Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vitu Maridadi Kutoka Ufuoni

Vitu Maridadi Kutoka Ufuoni

Vitu Maridadi Kutoka Ufuoni

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI NIKARAGUA

JE, UMEWAHI kuliona kombe zuri linalometa-meta kwenye mchanga wa ufuoni? Watu wengi, wazee kwa vijana, hupendezwa na makombe kwa sababu ya uzuri wake wa kipekee, na kwa sababu kuna makombe aina nyingi sana.

Makombe yanapatikana kwenye karibu pwani zote za dunia. Hata hivyo, awali, makombe hayo maridadi yalikuwa makao ya viumbe wadogo wenye mwili laini walioyatengeneza. Viumbe hao wanajulikana kama moluska. Imekadiriwa kwamba kuna zaidi ya aina 50,000 za moluska leo!

Makombe yote yanayozungumziwa katika makala hii yanapatikana kwenye Pwani ya Bahari ya Pasifiki huku Nikaragua. Niliokota makombe mengi kwenye sehemu ya pwani iliyo na urefu wa kilometa tatu inayoitwa Poneloya na Las Peñitas. Na makombe mengine nilipewa na wavuvi wa hapo. Tafadhali niruhusu nikueleze kuhusu baadhi ya makombe hayo, pamoja na viumbe wa baharini walioyatengeneza.

Moluska Wakubwa Wenye Kombe Moja

Karibu makombe yote yanatengenezwa na moluska wa aina mbili: Moluska wenye kombe moja na moluska wenye makombe mawili (koambili). Moluska wote wenye kombe moja, kutia ndani aina zote za konokono, wana kichwa ambacho kwa kawaida kina pembe na macho. Moluska hao hutambaa au kuteleza kwa kutumia mguu mmoja ulio mnene na laini.

Moluska hao wenye kombe moja hupumua na kula jinsi gani? Aina nyingi za moluska wanaoishi baharini hupumua kupitia kiungo kinachofanana na mrija kinachotokeza kichwani. Kiungo hicho kinawawezesha kufyonza maji kupitia mashavu yao. Wengine wana kiungo kingine chenye umbo la mrija wanachotumia wanapokula. Isitoshe, baadhi yao wana kitu kinachofanana na utepe kinywani ulio na meno madogo magumu. Moluska hutumia utepe huo wenye meno kurarua chakula chake. Moluska wote wenye kombe moja wana mfumo wa neva, mfumo wa kuzungusha damu, mfumo wa kumeng’enya chakula, na viungo vya uzazi.

Makombe ya moluska wenye kombe moja yana umbo gani? Kwa kawaida yana umbo lenye kujiviringa. Hayo yanatia ndani makombe aina ya murex, tun, kauri, cone, na turritella. Hebu tuchunguze baadhi ya makombe hayo kindani.

Kutengeneza Kombe na Mashimo ya Kufyonzea Chakula

Makombe mengi aina ya murex kutoka sehemu zote za dunia yana maumbo tata. Mimi niliokota makombe aina mbili, kombe maridadi linaloitwa royal murex lenye rangi ya waridi na hudhurungi na root murex. Matuta yao madogo yanatokana na nini? Moluska hutengeneza matuta hayo wakati wa kile kipindi cha kutengeneza kombe polepole. Katikati ya matuta unaweza kuona sehemu zilizotengenezwa wakati wa vile vipindi vya kutengeneza kombe haraka. Kitabu Shells—Treasures of the Sea, kinasema hivi: “Moluska wengi hutumia nguvu nyingi sana wanapotengeneza kombe kwa haraka hivi kwamba wao hupunguza utendaji mwingine ili nguvu zote ziweze kutumiwa kwa ajili ya kutengeneza kombe kwa haraka. Kwa kawaida mnyama huyo hujifukia au kujificha kwa njia nyingine ili asisumbuliwe na wanyama wawindaji. . . . Ikitegemea aina ya moluska, kutengeneza kombe kwa haraka kunaweza kuchukua siku chache hadi majuma kadhaa.”

Moluska aina ya murex ni mwindaji stadi. Nyakati nyingine nilipokuwa nikiokota makombe sikujua ni kwa nini makombe mengine yalikuwa na mashimo madogo yaliyokuwa yametobolewa kwa ustadi sana. Baadaye nilijua kwamba moluska aina ya murex ni mmojawapo wa moluska wanaoweza kutoboa shimo dogo katika kombe la windo lao kwa kutumia meno yaliyoko kwenye utepe wake. Kisha moluska huyo huingiza kiungo chake kinachofanana na mrija katika shimo hilo na kufurahia mlo!

