Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mambo Unayohitaji Kujua Kuhusu Krismasi

Mambo Unayohitaji Kujua Kuhusu Krismasi

Maoni ya Biblia

Mambo Unayohitaji Kujua Kuhusu Krismasi

MAMILIONI ya watu duniani kote wanajitayarisha kusherehekea Krismasi ya mwaka wa 2002. Huenda ukawa mmoja wao. Au, pengine hujazoea kushiriki desturi za kidini za sherehe hiyo maarufu. Vyovyote vile, yaelekea kwa hakika utaathiriwa na sherehe ya Krismasi. Sherehe hiyo huathiri biashara na vitumbuizo, hata katika nchi zisizo za Kikristo.

Ni mambo gani unayojua kuhusu Krismasi? Je, Biblia inaunga mkono kusherehekea kuzaliwa kwa Kristo? Ni mambo gani yanayohusika katika sherehe hiyo inayofanywa Desemba 25 kila mwaka?

Krismasi Yapigwa Marufuku

Ukitumia wakati kuchunguza kuhusu Krismasi, utagundua kwamba sherehe hiyo haitokani na Ukristo wa kweli. Wasomi wengi wa Biblia kutoka dini mbalimbali wanakubali jambo hilo. Ukiwa na jambo hilo akilini, huenda usishangae kujua kwamba katika mwaka wa 1647, Bunge la Cromwell huko Uingereza liliamua kwamba Krismasi ingekuwa siku ya kutubu. Halafu katika mwaka wa 1652 bunge hilo likapiga marufuku Krismasi. Kwa sababu hiyo bunge lilikutana katika Desemba 25 kila mwaka kuanzia mwaka wa 1644 hadi 1656. Kulingana na mwanahistoria Penne L. Restad, “viongozi wa kidini waliohubiri kuhusu kuzaliwa kwa Yesu walijua kwamba wangeweza kufungwa gerezani. Wafanya-kazi wa kanisa walitozwa faini kwa kutia madoido makanisani mwao. Kisheria, maduka yalipaswa kufunguliwa kama wakati mwingine wowote wa kazi.” Kwa nini hatua hizo kabambe zilichukuliwa? Wanamapinduzi wa kidini waliamini kwamba kanisa halikupaswa kubuni mapokeo ambayo hayakuwa katika Maandiko. Wao walihubiri kwa bidii na kutawanya vichapo vilivyopinga sherehe za Krismasi.

Mitazamo kama hiyo ilionekana pia huko Amerika Kaskazini. Katikati ya mwaka wa 1659 na 1681, Krismasi ilipigwa marufuku katika Koloni la Ghuba ya Massachusetts. * Sheria iliyotungwa wakati huo ilipiga marufuku kusherehekea Krismasi kwa njia yoyote. Watu waliovunja sheria hiyo walitozwa faini. Mbali na Wanamapinduzi wa New England, makundi mengine katika makoloni ya kati yalipinga pia sherehe za Krismasi. Wafuasi wa Dini ya Quakers huko Pennsylvania walishikilia mtazamo mkali kama ule wa Wanamapinduzi kuhusu sherehe hiyo. Chanzo kimoja chasema kwamba “punde tu baada ya Waamerika kunyakua uhuru wao, mfuasi wa Dini ya Quakers, Elizabeth Drinker aliwaorodhesha watu wa Philadelphia katika makundi matatu. Kikundi kimoja cha Quakers ‘kiliona [Krismasi] ikiwa siku ya kawaida tu,’ kikundi kingine kilisherehekea kwa sababu za kidini, na wale waliobaki ‘walitumia siku hiyo kufanya maandamano na kisha wakatawanyika.’”

Kiongozi maarufu wa kidini Mwamerika, Henry Ward Beecher, aliyezaliwa katika familia ya wafuasi wa Calvin wa Othodoksi, hakujua mambo mengi kuhusu Krismasi hadi alipokuwa mwenye umri wa miaka 30. “Kusherehekea Krismasi kulikuwa jambo geni kwangu,” aliandika Beecher katika mwaka wa 1874.

