Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kusafiri Baharini kwa Meli ya Matete!

Kusafiri Baharini kwa Meli ya Matete!

Kusafiri Baharini kwa Meli ya Matete!

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BOLIVIA

HEBU wazia ukisafiri maelfu ya kilometa baharini. Meli unayosafiria si meli kubwa yenye nguvu iliyo kama hoteli ya kisasa, bali ni meli inayoonekana kuwa dhaifu ambayo imetengenezwa kwa matete yaliyofungwa kwa kamba! Japo meli hiyo ina uzito wa tani 50, je, unaweza kujihisi salama unapofika katikati ya Bahari ya Pasifiki huku mawimbi yenye nguvu yakipigapiga meli hiyo?

Amini usiamini, watu wengi wamefunga safari kama hizo. Ijapokuwa safari nyingi kama hizo hazikufua dafu, jambo moja limebainika—meli hizo zina nguvu sana licha ya kwamba zimeundwa kwa matete. Je, ungependa kuona jinsi meli hizo zinavyoundwa? Ikiwa ndivyo, jiunge nasi tunapotembelea eneo moja linalojulikana sana kwa utengenezaji wa meli hizo.

Kutembelea Ziwa Titicaca

Tunasafiri hadi kwenye Milima ya Andes huko Amerika Kusini na kufika kwenye Ziwa Titicaca. Kati ya maziwa yote yanayotumiwa na waendeshaji wa mashua, Ziwa Titicaca ndilo limeinuka zaidi, likiwa meta 3,810 juu ya usawa wa bahari. Tunapopita kwenye kingo za ziwa hilo, tunaona nyumba za matofali ambazo zimeezekwa mapaa ya nyasi. Nyumba hizo ni za watu wa kabila la Aymara. Baadhi yao ni mafundi stadi wa meli za matete. Tunapokaribia nyumba hizo, tunasalimiwa na wanawake wawili ambao wanashona nguo maridadi za sufu ambazo zinafaa kabisa uwanda huo wenye baridi kali. Wanawake hao wanaacha kushona na kutujulisha kwa waume zao.

Baada ya kutukaribisha kwa uchangamfu, wanaume hao wanatualika twende ziwani kwa mashua yao yenye injini. Tunaposafiri karibu na kingo za ziwa hilo, tunaona matete mengi yanayoitwa totora. Matete hayo yanaweza kufikia urefu wa meta mbili, upana wake hauzidi upana wa penseli, na yanaweza kukunjwa kwa urahisi. Pia, wanaume hao wanatuambia kwamba hayapenywi na maji. Sifa hizo hufanya matete hayo yafae kabisa kutumiwa kutengeneza meli, na ndiyo sababu wajenzi wa meli hizo huvutiwa na Ziwa Titicaca.

Wanaume hao wa kabila la Aymara wanatuonyesha miundo na picha mbalimbali za meli zao na kutuambia hivi huku wakitabasamu: “Meli zetu kadhaa zimesafiri maelfu ya kilometa baharini.” Wao hufikishaje meli hizo baharini? Ikiwa meli si kubwa sana, wao huisafirisha kwa lori hadi kwenye Pwani ya Pasifiki. La sivyo, wanasafirisha vifaa vya kuunda meli hadi pwani kisha wanaiundia meli huko. Kutokana na ustadi wao, mafundi hao wa kabila la Aymara wamewahi kualikwa huko Morocco, Iraq, na Kisiwa cha Easter ili waunde meli kwa kutumia matete yanayopatikana katika maeneo hayo.

Tunajifunza kwamba meli moja inaweza kuundwa kwa matete yenye uzito wa tani nyingi, hasa ikiwa itasafiri mbali sana. Kwa nini? Kwa sababu matete hulowa pole kwa pole. Kwa hiyo ikiwa safari ni ndefu, matete mengi zaidi huhitajiwa na meli inapasa kuwa kubwa zaidi. Kwa mfano, meli yenye uzito wa tani saba hivi inaweza kutumiwa kwa kipindi cha miaka miwili hivi. Lakini tunawauliza wanaume hao hivi, “Meli zilizotengenezwa kwa matete yaliyokauka zinawezaje kustahimili msukosuko unaotokea baharini?”

Chombo Kilichotengenezwa kwa Matete, Kamba, na Mianzi

Meli za matete huwa zenye nguvu kwa sababu zinatengenezwa kwa vifaa imara na hasa kwa sababu zinatengenezwa kwa njia ya kipekee. Mafundi wamewafundisha watoto wao ustadi huo. Mwanamume mmoja aliyetutembeza, ambaye alivalia joho lililo kama blanketi na kofia ya sufu yenye sehemu za kukinga masikio dhidi ya baridi, alitueleza baadhi ya mbinu hizo za kale.

