Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Melesi wa Uingereza Mkuu wa Msituni

Melesi wa Uingereza Mkuu wa Msituni

Melesi wa Uingereza Mkuu wa Msituni

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

KIMYA kilichokuwapo msituni kilikatizwa na wimbo wa ndege aina ya blackbird. Jua lilipokuwa likitua, niliketi juu ya gogo la mbetula lenye rangi ya fedha, nikifurahia harufu ya mimea iliyolowa maji ya mvua.

Niliketi mahali palipokuwa na upepo kwa sababu nilitaka kuwatazama melesi. Melesi ni mnyama mwenye macho madogo na masikio madogo yenye ncha nyeupe. Hata hivyo, ana uwezo mkubwa wa kusikia na kunusa. Kwa hiyo, iwapo angesikia sauti au kuhisi harufu yangu, hangetoka shimoni usiku huo.

Melesi wa Ulaya ni mkubwa, haonekani sana, ana urefu wa meta moja hivi na kimo cha sentimeta 30, na ana uzani wa kilogramu 12 hivi. Ana manyoya ya kijivu yasiyo laini, uso na sehemu zake za chini ni nyeusi, ana miguu mifupi myeusi, na mkia mfupi mnene wa rangi ya kijivu. Ana kucha tano kali kwenye kila mguu.

Melesi ana mistari mitatu myeupe mipana inayoonekana wazi kuanzia puani mwake hadi nyuma ya masikio. Mistari hiyo pia imezusha mjadala. Watu fulani husema kwamba melesi huitumia kutambuana wakati wa giza—ingawa twajua kwamba wao hutambuana kwa harufu. Kwa vyovyote vile, mistari hiyo humfanya awe maridadi.

Melesi hupatikana sana katika sehemu za mashambani huko Uingereza. Kwa kuwa melesi ni mchimbaji hodari, yeye huchimba mitaro, vijia vya ardhini, na mashimo ili aishi humo. Baadhi ya mapango yana kipenyo cha meta 30, na vijia vyote vikijumlishwa vinaweza kufikia umbali wa meta 300! Melesi hutoka shimoni usiku na kulala mchana. Melesi wa kike huzaa katika mashimo yenye matandiko ya majani.

Mashimo huwa na milango mingi ya kuingilia ambayo huwa mahali palipo wazi na mara nyingi karibu na aina fulani ya miti ya mibetula au katika kichaka cha miti ya hawthorn au mikwamba. Baadhi ya mapango huko Uingereza yana zaidi ya milango 50. Mapango hayo yamekuwapo kwa zaidi ya miaka 150 na vizazi kadhaa vya melesi vinaweza kuishi humo. Kwa kawaida melesi huishi kwa miaka 2 hadi 3, lakini wanaweza pia kuishi kwa miaka 15 au hata zaidi.

Si vigumu kutambua pango la melesi kwa sababu mlangoni huwa pana udongo mwingi uliorundikwa, na mawe na vitu vingine ambavyo vimeondolewa shimoni. Unaweza kutambua jinsi alivyo mnyama mwenye nguvu ukiona vitu ambavyo ameondoa shimoni.

Unaweza kujuaje kwamba melesi wamo ndani ya shimo? Kwanza chunguza uone kama kuna mashimo yenye ukubwa wa sentimeta 15 hadi 23 na kina cha sentimeta 23 yanayozunguka mapango na ambayo melesi huyatumia kama choo. Ukiona kinyesi, hasa ikiwa hakijakauka, basi melesi wamo shimoni. Pia chunguza uone kama vijia vimekanyagwa-kanyagwa, na ikiwa ni miezi ya kiangazi chunguza ikiwa mimea imeangushwa chini. Ikiwa kuna matope, tafuta nyayo za melesi, au ikiwa mashimo yako karibu na miti angalia uone kama miti hiyo imetiwa matope au kukwaruzwa kwa kucha kali. Pango likiwa kubwa, huenda ikawa vigumu kuwaona melesi, kwa sababu wanaweza kuingia na kutokea milango tofauti. Kwa hiyo, amka mapema, na uweke vijiti juu ya kila shimo. Asubuhi inayofuata, utajua milango waliyotokea kwa sababu vijiti vitakuwa vimesukumwa kando ya mashimo hayo.

Melesi husafiri mbali sana wakati wa usiku akitafuta mbegu za mialoni au miti inayofanana na mifune, au akinusa na kufukua sungura wachanga ama kuchakura-chakura ndani ya masega ya nyigu akitafuta mabuu. Melesi hula nini sanasana? Minyoo! Yeye hula karibu kila kitu kutia ndani matunda ya msituni, matunda yenye maua kama kengele, uyoga, na mbawakavu. Usiku mmoja wa Julai kulipokuwa na mvua nyingi, melesi hawakuenda mbali na mapango yao kwa sababu walipata mlo mtamu kwa wingi, yaani, konokono weusi walioletwa na mvua kutoka eneo la juu lenye nyasi.

Kwa kawaida, melesi hujamiiana katika mwezi wa Julai na kuzaa watoto wanne au watano katika mwezi wa Februari. Melesi wachanga wenye umri wa miezi mitatu hivi hutoka pangoni na kuchezea karibu na mlango. Wachanga hao wanapokuwa nje, melesi wa kiume na wa kike hubadilisha matandiko. Melesi hudumisha usafi wa hali ya juu katika makao yao. Kwa kawaida wao huanika matandiko yao katika majira ya kuchipua na ya kupukutika kwa majani, lakini wanaweza kufanya hivyo wakati mwingine wowote wa mwaka. Wazazi hutoa nyasi kavu na matandiko mengine, na kuweka mapya—wakikusanya karibu matita 30 usiku mmoja. Matita hushikiliwa kati ya kidevu na miguu ya mbele na kukokotwa kinyume-nyume mpaka mlangoni.

Melesi hutoa umajimaji wenye harufu kali kutoka sehemu iliyo chini ya mkia wake na kuumwagilia nyasi, mawe, au vigingi ili kutia alama mpaka wa eneo lake. Wao hata hutiana alama ili kutambuana. Kwa kutumia alama hizo za harufu, melesi hutambua mapango yao kwa urahisi wanaporudi nyumbani.

Wimbo wa blackbird ulififia, na msitu ukawa kimya na wenye giza. Nilinyamaza kimya, hadi nilipomwona melesi mmoja akitoa kichwa chake cheupe na cheusi. Kwa muda, alisimama mlangoni mwa pango akichunguza kama kuna hatari yoyote kabla ya kutoka nje gizani—kama bwana-mkubwa wa shamba akizuru shamba lake.

[Picha katika ukurasa wa 12, 13]

Pango la kuzalia

Pango la kulala

Matandiko

[Picha katika ukurasa wa 13]

Melesi wachanga

[Picha katika ukurasa wa 13]

Chakula cha melesi ni mbegu, uyoga, na minyoo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

Badger photos: © Steve Jackson, www.badgers.org.uk