Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Chui wa Ajabu wa Theluji

Chui wa Ajabu wa Theluji

Chui wa Ajabu wa Theluji

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FINLAND

SI WANYAMA wengi walio wa ajabu kama chui wa theluji. Ni watu wachache tu ambao wamemwona mwituni, si mengi yanayojulikana kuhusu maisha yake.

Chui wa theluji anavutia watu wengi katika Bustani ya Wanyama ya Helsinki, nchini Finland. Anavutia sana kwa tabia zake za ajabu, na hata wengi humwona kuwa mrembo zaidi katika familia ya wanyama ya paka wakubwa.

Paka Anayeishi Kwenye Milima ya Ulimwengu

Ingawa anapatikana angalau katika nchi 12 kutoka Bhutan hadi Urusi, chui wa theluji anakaa sanasana katika Milima ya Himalaya. Milima hiyo mirefu zaidi duniani ni maridadi sana. Lakini wanadamu hawawezi kuishi huko. Kwa hakika, milima hiyo iliyo katika Asia ya Kati ni kati ya maeneo yenye baridi kali zaidi na miamba mingi zaidi ulimwenguni.

Hata hivyo, chui wa theluji hufurahia kuishi kwenye maeneo yenye mwinuko wa meta 3,000 hadi 4,500. Manyoya yake mengi humkinga kabisa na baridi kali, na pua yake kubwa humwezesha kuvuta oksijeni anayohitaji katika mazingira hayo ya milimani yasiyo na hewa ya kutosha. Nyayo zake pana zilizo na manyoya mengi humwezesha kusafiri kasi juu ya theluji nyingi. Namna gani juu ya ile milima yenye miamba mingi? Hilo si tatizo kwa sababu mkia wake mrefu wenye manyoya humsaidia kuruka meta 15 hivi kutoka kwenye jabali moja hadi jingine, akimshinda hata kangaruu mwenye rangi ya kijivu.

Chui wa theluji ana uzani wa kati ya kilogramu 27 na 45, kimo cha sentimeta 60, na urefu wa meta 2 kutoka kwenye pua hadi kwenye mkia. Jambo linalomfanya kuwa wa kipekee ni tabia yake. Kulingana na Leif Blomqvist, msimamizi wa Bustani ya Wanyama ya Helsinki, “chui wa theluji ni mpole sana. Yeye hufanya urafiki na wanadamu kwa urahisi, na yeye huja asubuhi kwenye bustani ya wanyama kumsalimia yule anayemhudumia.” Blomqvist anaongeza kusema kwamba chui wadogo wa theluji ni wapole pia. Anasema hivi: “Wao hawang’ang’ani na wafanyakazi wakati wanapopimwa au kupewa chanjo.” Lakini namna gani ukimshika chui wa aina nyingine wa umri huo? “Ni vigumu sana kuwashika,” Blomqvist anasema. “Unahitaji mavazi na glavu za kujikinga, kwa sababu wao wanaweza kumshambulia mtu.”

Kwa Nini Hawaonekani Sana?

Kujaribu kumpata huyo chui wa theluji mwenye rangi nyeupe na ya kijivu si rahisi. Hii ni kwa sababu yeye haonekani katika mazingira ya milimani na hii inaeleza kwa nini ni chui wachache tu wa theluji ambao wameonekana mwituni. Kwa sababu hiyo watafiti wengi ambao wamezunguka milimani kumchunguza paka huyo wa ajabu hawajamwona hata mmoja!

Isitoshe, chui wa theluji hukaa peke yake, na jambo hilo hufanya iwe vigumu kumwona. Pia, eneo wanakokaa ni pana sana kwa sababu wao kwa kawaida huwinda mbuzi-mwitu na kondoo-mwitu ambao hawapatikani kwa wingi milimani. Kwa kusikitisha, wawindaji haramu—wanaotafuta ngozi ya chui wa theluji kwa pupa—wamepunguza idadi ya wanyama hao hivi kwamba sasa wamo katika orodha ya wale wanyama walio karibu kutoweka. * Bustani za wanyama zinajitahidi sana kumhifadhi mnyama huyo wa kipekee.

Chui wa Theluji Katika Bustani ya Wanyama ya Helsinki

Bustani ya Wanyama ya Helsinki imefanikiwa sana kuzalisha chui wa theluji. Mnamo 1976 bustani hiyo ilipewa jukumu la kuweka rekodi za chui wa theluji ulimwenguni kote. Rekodi hiyo imekuwa muhimu katika kushughulikia chui wa theluji wanaohifadhiwa.

Kuna rekodi nyingine kama hizo za aina nyingi za wanyama wanaohifadhiwa katika bustani za wanyama, lakini hasa ni za wale walio karibu kutoweka. Rekodi hizo huorodhesha habari za wanyama wote wa aina moja wanaoishi katika bustani ya wanyama. Bustani za wanyama zina jukumu la kutoa habari kwa mweka-rekodi kuhusu wanyama wanaozaliwa na pia wale wanaohamishwa au kufa. Rekodi hizo hutumiwa kuchagua wanyama watakaotumiwa kuzalisha wanyama wengine. Blomqvist anaeleza: “Kwa kuwa wanyama si wengi, ubora wa wanyama wanaozaliwa unaweza kupungua kwa urahisi kwa sababu ya kuzaana kati yao tu.”

Zaidi ya chui wachanga mia moja wamezaliwa katika Bustani ya Wanyama ya Helsinki pekee, na wengi wao wamehamishwa hadi kwenye bustani nyingine za wanyama. Ili kuhakikisha kuna namna nyingi za chui wa theluji, wanyama hubadilishwa kutoka kwenye bustani moja ya wanyama hadi nyingine. Sasa kuna namna nyingi za chui wa theluji katika bustani za wanyama hivi kwamba hakuna haja tena ya kuwashika wale walioko mwituni.

Bustani nyingi za wanyama, kutia ndani ile ya Helsinki, zinasaidia kuhifadhi wanyama-pori wenye afya. Bila shaka, bustani hizo pia husaidia wale wanaozitembelea kuona wanyama wa kipekee. Kwa kweli, yule ambaye amemwona chui wa theluji hawezi kumsahau kwa urahisi na sifa zinamwendea Muumba ambaye ‘amefanya kila kitu kizuri.’—Mhubiri 3:11.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Ni vigumu kutaja kwa uhakika ni chui wangapi wa theluji ambao wamebaki. Makadirio yanaonyesha kwamba kuna kati ya chui wa theluji 3,500 hadi 7,000.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Ukurasa wa 16: Katikati: ©Aaron Ferster, Photo Researchers; ukurasa wa 17: Juu kulia: © Korkeasaaren Eläintarha/Markku Bussman; chini: ©T. Kitchin/V. Hurst, Photo Researchers

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Chuck Dresner/Saint Louis Zoo