Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Tulivyoponyoka Mlipuko wa Volkano Wenye Kuogofya!

Jinsi Tulivyoponyoka Mlipuko wa Volkano Wenye Kuogofya!

Jinsi Tulivyoponyoka Mlipuko wa Volkano Wenye Kuogofya!

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KONGO (KINSHASA)

LEO ni Jumanne, Januari 15, 2002—siku inayoonekana kuwa ya kawaida kabisa huku Afrika ya Kati. Tumewasili Goma, katika eneo la Kivu, Kongo (Kinshasa) pamoja na Shahidi mwingine wa Yehova, tukiwa na kusudi la kukutana na Mashahidi wengine kutoka eneo la Maziwa Makuu.

Je, Kuna Shida?

Ingawa mlima wa volkano wa Nyiragongo (wenye urefu wa meta 3,470) uko kilometa 19 tu kutoka jiji la Goma, unatustaajabisha kweli. * Unanguruma na tunaona ukitoa moshi. Wakazi wa hapa hawajali kwa kuwa hali hiyo ni ya kawaida wakati huu wa mwaka.

lasiri hii tunahudhuria mikutano ya makutaniko mawili ya Mashahidi wa Yehova. Bado kuna matetemeko ya ardhi na ngurumo. Lakini hayo hayawashangazi watu hata kidogo. Maafisa wa serikali za mitaa wanawahakikishia watu kwamba hali iko shwari. Ingawa kwa miezi mingi mtaalamu wa volkano huku Kongo amekuwa akisema kwamba kutakuwa na milipuko ya volkano, hakuna mtu anayemwamini. Rafiki yangu asema kwa mzaha: “Leo jioni anga litakuwa jekundu kwa sababu ya utendaji katika mlima wa volkano.”

“Ni Lazima Tukimbie Haraka!”

Tunaporudi mahali petu pa kulala, tunahimizwa hivi: “Ni lazima tukimbie haraka!” Kuna hatari kubwa. Jiji linakabili afa kubwa. Mambo yamebadilika ghafla! Mapema tulikuwa tunazungumza kuhusu kufanya jiji la Goma kuwa kitovu cha kazi ya kuhubiri. Lakini sasa, wakati wa jioni, tunaambiwa kwamba ni lazima tukimbie, kwani jiji linakabili hatari ya kuharibiwa!

Usiku unapokaribia, anga linakuwa jekundu kama moto—kwa sababu fulani. Lava kutoka Mlima Nyiragongo inatiririka kuelekea jijini. Kama chungu kinachochemka na kumwaga kilichomo, lava kutoka mlimani inaharibu kila kitu kilicho njiani. Tunapakia masanduku yetu upesi! Inakaribia saa 1:00 jioni.

Maelfu ya Watu Barabarani

Tunaharakisha kutoroka, lakini barabara inayotoka Goma imejaa watu wanaokimbia ili waokoe uhai wao. Wengi wanatembea huku wakibeba vitu vichache walivyoweza kuchukua. Wengi wamebeba mizigo kichwani. Wengine wamefinyana kwenye magari. Wote wanaelekea kwenye mpaka wa Rwanda ulio karibu. Hata hivyo, volkano haitambui mipaka iliyowekwa na wanadamu. Hakuna majeshi yanayoweza kuisimamisha! Tunawaona wanajeshi wenye hofu pia wakikimbia ili waokoe uhai wao. Magari hayawezi kusonga mbele. Tunalazimika kutembea kwa miguu. Tumo miongoni mwa watu hawa 300,000—wanaume, wanawake, vijana, na watoto wachanga—wote wanakimbia mlipuko wa volkano. Ardhi inanguruma na kutetemeka.

Kila mtu anakimbia ili aokoe uhai wake. Mimi na rafiki yangu ni wageni kutoka jiji kubwa, lakini tuko miongoni mwa watu, tukiwa na Mashahidi wachache wanaoandamana nasi ili watusaidie. Kuwapo kwao na kutuhangaikia ni mambo yanayogusa mioyo yetu na kutufanya tuhisi salama katika hali hii ngumu na yenye kutaabisha. Watu wanatoroka wakibeba vitu walivyoweza kuchukua—mavazi, vyungu na sufuria, na chakula kidogo. Umati wa watu unasukumana. Wengine wanagongwa na magari yanapojaribu kupita na kuangusha mizigo ambayo inakanyagwa-kanyagwa chini. Ole kwake anayeanguka. Watu wana wasiwasi mwingi. Kila mtu amejawa na hofu. Tunajaribu kufika mji wa Gisenyi ulio kilometa chache kutoka mpaka wa Rwanda. Tunaendelea na matembezi yetu yasiyo ya hiari.