Alitueleza kwamba, kwanza wajenzi hufunga matete hayo katika matita marefu ambayo yanalingana na urefu wa meli itakayotengenezwa. (Ona picha ya 1 na ya 2.) Kisha, wao huunganisha matita kadhaa pamoja ili kufanyiza matita mawili makubwa sana yenye kipenyo cha meta moja au zaidi. Halafu wanayaweka matita hayo pamoja ili kufanyiza kiunzi chenye sehemu mbili. Muundo wa aina hiyo unafaa sana safari za baharini.

Wakati huohuo, wao huweka tita jingine la tatu katikati na chini ya matita hayo mawili makubwa. Tita hilo huwa jembamba kuliko yale matita mengine. Kisha kila moja ya yale matita mawili makubwa hufungwa kwa kamba kwenye tita hilo jembamba. Kamba hiyo huzunguka matita hayo kuanzia mwanzo mpaka mwisho. (Ona picha ya 3.) Wanaume 12 hivi hukaza kamba hiyo. Hivyo, wao huunganisha matete hayo na kufanyiza viunzi viwili imara vilivyounganishwa. (Ona picha ya 4.) Ama kweli, kamba hiyo hukazwa sana hivi kwamba huwezi hata kupenyeza kidole katikati yake na matete hayo. Hiyo huzuia maji yasipenye.

Kiunzi kikiisha kukamilishwa (ona picha ya 5), wanaume hao huongeza mkuku, makasia, milingoti pacha (milingoti hiyo huunganishwa na vile viunzi viwili, nayo huwa na umbo la herufi ya V iliyopinduliwa juu chini), tanga, na kingo za meli, ambazo hutengenezwa kwa matete pia. Mwishowe, wao hutumia mianzi na matawi ya mitende kutengeneza sehemu ya juu ya sitaha ili kuwakinga mabaharia dhidi ya upepo na dhoruba. (Ona picha ya 6.) Lo! Hata chuma kimoja hakitumiwi kutengeneza meli hiyo!

Meli hiyo inaposhushwa majini, matete yaliyo katikati ya ile kamba iliyokazwa kabisa hupanuka, na hilo hufanya kiunzi kiwe imara hata zaidi. Basi, meli inapokamilika inakuwa imara kabisa. Lakini bado kuna swali hili la maana sana, Wale mabaharia wanaofunga safari ndefu kwa meli hizo sahili wanataka kuthibitisha nini?

Kuchunguza Dhana za Uhamaji

Meli za matete za Ziwa Titicaca zinafanana sana na zile meli za matete zenye umbo la mwezi ambazo zinapatikana katika sanaa ya kale ya Misri. Inaonekana kwamba baadhi ya meli hizo za Misri zilikuwa imara sana hivi kwamba huenda zilitumiwa katika safari ndefu za baharini. Je, meli hizo zinafanana tu? Au, je, yawezekana kwamba watu wa Misri na wenyeji wa Ziwa Titicaca walikutana hapo kale? Ijapokuwa ni vigumu kubainisha wakati hususa ambapo meli za matete zilionekana kwa mara ya kwanza huko Amerika Kusini, uthibitisho unadokeza kwamba huenda zilikuwapo hata kabla ya washindi wa Kihispania kuwasili huko.

Dhana zinazohusu uhamaji zimezua ubishi kuhusu uhusiano uliopo kati ya utamaduni wa Amerika Kusini, Mediterania, na Polinesia—hasa kwa sababu maeneo hayo yako mbalimbali. Mvumbuzi mmoja wa kisasa alisema: “Wenyeji wa Peru walifanya biashara kwa ukawaida pamoja na wenyeji wa Panama. Basi, si yawezekana kuwa wenyeji wa Amerika Kusini walifanya biashara pamoja na wenyeji wa Polinesia?”

Si watu wengi wanaounga mkono dhana za yule mvumbuzi wa Norway anayeitwa Thor Heyerdahl. Hata ingawa mabaharia wa leo wanathibitisha kwamba watu wa kale walisafiri mbali sana kwa meli za matete, kama vile Heyerdahl alivyofanya kwa meli ya Ra II iliyotengenezwa na watu wa kabila la Aymara, bado kuna shaka kuhusu jambo hilo. Huenda mambo mengi zaidi yatabainika siku za usoni. Vyovyote iwavyo, meli za matete zinathibitisha kwamba meli zenye nguvu zinaweza kutengenezwa hata kwa vifaa sahili sana.

[Picha katika ukurasa wa 22]

Sehemu mbalimbali za kiunzi

Kabla ya kukaza kamba

Baada ya kukaza kamba

Kingo za meli na sitaha zinaongezwa kwenye kiunzi

[Hisani]

Source of sketches: Dominique Görlitz, www.abora2.com

[Picha katika ukurasa wa 23]

KUUNDA MELI YA MATETE

[Hisani]

Foto: Carmelo Corazón, Coleccion Producciones CIMA

Steps 1, 2, 5, and 6: Tetsuo Mizutani (UNESCO); Step 4: Christian Maury/GAMMA

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

Top: Tetsuo Mizutani (UNESCO)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]

◀ Foto: Carmelo Corazón, Coleccion Producciones CIMA