Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Wanavyosoma Midomo

Jinsi Wanavyosoma Midomo

Jinsi Wanavyosoma Midomo

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

WATU wawili walioshukiwa kuwa magaidi walipigwa picha za video. Hakuna aliyesikia yale waliyokuwa wakisema—hata hivyo, walikamatwa na polisi, na baadaye wakafungwa gerezani kwa miaka mingi. Mazungumzo yao yaliyopigwa picha za video yalisimuliwa na msomaji wa midomo wa Uingereza anayejulikana kuwa stadi wa kusoma midomo na aliyetajwa kuwa “silaha kimya” ya polisi wa Uingereza.

Ili nifahamu mengi zaidi kuhusu ustadi wa kusoma midomo, niliwatembelea Mike na Christina. Christina amekuwa kiziwi tangu alipokuwa na umri wa miaka mitatu. Baadaye alihudhuria shule ya viziwi, ambapo alifundishwa kusoma midomo. Mike alijifunza kusoma midomo baada ya kumuoa Christina.

Ni vigumu jinsi gani kusoma midomo? “Ni lazima uangalie kwa makini jinsi midomo ya mtu, ulimi na utaya wa chini unavyosonga anapozungumza,” asema Mike. Christina anaongeza: “Lazima umtazame kwa makini mtu anapozungumza, na ujuzi wako wa kusoma midomo unapoendelea kuongezeka, unaanza kutambua pia ishara zake za mwili na za uso.”

Nimetambua kwamba mtu aweza kushindwa kutambua maana iwapo mtu anayezungumza anapaza sauti au anabadili midomo yake isivyo kawaida anapozungumza. Mazoea hayo hupotosha na kumkanganya mtu anayesoma midomo. Lakini mtu anapofahamu vizuri kusoma midomo, yeye aweza hata kujua lafudhi ya yule anayezungumza. Bila shaka, hilo si jambo rahisi! Shirika la Hearing Concern linalowafundisha watu kusoma midomo, linasema hivi waziwazi: “Kusoma midomo kunahitaji mazoezi, mazoezi na mazoezi zaidi.”

Christina anasema kwamba wakati mwingine yeye husumbuka anapojikuta “akisikiliza mazungumzo ya watu wengine” ndani ya basi au gari-moshi bila kukusudia. Yeye hugeuka mbali mara moja anapotambua jambo hilo. Lakini ustadi wake unaweza kuwa ulinzi pia. Sasa Christina ameacha kutazama mpira kwenye televisheni kwa sababu yeye huchukizwa na mambo anayoona wachezaji wakisema.

Ni watu wachache watakaopata ustadi huo wa “silaha kimya” ya polisi wa Uingereza. Lakini hata kusoma midomo kwa kadiri fulani kunaweza kumfaa sana mtu aliye na tatizo kubwa la kusikia.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Christina

[Picha katika ukurasa wa 31]

Mike