Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Utalii Biashara ya Ulimwenguni Pote

Utalii Biashara ya Ulimwenguni Pote

Utalii Biashara ya Ulimwenguni Pote

Na mwandishi wa Amkeni! katika Visiwa vya Bahamas

MARA yako ya mwisho kutaka kwenda likizo ilikuwa lini? Huenda ulihisi kwamba ulihitaji kupumzika na kusahau taabu za kila siku. Je, umewahi kwenda likizo katika nchi ya mbali? Fikiria jambo hili: Karne moja hivi iliyopita, watu wengi duniani hawakuwa wakienda likizo kwa ukawaida. Na zaidi, watu wengi walikaa karibu na kwao maisha yao yote bila kutembelea maeneo ya mbali. Kusafiri nchi za mbali ili kustarehe au kujielimisha kulikuwa jambo la pekee na ni watu wachache tu matajiri au waliopenda kusafiri ambao waliweza kufanya hivyo. Lakini siku hizi, mamia ya maelfu ya watu wanaweza kusafiri kokote katika nchi yao au hata ulimwenguni. Ni nini kilichosababisha badiliko hilo?

Baada ya yale maendeleo makubwa ya kiviwanda, mamilioni ya watu waliajiriwa kazi za kutengeneza bidhaa na kutoa huduma. Matokeo yakawa kwamba watu walichuma mapato mengi. Kwa sababu ya maendeleo ya tekinolojia, mashine zilibuniwa nazo zilipunguza kazi na gharama. Hivyo, watu wengi walipata wasaa wa kustarehe. Kwa kuongezea mambo hayo, usafiri wa umma wa bei nafuu ulipoanzishwa katikati ya miaka ya 1900, biashara ya utalii ilisitawi. Kisha, matangazo ya televisheni yaliyokuwa tu yametoka kuanzishwa, yaliwachochea watu kusafiri kwa kuwaonyesha watu ulimwenguni pote picha za maeneo ya mbali wakiwa nyumbani mwao.

Basi, biashara ya utalii ulimwenguni pote ikasitawi haraka. Shirika la Utalii Ulimwenguni lilitabiri kwamba idadi ya watu wanaotalii nchi za nje ingeongezeka kutoka milioni 613 kama ilivyokuwa katika mwaka wa 1997, hadi bilioni 1.6 katika mwaka wa 2020, na hakukuwa na dalili yoyote ya kupungua wakati huo. Kukiwa na ongezeko hilo la watalii, idadi ya biashara, hoteli, na nchi zinazowahudumia watalii iliongezeka pia.

Nchi Nyingi Zaanzisha Utalii

Utalii hufaidi wahusika wote. Mtalii anapotembelea nchi ya kigeni yeye hutumbuizwa au kuelimishwa. Lakini nchi zinazowahudumia watalii hufaidikaje? Utalii wa kimataifa huwezesha nchi hizo kupata fedha za kigeni. Nchi nyingi huhitaji fedha za kigeni ili kulipia huduma na bidhaa zinazotoka katika nchi nyingine.

Ripoti moja ya Shirika la Utalii Ulimwenguni ilisema hivi: ‘Utalii wa kimataifa ndio huingiza fedha nyingi za kigeni ambazo ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi nyingi. Mnamo mwaka wa 1996, utalii wa kimataifa ulichuma fedha za kigeni zenye thamani ya dola bilioni 423 za Marekani. Mapato hayo yalikuwa zaidi ya yale yaliyochumwa kwa kuuza mafuta, magari, vyombo vya mawasiliano, nguo, na kadhalika, katika nchi nyingine.’ Ripoti iyo hiyo ilisema hivi: “Utalii ndio biashara inayositawi zaidi ulimwenguni,” na ilitokeza ‘asilimia 10 ya Jumla ya Pato la Nchi zote ulimwenguni.’ Haishangazi kwamba nchi nyingi, kutia ndani baadhi ya zile zilizokuwa Muungano wa Sovieti, zimejiunga—au zinaharakisha kujiunga—na biashara ya utalii wa kimataifa.

