Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Visima vya Ajabu Katika Rasi ya Yucatán

Visima vya Ajabu Katika Rasi ya Yucatán

Visima vya Ajabu Katika Rasi ya Yucatán

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

RASI ya Yucatán ina visima vya kiasili ambavyo ni mojawapo ya maajabu ya kimaumbile yaliyo maridadi zaidi nchini Mexico na katika ulimwengu mzima.

Hivyo ni visima vya aina gani? Jina lake la Kimaya dz’onot, linamaanisha “pango lenye maji,” nalo hutumiwa na wataalamu wanaochunguza mawe kurejelea kisima cha kiasili cha mawe ya chokaa. Rasi ya Yucatán ina mawe ya chokaa yenye vitundu vingi ambavyo vilitobolewa na maji ya mvua yaliyokuwa yanapenya kwenye udongo wa chini. Halafu, katika sehemu ambapo mianya ilitokea, jiwe la chokaa liliporomoka na kufanyiza kisima cha kiasili chenye kina kirefu, chenye maji ya kijani na bluu. Visima vingi vimezungukwa na mimea iliyonawiri vizuri. Baadhi ya visima ni vifupi lakini vingine ni virefu sana. Wataalamu wa mapango na wapiga-mbizi wamejaribu kuchunguza visima hivyo lakini mara nyingi hawajaweza kufikia vina vyake virefu sana.

Wamaya walijenga majiji na vituo vya sherehe kuzunguka visima hivyo, kwa kuwa wangeweza kupata maji kwa urahisi hapo na pia waliviona visima hivyo kuwa makao ya mungu wa mvua aliyeitwa Chac. Visima vingi vya kiasili vinapatikana karibu na magofu yanayojulikana sana ya Chichén Itzá. Kisima kimojawapo kinaitwa Kisima Kitakatifu, au Kisima cha Dhabihu. Wataalamu wa kuchimbua vitu vya kale walipata mifupa ya watu (hasa watoto) na vitu vingine vyenye thamani kama yadi, dhahabu, na shaba nyekundu katika kisima hicho. Vitu hivyo vinathibitisha kuwa hekaya zinazosema kwamba dhabihu za wanadamu na matoleo mengine yalitupwa humo ili kuomba dua kwa mungu wa mvua ni za kweli.

Kisima cha Azul (Kisima cha Bluu) kilicho karibu na Chetumal, Quintana Roo, ni mojawapo ya visima ambavyo hutembelewa sana na watu wengi. Kimezungukwa na mimea mingi na kina rangi ya bluu nzito. Kisima hicho kina ukuta mrefu, na upana wa meta 200 kwa meta 300. Kisima hicho kinakadiriwa kuwa na kina cha meta 90 hivi na kimeunganishwa na Kidimbwi cha Bacalar chenye rangi tofauti-tofauti kupitia mitaro ya chini ya ardhi. Kuogelea katika maji safi ya visima hivyo hupendeza wee!

Mbali na Mexico, visima hivyo vinapatikana nchini Australia, Kuba, Uturuki na sehemu za Ulaya. Mamia ya visima vimegunduliwa katika Rasi ya Yucatán, lakini ni nadra sana kuvipata nje ya eneo hilo. Unakaribishwa utembelee visima hivyo ili ujionee mwenyewe maajabu hayo ya kiasili.

[Ramani katika ukurasa wa 22]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

RASI YA YUCATÁN

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kisima cha X-Keken, Yucatán

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kisima cha Crystal, Quintana Roo

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kidimbwi cha Bacalar na Kisima cha Azul (chini)

[Hisani]

© Michael Friedel-Woodfin Camp and Associates