Tunawasili Usiku Tukiwa Salama

Tunafika hotelini, lakini kama vile huenda ukawazia, hakuna nafasi zaidi ya kulala. Ni lazima turidhike kuketi tukiwa tumezunguka meza iliyo bustanini hata ingawa tumechoka sana baada ya kutembea kwa muda wa saa tatu na nusu. Tunafurahi kutoka katika eneo la hatari na kuwa hai, tukiwa na ndugu zetu Wakristo ambao wamesafiri pamoja nasi. Tunafurahi hakuna Shahidi aliyekufa.

Itatubidi tulale nje leo. Kutoka hapa tunaweza kuona anga jekundu la jiji la Goma. Linaonekana maridadi na lenye kupendeza wee! Mchana unafika hatimaye. Ngurumo na matetemeko yameendelea usiku kucha. Tunapokumbuka matukio ya jana, hatuna budi kusikitikia maelfu ya jamaa zilizolazimika kukimbia pamoja na watoto wao.

Msaada Waja Haraka

Mashahidi kutoka Kigali, mji mkuu wa Rwanda, wanajiunga nasi Ijumaa adhuhuri, Januari 18. Halmashauri ya kutoa msaada iliyofanyizwa na ndugu kutoka Goma na Gisenyi inaanza kazi. Jambo la kwanza ni kuwaandalia wakimbizi Mashahidi mahali pa kukaa katika Majumba sita ya Ufalme yaliyo katika eneo hili. Hilo lafanywa siku iyo hiyo. Ishara iliyoandikwa katika Kifaransa na Kiswahili inawekwa kando ya barabara, kuonyesha njia ya kuingia Jumba la Ufalme, ambapo wakimbizi wanaweza kupata msaada na faraja. Pia, siku iyo hiyo, tani tatu za bidhaa za kutosheleza mahitaji ya msingi zawasili katika Majumba ya Ufalme ambapo Mashahidi wanakaa. Siku inayofuata, Jumamosi, lori lililojaa chakula, mablanketi, makaratasi ya plastiki, sabuni, na dawa lawasili kutoka Kigali.

Wasiwasi Waongezeka

Hata hivyo, bado kuna mambo mengi ya kuhangaikia. Mahitaji ya watu wote hawa yatatoshelezwaje? Vipi juu ya volkano? Mlima utakoma kulipuka lini? Jiji la Goma limeharibiwa kiasi gani? Habari zinazoendelea kupokewa na matetemeko ya ardhi yanayoendelea yanazidi kuongeza wasiwasi. Wataalamu wanahofia kuwa kiasi kikubwa cha gesi ya salfa-dayoksaidi kitachafua hewa. Pia inahofiwa kuwa maji ya Ziwa Kivu yatachafuliwa na kemikali.

Saa 48 baada ya mlipuko, habari zenye kutia wasiwasi zimeenea sana. Halafu, Jumamosi alasiri tunasikia kwamba watu 10,000 hivi, kutia ndani Mashahidi 8 na mtoto, wamezingirwa na lava. Katika maeneo fulani, lava imefunika ardhi kufikia kina cha meta mbili. Hewa imejaa gesi zenye sumu. Tunahofia usalama wao. Hali inasikitisha. Karibu kanisa lote la Goma limeharibiwa na lava inayoendelea kutiririka. Kufikia sasa hakuna mtu anayedhani kwamba jiji la Goma litabaki.

Habari Njema

Jumamosi saa 3:00 asubuhi, mmoja wa akina ndugu ambao wamezingirwa na lava anatupigia simu. Anasema kwamba hali inabadilika. Hali inakuwa bora. Mvua inanyesha, lava inaanza kupoa, na hewa inakuwa safi. Ingawa bado lava ni moto na ni hatari, watu wanaanza kuvuka wakiingia katika maeneo yaliyo salama zaidi. Jiji halijaharibiwa lote.

Hizo ndizo habari njema za kwanza tangu matukio hayo mabaya yaanze. Inaonekana utendaji wa volkano umepungua. Wataalamu waliopo wanatoa habari zenye kupingana. Tunawasiliana na jiji jirani la Bukavu, lililoko upande ule mwingine wa Ziwa Kivu. Tunaambiwa kwamba jamaa tano za Mashahidi, na watoto watatu wasio na wazazi wao, wamewasili Bukavu kwa mashua. Mashahidi walio katika jiji hilo watawashughulikia.

Twaweza Kurudi!

