Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutafuta Suluhisho

Kutafuta Suluhisho

Kutafuta Suluhisho

MWANZONI mwa mwaka wa 1972 zaidi ya mataifa mia moja yalitia sahihi mkataba wa kimataifa uliopiga marufuku kubuni, kuunda, na kuhifadhi silaha za kibiolojia. Mkataba huo ulioitwa Biological and Toxin Weapons Convention (BTWC), ulikuwa wa kwanza kupiga marufuku silaha zote za aina moja. Lakini mkataba huo haukuonyesha njia ya kuhakikisha kwamba mataifa yaliutii.

Ni vigumu kujua kama mataifa yanaunda silaha za kibiolojia, kwani mbinu na ujuzi ambao hutumiwa kuunda bidhaa nyingine zenye manufaa zinaweza kutumiwa pia kutengeneza silaha. ‘Utumizi huo wenye pande mbili’ hufanya iwe rahisi kuficha uundaji wa silaha katika viwanda vya kuchachusha na kwenye maabara ambazo huonekana zikiendelea na shughuli za kawaida.

Ili kutatua tatizo hilo, wajumbe wa nchi kadhaa walianza kujadili mkataba mwingine katika mwaka wa 1995. Zaidi ya miaka sita ilipita wakijadiliana kuhusu hatua maalumu ambazo zingechukuliwa ili kuhakikisha kwamba mataifa yalifuata kanuni za mkataba wa BTWC. Mnamo Desemba 7, 2001, mkutano wa majuma matatu uliohudhuriwa na mataifa 144 kati ya yale yaliyotia sahihi mkataba wa 1972 ulimalizika kwa vurugu. Tatizo lililetwa na Marekani wakati ilipopinga mapendekezo makuu ya mkutano huo kuhusu jinsi ya kujua kama mataifa yalifuata kanuni za BTWC. Marekani iliona kuwa kuruhusu watu wengine wachunguze vituo vyake vya kijeshi na viwanda kungekuwa ujasusi.

Matazamio ya Wakati Ujao

Ufundi wa kibiolojia unaruhusu watu wafanye mambo mema na mabaya pia. Ufundi wa aina nyingine—kama ufundi wa vyuma, vilipukaji, injini, ufundi wa ndege, elektroni—umetumiwa kwa njia yenye manufaa na katika vita pia. Je, ni hali moja na ufundi wa kibiolojia? Watu wengi wanaamini kuwa jibu la swali hilo ni ndiyo.

Ripoti iliyoandikwa na Tume ya Usalama wa Kitaifa ya Marekani mnamo mwaka wa 1999 ilisema: “Watu mmoja-mmoja na vikundi . . . vitakuwa na mamlaka na ushawishi mwingi zaidi, na watu wengi watakuwa na mbinu zenye kuogofya za kusababisha maafa. . . . Magenge na watu wengi zaidi, walio na bidii ya kidini, wafuasi sugu wa madhehebu, au wenye chuki nyingi kupita kiasi, watafanya kazi hiyo kihususa. Magaidi sasa wanaweza kushambulia vituo muhimu vya kijamii wakitumia tekinolojia ambazo wakati mmoja zilitumiwa na mataifa makubwa pekee.”

Ingawa hatujui mambo yatakayotukia karibuni, tuna uhakika juu ya yale ambayo Mungu amewakusudia wanadamu. Biblia huahidi wakati ambapo watu duniani “watakaa salama salimini, wala hapana mtu atakayewatia hofu.” (Ezekieli 34:28) Ili ufahamu zaidi kuhusu ahadi hiyo yenye kufariji, wasiliana na Mashahidi wa Yehova wa kwenu au utuandikie barua ukitumia anwani ifaayo iliyoonyeshwa katika ukurasa wa 5 wa gazeti hili.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Watafiti wanabuni njia za kukabiliana na ugonjwa wa kimeta

[Hisani]

Photo courtesy Sandia National Laboratories

[Picha katika ukurasa wa 10]

Mkutano kuhusu Silaha za Kibiolojia, Novemba 19, 2001, Uswisi

[Hisani]

AP Photo/Donald Stampfli

[Picha katika ukurasa wa 11]

Biblia inaahidi wakati ambapo watu wote “watakaa salama salimini”