Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Stafeli Ni Tunda la Pekee

Stafeli Ni Tunda la Pekee

Stafeli Ni Tunda la Pekee

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

HEBU wazia tunda ambalo lina ladha tamu ya stroberi, mdalasini, embe, na nanasi! Hivyo ndivyo watu wengine hufafanua tunda la stafeli. Iwapo huishi katika eneo la kitropiki basi huenda ikawa hujalionja. Tunda la stafeli (Annona muricata), lina umbo la yai na ngozi ya kijani yenye miiba-miiba na lina nyama nyeupe yenye mbegu nyangavu za kahawia.

Mstafeli ni mti ambao huwa na majani ya kijani mwaka mzima na hauwezi kusitawi katika eneo lenye baridi kali. Maua yake huchavushwa na wadudu wadogo, kama vile chungu na mbawakawa wa aina fulani. Wadudu wengi wa kuchavusha hawavutiwi na mti huo kwani maua yake hayana umajimaji mtamu na rangi za kupendeza. Isitoshe, sehemu za kike na za kiume za maua hayo hupevuka wakati tofauti. Hivyo, mistafeli inayopandwa kwa ajili ya biashara huchavushwa na watu. La sivyo, mstafeli mmoja ungetokeza kati ya matunda 12 na 20 tu kila majira. Matunda ya stafeli huvunwa yanapoelekea kukomaa na huwa mabivu haraka sana. Kwa hiyo, matunda hayo huharibika upesi sana.

Tunda la stafeli linaweza kufikia uzani wa kilogramu tano, nalo ni chanzo cha niacin, riboflavini, na vitamini C, na asilimia 12 ya tunda hilo ina sukari. Hata hivyo, watu wengi hupenda kuongeza sukari wanapokula tunda hilo. Nyama ya tunda hilo husagwa na kuchujwa iwe rojo kisha hutumiwa kutengeneza kinywaji kitamu na barafu ya tunda la stafeli. Chai iliyotengenezwa kwa majani ya mstafeli imetumiwa kutibu ugonjwa wa kuhara damu, mafua, na matatizo ya kumeng’enya chakula. Huko Mexico, chai hiyo imetumiwa kutibu mshtuko wa mwili na vilevile vidonda. Mizizi ya mti huo hutumiwa kuua minyoo, na mbegu zake hutumiwa kufukuza au kuwaua wadudu waharibifu.

Huenda ungependa kuonja tunda hilo la stafeli iwapo linapatikana mahali unapoishi. Utafurahia sana ladha yake!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

Barafu ya Tunda la Stafeli

Vikombe 2 vya rojo ya tunda la stafeli

Kijiko 1 kikubwa cha maji ya limau

Gramu 200 za sukari

Kikombe 1 cha maji

Kikombe 1 cha malai ya maziwa

1. Saga nyama ya stafeli na uichuje kwa kutumia kichujio au kitambaa chembamba. 2. Tia sukari ndani ya maji, kisha uchemshe mchanganyiko huo kwa dakika tano. Acha mchanganyiko huo uwe vuguvugu. 3. Ongeza rojo ya stafeli, malai, na maji ya limau. 4. Mwaga mchanganyiko huo kwenye bakuli yenye kina kifupi, kisha uufunike na kuuweka kwenye friji ya kugandisha hadi ukaribie kuwa mgumu. Koroga mchanganyiko huo sana. Kisha uuweke tena kwenye friji ya kugandisha, na kuuacha uwe mgumu.

[Hisani]

Ukurasa wa 14 juu: Geo Coppens, CIRAD-FLHOR/IPGRI; ukurasa wa 15 juu-kulia: IPGRI-Americas