Mapato ya serikali yanayochumwa kutokana na utalii yanatumiwa kuboresha mifumo ya umma, viwango vya elimu, na kutimiza mahitaji mengine makubwa ya taifa. Karibu serikali zote hutaka raia wake wawe na kazi ya kuajiriwa. Utalii husaidia kutokeza kazi za kuajiriwa.

Ili kuonyesha jinsi utalii unavyoweza kuboresha uchumi wa nchi, fikiria Visiwa vya Bahamas, taifa dogo la visiwa vilivyo karibu na Ghuba ya Mexico kati ya jimbo la Florida huko Marekani na kisiwa cha Kuba. Visiwa vya Bahamas havina mali ghafi nyingi wala wenyeji wake hawafanyi ukulima kwa kadiri kubwa. Lakini visiwa hivyo huwa na halihewa yenye joto, pwani safi za tropiki, wakazi wenye urafiki wapatao 250,000, na viko karibu na Marekani. Mambo hayo yamewezesha biashara ya utalii isitawi. Lakini ni nini kinachohitajiwa ili kuwafurahisha na kuwalinda watalii wanapokuwa likizoni?

Kuwaridhisha Watalii wa Kisasa

Biashara ya utalii wa kimataifa ilipoanza, watalii wengi walifurahia tu kutembelea nchi nyingine—japo kulikuwa na magumu ya usafiri. Hata hivyo, watu wengi leo huona maeneo ya mbali kwenye televisheni wanapostarehe nyumbani mwao. Hivyo, wenye hoteli hukabili ugumu wa kufanya safari ya mtalii iwe yenye kufurahisha huku wakimfanya astarehe kana kwamba yuko nyumbani kwake au hata zaidi. Isitoshe, kwa kuwa watalii wengi husafiri mara nyingi, nchi mbalimbali hushindana kutoa huduma bora.

Jambo hilo limetokeza vivutio na hoteli zenye kupendeza. Kwa mfano, fikiria hoteli moja kubwa ya hali ya juu kwenye Visiwa vya Bahamas. “Jengo hilo limeundwa ili kufurahisha,” asema Beverly Saunders, mkurugenzi wa usimamizi kwenye hoteli hiyo. “Lakini bado tunataka ufurahi hata zaidi. Tunataka ushirikiano wako pamoja na wenyeji ukufurahishe pia.” Hoteli hizo hushughulikiaje mahitaji ya wageni?

Kazi Inayofanywa Hotelini

Beverly asema hivi: “Hoteli yetu yenye vyumba 2,300 inapojaa, sisi hushughulikia mahitaji ya wageni kati ya 7,500 na 8,000 kwa kipindi kimoja. Kazi ya usimamizi ni ngumu sana. Utaratibu unaohitajika ili kutosheleza mahitaji ya wageni wote hao unalingana na ule wa kusimamia jiji dogo lakini kukiwa na magumu mengi zaidi. Tunapaswa kuandaa vyakula ambavyo wageni hao wamezoea kula nyumbani kwao. Lakini ili waweze kufurahia safari yao, ni lazima pia tuandae vyakula na tafrija ambayo hawajazoea. Katika hoteli nyingi, asilimia 50 au zaidi ya wafanyakazi hushughulikia vyakula na vinywaji.”

Hata hivyo, kama vile I. K. Pradhan anavyosema katika makala yake yenye kichwa “Athari ya Utalii Juu ya Jamii na Utamaduni Huko Nepal,” ‘kile kinachowafurahisha watalii zaidi ni jinsi wanavyotendewa na wenyeji na kujihisi wako salama.’

