Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mambo Yaliyotarajiwa na Kuhofiwa Kuhusu Polisi

Mambo Yaliyotarajiwa na Kuhofiwa Kuhusu Polisi

Mambo Yaliyotarajiwa na Kuhofiwa Kuhusu Polisi

MAPEMA katika miaka ya 1800, watu wengi huko Uingereza walipinga mapendekezo ya kuwa na jeshi la polisi lenye mavazi rasmi. Walihofu kwamba polisi wenye silaha ambao wangeongozwa na serikali, wangewanyang’anya uhuru wao. Wengine walihofu kwamba jeshi hilo la polisi lingekuwa kama jeshi la wapelelezi wakali wa Ufaransa ambao walisimamiwa na Joseph Fouché. Hata hivyo, walihitaji sana jeshi la polisi.

Wakati huo London ndilo lililokuwa jiji kubwa na lenye ufanisi mwingi ulimwenguni pote. Uhalifu ulikuwa ukiongezeka na kuhatarisha biashara. Mabawabu waliojitolea kufanya kazi usiku na vilevile majasusi walioitwa Bow Street Runners waliokuwa wakilipwa na watu binafsi hawakuweza kuwalinda watu wala mali zao. Clive Emsley anasema hivi katika kitabu chake The English Police: A Political and Social History: “Watu walizidi kuona kwamba uhalifu na fujo ni mambo ambayo hayapaswi kuwepo katika jamii iliyostaarabika.” Hivyo, wakazi wa London wakaamua kwamba wanataka kuwa na jeshi la polisi, nalo likasimamiwa na Bwana Robert Peel. Mnamo Septemba 1829, polisi wenye mavazi rasmi kutoka katika Kituo cha Polisi cha London wakaanza kufanya doria mitaani.

Tangu wakati ambapo polisi walianza kazi yao katika siku za kisasa, watu wamehofu mambo fulani na vilevile kutarajia mazuri. Wametarajia kwamba polisi wanaweza kuleta usalama na wamehofu kwamba polisi watatumia mamlaka yao vibaya.

Mwanzo wa Jeshi la Polisi Huko Marekani

New York City ndilo lililokuwa jiji la kwanza kuwa na jeshi la polisi huko Marekani. Kadiri jiji hilo lilivyozidi kuwa na mali, ndivyo uhalifu pia ulivyoongezeka. Kufikia miaka ya 1830, habari zenye kushtua kuhusu uhalifu zilichapwa katika magazeti yaliyouzwa kwa bei rahisi ambayo yalikuwa yameanza kuchapishwa. Watu wengi wakalalamika, na jeshi la polisi likaanzishwa huko New York mnamo mwaka wa 1845. Tangu wakati huo wakazi wa New York wamependezwa na jeshi la polisi la London na wakazi wa London wamependezwa na jeshi la polisi la New York.

Sawa na Waingereza, Wamarekani pia waliogopa wazo la kuwa na jeshi la polisi lenye silaha ambalo lingesimamiwa na serikali. Lakini mataifa hayo mawili yalitatua jambo hilo kwa njia tofauti-tofauti. Waingereza waliamua kwamba polisi wao wangekuwa waungwana na wangevaa kofia ndefu na mavazi rasmi ya rangi ya bluu. Walibeba kirungu kifupi tu ambacho walikificha. Hadi leo hii polisi wa Uingereza hawabebi bunduki isipokuwa tu katika hali za dharura. Hata hivyo, kama vile ripoti moja inavyosema, ‘yaonekana kwamba hatimaye polisi wote wa Uingereza watalazimika kuwa na silaha.’

