Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Giza Lililotokea Adhuhuri

Giza Lililotokea Adhuhuri

Giza Lililotokea Adhuhuri

NA WAANDISHI WA AMKENI! NCHINI ANGOLA NA ZAMBIA

‘GIZA wakati wa adhuhuri? Haiwezekani!’ huenda wengine wakasema. Jambo hilo linawezekana na hutokea mara kadhaa kila miaka kumi—jua linapopatwa kabisa. Ni nini husababisha kupatwa kwa jua, na kwa nini hilo ni jambo lenye kuvutia? Ili tupate jibu, kwanza tutachunguza mwezi.

Je, unafahamu jinsi mwezi hubadilika-badilika unapozunguka dunia? Mwezi na jua vinapokuwa katika pande tofauti za anga, sisi huona kile kinachoitwa mwezi mpevu ukichomoza upande wa mashariki jua linapotua upande wa magharibi. Kadiri siku zinavyosonga, mwezi huchelewa kuchomoza kila usiku, pole kwa pole ukizidi kukaribia jua. Mwezi huendelea kuonekana ukiwa mdogo, na hatimaye huandama. Wakati jua na mwezi viko upande mmoja wa anga siku nzima, mwezi hupotea kabisa kwa kuwa upande wake wenye giza unaangalia dunia. Huo unaitwa mwezi mpya. Kisha mambo huanza kurudi kama yalivyokuwa awali, huku mwezi ukianza kusonga mbali na jua na mwishowe kuwa mpevu tena. Mzunguko huo hujirudia kila baada ya siku 28.

Kupatwa kwa jua huamuliwa na mwezi mpya. Kwa kawaida mwezi huenda sambamba na jua wakati wa mchana bila sisi kutambua jambo hilo kwa sababu wakati huo mwezi na jua huwa katika mistari tofauti. Hata hivyo, wakati mwingine jua, mwezi, na dunia hujipanga katika mstari mmoja. Wakati huo, kivuli cha mwezi hufunika uso wa dunia, na jua hupatwa.

Jua hupatwa kunapokuwa na mpangilio wa kipekee wa jua, mwezi, na dunia. Jua ni kubwa sana, kipenyo chake kikiwa karibu mara 400 zaidi ya kile cha mwezi. Hata hivyo, jambo la kustaajabisha ni kwamba jua liko mbali nasi mara 400 zaidi kuliko mwezi. Ndiyo sababu sisi huliona jua likiwa na ukubwa unaoelekea kuwa sawa na ule wa mwezi. Hivyo, mara nyingine mwezi huonekana kama umefunika jua kabisa.

Ili jua lipatwe kabisa, lazima jua, mwezi na dunia ziwe katika mstari mmoja, na wakati huohuo mwezi uwe katika sehemu ya mzunguko wake iliyo karibu na dunia. * Wakati huo kivuli cha mwezi chenye umbo la pia hutia giza ukanda mwembamba wa dunia.

Mnamo Juni 21, 2001, jua lingepatwa kabisa na giza lingefunika eneo lenye upana wa kilometa 200. Giza hilo lingeanza wakati wa mapambazuko karibu na pwani ya mashariki ya Amerika Kusini kupitia Atlantiki Kusini, ambapo lingedumu zaidi kwa dakika tano hivi. Giza hilo lingeonekana Angola, Zambia, Zimbabwe, na Msumbiji, hadi pwani ya mashariki ya Madagaska, wakati wa machweo. Hebu tuone jinsi mambo yalivyokuwa angani kulingana na watazamaji waliokuwa Angola na Zambia.

Matayarisho kwa Ajili ya Tukio Hilo

Wataalamu wa anga pamoja na wapenzi wengine wa mambo ya anga, walisafiri hadi Afrika wakitazamia kwa hamu kuona jua likipatwa kabisa kwa mara ya kwanza katika milenia mpya. Jiji la Lusaka, Zambia, ndilo lililokuwa jiji kuu pekee ambapo tukio hilo lingeonekana, kwa hiyo wageni wengi walisafiri huko ili kujionea.

Huenda hilo ndilo tukio kubwa zaidi la kuwavutia watalii ambalo Zambia imewahi kupata. Siku chache tu kabla ya tukio hilo, maelfu ya wageni walifurika jijini Lusaka. Matayarisho yalifanywa miezi mingi mapema. Mahoteli, nyumba za kulala, na nyumba za watu binafsi zilihifadhiwa kwa ajili ya wageni hao wengi.

Uwanja wa ndege wa Lusaka ulikuwa mojawapo ya sehemu za kutazama tukio hilo ambapo watu wangewasili asubuhi, watazame, na kisha kuondoka jioni. Kwa majuma mengi, vituo vya televisheni na redio viliwatangazia watu kuhusu tukio hilo lililokuwa likitazamiwa, vikiwaonya mara nyingi kuhusu hatari ya kutazama jua bila kutumia miwani maalum ya jua. Miwani hiyo iliuzwa kwa wingi hata kuliko vile ilivyokuwa imetarajiwa, nayo ikamalizika katika maduka mengi.

