Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Magari ya zamani na ya kisasa

Magari ya zamani na ya kisasa

 Magari ya zamani na ya kisasa

MWANADAMU amependa kusafiri tangu nyakati za kale. Mwanzoni, alitumia wanyama. Lakini kukawa na uhitaji wa njia bora zaidi za kusafiri. Uvumbuzi wa gurudumu ulikuwa muhimu kwa sababu ulisaidia kuanzishwa kwa vigari na magari yaliyokokotwa na farasi. Hata hivyo, uvumbuzi uliofanywa katika karne ya 19 ulibadili usafiri kwa kiwango ambacho hakingefikiriwa.

Injini Zilizoboreshwa

Katika nusu ya pili ya karne ya 19, Mjerumani Nikolaus August Otto alivumbua injini ya mipigo minne iliyotumia mafuta. Hatimaye injini hiyo ilitumiwa badala ya injini zilizoendeshwa kwa mvuke na umeme. Wajerumani Carl Benz na Gottlieb Daimler walianzisha viwanda vya magari huko Ulaya. Mnamo mwaka wa 1885, Benz aliendesha gari lililokuwa na magurudumu matatu ambalo lilitumia injini ya mipigo miwili, na silinda moja, na lilizunguka mara 250 kwa dakika.  Kuanzia mwaka wa 1872, Daimler aliunda injini za mafuta zilizoshikiliwa kwa uthabiti. Kwa zaidi ya miaka kumi, Daimler na Wilhelm Maybach, waliunda injini ya mwako wa ndani iliyoenda kasi sana ambayo ilitumia mafuta.

Muda si muda, Daimler na Maybach waliunda injini iliyozunguka mara 900 kwa dakika. Baadaye, waliunda injini nyingine na wakaitumia kuendeshea baiskeli kwa mara ya kwanza mnamo Novemba 10, 1885. Katika mwaka wa 1926 makampuni ya Daimler na Benz yaliungana na kuuza magari yao kwa jina Mercedes-Benz. * Kwa kushangaza, wanaume hao wawili hawakuwahi kukutana.

Mnamo mwaka wa 1890, Wafaransa wawili, Emile Levassor na René Panhard, waliunda gari lililoendeshwa kwa magurudumu manne katika kiwanda chao. Gari hilo lilikuwa na mota iliyokuwa katikati. Mwaka uliofuata waliiweka injini upande wa mbele wa gari ili kuizuia isipate vumbi liliposafiri kwenye barabara zisizotiwa lami.

Magari Yapatikana kwa Urahisi Zaidi

Kwa kuwa magari ya kwanza yaligharimu pesa nyingi sana, watu wengi hawakuweza  kuyanunua. Hata hivyo, hali zilibadilika katika mwaka wa 1908, Henry Ford alipoanza kutengeneza magari aina ya Ford T. Magari hayo yalibadili kabisa biashara ya magari. Hayakugharimu pesa nyingi, yalitumiwa kufanya kazi mbalimbali, na yalikuwa rahisi kudumisha. Hata watu waliokuwa na mapato ya kadiri waliweza kuyanunua. * Kulingana na kitabu Great Cars of the 20th Century, magari ya Ford T “yaliwezesha Wamarekani—na hatimaye ulimwengu mzima—kumiliki magari.”

Leo, miaka 100 hivi baadaye, watu wengi wanaona magari yakiwa vifaa muhimu badala ya kuwa chombo cha starehe. Uchunguzi mmoja uliochapishwa katika gazeti la kila siku Independent la London unaonyesha kwamba watu hutumia magari hata kusafiri umbali usiozidi kilometa moja.

Tekinolojia haijaruhusu magari yasafiri kwa mwendo wa kasi zaidi tu bali pia imeyafanya yawe salama zaidi. Kwa kweli, katika miaka ya majuzi misiba ya magari imepunguka katika nchi kadhaa. Watu wengine hujali usalama kuliko kuangalia muundo wanaponunua gari. Kwa mfano, vifaa vya kupunguza vishindo garini huwezesha sehemu inayozunguka kiti cha dereva kubaki ikiwa salama. Mfumo wa kuzuia magurudumu yasiteleze barabarani husaidia kudhibiti  gari wakati kuna unyevunyevu. Mkanda wa usalama uliofungwa katika sehemu tatu hulinda kifua na nyonga, na mifuko ya hewa huzuia kichwa kisijeruhiwe na usukani au ubao wa mita wakati wa msiba. *

Bila shaka ni lazima uendeshe gari vizuri ili uwe salama. “Ni kazi bure kuunda magari yenye vifaa vya usalama ambayo hayaendeshwi vizuri; hata tekinolojia ya hali ya juu zaidi ya usalama haiwezi kutulinda tunapovunja sheria fulani za asili,” lasema gazeti El Economista, la Mexico City.