Hata hivyo, watu huko Marekani waliogopa kwamba serikali ingetumia mamlaka yake vibaya na hilo lilisababisha Marekebisho ya Pili ya Katiba ya Marekani. Katiba hiyo inawapa watu ‘haki ya kuwa na silaha.’ Hivyo, polisi wakataka kuwa na bunduki. Muda si muda, wakatumia bunduki hizo walipokuwa wakiwafukuza wezi katika barabara za miji. Sababu nyingine iliyowafanya Wamarekani wawe na maoni hayo kuhusu kubeba bunduki ni kwamba jeshi la kwanza la polisi huko Marekani lilianzishwa katika hali tofauti sana na zile za London. Ghasia ziliongezeka huko New York kadiri idadi ya watu ilivyozidi kuongezeka. Baada ya Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe iliyotokea katika mwaka wa 1861-1865, kulikuwa na ongezeko la maelfu ya wahamiaji kutoka Ulaya na vilevile Wamarekani wenye asili ya Kiafrika, na hilo lilisababisha ujeuri katika jamii. Polisi walionelea kwamba wanapaswa kuchukua hatua kali zaidi.

Kwa hiyo, ijapokuwa polisi hawakupendwa, bado walihitajiwa. Watu walikuwa tayari kuvumilia matendo maovu ya polisi wakitumaini kwamba wangekuwa na usalama na utaratibu wa kadiri fulani. Hata hivyo, katika sehemu fulani za ulimwengu kulitokea polisi wenye tabia tofauti.

Polisi Wakali

Mapema katika miaka ya 1800, wakati ambapo majeshi ya polisi ya kisasa yalipokuwa yakianzishwa, sehemu nyingi za dunia zilikuwa zikiongozwa na milki za Ulaya. Kwa ujumla, polisi huko Ulaya walipewa kazi ya kulinda watawala bali si raia. Yaonekana kwamba hata Waingereza, ambao hawakupenda kuwa na polisi wenye silaha katika nchi yao, hawakuona ubaya kutumia polisi wenye silaha ili kutawala makoloni yao. Katika kitabu chake cha Policing Across the World, Rob Mawby anasema hivi: “Visa vya ukatili wa polisi, ufisadi, ujeuri, mauaji na kutumia mamlaka vibaya vilikuwepo karibu katika miaka yote ya ukoloni.” Baada ya kuonyesha kwamba kazi ya polisi chini ya serikali za kikoloni ilileta pia faida fulani, kitabu hicho kinaongeza kwamba kazi yao ilifanya ‘mataifa ulimwenguni pote yawaone kuwa chombo cha serikali wala si watu wanaotoa utumishi kwa wote.’

Karibu sikuzote, serikali za kidikteta ambazo zinahofia kupinduliwa zimetumia polisi wa siri kuwapeleleza raia. Polisi hao hupata habari kwa kuwatesa watu na huwaua watu wanaodhaniwa kuwa wanataka kufanya mapinduzi au kuwafunga bila kuwapa nafasi ya kuhukumiwa mahakamani. Wanazi walikuwa na polisi wa siri walioitwa Gestapo, polisi wa Muungano wa Sovieti waliitwa KGB, na polisi wa Ujerumani Mashariki waliitwa Stasi. Kwa kushangaza, ili kudhibiti watu wapatao milioni 16, shirika la Stasi liliajiri maafisa 100,000 na watafutaji wa habari wapatao nusu milioni. Maafisa hao walikuwa wakisikiliza mazungumzo ya simu kwa siri kila wakati na walihifadhi habari kuhusu thuluthi ya idadi ya wakazi. Katika kitabu chake kinachoitwa Stasi, John Koehler anasema hivi: ‘Maafisa wa Stasi hawakuogopa wala hawakuona haya. Makasisi wengi, kutia ndani watu wenye madaraka katika makanisa ya Protestanti na Katoliki, walipewa kazi ya kutafuta habari kwa siri. Ofisi zao na vyumba vya kuungama dhambi viliwekwa vifaa vingi vya kusikiliza mazungumzo ya watu kwa siri.’

