi kwa ufupi. Amefanya kazi hapo tangu mwaka wa 1959 na anajua kazi yake vizuri sana. Bwana Slavnyi anatupeleka kwenye jumba la makumbusho lenye habari za usafiri ambalo lina picha za wanaume na wanawake waliojenga njia hiyo ya basi la umeme. “Basi la umeme halihitaji tu barabara ya lami,” anaeleza. “Wajenzi walijenga mamia ya minara ya kushikilia nyaya ndefu sana za umeme zinazopita juu. Mafundi walibuni mitambo ya nguvu za umeme.”

Tunamwuliza hivi: “Kwa nini mnatumia mabasi ya umeme kwenye barabara hii ndefu ya milimani badala ya kutumia mabasi ya petroli?”

“Mabasi ya umeme hayachafui mazingira kama mabasi ya petroli,” anajibu. “Tulitaka kuzuia milima na fuo zetu safi zisizichafuliwe.”

Lakini tumamwuliza: “Je, mabasi machache tu yangeweza kuchafua mazingira?”

“Ati mabasi machache!” anasema. “Miaka michache iliyopita mabasi hayo yalipokuwa maarufu sana, basi moja liliondoka baada ya kila dakika mbili hadi tatu katika majira ya kiangazi na yalifunga jumla ya safari 400 kwa siku.”

Tuna hamu ya kuanza safari tukikumbuka mambo hayo.

Safari Yaanza

Tunaanza safari yetu kwenye kituo kikuu cha mabasi cha Simferopol. Nyaya nyingi za umeme zinazoonekana kama nyavu za fedha ziko juu ya barabara. Tunafika kwenye kibanda na kukata tikiti. Kisha tunapanda basi la umeme Na. 52. Na safari inaanza!

Baada ya kusafiri kilometa 29 basi linaanza kupanda kwenye milima. Muda si muda tunafika kwenye uvuli wenye baridi wa milima mirefu sana. Kwenye miteremko mikali ya milima kuna misitu ya misonobari na miti yenye mbao ngumu inayoenea hadi mabonde yenye theluji. Tunapofika kwenye kilele cha mlima tunasisimuka tunapoanza kuteremka milima na kuona mandhari yenye kuvutia sana. Tunaona barabara ndefu yenye kupindapinda mbele yetu. Breki zenye nguvu za basi la umeme zinapunguza mwendo wetu. Dereva wetu anatufikisha kwa usalama!

Tunawasili kwenye mji wa Alushta ulio chini ya mlima, tunageuka mkono wa kulia, na kuelekea kusini kwenye barabara iliyo kandokando ya ufuo. Tunaiona Bahari Nyeusi upande wa kushoto wa basi letu la umeme. Upande wa kulia kuna Milima mikubwa ya Krimea.

Tunaposonga mbele tunaona Mlima wa Dubu karibu tu na kijiji cha Pushkino. Wenyeji wanasimulia hekaya kumhusu dubu mkubwa sana aliyegeuka kuwa jiwe alipojaribu kunywa maji yote ya Bahari Nyeusi. Wanasema kwamba kichwa chake kingali ndani ya maji akiendelea kunywa. Ninajiuliza ‘Kwa nini wana-kijiji hawasemi kwamba dubu alianguka majini kwa sababu alikunywa divai kupindukia? Kwani tumeona mashamba mengi ya zabibu.’ Divai hutengenezwa sana katika eneo hilo na Shamba la Mizabibu la Massandra ambalo limeshinda tuzo katika mashindano ya kimataifa liko huko.

