Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Barabara Ndefu Zaidi ya Chini ya Ardhi

Barabara Ndefu Zaidi ya Chini ya Ardhi

Barabara Ndefu Zaidi ya Chini ya Ardhi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI NORWAY

UKITAKA kutazama milima mirefu na mikono ya bahari kati ya milima (fiodi), njoo huku sehemu ya magharibi ya Norway! Bila shaka utavutiwa sana! Zaidi ya hayo, kuna barabara nyembamba zinazojipinda na zinazopita chini ya ardhi mara nyingi, ambazo zimejengwa kwa ustadi mwingi. Hivi majuzi barabara ya chini ya ardhi iliyo ndefu kushinda zote duniani ilikamilishwa. Wajenzi walipenya miamba migumu sana. Barabara hiyo inaitwa Barabara ya Chini ya Ardhi ya Laerdal nayo ina urefu wa kilometa 24.5. Wazia kusafiri kwenye barabara hiyo ukijua kwamba juu yako kuna mlima wenye kimo cha meta 1,000!

Barabara hiyo inayopita ya chini ya ardhi ina faida gani? Hiyo ni sehemu ya barabara kuu kati ya miji miwili mikubwa ya Norway, Oslo (mji mkuu, upande wa mashariki) na Bergen (upande wa magharibi wa pwani). Ni vigumu sana kusafiri kutoka mji mmoja hadi mwingine kwenye barabara za milimani katika majira ya theluji yenye dhoruba. Kwa hiyo, barabara inayopitika hata katika hali mbaya ya hewa ilihitajika. Mnamo mwaka wa 1992, bunge la Norway liliamua kwamba sehemu ya barabara hiyo mpya ingepita chini ya ardhi katikati ya vijiji vya Aurland na Laerdal. Barabara hiyo inayopita chini ya ardhi ilifunguliwa mnamo Novemba 2000, baada ya ujenzi wa miaka mitano. Kazi hiyo ngumu ilitimizwaje? Je, ni hatari kusafiri kwenye barabara hiyo ya chini ya ardhi? Kusafiri kwenye barabara hiyo kukoje? Acha tuone.

Matatizo ya Ujenzi

Barabara hiyo ya chini ya ardhi inaanzia Laerdal na kufika Aurland, lakini wafanyakazi walianza kufanya kazi katika sehemu tatu tofauti. Kikundi kimoja kilianzia Laerdal na kingine Aurland. Kikundi cha tatu kilianza kutengeneza kijia cha chini ya ardhi cha hewa chenye urefu wa kilometa mbili. Hicho kingeunganishwa na barabara kuu umbali wa kilometa 6.5 kutoka mlango wa Laerdal. Vikundi hivyo vitatu viliwezaje kuambatanisha uchimbaji ili vyote vikutane chini ya mlima? Setilaiti zilitumiwa kuamua mahali ambapo kila kikundi kingeanzia, na uchimbaji ulielekezwa kwa miale ya leza. Miale hiyo ya leza iliongoza mashine za kuchimbia ili mashimo ya baruti yachimbwe mahali palipofaa kabisa.

Kwa kila mlipuko, mashimo 100 hivi yenye kina cha meta 5.2 yalichimbwa. Mashimo hayo yalijazwa kilogramu 500 hivi za baruti. Kila mlipuko ulivunja meta mchemraba 500 za miamba. Kisha vifusi hivyo viliondolewa kwa lori. Kabla ya kuendelea kuchimba mashimo mengine, kuta zote na vilevile sehemu za juu zilihitaji kuimarishwa. Kuta ziliimarishwa kwa bolti ndefu za feleji na saruji ngumu ikapuliziwa pande zote. Kila kikundi kilisonga mbele meta 60 hadi 70 kwa juma. Mnamo Septemba 1999, vikundi vya wafanyakazi waliochimba barabara kuu walikutana na walikuwa wameachana kwa nusu meta tu. Miezi 14 baadaye, barabara hiyo ya chini ya ardhi ilifunguliwa kufuatana na ratiba. Kufikia hatua hiyo, mradi huo ulikuwa umegharimu dola milioni 120 za Marekani.