Hata hivyo, polisi wakali hawapatikani tu katika nchi zenye serikali za kidikteta. Katika majiji fulani makubwa, polisi wameshtakiwa kwa kuwatisha watu wakati wanapotekeleza sheria kwa ukatili, hasa wanapodhulumu vikundi vya watu wachache ambao ni tofauti na wakazi wengine wengi. Likizungumzia kisa kimoja kibaya huko Los Angeles ambacho kilijulikana sana, gazeti moja lilisema kwamba kisa hicho ‘kilionyesha kuwa mwenendo mbaya wa polisi umezidi sana na hata umetokeza usemi mpya, yaani, polisi wakora.’

Kwa hiyo, wenye mamlaka wamekuwa wakijiuliza kile ambacho idara za polisi zinaweza kufanya ili kuboresha sifa zao. Ili kutilia maanani kazi yao kuu ya kuwatumikia watu wote, majeshi mengi ya polisi yamejitahidi hasa kufanya mambo yanayowasaidia watu katika jumuiya.

Msaada wa Polisi Katika Jumuiya

Watu katika nchi nyingine wamevutiwa na utaratibu nchini Japani wa kuwa na polisi katika mitaa mbalimbali. Kwa kawaida, polisi wa Japani hufanya kazi katika vituo vidogo vya maeneo mbalimbali. Kila kituo chaweza kuwa na polisi 12 wanaofanya kazi kwa zamu. Frank Leishman, Mwingereza ambaye ni mhadhiri wa elimu ya uhalifu ambaye ameishi kwa muda mrefu nchini Japani, anasema hivi: ‘Inajulikana sana jinsi maafisa wa polisi katika vituo hivyo vidogo wanavyowasaidia watu kwa urafiki: wao huwasaidia watu wanaotafuta njia katika mitaa ya Japani ambayo haina majina; wakati wa mvua, wao huwaazima miavuli watu wanaonyeshewa wakitoka kazini; wao huwasaidia wafanya-biashara walevi kupanda gari-moshi la mwisho; na kuwapa watu mashauri kuhusu matatizo yao.’ Kwa kuwa kuna polisi katika mitaa ya nchi hiyo, inajulikana kwamba ni salama kutembea kwenye barabara za Japani.

Je, utaratibu huo unaweza kufanikiwa kwingineko? Baadhi ya watu ambao huchunguza uhalifu walipata somo fulani kutokana nao. Ni kana kwamba maendeleo ya mawasiliano yamewatenganisha polisi na watu katika jumuiya. Katika majiji mengi leo, yaonekana kwamba mara nyingi polisi hushughulikia hasa visa vya dharura. Nyakati nyingine ni kana kwamba kazi ya kuzuia uhalifu haitiliwi maanani sana kama ilivyokuwa hapo zamani. Ndiyo sababu majirani wameamua kushirikiana ili kuzuia uhalifu katika mitaa yao.

Ushirikiano ili Kuzuia Uhalifu Mitaani

Dewi, ambaye ni afisa wa polisi, anasema hivi kuhusu kazi yake huko Wales: ‘Ushirikiano huo una faida; unapunguza uhalifu. Majirani hushirikiana pamoja ili kuhakikisha kwamba wenzao wako salama. Sisi hupanga mikutano ili majirani wajuane vizuri, wajue majina na nambari za simu za majirani zao, na kujua jinsi wanavyoweza kuzuia uhalifu. Ninafurahia sana mradi huo kwani unawafanya majirani wawe na ukaribu kama ilivyokuwa zamani. Mara nyingi, watu hata hawajui majirani zao. Mradi huo una matokeo kwa sababu unawasaidia watu kuwa macho.’ Ushirikiano huo pia huboresha uhusiano kati ya polisi na raia.