Makanisa ya mapema ya Baptisti na Congregationalist pia hayakupata sababu za Kimaandiko za kusherehekea kuzaliwa kwa Kristo. Kitabu kimoja chasema kwamba Kanisa la Baptisti la Newport [katika Kisiwa cha Rhode] lilisherehekea Krismasi kwa mara ya kwanza mnamo Desemba 25, 1772. Hiyo ilikuwa miaka 130 hivi baada ya kuanzishwa kwa kanisa la Baptisti huko New England.

Chanzo cha Krismasi

Kichapo New Catholic Encyclopedia husema: “Tarehe ya kuzaliwa kwa Kristo haijulikani. Vitabu vya injili havitaji siku wala mwezi . . . Kulingana na makadirio ya H. Usener ambayo yamekubaliwa na wasomi wengi leo, siku ya kuzaliwa kwa Kristo ilitokana na tarehe ya kuisha kwa msimu wa jua wakati wa majira ya baridi kali (Desemba 25 kulingana na Kalenda ya Julian, na Januari 6 kulingana na Kalenda ya Misri), kwa sababu siku hiyo jua lilianza kurudi kaskazini, waabudu wapagani wa mungu aitwaye Mithra walisherehekea dies natalis Solis Invicti (siku ya kuzaliwa kwa jua lisiloweza kushindwa). Mnamo Desemba 25, 274, Aurelian alimtaja mungu-jua kuwa mlinzi mkuu wa milki na akaweka wakfu hekalu huko Campus Martius kwa ajili yake. Krismasi ilianza wakati madhehebu ya kuabudu jua yalipopata nguvu nyingi huko Roma.”

Kichapo Cyclopœdia cha M’Clintock na Strong chasema: “Mungu hakuamuru watu washerehekee Krismasi, wala sherehe hizo hazitokani na A[gano] J[ipya]. Siku ya kuzaliwa kwa Kristo haiwezi kuthibitishwa kwa kutumia A[gano] J[ipya] wala kwa chanzo kingine chochote.”

Ni “Udanganyo Mtupu”

Kwa kuzingatia mambo yaliyotajwa, je, Wakristo wa kweli wanapaswa kushiriki desturi za Krismasi? Je, sisi humpendeza Mungu tunapochanganya ibada yake na itikadi na desturi za watu wasiomwabudu? Mtume Paulo alionya hivi katika Wakolosai 2:8: “Jihadharini: labda huenda kukawa na mtu fulani ambaye atawachukua nyinyi kama windo lake kupitia falsafa na udanganyo mtupu kulingana na mapokeo ya wanadamu, kulingana na mambo ya msingi ya ulimwengu na si kulingana na Kristo.”

Pia mtume huyo aliandika: “Msiwe wenye kufungwa nira isiyosawazika pamoja na wasio waamini. Kwa maana uadilifu na uasi-sheria vina ushirika gani? Au nuru ina ushiriki gani na giza? Na zaidi, kuna upatano gani kati ya Kristo na Beliali [Shetani]? Au mtu mwaminifu ana fungu gani na asiye mwamini?”—2 Wakorintho 6:14, 15.

Kwa kuzingatia ushuhuda huo usiokanushika, Mashahidi wa Yehova hawasherehekei Krismasi. Kwa kupatana na Maandiko, wao hujitahidi kutoa “ibada iliyo safi na isiyo na unajisi kwa maoni ya Mungu wetu,” kwa kujitunza “bila doa kutokana na ulimwengu.”—Yakobo 1:27.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Koloni la Ghuba ya Massachusetts lilibuniwa katika mwaka wa 1628 na mojawapo ya makundi ya Kiprotestanti yaliyopingana nchini Uingereza, na lilikuwa koloni kubwa na lenye ufanisi zaidi katika makazi ya mapema ya New England.

[Blabu katika ukurasa wa 16]

Bunge la Uingereza lilipiga marufuku Krismasi katika mwaka wa 1652

[Blabu katika ukurasa wa 17]

“Kusherehekea Krismasi kulikuwa jambo geni kwangu”—KIONGOZI WA KIDINI MWAMERIKA, HENRY WARD BEECHER

[Picha katika ukurasa wa 17]

Waabudu wapagani wa Mithra na wa mungu-jua (kwenye sanamu) walisherehekea Desemba 25

[Hisani]

Musée du Louvre, Paris