Jumatatu, Januari 21, tunawatia moyo na kuwafariji akina ndugu huko Gisenyi, na pia kujua mahitaji yao. Tunaambiwa kwamba ndugu wanaoishi kwa muda katika yale Majumba sita ya Ufalme wanaendelea vyema. Tunafahamishwa idadi hususa ya wale waliokimbia—watu 1,800 kutia ndani watoto.

Vipi kuhusu wakati ujao? Serikali za mitaa zinapanga kuandaa kambi za wakimbizi haraka. Hata hivyo, watu bado wanakumbuka mambo mabaya kuhusu kambi za wakimbizi zilizokuwapo mwaka wa 1994 baada ya yale mauaji ya kikabila. Tunaamua kurudi Goma, na inapokaribia adhuhuri tunawasili huko. Karibu asilimia 25 ya jiji hilo limeharibiwa. Tunaweza kutembea juu ya lava inayokauka iliyotiririka katika barabara za jiji. Bado ina joto, na inatoa gesi. Watu wengi wameamua kurudi jijini.

Saa 7:00 adhuhuri, tunakutana na wazee Wakristo 33 katika Jumba la Ufalme la Kutaniko la Goma ya Kati. Wote wanakubaliana: Wanaamua kurudi Goma. “Huko ndiko nyumbani,” wanasema. Vipi kuhusu hatari ya kutokea kwa mlipuko mwingine? “Tumezoea hali hiyo,” wanajibu. Wanahofu kwamba wasiporudi haraka mali zao zitaporwa. Siku inayofuata familia zote za Mashahidi zilizokimbia zinarudi Goma. Wengi kati ya watu 300,000 waliovuka mpaka wamerudi katika jiji hilo lililoharibiwa.

Juma Moja Baadaye

Mambo yanaendelea tena kama kawaida jijini. Inaonekana, jiji litaokoka. Baada ya muda mfupi kazi ya kutandaza lava inaanza ili kuunganisha tena sehemu mbili za jiji zilizotenganishwa. Kila kitu kilichokuwa katika njia ya lava kiliharibiwa. Maeneo ya biashara na ya usimamizi wa jiji yaliharibiwa kabisa. Inakadiriwa kuwa thuluthi moja ya njia ya ndege katika uwanja wa ndege iliharibiwa.

Hesabu sahihi inaonyesha kwamba familia 180 za Mashahidi ni miongoni mwa zile zilizopoteza kila kitu na hazina mahali pa kuishi. Halmashauri ya kutoa misaada inapanga kuwasaidia wanaume, wanawake, na watoto wapatao 5,000 kupata chakula chao cha kila siku. Plastiki za kutengenezea mahema zilizotolewa na Mashahidi wa Yehova wa Ubelgiji, Ufaransa, na Uswisi zitatumiwa kuunda makao ya muda kwa wale wasio na mahali pa kuishi na vilevile mahali pa kukutana kwa makutaniko ambayo Majumba yao ya Ufalme yaliharibiwa. Baadhi ya jamaa zitaishi pamoja na jamaa nyingine za Mashahidi ambazo nyumba zao hazikuharibiwa, na nyingine zitaishi katika makao hayo ya muda.

Mnamo Ijumaa, Januari 25, siku kumi hivi baada ya usiku wa mlipuko, watu 1,846 wanahudhuria mkutano katika uwanja wa shule huko Goma kusikiliza maneno yenye kutia moyo kutoka kwa Maandiko. Ndugu wengi wanatoa shukrani kwa ajili ya faraja na msaada waliopokea kutoka kwa Yehova kupitia tengenezo lake. Mioyo yetu sisi wageni inaguswa na ujasiri na imani yenye nguvu ya ndugu hao licha ya masaibu yaliyowapata. Katika hali hizo ngumu, ni vyema kama nini kuwa sehemu ya udugu ulioungana katika ibada ya Mungu wa kweli, Yehova, aliye Chanzo cha faraja ya milele!—Zaburi 133:1; 2 Wakorintho 1:3-7.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Mlima huo unaitwa “mulima ya moto.”

[Ramani katika ukurasa wa 22, 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Vishale vinaonyesha mahali lava ilipitia

KONGO (KINSHASA)

Mlima Nyiragongo

↓ ↓ ↓

Uwanja wa Ndege wa Goma ↓ ↓

↓ GOMA

↓ ↓

ZIWA KIVU

RWANDA

[Picha katika ukurasa wa 23]

Lava iliwalazimisha makumi ya maelfu ya watu kukimbia jiji la Goma

[Hisani]

AP Photo/Sayyid Azim

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Katika juma moja tu Mashahidi walifanya mikutano ya Kikristo