Nilipendezwa kujua kwamba kombe aina ya murex linatajwa katika Biblia isipokuwa halitajwi moja kwa moja. Aina mbili za murex ambazo ni za kawaida katika Bahari ya Mediterania, Murex trunculus na Murex brandaris zilikuwa chanzo cha rangi ghali ya zambarau iliyotumiwa kutia nguo rangi nyakati za Biblia. (Esta 8:15; Luka 16:19) Tezi fulani la moluska wa murex hutokeza umajimaji wa manjano unaobadilika kuwa wa zambarau unapofikiwa na hewa na kuchomwa na jua. Kwa kuwa moluska mmoja hutoa kiasi kidogo sana cha umajimaji huo, imekadiriwa kwamba moluska 12,000 walihitajika kutengeneza gramu moja na nusu ya rangi hiyo. Si ajabu kwamba ni matajiri tu waliokuwa na uwezo wa kununua rangi hiyo iliyoitwa zambarau ya Tiro! *

Makombe “Yanayotabasamu”

Nimeokota pia kombe moja aina ya tun, linaloonekana kama linatabasamu. Makombe aina ya tun yanapatikana kotekote duniani, kwa maana kiluwiluwi wa moluska huyo wanaweza kuelea majini kwa majuma kadhaa au hata kwa miezi kadhaa kabla ya kutua kwenye sakafu ya bahari ili wakue. Ni rahisi kuyaona yale matuta mapana maridadi yanayozingira kombe hilo na vilevile ule ukingo mpana wenye meno kwenye tundu lake, unaofanya kombe hilo lionekane kama linatabasamu. Inadhaniwa kwamba ukingo huo ndio unaomlinda konokono mtamu anayeishi humo ndani asiliwe na kaa wenye njaa.

Pia nina makombe machanga na yaliyokomaa aina ya crown conch, ambalo lina “taji” yenye miiba. Nina kombe moja changa aina ya triton, linaloweza kukua kufikia urefu wa sentimeta 15, na vilevile kombe moja linaloitwa Pleuroploca princeps, ambalo hupendwa hasa kwa sababu ya rangi yake ya machungwa isiyo ya kawaida. Makombe hayo makubwa yanayokua katika vilindi vya maji hayapatikani ufukoni mara nyingi. Nimepewa makombe hayo mazuri na rafiki zangu wavuvi, ambao waliyapata katika nyavu zao au mitego ya kambamti. Wao walibaki na moluska waliokuwa ndani kwa ajili ya chakula na wakanipa makombe hayo maridadi.

Madogo Lakini Yenye Kupendeza

Wakati ambapo maji ya kupwa huacha mstari mrefu wa makombe ufukoni, unaweza kupata makombe mengi madogo ya moluska wenye kombe moja. Mengine yanavutia sana, kama vile kombe aina ya kauri, cone, olive, auger, sundial, turritella, na moon. Kwa kuwa kuna aina nyingi za makombe duniani, watu wengine wanaokusanya makombe hukusanya makombe ya aina moja tu. Kwa mfano kuna aina 500 za makombe ya cone!

Makombe ya moluska wenye kombe moja yanapendeza hasa kwa sababu ya umbo la kujiviringa. Makombe ya aina ya sundial na auger yana umbo hilo maridadi sana. Makombe hayo hayabadiliki umbo yanapokua. Moluska huyo hudumisha umbo la kuviringa la kombe anapolitengeneza kwa kuongezea dutu kwenye ukingo wa kombe kana kwamba anazunguka mhimili usioonekana ulio katikati ya kombe. Kwa njia hiyo moluska huyo hujitengenezea makao imara yanayomfaa na yaliyo maridadi sana!

Chaza, Scallop, na Koambili Wengine

Vipi wale moluska wengine waliotajwa mwanzoni, wale koambili? Makombe yao pia yanapatikana kwa wingi kwenye pwani ya Nikaragua. Makombe hayo yana vipande viwili vilivyounganishwa kwenye upande moja na vinavyofungika vizuri ili kumkinga mnyama aliye ndani. Chaza ni mmojawapo wa koambili anayejulikana sana. Moluska hao hawana kichwa, bali wana vionjio vinavyowawezesha kutambua ladha na harufu majini. Kwa kawaida, koambili huchuja maji ya baharini ili wapate chakula. Wengine wana mguu mwembamba ulio laini ambao wao hutumia kuogelea. Moluska aina ya scallop huogelea kwa kufunga makombe yake mawili kwa nguvu, naye husukumwa nyuma na maji anayorusha. Yeye hurusha maji nyuma anapotaka kuogelea kuelekea mbele. Lakini moluska aina ya scallop anajuaje iwapo adui anamkaribia? Yeye ana mistari miwili ya macho madogo ya samawati inayozunguka mwili wake. Macho hayo yanaweza kuona kivuli cha mnyama mwindaji.