Magari mengine ya kisasa yana vifaa vingi sana. Mengine yana vinanda vya kuchezea CD, televisheni, simu, na mifumo tofauti ya sauti na ya joto au baridi nyuma na mbele. Pia kuna magari yenye mifumo ya kupokea habari kutoka kwa satelaiti ili kumsaidia dereva atambue barabara inayofaa kufika mahali anapoenda. Mifumo mingine hutoa habari za karibuni zaidi kuhusu matatizo barabarani. Bila shaka vifaa hivyo vya kisasa zaidi na magari ya kisasa yametumiwa na watu wengi kujionyesha katika jamii—jambo ambalo watengenezaji na watangazaji wa magari wametumia kujinufaisha.

Kama vile tumeona tayari, magari yameboreshwa sana tangu yalipoanza kuundwa zaidi ya miaka 100 iliyopita. Yakitumiwa vizuri na kwa usalama, yanaweza kuleta faida nyingi kibiashara na kusafiri kwa starehe.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Mweka-rasilimali mkuu katika kampuni ya Daimler, Emil Jellinek, alidokeza magari hayo yaitwe jina la binti yake, Mercedes. Alihofia kwamba magari hayo hayangenunuliwa na watu wengi nchini Ufaransa, iwapo yangeitwa jina la Kijerumani Daimler.

^ fu. 8 Mwanzoni magari hayo ya Ford T yaligharimu dola za Marekani 850, lakini kufikia mwaka wa 1924 gari jipya aina ya Ford lilinunuliwa kwa dola 260 tu. Uundaji wa magari ya Ford T uliendelea kwa muda wa miaka 19, wakati magari milioni 15 yalitengenezwa.

^ fu. 10 Mifuko ya hewa inaweza kuwa hatari ikitumiwa kama kifaa pekee cha usalama, hasa kwa watoto na watu wazima wenye miili midogo.

[Chati/Picha katika ukurasa wa 22-25]

Miaka inaonyesha wakati gari lilipoundwa

1885 Benz

Gari la kwanza ulimwenguni

1907-1925 Rolls-Royce Silver Ghost

Lilikuwa na nguvu, utulivu, starehe, lenye kutegemeka na lilienda kasi sana

1908-1927 Ford T

Gari la kwanza kuundwa kwa wingi; zaidi ya magari milioni 15 yaliuzwa

Nyuma: Kiwanda cha kuunda magari aina ya Ford

1930-1937 Cadillac V16 7.4-L

Gari la kwanza ulimwenguni na lenye matokeo zaidi kutumia injini yenye silinda 16

1939 hadi leo Volkswagen Beetle

Zaidi ya magari milioni 20 yameundwa. Gari jipya aina ya Beetle (chini kushoto) lilitolewa katika mwaka wa 1998

1941 hadi leo Jeep

Huenda ndilo gari lenye fahari zaidi ulimwenguni

1948-1965 Porsche 356

Lina muundo wa Volkswagen Beetle; na lilipendwa sana

1952-1957 Mercedes-Benz 300SL

Lililoitwa kwa jina la utani Gullwing, lilikuwa gari la kwanza lililoundwa kwa alumini na lenye injini ya mdungo

1955-1968 Citroën DS 19

Lilikuwa na breki zilizotumia mafuta, gia nne, na springi zinazofyonza vishindo bila kupoteza usawaziko

1959 hadi leo Mini

Gari hili lenye madoido mengi lililopendwa sana na lililoshinda mara nyingi katika mashindano

1962-1964 Ferrari 250 GTO

Lenye injini yenye nguvu-farasi 300 ya muundo wa V-12, maarufu sana kwenye mashindano

1970-1973 Datsun 240Z

Lilikuwa gari la mashindano lenye bei nafuu na lenye kutegemeka

1970 hadi leo Range Rover

Linaonwa kuwa gari bora zaidi ulimwenguni linaloendeshwa kwa magurudumu manne kwenye barabara mbaya

1984 hadi leo Chrysler Minivan

Lilipendwa na watu wengi

Thrust SSC

Mnamo Oktoba 15, 1997, liliweka rekodi rasmi ya kusafiri mwendo wa kasi zaidi wa kilometa 1228 kwa saa, lilipovuka jangwa la Black Rock, huko Nevada, Marekani

[Hisani]

Benz-Motorcar: DaimlerChrysler Classic; background: Brown Brothers; Model T: Courtesy of VIP Classics; Rolls-Royce: Photo courtesy of Rolls-Royce & Bentley Motor Cars

Jeep: Courtesy of DaimlerChrysler Corporation; black Beetle: Courtesy Vintage Motors of Sarasota; yellow Beetle: VW Volkswagen AG

Citroën: © CITROËN COMMUNICATION; Mercedes Benz: PRNewsFoto

Chrysler Minivan: Courtesy of DaimlerChrysler Corporation; Datsun: Nissan North America; Thrust SSC: AP Photo/Dusan Vranic