Hewa Inaingizwaje?

Kuingiza hewa safi katika barabara za chini ya ardhi ni tatizo ambalo wahandisi hukabili. Kusafiri kwenye barabara hiyo ya chini ya ardhi kutoka upande mmoja hadi mwingine huchukua dakika 20 hivi, kwa hiyo ni lazima hewa safi iwepo. Hewa safi inaingizwaje?

Kijia cha hewa chenye urefu wa kilometa 2 kilicho umbali wa kilometa 6.5 kutoka mlango wa Laerdal, na hewa hutokea kwenye bonde lililo karibu. Hewa safi huvutwa ndani kupitia milango yote miwili ya barabara hiyo ya chini ya ardhi na hewa chafu huondolewa kupitia kijia kidogo. Katika kijia hicho cha hewa kuna feni mbili. Feni hizo zinapofanya kazi kwa wakati mmoja zinaweza kuvuta meta mchemraba milioni 1.7 za hewa kwa saa, na zinaweza kuongeza mtiririko wa hewa uchafuzi ukiwa mwingi. Mfumo huo huleta hewa safi ya kutosha upande wa Laerdal, lakini upande wa Aurland unahitaji hewa zaidi kwa sababu ni mrefu. Kwa hiyo, feni 32 ndogo ziliwekwa upande huo ili kuzidisha mtiririko wa hewa kuelekea kijia cha hewa. Hata hivyo, hewa inayoingia kwenye mlango wa Aurland huzidi kuchafuliwa ikielekea kwenye kijia cha hewa. Tatizo hilo lilisuluhishwa jinsi gani?

Njia nyingine ya chini ya ardhi ilijengwa kando ya barabara kuu, kilometa 9.5 kutoka Aurland, na mtambo wa kusafisha hewa uliwekwa kwenye barabara hiyo. Pande zote mbili za njia hiyo yenye urefu wa meta mia moja zimeunganishwa na barabara kuu. Hewa iliyo katika barabara kuu huelekezwa kwenye njia hiyo na kuvutwa na ule mtambo ambao huondoa asilimia 90 ya mavumbi na nitrojeni dioksidi.

Kwa sababu ya mbinu hizo za kuingiza na kusafisha hewa, magari 400 kwa saa yanaweza kupita kwenye barabara hiyo. Kuna vifaa vya kupima hewa vinavyoonyesha kiwango cha uchafuzi na vinavyoongoza feni. Uchafuzi ukizidi barabara itafungwa, lakini mpaka wakati huu jambo hilo halijahitajika.

Je, Ni Hatari Kusafiri Kwenye Barabara Hiyo?

Watu wengi huogopa kusafiri kwenye barabara ya chini ya ardhi. Kwa sababu hiyo, na kwa sababu ya misiba mibaya na mioto ambayo imetokea kwenye barabara kadhaa za chini ya ardhi huko Ulaya, usalama wa barabara ya chini ya ardhi ya Laerdal umekaziwa sana. Hatari imepunguzwa jinsi gani?

Kituo kimoja huko Laerdal hufuatilia daima mifumo mbalimbali ya kuzuia hatari kwenye barabara hiyo, na hatari ikitokea, barabara itafungwa. Hatua nyingi zimechukuliwa kuwezesha kufunga barabara hiyo kwa haraka na magari kutoka bila kuchelewa. Pia, simu za dharura zinapatikana kila meta 250, na kila meta 125 kuna vizimamoto viwili. Kizimamoto kikiondolewa mahali pake, jambo hilo litagunduliwa mara moja kwenye kituo. Taa nyekundu huonya magari yasiingie kwenye barabara hiyo, na ishara na taa ndani ya barabara hiyo huwaonyesha madereva njia salama ya kutokea. Madereva wanaweza kugeuka kwa kuwa kila baada ya meta 500 kuna sehemu ya kugeukia, na kuna sehemu 15 za kugeuza magari makubwa. Pia, inawezekana kuwasiliana na madereva kupitia redio za magari. Kuna mifumo inayohesabu na kupiga picha magari yote yanayoingia na kutoka katika barabara hiyo. Wenye mamlaka wanaona kwamba usalama huo ni wa hali ya juu kwa kuwa magari machache tu hupita hapo.