Polisi pia wamehimizwa kuwahurumia watu walioathiriwa na uhalifu. Jan van Dijk, mtaalamu wa elimu ya watu walioathiriwa na uhalifu, aliandika hivi: “Maafisa wa polisi wanapasa kufundishwa kwamba ni muhimu kushughulika vizuri na watu ambao wameathiriwa na uhalifu sawa na jinsi ilivyo muhimu kwa madaktari kushughulika vizuri na wagonjwa.” Katika sehemu nyingi polisi bado hawaoni ujeuri na ubakaji kuwa matendo ya uhalifu. Lakini Rob Mawby anasema hivi: “Katika miaka ya karibuni polisi wamefanya maendeleo makubwa kwa habari ya jinsi wanavyoshughulikia ujeuri nyumbani na ubakaji. Hata hivyo, bado wanahitaji kufanya maendeleo zaidi.” Pia, polisi katika karibu sehemu zote wanaweza kufanya maendeleo ili watumie mamlaka yao vizuri.

Kuhofu Ufisadi Miongoni mwa Polisi

Mara nyingi inaonekana kuwa upumbavu kufikiri kwamba polisi hutulinda, hasa wakati habari za polisi wafisadi zinaposambaa. Ripoti kuhusu ufisadi zimekuwepo tangu jeshi la polisi lilipoanzishwa. Kikitaja kuhusu mwaka wa 1855, kitabu NYPDA City and Its Police kilieleza “jinsi wakazi wengi wa New York walivyoona ni vigumu kutofautisha kati ya polisi na wakora.” Kitabu Faces of Latin America, kilichoandikwa na Duncan Green, kinaripoti kwamba watu wengi huko huwaona polisi kuwa “wafisadi, kwamba hawawezi kazi, na wanapuuza haki za binadamu.” Afisa-mkuu anayesimamia polisi 14,000 huko Amerika Kusini alisema hivi: “Unatazamia hali iweje wakati polisi mmoja anapolipwa chini ya [dola 100 za Marekani] kwa mwezi? Akihongwa, atafanya nini?”

Ufisadi ni tatizo kubwa kadiri gani? Maoni yanatofautiana. Polisi mmoja huko Amerika Kaskazini ambaye alifanya kazi kwa miaka mingi katika jiji lenye wakazi 100,000 anasema hivi: “Ni kweli kwamba kuna polisi kadhaa ambao ni wakora, lakini polisi wengi ni waaminifu. Nimejionea jambo hilo.” Kwa upande mwingine, jasusi mmoja ambaye amefanya kazi hiyo kwa miaka 26 katika nchi nyingine anasema hivi: “Kwa maoni yangu, ufisadi uko karibu kila mahali. Si rahisi umpate polisi mwaminifu. Polisi akipata pesa wakati anapopekua nyumba iliyoibiwa, anaweza kuchukua pesa hizo. Akipata vitu vyenye thamani vilivyoibwa, atachukua baadhi ya vitu hivyo.” Mbona polisi wengine huwa wafisadi?

Wengine huanza wakiwa wazuri kabisa lakini baadaye wanaathiriwa na polisi wenzao wafisadi na vilevile maovu ya wahalifu wanaoshughulika nao. Kitabu What Cops Know kinamnukuu polisi mmoja wa doria huko Chicago aliyesema hivi: ‘Maafisa wa polisi hushughulika na uovu moja kwa moja. Wamezungukwa na watu waovu, wanaona maovu, na ni lazima washughulike na uovu.’ Mtu anaposhughulika na uovu mwingi hivyo anaweza kuathiriwa vibaya kwa urahisi.

Ijapokuwa polisi hutoa huduma muhimu sana, bado huduma zao si bora kabisa. Je, twaweza kutazamia jambo bora zaidi?

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

“Polisi wa Uingereza Ni Wazuri Sana”

Uingereza ni mojawapo ya nchi za kwanza-kwanza kuwa na jeshi la polisi. Waingereza walitaka jamii yao iwe na utaratibu wa hali ya juu—kama vile magari yao ya abiria ya kukokotwa na farasi yalivyokuwa yakiendeshwa kupatana na saa kabisa. Mnamo mwaka wa 1829, Katibu-Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Bwana Robert (Bobby) Peel, alishawishi Bunge liidhinishe Jeshi la Polisi la London, ambalo lingekuwa na makao makuu huko Scotland Yard. Ijapokuwa hapo mwanzoni polisi hao hawakupendwa kwa sababu ya kuchukua hatua kali dhidi ya walevi na watu waliocheza kamari mitaani, baada ya muda watu wengi wakaanza kuwapenda.

