Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Miwati ya Kidhahabu Ishara ya Majira ya Kuchipua Australia

Miwati ya Kidhahabu Ishara ya Majira ya Kuchipua Australia

Miwati ya Kidhahabu Ishara ya Majira ya Kuchipua Australia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

UA LINALOCHANUA unaloliona katika kurasa hizi si la kawaida. Linajulikana na kupendwa sana nchini Australia. Kwa kweli, tangu mwaka wa 1912, nembo ya Australia imerembwa kwa ua hilo, na mnamo 1988 lilitangazwa kuwa ua rasmi la Australia. Ua hilo pia limechorwa katika sarafu na stampu za Australia. Kwa nini likawa maarufu hivyo?

Shairi lililoandikwa na Veronica Mason na kuchapishwa katika mwaka wa 1929, linajibu swali hilo. Baada ya kuelezea mimea yenye rangi za huzuni za “bitimarembo na kahawia na kijivu” inayotokeza sana mwishoni mwa majira ya baridi kali, shairi hilo latangaza hivi kwa furaha: “Lakini sasa majira ya Kuchipua yamefika / Na Miwati imechanua.”

Inaonekana kwamba karibu kila mtu anapenda kuyakaribisha majira ya kuchipua. Nchini Australia, majira ya kuchipua huanza wakati majira ya kupukutika kwa majani yanapoanza Kaskazini mwa Ikweta. Miwati yenye rangi ya dhahabu inapochanua, hiyo ni ishara ya mapema kwamba majira ya kuchipua yanakaribia katika bara hilo la kusini. Kwa hiyo, unaweza kuwasikia watoto wa shule wakikariri shairi la Mason mwezi wa Agosti. Na katika mwaka wa 1992, gavana wa Australia alitangaza Septemba 1 kuwa Siku ya Kitaifa ya Miwati.

Miwati ya kidhahabu hutangaza mwanzo wa majira ya kuchipua kwa uzuri na umaridadi. Shairi la Mason pia linataja “Miwati yenye fahari na yenye kuinama,” likielezea jinsi matawi yake yenye maua yanavyopeperushwa huku na huku na upepo wa majira ya kuchipua. Miwati ni miongoni mwa miti inayokua katika maeneo yenye joto duniani.

Miti Maarufu na Yenye Nguvu

Jina la kisayansi la miwati ya kidhahabu ni Acacia pycnantha. Miwati ni miti mifupi yenye urefu wa meta 4 hadi 8. Lakini kuna aina 600 hadi 1,000 hivi za mijohoro (acacia) nchini Australia, ambayo kwa kawaida huitwa miwati. Kwa kweli, zaidi ya nusu ya mijohoro inayojulikana duniani inapatikana Australia. Huko Ulaya na Marekani mijohoro inaitwa mimosa. Aina fulani ya mjohoro imetajwa mara nyingi katika Biblia. Mungu aliagiza kwamba sanduku la agano na sehemu za tabenakulo zitengenezwe kwa mjohoro.—Kutoka 25:10; 26:15, 26, Biblia Habari Njema.

Mjohoro mmoja unaojulikana sana unapatikana Afrika na una umbo la mwavuli. Twiga hupenda sana kula majani yake. Kwa kweli wangeambua maganda ya mti huo kabisa pasingekuwa na ushirikiano wa kipekee kati ya mti huo na aina fulani ya siafu. Mti huo humpa mdudu huyo makao na kinywaji kitamu. Naye mdudu humwuma twiga mlafi, na kumfukuza aende kwenye mti mwingine. Uhusiano huo unatoa uthibitisho ulioje wa kuwapo kwa mbuni mwenye akili!

Mijohoro ya Australia haikabili hatari ya kuharibiwa na twiga. Hata hivyo, mijohoro hiyo inahatarishwa na mambo mengine, kama vile ukame. Hata hivyo miti hiyo hustahimili hali hiyo. Mbegu ya mjohoro ina ngozi ngumu sana hivi kwamba inahitaji kuharibiwa kwa njia fulani ili maji yapenye na ukuzi uanze. Mbegu hizo ni ngumu sana hivi kwamba wakulima huzichemsha kwa maji ili ziambuke na kuota zinapopandwa. Katika msitu, mbegu za mijohoro zinaweza kukaa bila kuota kwa makumi ya miaka! Hatimaye moto wa msitu unaweza kuifanya mbegu hiyo ngumu iote. Hivyo, hata wakati wa ukame mbaya sana bado kuna “hifadhi ya mbegu” za mijohoro ardhini zinazongojea kuota.

Kwa miaka mingi sasa, miwati ya Australia ambayo hustahimili hali ngumu imepelekwa Afrika ili iliwe wakati wa ukame. Mojawapo ya faida yake ni kwamba inaweza kukua katika udongo usio na rutuba. Mijohoro fulani hata inaweza kukua katika matuta ya mchanga! Miti hiyo huunganisha udongo, huuongezea nitrojeni, na kuzuia upepo, hivyo kuifaidi mimea mingine.

Mti Wenye Matumizi Mengi

Wanasayansi fulani huonelea kwamba mbegu za miwati zinaweza kuliwa, kwani zina protini nyingi na ni bora zikilinganishwa na nafaka nyingine. Mbegu zake zinapochomwa huwa tamu kama njugu; na aina fulani huwa na ladha ya dengu zinapochemshwa. Mbegu za miwati zimesagwa na kutumiwa kuoka mkate na kutengeneza tambi. Aina fulani za miwati hutoa kilogramu 10 za mbegu kila mwaka.

Maua ya miwati yenye harufu tamu hutumiwa kutengeneza marashi. Zaidi ya hilo, mijohoro hutumiwa katika sehemu nyingi kulisha mifugo na kuzuia mmomonyoko wa udongo. Lakini tumetaja tu matumizi machache ya mjohoro.

Waaborijini wa mapema wa Australia walitumia mijohoro kutengeneza marungu. Aina moja ya miwati, Acacia acuminata, imeitwa jamu ya rasiberi kwa sababu miti yake ikikatwa hutoa harufu kama ya rasiberi zilizopondwa-pondwa.

Waaustralia wa mapema walitumia mijohoro na udongo kujenga nyumba zao. Kuta za nyumba zilitengenezwa kwa kukandika matope kwenye miti iliyounganishwa.

Inashangaza jinsi miwati ilivyo na matumizi mengi! Hata hivyo, majira ya kuchipua yanapofika matumizi hayo hayakumbukwi. Badala yake, maua ya dhahabu yenye nyuzi nyingi fupi yanapoonekana kwenye miinuko, mioyo hushangilia na watu hukumbuka mashairi yanayohusu miwati. Umaridadi na matumizi yake mengi huwakumbusha watu wengi wanaovutiwa nayo kuhusu ustadi na hekima ya Mungu, “aliyejenga vitu vyote.”—Waebrania 3:4.

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Maua na mbegu za miwati

[Hisani]

© Australian Tourist Commission

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Miwati: © Copyright CSIRO Land and Water; stampu: National Philatelic Collection, Australia Post; nembo: Used with permission of the Department of the Prime Minister and Cabinet