Barabara Hii ya Chini ya Ardhi Ni Tofauti kwa Njia Gani?

Kuendesha kwenye barabara ya chini ya ardhi kukoje? Wahandisi walijitahidi kufanya barabara hiyo ipendeze ili madereva wasiwe na wasiwasi na wasisababishe misiba. Ili kutimiza lengo hilo, wataalamu mbalimbali na wabuni wa taa kwenye taasisi moja ya utafiti walisaidia kuchora ramani na vilevile kifaa kinachoigiza mwendo wa gari kilitumiwa.

Matokeo yakawa nini? Barabara hiyo inajipinda kidogo. Hiyo inawazuia madereva wasisinzie, hata hivyo, wanaweza kuona umbali wa meta 1,000. Pia ni rahisi kwa madereva kukadiria umbali kati ya magari yao na magari mengine kwenye barabara isiyonyooka sana. Kuna majumba matatu makubwa ambayo yamzuia msafiri asichoshwe na safari. Dereva anapoingia katika mojawapo ya majumba hayo anahisi kana kwamba anatoka nje, kwa sababu majumba hayo yana mwangaza wa manjano au kijani kibichi kwenye sehemu ya chini na mwangaza wa rangi ya samawati kwenye sehemu ya juu. Hayo yote pamoja na mwangaza wa kutosha kwenye sehemu zote za barabara hiyo huondoa wasiwasi na kuwastarehesha madereva.

Sasa wasafiri wanaweza kufurahia safari ya pekee kwenye barabara ya chini ya ardhi iliyo ndefu kushinda zote duniani. Barabara hiyo ilijengwa kwa ustadi mwingi. Sasa, hata hali ya hewa iweje, inawezekana kusafiri kutoka mashariki mwa Norway hadi magharibi. Barabara hiyo ya chini ya ardhi inaonyesha jinsi wanadamu wanavyoweza kutumia ustadi na ubunifu wao kwa faida nyingi sana.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mahali ambapo barabara ya chini ya ardhi inapita

Laerdal ← → Aurland

[Mchoro/Ramani katika ukurasa wa 27]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Barabara ya Chini ya Ardhi ya Laerdal

Barabara kuu

↑ Kuelekea Laerdal

→ E16 kuelekea Oslo

* Feni kwenye sehemu hizo

Mwelekeo wa hewa

jumba la chini ya mlima

Kituo cha feni → kijia cha hewa

*

jumba la chini ya mlima

*

mtambo wa kusafishia hewa

*

mtambo wa kusafishia hewa

*

*

Mwelekeo wa hewa

Aurland

↓ E16 kuelekea Bergen

Maili 1

Kilometa 1

[Hisani]

Statens vegvesen, Sogn og Fjordane

[Ramani katika ukurasa wa 24]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

NORWAY

Barabara ya Chini ya Ardhi ya Laerdal

Bergen E16 OSLO

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mlango wa Laerdal

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mchoro wa mtambo wa kusafishia hewa

[Picha katika ukurasa wa 25]

Bolti za feleji zinazoimarisha kuta na sehemu ya juu ndani ya barabara

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kuna simu za dharura 100 hivi na vizimamoto 400 hivi

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kuna majumba matatu makubwa yenye mwangaza wa pekee

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Kutoka juu: Picha: Leiv Bergum; mtambo wa kusafishia hewa: ViaNova A/S; picha nyingine zote kwenye ukurasa 24-26: Statens vegvesen, Sogn og Fjordane