Hata hivyo, watu wa mji wa pwani wa Sumbe, nchini Angola, wangekuwa wa kwanza kuona tukio hilo barani Afrika. Hapo ndipo watazamaji wangeona jua likiwa limepatwa kabisa kwa muda mrefu zaidi katika nchi kavu, yaani, muda wa dakika nne u nusu.

Miezi mingi mapema, vibao vya kutangaza tukio hilo viliwekwa katika jiji kuu la Angola, Luanda, na katika miji mingine mikubwa. Kivuli cha mwezi kingepitia katikati ya Angola, hivyo watu nchini kote wangeona angalau sehemu fulani ya jua ikiwa imepatwa. Jijini Luanda, watu wangeona asilimia 96 ya jua likiwa limefunikwa. Serikali, ikishirikiana na kampuni za kibinafsi, ilipanga kununua mamilioni ya miwani maalum ya jua kutoka nchi nyingine. Watu wengi ambao hawakuweza kuigharimia walipewa bure.

Mji wa Sumbe ulioko kwenye sehemu maridadi na iliyo tambarare ya pwani kati ya Atlantiki Kusini na uwanda wa juu wa Angola, ulikuwa kitovu cha tukio hilo nchini Angola. Sehemu hiyo haijapatwa na mapigano mabaya zaidi ambayo yameikumba Angola, kwa hiyo wageni walikuta mji ulio shwari wenye wakazi 25,000 ambao ni wachangamfu na wenye urafiki. Matayarisho yalifanywa ili kuongeza sehemu za kukaa na za kula kwa ajili ya watalii na kituo cha umeme kikarekebishwa, ili kutosheleza mahitaji ya wageni wote. Mkutano wa kipekee ulipangwa kwa ajili ya wanasayansi, mawaziri wa serikali, na wafadhili kutoka Angola na mataifa mengine. Jukwaa kubwa sana lilijengwa ufuoni mwa bahari kwa ajili ya burudani ambayo haijawahi kamwe kuonekana huko Sumbe.

Siku Kubwa Yafika

Sababu moja iliyofanya Angola iwe nchi nzuri ya kutazama jua likipatwa ni kwamba mwezi wa Juni huwa mkavu. Lakini kulikuwa na wasiwasi siku iliyotangulia tukio hilo kwa sababu mawingu yalifunika eneo la Sumbe. Mawingu mazito yalifunika eneo la mji kuanzia jioni hadi asubuhi. Je matazamio yote ya kutazama tukio hilo yangekatishwa? Baadaye asubuhi mawingu yalianza kutawanyika na anga likawa wazi bila wingu lolote. Kilikuwa kitulizo kilichoje! Nchini Zambia pia, mawingu yaliyokuwapo wakati wa mapambazuko yalileta wasiwasi. Lakini huko pia mawingu yalitoweka kwa wakati mzuri. Sikiliza masimulizi ya watu waliojionea matukio hayo.

Angola: “Tuliamua kutazama kupatwa kwa jua tukiwa mahali palipoinuka karibu na bahari. Wakati ulipokaribia, watu walimiminika ufuoni na sehemu nyingine zilizotengwa za kutazama tukio hilo. Saa sita kamili, jua lilipokaribia kupatwa, watu wengi walivalia miwani yao na kuanza kutazama jua likianza kufunikwa. Muda mfupi baada ya saa sita jua lilianza kupatwa. Kwa kutumia darubini, madoa meusi yalionekana katika jua. Watazamaji waliona madoa hayo yakifunikwa moja baada ya jingine. Jua lilipoendelea kufunikwa, joto lilipungua sana na nuru ikaanza kubadilika na kuwa na rangi isiyo ya kawaida. Hatimaye, jua lilipofunikwa kabisa, kukawa na giza.”

Zambia: “Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova ya Zambia iliyopo Makeni, Lusaka, ilikuwa mahali pazuri pa kutazama tukio hilo. Saa 9:07 alasiri, mwezi ulianza kufunika jua. Giza lilianza kufunika majengo. Upepo uliacha kuvuma, na ndege wakawa kimya. Wanyama wa mwitu walianza kujitayarisha kulala. Saa 9:09, sekunde chache kabla ya jua kupatwa kabisa, madoa machache ya mwangaza yalionekana, halafu kukabaki kipande kimoja tu. Matukio hayo yanaitwa shanga za Baily na pete ya almasi. * Kisha, miali ya jua ilibadilika, kutoka rangi ya waridi-nyekundu hadi jua likapatwa kabisa na kukawa na giza!”

