Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kamera Inayofanana na Macho ya Mdudu

Gazeti la The Australian linaripoti kwamba “kituo cha NASA kimenunua kamera ya roboti inayofanana na macho ya mdudu iliyobuniwa na wanasayansi wa Australia. Itatumiwa kwenye roketi ya kuchunguza Mihiri.” Watafiti wa Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia walitengeneza kamera hiyo kwa kuiga macho ya nzige. Ripoti hiyo inasema kwamba “maabara ya chuo hicho kikuu inayobuni macho ya roboti imetumia miaka mingi kuchunguza jinsi macho yanavyowasaidia nzige, nyuki na kereng’ende wanaporuka hewani. Wamebuni sheria za kuruka angani na sheria za hesabu ili kuiga wadudu hao.” Kituo cha NASA kinakusudia kutia kamera hiyo inayofanana na macho ya nzige kwenye chombo kidogo cha kukusanya habari angani, ambacho “kitaruka kwa kasi kama mdudu juu ya uso wa Mihiri wenye milima-milima bila kugonga miamba.” Chombo hicho kitakapoanza kufanya kazi “kitachunguza tabaka ya miamba kwenye korongo kubwa zaidi katika mfumo wa jua linaloitwa Valles Marineris, lenye urefu wa kilometa 4,000 na kina cha kilometa 7, ili kuonyesha jinsi sayari ya Mihiri ilivyobadilika.”

Nyangumi-Wauaji Huvutiwa na Nyangumi Wengine Wenye Milio Tofauti

“Nyangumi-wauaji wanaoishi maisha yao yote katika makundi madogo huepukaje kujamiiana na nyangumi wa jamii yao?” lauliza gazeti la The Vancouver Sun la Kanada. “Mwanasayansi mkuu wa kituo cha Vancouver Aquarium, Lance Barrett-Lennard, amechunguza utafiti wa miaka saba wa chembe za urithi na wa sampuli 340 za DNA kutoka kwa nyangumi-wauaji huko British Columbia na Alaska, na amegundua kwamba nyangumi wa kike hujamiiana tu na nyangumi wa makundi mengine” jirani. Barrett-Lennard asema kwamba ‘hakuna ushuhuda kwamba nyangumi hujamiiana na nyangumi wa jamii yao. Karibu nyangumi wote hujamiiana na nyangumi wa makundi mengine yenye milio tofauti.’ Makala hiyo yasema pia kwamba “nyangumi-wauaji humchagua mwenzi ambaye hawana uhusiano wa karibu. Na huenda wanafanya hivyo kwa kusikiliza milio au sauti za nyangumi wengine na kutambua zile ambazo ni tofauti sana.”

Kuchunguza Tabia za Papa Mweupe

Gazeti la The Daily Telegraph la London linasema kwamba “setilaiti zimegundua kwamba papa mweupe ambaye ndiye samaki mkubwa zaidi anayekula viumbe wengine, husafiri kwa maelfu ya kilometa baharini.” Ripoti hiyo iliyochapishwa katika gazeti la Nature, imefutilia mbali maoni ya awali kuhusu papa weupe. Ingawa papa hao hupatikana ulimwenguni pote, ilidhaniwa kwamba wao huogelea tu karibu na fuo, wakiwinda sili bila kwenda mbali sana na maeneo yao. Hata hivyo, hivi majuzi watafiti wa California waliwachunguza papa wanne wa kiume na wawili wa kike, wakagundua kwamba papa mmoja aliogelea hadi Visiwa vya Hawaii—umbali wa kilometa 3,700 kutoka pwani ya California—akiogelea kwa mwendo wa angalau kilometa 70 kwa siku. Uchunguzi huo pia ulifunua kwamba papa weupe, ingawa kwa kawaida hawashuki kufikia kina cha meta 30 karibu na fuo, nyakati nyingine wanashuka kwa kina kirefu wanapokuwa kwenye vilindi vya bahari.

Matatizo ya Kiuchumi Yameathiri Hospitali

Matatizo ya kiuchumi yaliyosababishwa na kushuka sana kwa thamani ya pesa za Argentina yanawafanya raia wengi wa nchi hiyo wamiminike hospitalini kwa sababu ya magonjwa yanayoletwa na mfadhaiko hivi kwamba hospitali zimelemewa mno na idadi ya wagonjwa, laripoti gazeti la Clarín. Wagonjwa wana matatizo kama vile “maumivu ya kichwa, shinikizo la damu, vidonda vya tumbo, uvimbe wa tumbo, ukosefu wa usingizi, na mahangaiko.” Mtaalamu mmoja wa tiba alisema kwamba baadhi ya watu wanazimia tu “bila tatizo lolote la neva.” Katika hospitali moja idadi ya wagonjwa wenye mfadhaiko, walioshuka moyo na wenye wasiwasi iliongezeka kwa asilimia 300 kwa siku chache tu. Mbali na kufurika kwa wagonjwa hospitalini, madaktari na wauguzi wanahangaishwa na wagonjwa wenye hasira kwa sababu ya matatizo ya kifedha. Baadhi ya wagonjwa hata wamewashambulia madaktari na wauguzi. Muuguzi mmoja wa kike alipigwa kichwani.