Kisha tunafika kwenye kijiji cha Nikita na kushuka kutoka katika basi kwenye Bustani ya Mimea ya Nikitskyi. Bustani hiyo ina maelfu ya mimea kutoka sehemu zote za ulimwengu. Tunafurahia harufu nzuri ya misonobari mikubwa karibu na mlango tukiongozwa na Tamara aliye na ujuzi mwingi. “Hii ni mierezi ya Lebanoni,” anaeleza. “Sulemani alijenga hekalu lake kwa miti hii mikubwa.” Kiongozi wetu hajakosea, kwa kuwa Biblia inasema kwamba mierezi mingi ilitumiwa katika kazi hiyo kubwa ya ujenzi ambayo ilisimamiwa na Sulemani.—1 Wafalme 5:6-18.

Tunaona vichaka vyenye miiba tunapotembea polepole kwenye vijia vya changarawe. “Hayo ni maua ya waridi,” Tamara anasema. “Bustani hii ina aina 200 za waridi na maua hayo huchanua mwishoni mwa mwezi wa Mei na mapema Juni.” Baadaye tunafika kwenye kichaka kisichovutia sana chenye urefu wa meta mbili na nusu. “Huu ni mti wa chuma,” Tamara anatuambia akiwa amependezwa sana na mti huo. “Mbao zake ngumu zinaweza kutumiwa badala ya chuma na hata zinaweza kutumiwa kama msumari. Hata zinazama majini.” Punde basi la umeme linafika, na tunafurahi kuketi chini tena na kupumzika tunaposafiri hadi Yalta, mwisho wa safari yetu. Wengi hukumbuka Yalta hasa kwa sababu ya mkutano wa kihistoria kuhusu Vita ya Pili ya Ulimwengu uliofanywa kwenye Jumba la Kifalme la Livadia katika mwaka wa 1945. Viongozi wa Mataifa matatu makuu ya Muungano walikutana ili kujadiliana jinsi ya kushambulia na kuishinda Ujerumani ya Nazi.

Safari ya Kurudi

Jioni inaingia, na inatubidi kupanda basi lingine ili turudi nyumbani. Njiani tunawaona watoto wanaouza mashada ya maua mbalimbali. Twashuka kutoka katika basi ili tununue maua, na mara moja tunazingirwa na watoto wenye bidii ya kuuza maua. “Maua yale meupe ni yapi?” ninamwuliza Yana, msichana mwenye umri wa miaka 15 mwenye nywele za rangi ya mchanga. “Snowdrops,” anajibu huku akijivunia maua hayo. “Tunayachuna mapema asubuhi kwenye mteremko mahali ambapo theluji imetoka tu kuyeyuka,” anasema akiashiria kwa kichwa mlima mkubwa ng’ambo ya barabara.

Muda si muda tunapanda basi la umeme tena, na kuendelea na safari yetu hadi mwisho. Kama tu watoto wanaofurahia jambo fulani kwa mara ya kwanza, tuna hamu ya kupanda basi hilo tena.

[Ramani katika ukurasa wa 22, 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

UKRAINIA

KRIMEA

Bahari Nyeusi

SIMFEROPOL

↓ Mlima wa Chatyr-Dag

Alushta

Pushkino

↓ Mlima wa Dubu

Nikita

↓ Massandra

Yalta

Livadia

Mlima wa Ai Petri

Alupka

[Picha katika ukurasa wa 22, 23]

Mlima wa Ai Petri

[Picha katika ukurasa wa 23]

Jumba la Kifalme la Vorontsov, Alupka

[Picha katika ukurasa wa 23]

Pango la Marimari, Mlima wa Chatyr-Dag

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mlima wa Dubu

[Picha katika ukurasa wa 24]

Ngome ya ‘Kiota cha Mbayuwayu,’ Yalta

[Picha katika ukurasa wa 24]

Hifadhi ya chini ya ardhi ya divai ya Massandra, Yalta, yenye chupa za divai ya “sherry” iliyotengenezwa mwaka wa 1775

[Picha katika ukurasa wa 24]

Maporomoko ya Uchansu, Yalta, yenye kina cha meta 90 hivi ambayo ni marefu zaidi huko Krimea

[Picha katika ukurasa wa 24]

Jumba maarufu la Kifalme la kale la Livadia, Yalta