Angola: “Mng’aro wa pete ya almasi ulisababisha vifijo na nderemo. Kisha, saa 7:48 adhuhuri, saa za hapa, jua likapatwa kabisa. Watu waliitikia kwa njia tofauti-tofauti. Wengine walijishughulisha kupiga picha. Wengine walipaaza sauti pamoja wakisema, ‘Limefunikwa! Limefunikwa! Limefunikwa! Wengine walipiga mbinja na kutoa sauti za mshangao kwa sababu ya giza hilo lililotokea adhuhuri. Miali iliyozunguka jua lenye joto la mamilioni ya digrii ilionekana ikizunguka kuelekea pande zote. Tuliona miali ya gesi ikizunguka mwezi uliokuwa gizani. Kwa ghafula, jua likaanza kuonekana na miali ya mwangaza ikaangaza kutoka upande wa pili wa kivuli.

“Wakati jua lilipoanza kutokea, tuliona madoa meusi ya jua yaliyokuwa yamefunikwa hapo awali, yakitokea moja baada ya jingine kutoka gizani na mviringo wa jua ukatokea polepole.”

Zambia: “Hapa jua lilipatwa kabisa kwa dakika 3 na sekunde 14, kwa hiyo kulikuwa na muda wa kutosha kutafakari kuhusu tukio hilo. Giza lilitokea, lakini nuru kidogo ilitokea mbali kwenye upeo wa macho. Anga bado lilikuwa na rangi ya buluu na sayari ambazo kwa kawaida hazionekani kwa sababu ya kufunikwa na jua kama Sumbula na Zohali, zilionekana vizuri. Pengine jambo lililovutia zaidi katika tukio hilo ni miali iliyozunguka jua. Ilionekana kama mwangaza wa rangi ya waridi-nyeupe uliozunguka mviringo mweusi. Watazamaji walioshikwa na mshangao walisema kwamba lilikuwa tukio lenye ‘kushtua, lenye kustaajabisha.’ Polepole mwezi ulisonga kando, na miali ya jua ikaanza kuonekana tena hatua kwa hatua. Mnamo saa 10:28 alasiri, jua liliangaza kabisa na giza likatokomea!”

Mambo Tuliyojifunza Kutokana na Tukio Hilo

Baadaye watu wengi walieleza jinsi tukio hilo lilivyowaathiri. Huko Angola, mwanamke mmoja alisema kwamba alikuwa karibu kulia. Mwingine alilieleza kuwa zawadi nzuri kutoka kwa Mungu. Mwingine alisema ni Muumba mwenye upendo tu ambaye angesababisha tukio kama hilo ili watu wathamini umaridadi wa ajabu wa chanzo cha nuru duniani.

Ilikuwa wazi kwamba watu wengi Afrika wanamheshimu sana Muumba na Biblia. Wakazi wa Sumbe walipendezwa sana Mashahidi wa Yehova walipozungumza nao kuhusu tukio hilo, na kulitaja kuwa mojawapo ya kazi za ajabu za Muumba wetu, Yehova. Wengi walifurahi kubaki na nakala za gazeti la karibuni la Mnara wa Mlinzi lililozungumzia kazi hizo za ajabu.

Tukio hilo la angani liliwafanya mamilioni ya watu wasahau matatizo yao kwa dakika chache na kukazia fikira jambo lenye kutia moyo na lenye kustaajabisha kwelikweli. Wengine walipoona utukufu wa jua usioonekana kwa kawaida, walifikiri kuhusu utukufu mwingi zaidi usioonekana wa Muumba wa jua, Yehova Mungu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Kwa kuwa mizunguko ya mwezi na dunia ina umbo la yai, ukubwa wa jua na mwezi huonekana ukibadilika ikitegemea mahali vilipo kwenye mizunguko hiyo. Wakati mwezi uko katika sehemu ya mzunguko wake iliyo mbali zaidi na dunia, sehemu yenye giza zaidi ya kivuli chake haiwezi kufikia dunia. Wakati jambo hilo linapotokea, watazamaji walio katika sehemu ya kivuli hicho huona jua limepatwa, likiwa kama pete nyangavu yenye giza katikati.

^ fu. 19 Tukio linaloitwa shanga za Baily husababishwa na miali ya jua inayopitia kwenye mabonde yaliyo katika mwezi kabla tu ya jua kupatwa kabisa. Usemi “pete ya almasi” hufafanua jinsi jua linavyoonekana kabla tu ya kupatwa kabisa, kipande kidogo tu ndicho kinachoonekana kama pete nyeupe inayometameta ya almasi.

[Mchoro katika ukurasa wa 21]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

→ →

Jua → Mwezi ⇨ Sehemu ya giza ⇨ Dunia

→ →

[Hisani]

© 1998 Visual Language

[Picha katika ukurasa wa 23]

Shanga za Baily

Kupatwa kabisa

Pete ya almasi

[Hisani]

Courtesy Juan Carlos Casado, www.skylook.net

[Picha katika ukurasa wa 23]

Watazamaji wa tukio hilo huko Lusaka, Zambia