Treni ya Burudani Inayoenda kwa Kasi Zaidi

Gazeti la IHT Asahi Shimbun la Japan linaripoti kwamba “treni ya burudani inayoenda kwa kasi zaidi ulimwenguni ilizinduliwa kwenye bustani ya michezo ya Fujikyu Highland.” “Watu waoga hawawezi kustahimili mwendo huo kwa sababu kwa muda usiozidi sekunde mbili, treni hiyo hufikia kasi ya kilometa 172 kwa saa. Ni kana kwamba inarushwa na roketi. Abiria wanaweza kuhisi nguvu za uvutano ambazo huhisiwa na marubani wa ndege za vita zinazoenda kwa kasi sana.” Mkurugenzi wa mradi huo, Heith Robertson alisema hivi: “Ndege inapoanza kupaa inaweza kuwa na nguvu zenye kipimo cha 2.5 [mara 2.5 ya nguvu za uvutano]. Treni hii ina nguvu za uvutano zenye kipimo cha 3.6.” Treni hiyo ya burudani ina “magurudumu ya ndege ndogo” na inaendeshwa na kompresa tatu za hewa ambazo hutokeza msukumo wa nguvufarasi 50,000, “sawa na roketi ndogo.”

Sigara Yasababisha Ugonjwa wa Moyo Huko India

“Madaktari wakuu wa magonjwa ya moyo [huko India] wanasema kwamba idadi ya watu wenye ugonjwa wa moyo inaongezeka,” laeleza gazeti la Mumbai. “Dakt. Ashwin Mehta, mkurugenzi wa matibabu ya moyo katika Hospitali ya Jaslok, asema kwamba Wahindi hushikwa sana na magonjwa ya moyo kiasili.” Lakini jambo linalohangaisha sana ni kwamba vijana wengi zaidi wanashikwa na “magonjwa ya moyo kwa sababu ya kuvuta sigara.” Dakt. P. L. Tiwari, daktari stadi wa magonjwa ya moyo katika Hospitali ya Bombay, anaamini kwamba siku moja India itakuwa na idadi kubwa zaidi ya watu wenye magonjwa ya moyo ulimwenguni ikiwa hatua haitachukuliwa haraka. Katika nchi jirani ya Bangladesh, zaidi ya asilimia 70 ya wanaume wenye umri wa kati ya miaka 35 hadi 49 huvuta sigara, lasema gazeti la The Times of India, na “uvutaji wa sigara uliongezeka kadiri mapato yalivyopungua.” Kwa wastani, kila mtu anayevuta sigara ‘hutumia zaidi ya nusu ya mapato kununua sigara kuliko jumla ya pesa anazotumia kununua mavazi, kugharimia makao, afya na elimu.’ Ikiwa pesa zinazotumiwa kununua sigara zinaweza kutumiwa kununua chakula katika nchi hiyo maskini, inakadiriwa kwamba wakazi milioni 10.5 wasiopata chakula cha kutosha wanaweza kupata chakula cha kutosha.

Bado Majengo Marefu Yanahitajiwa

“Wachoraji wa ramani za majengo na wahandisi walishtuka sana walipoona ile minara miwili ikiporomoka,” lasema gazeti la U.S.News and World Report. “Licha ya wasiwasi huo, majengo marefu bado yanahitajiwa.” Sababu moja ni kwamba ardhi haipatikani kwa urahisi katika sehemu nyingine na ni ghali sana. Isitoshe, wakazi wa miji hupenda kitu cha kujivunia. William Mitchell, mkuu wa kitivo cha uchoraji wa ramani za majengo katika Taasisi ya Tekinolojia ya Massachusetts asema kwamba ghorofa ndefu sana hujengwa “ili kujipatia sifa na kufuata mitindo ya kisasa na sababu nyinginezo kama hizo.” Hata hivyo, wachoraji wa ramani wanatafuta njia ya kuongeza usalama wa majengo hayo. Majengo yanaweza kujengwa kwa kuta na madirisha yanayostahimili mlipuko wa bomu, lakini vifaa hivyo vinaongeza uzito na ni ghali sana. Kulingana na sheria za ujenzi huko China, ni lazima kila jengo liwe na ‘sehemu ya usalama’ iliyo wazi baada ya kila ghorofa 15. Kwingineko, sheria za ujenzi zinasisitiza kila jengo liwe na lifti inayofika ghorofa ya juu kwa ajili ya wazima-moto, na pia sehemu ya ngazi isiyopenywa na moshi. Tayari, wachoraji wa ramani ya jengo la Shanghai World Financial Center, ambalo huenda likawa jengo refu zaidi ulimwenguni, wanachukua tahadhari zaidi za usalama.

Kelele Huharibu Masikio

Gazeti la Poland la kila juma Polityka lasema kwamba “mtoto mmoja kati ya watano wenye umri wa kwenda shule na mtu mmoja mzima kati ya watatu huko Poland ana matatizo ya kusikia.” Uchunguzi unaonyesha kwamba magari, redio, video na vifaa vya nyumbani huwa na kelele nyingi sana. Ripoti moja kuhusu mazingira ilisema kwamba kuongezeka kwa magari katika jiji la Warsaw kumeongeza kiasi cha kelele katika mtaa mmoja hadi desibeli 100. Mayowe ya watoto wanaocheza hufikia kiwango hichohicho. Redio zenye amplifaya kwenye madisko zinaweza kuwa na kelele za kiwango cha desibeli 120, karibu tu na kipimo cha desibeli 130 hadi 140 ambacho huumiza masikio. Wataalamu wanasema kwamba kelele hizo zinaharibu masikio. Profesa Henryk Skarżyński, ambaye ni mtaalamu katika Taasisi ya Kuchunguza Utendaji wa Masikio na Visababishi vya Matatizo ya Kusikia, asema hivi: “Matatizo ya kusikia husababisha matatizo mabaya sana ya kijamii. Watu wenye matatizo ya kusikia hukasirika kwa urahisi, hushindwa kusoma, [na] hata hushindwa kujifunza lugha ya kigeni.”