Mnamo mwaka wa 1851, watu kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu walikaribishwa kwenye Maonyesho Makubwa huko London ili wajionee vitu vilivyotengenezwa katika viwanda vya Uingereza. Wageni walishangazwa na utaratibu uliokuwepo katika barabara za jiji, na hakukuwa na walevi, makahaba, wala wazururaji. Polisi waliwaonyesha watu njia, waliwabebea wageni mizigo yao, waliwasaidia watu kuvuka barabara, na hata kuwabeba wanawake wazee hadi kwenye teksi. Basi ndiyo sababu Waingereza na wageni kutoka nchi za nje walisema hivi, “Polisi wa Uingereza ni wazuri sana.”

Polisi hao walizuia uhalifu sana hivi kwamba mnamo mwaka wa 1873 afisa-mkuu wa polisi wa jiji la Chester alisema kwamba siku moja uhalifu ungekomeshwa kabisa! Pia, polisi walianza kutoa huduma za gari la wagonjwa na za wazimamoto. Walianzisha mashirika ya misaada ili kuwapa maskini viatu na mavazi. Wengine walianzisha vyama vya vijana, wakawapangia safari fupi, na kuwapangia mahali ambapo wangeweza kukaa wakati wa likizo.

Ni wazi kwamba jeshi hilo jipya la polisi lilihitaji kuwaadhibu polisi wengine waliohusika katika ufisadi au visa vya ukatili. Lakini wengi wao hawakutumia ukatili ili kudumisha amani. Mnamo mwaka wa 1853, iliwabidi polisi huko Wigan, Lancashire, watulize ghasia zilizosababishwa na wachimbaji wa migodi waliokuwa wamegoma. Wakati sajenti mmoja mjasiri aliyesimamia polisi kumi tu alipopewa bunduki na mwenye mgodi huo, sajenti huyo alikataa katakata. Hector Macleod, ambaye alifuata nyayo za babake na kujiunga na jeshi la polisi, alipokea barua moja mnamo mwaka wa 1886 ambayo inaonyesha mtazamo wa polisi wa wakati huo. Barua hiyo ilinukuliwa katika kitabu The English Police, nayo ilisema hivi: ‘Unapokuwa mkali, raia hawawezi kukuunga mkono. Mimi huwajali watu kwanza, kwa sababu polisi ni mtumishi wa watu, ambao nimeagizwa niwahudumie kwa sasa, na ni wajibu wangu kuwapendeza watu hao na vilevile kumpendeza afisa anayenisimamia.’

Hayden, afisa wa polisi aliyestaafu kutoka Jeshi la Polisi la London, anasema hivi: “Tulifundishwa kwamba twapaswa kujizuia kila wakati kwa sababu tunahitaji kuungwa mkono na watu katika jumuiya ili kazi yetu ifanikiwe. Kile kirungu chetu kifupi cha mbao kilipasa kutumiwa wakati ambapo hatukuwa na chaguo jingine, na polisi wengi hata hawakukitumia kamwe katika kazi yao.” Jambo jingine lililofanya polisi wa Uingereza wapendwe ni kile kipindi maarufu cha televisheni kilichoitwa Dixon of Dock Green kuhusu polisi mmoja mwaminifu ambaye alijua kila mtu katika mtaa aliokuwa akilinda. Kipindi hicho kilionyeshwa kwa miaka 21 na huenda ikawa kiliwatia moyo polisi kuiga mfano wa polisi huyo, lakini ni wazi kwamba kipindi hicho kilifanya Waingereza wapende polisi.