Yaelekea makombe ya moluska aina ya koambili hupendwa hasa kwa sababu ya lulumizi yake. Makombe yanatengenezwa hasa kwa kalisi kaboneti iliyomo katika chumvi ya maji ya baharini. Hata hivyo, lulumizi hutengenezwa kwa aina ya pekee ya kalisi kaboneti inayoitwa aragonite. Moluska fulani hupanga chembe za aragonite kwenye upande wa ndani wa makombe yao sawa tu na jinsi paa linavyoezekewa kwa matofali. Chembe hizo hurudisha mwangaza na hivyo rangi zenye kuvutia za upinde wa mvua huonekana. Aina fulani za koambili hutumia lulumizi kufunika vitu vinavyowachubua, kama vile chembe ya mchanga ambayo imeingia katikati ya makombe. Moluska huongeza tabaka moja baada ya lingine la lulumizi kwenye chembe hiyo linayomchubua na muda si muda chembe hiyo huenda ikawa lulu maridadi yenye thamani.

Kiungo cha Pekee cha Moluska

Kwa kumalizia, nimeamua kuzungumzia sehemu ya kustaajabisha zaidi ya mwili wa moluska, yaani, ule utando ambao kila moluska anao. Ni utando huo kwenye sehemu ya juu ya mwili wa mnyama huyo unaofanyiza kombe. Kitabu Shells—Treasures of the Sea kinasema hivi: ‘Moluska huyo husafirisha [kalisi kaboneti] iliyoyeyuka katika damu yake, nayo hufikia ukingo unaokua wa kombe kupitia vitundu vidogo katika utando.’ Moluska hutoa pia aina fulani ya protini inayofanya kalisi iliyoyeyuka igande inapoguswa na maji.

Wakati uo huo, chembe za rangi katika utando hutia makombe yanayokua rangi na mapambo mbalimbali yenye kupendeza. Wanasayansi wanaochunguza moluska hawaelewi kusudi la rangi na mapambo maridadi ya makombe. Haielekei kwamba rangi na mapambo huwasaidia moluska kutambuana wala kujificha na maadui wake. Hata hivyo, bila shaka rangi nyingi za makombe hao na vilevile mapambo na maumbo yake tofauti-tofauti hutupendeza!

Kwa hiyo, wakati ujao unapotembea kwenye ufuo wenye mchanga kumbuka jambo moja unapookota kombe linalometa-meta. Haidhuru umeokota kombe la aina gani, kumbuka kwamba kombe hilo maridadi awali lilikuwa makao ya kiumbe mdogo mwenye mwili laini anayeitwa moluska.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Kwa habari zaidi, ona kichapo Insight on the Scriptures, Buku la 1, ukurasa wa 661-662, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

[Blabu katika ukurasa wa 26]

Kuna moluska wenye kombe moja na wengine wenye makombe mawili (KOAMBILI)

[Picha katika ukurasa wa 25]

ROOT MUREX

[Picha katika ukurasa wa 25]

ROYAL MUREX

[Picha katika ukurasa wa 25]

TUN “LINALOTABASAMU”

[Picha katika ukurasa wa 26]

KAURI

[Picha katika ukurasa wa 26]

CONE

[Picha katika ukurasa wa 26]

OLIVE

[Picha katika ukurasa wa 26]

AUGER

[Picha katika ukurasa wa 26]

SUNDIAL

[Picha katika ukurasa wa 26]

TURRITELLA

[Picha katika ukurasa wa 26]

MOON

[Picha katika ukurasa wa 26]

PLEUROPLOCA PRINCEPS

[Picha katika ukurasa wa 26]

CROWN CONCH

[Picha katika ukurasa wa 26]

TRITON

[Picha katika ukurasa wa 26]

CHAZA ANAYETENGENEZA LULU

[Picha katika ukurasa wa 27]

CHAZA AINA YA VENUS

[Picha katika ukurasa wa 27]

SCALLOP