Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Buibui Anayejifanya Kuwa Chungu

Buibui Anayejifanya Kuwa Chungu

Buibui Anayejifanya Kuwa Chungu

KUNA buibui mmoja mdogo ambaye huingia ndani ya kichuguu na kuishi humo kisiri miongoni mwa adui zake. Ili asitambuliwe, yeye hubadili sura yake na tabia yake. Hilo ni la maana kwa kuwa chungu wanaweza kuwa wakali sana wanapochokozwa. Lakini jambo hilo si rahisi kwani mwili wa buibui huyo ni tofauti na ule wa chungu.

Chungu ana miguu sita na vipapasio viwili, na buibui huyo ana miguu minane lakini hana vipapasio. Basi buibui huyo hufanya nini ili kufanana na chungu? Yeye hutembea humo kichuguuni akitumia miguu sita, naye huifanya miguu yake miwili ya mbele iwe kama vipapasio.

Isitoshe, buibui huyo husogeza vipapasio vyake bandia kama vile chungu wanavyosogeza vipapasio vyao, hivi kwamba vinadhaniwa kuwa vipapasio halisi vya chungu. Mwigizaji huyo hata hutembea huku akitua mara kwa mara na kwa mwendo wa kujipindapinda kama vile chungu wanavyofanya!

Buibui huyo hujaribu kujifanya afanane kabisa na chungu kwa sababu ni lazima akubaliwe kuwa mkazi wa kichuguu ili awe salama. Ndani ya kichuguu, buibui huyo hawezi kushambuliwa na adui zake kama vile nyigu anayewinda buibui. Chiriku wanaopenda kula buibui pia hawamshambulii. Hata buibui wanaowinda buibui wengine hudanganywa kwa sababu ya vipapasio vyake bandia.

Lakini, wakati ndege, mjusi, au kiumbe mwingine anapowashambulia chungu, buibui huyo huacha kujifanya na kutoroka. Buibui wanaweza kutoroka kwa urahisi kwa sababu wao huona vizuri kuliko chungu na wanaweza kuruka, lakini chungu hawawezi kuruka.

Mchana wote, buibui hukaa ndani ya kichuguu huku akifanya yote awezayo ili asitambuliwe na chungu. Hata hivyo, wakati wa usiku yeye huwinda na kuwakamata chungu wale anaoishi nao! Buibui huyo anapogunduliwa, yeye hutumia miguu yake minane kutoroka haraka.

Huenda buibui jike akajiunga na buibui wa kiume anayeishi kichuguuni. Buibui-jike ni mwaminifu kwa mwenzi wake na vilevile mbunifu. Buibui-jike hujijengea utando ndani ya kichuguu. Utando huo humlinda mwenzi wake na vilevile mayai yake.

Hapana shaka kwamba kuna mambo mengi yasiyojulikana kuhusu buibui huyo. Wakati ujao, tutafurahia kujifunza mengi zaidi kuhusu uumbaji wa ajabu wa Mungu!

[Picha katika ukurasa wa 31]

Buibui akiwa katikati ya chungu wawili

[Hisani]

Bill Beatty