Katika miaka ya 1960, maoni ya watu huko Uingereza yalibadilika. Watu waliacha kuwa wazalendo na wakaanza kulalamika kuhusu mamlaka. Katika miaka ya 1970, ripoti kuhusu polisi wafisadi na wenye ubaguzi wa rangi ziliharibu sifa ya polisi japo walijitahidi kuwapendeza watu kwa kuanzisha ule mpango wa ushirikiano wa majirani ili kuzuia uhalifu. Hivi karibuni, baada ya polisi kushtakiwa kuhusu ubaguzi wa rangi na kutunga ushahidi wa uwongo ili kuwapata watu na hatia, polisi wamejitahidi sana kubadili tabia yao.

[Hisani]

Picha iliyo juu: http://www.constabulary.com

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

Je, Kulitukia Muujiza Huko New York?

Polisi wanapojitahidi sana, wanaweza kupata matokeo ya kustaajabisha sana. Kwa muda mrefu jiji la New York lilionwa kuwa mojawapo ya majiji hatari zaidi ulimwenguni, na kufikia miaka ya mwisho-mwisho ya 1980, ilionekana kwamba maafisa wa polisi waliokuwa wamekata tamaa hawakuweza kuzuia uhalifu. Matatizo ya kiuchumi yalizuia mamlaka ya jiji hilo kuongeza mishahara na kuilazimu kupunguza idadi ya polisi. Wauzaji wa dawa za kulevya walipanua biashara yao na hivyo jeuri ikaongezeka sana. Mara nyingi, watu walioishi katikati ya jiji walisikia milio ya bunduki usiku. Kulikuwa na ghasia za kijamii katika mwaka wa 1991, na polisi walifanya maandamano kwa kelele ili kueleza malalamiko yao.

Hata hivyo, kulitokea afisa-mkuu mpya wa polisi ambaye alipenda kuwatia moyo maafisa wake kwa kukutana nao kwa ukawaida ili kupanga kazi. Alifanya hivyo katika kila kituo cha polisi. James Lardner na Thomas Reppetto walisema hivi katika kitabu chao NYPD: “Maafisa-wakuu wa vituo vya polisi walisoma tu katika magazeti kuhusu mkuu wa wapelelezi au mkuu wa Idara ya Kuzuia Dawa za Kulevya, lakini hawakukutana nao mara nyingi. Sasa walikutana pamoja kwa muda mrefu.” Visa vya uhalifu vikaanza kupungua. Visa vya mauaji vilivyoripotiwa vilipungua pole kwa pole. Mnamo mwaka wa 1993 watu 2,000 hivi waliuawa na mnamo mwaka wa 1998 watu 633 waliuawa. Hiyo ndiyo idadi ndogo zaidi ya mauaji katika kipindi cha miaka 35. Wakazi wa New York waliona badiliko hilo kuwa muujiza. Visa vya uhalifu ambavyo huripotiwa vimepungua kwa asilimia 64 katika miaka minane iliyopita.

Ni nini kilicholeta badiliko hilo? Gazeti la The New York Times la Januari 1, 2002, lilisema kwamba jambo moja ambalo limeleta mafanikio hayo ni programu ya kompyuta inayoitwa Compstat, ambayo ni “mfumo wa kutambua uhalifu kwa kuchunguza takwimu za vituo mbalimbali vya polisi kila juma ili kutambua na kushughulikia matatizo mara tu yanapotokea.” Bernard Kerik, aliyekuwa kamishna-mkuu wa polisi, alisema hivi: “Tulichunguza mahali ambapo uhalifu ulitokea na kwa nini ulitokea, kisha tukawatuma polisi kwenda huko ili kuhakikisha kwamba maeneo hayo yana ulinzi mkali. Hiyo ndiyo njia ya kupunguza uhalifu.”

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kituo cha polisi huko Japani

[Picha katika ukurasa wa 7]

Polisi wa barabarani huko Hong Kong

[Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Polisi wadhibiti umati wakati wa mechi ya kandanda huko Uingereza

[Picha katika ukurasa wa 9]

Kazi za polisi zinatia ndani kuwasaidia watu waliopatwa na aksidenti