Hoteli za ulimwengu zenye mafanikio huwezaje kutosheleza matakwa hayo? Meneja mmoja anayesimamia mazoezi ya wafanyakazi kwenye hoteli maarufu ya Visiwa vya Bahamas alijibu swali hilo hivi: ‘Jitihada ya kuendelea kuwazoeza, kuwakosoa, na kuwafunza wafanyakazi adabu nzuri yatakikana, ili kuandaa huduma bora. Wenyeji wengi wa Visiwa vya Bahamas ni wenye urafiki. Lakini ni vigumu kuendelea kuwa mchangamfu, mwenye furaha, na kutabasamu kila wakati ukiwa kazini. Ndiyo sababu tunakazia umuhimu wa kuchukua kwa uzito kazi yoyote ile wanayofanya kama vile daktari, wakili, au wakala wa bima wanavyofanya kazi yao. Sisi hufanya kazi yoyote ile kwa kupatana kabisa na viwango vya kimataifa. Kadiri tunavyofanya kazi kwa bidii tukiwa pamoja ili kufikia viwango hivyo, ndivyo tunavyoendelea kufanya kazi yetu kwa njia bora na kwa kiwango cha juu.’

Matatizo ya Utalii

Iwapo umewahi kusafiri, je, umeona kwamba licha ya kupanga mambo kikamili, huenda hukupangia gharama fulani? Watu wanaofanya biashara ya utalii wanapatwa na hali iyo hiyo.

Pradhan, aliyenukuliwa awali, anasema kwamba “biashara ya utalii inaweza kunufaisha sana jamii yetu inayoendelea.” Hata hivyo, anasema kwamba pasipo kuchukua hatua zifaazo, “matatizo makubwa ya kijamii yanaweza kutokea.” Anaongeza hivi: “[Twahitaji] kujitayarisha ifaavyo tukiwa chonjo kuhusu athari mbalimbali za utalii wa kisasa.” Alikuwa akizungumzia matatizo gani?

“Mara nyingi, utamaduni wa mataifa yanayowahudumia watalii wengi huharibika bila kukusudia. Katika maeneo fulani, utamaduni wa wenyeji umetoweka.” Hivyo ndivyo Cordell Thompson, afisa mmoja mkuu katika Wizara ya Utalii ya Visiwa vya Bahamas, anavyoeleza athari moja ya kawaida. Thompson anaonea fahari faida zote ambazo nchi hiyo imepata kutokana na biashara ya utalii. Hata hivyo, anakubali kwamba athari nyingine zisizotazamiwa zimetokea katika nchi zenye watalii wengi kuliko wenyeji.

Kwa mfano, watu fulani wanaofanya kazi ya kuwahudumia watalii huanza kufikiri kimakosa kwamba mtalii huwa likizoni daima. Huenda wenyeji hao wakajaribu kuishi maisha hayo ya starehe. Wengine huathiriwa kwa njia tofauti. Kwa kutumia muda mwingi sana katika sehemu za starehe za watalii, wao husahau utamaduni wao hatimaye. Nyakati nyingine wenyeji wengi huzoea kutembelea sehemu za tafrija za watalii hivi kwamba vituo vya utamaduni hukosa watu, na kufungwa.

Nchi nyingi zinazotembelewa sana na watalii hukabili uchaguzi mgumu. Nchi hizo hutaka mapato yanayotokana na idadi kubwa ya watalii. Lakini, zinakumbwa na matatizo mengi ya kijamii yanayosababishwa na biashara zinazoanzishwa ili kutosheleza tamaa mbaya za watalii fulani.

Utalii Ambao Hausababishi Hasara

Kwa kuwa faida kubwa zinazotokana na utalii wa kisasa zinasababisha pia hasara kubwa ambazo zinaharibu biashara hiyo, siku hizi watu wengi wanazungumza kuhusu utalii ambao hausababishi hasara. Hivyo, watu wengi wameng’amua kwamba faida za muda mfupi zinazotokana na biashara fulani za kuwafurahisha watalii zinahatarisha utalii. Masuala fulani tata yatahitaji kushughulikiwa ili biashara hiyo iweze kudumu.

Baadhi ya masuala ambayo yatahitaji kushughulikiwa wakati ujao yanatia ndani athari ya utalii juu ya mazingira na utamaduni wa wenyeji, na upatano kati ya miradi ya hoteli kubwakubwa na miradi ya nchi zinazotembelewa na watalii. Hivi majuzi, mahangaiko kuhusu usalama yameathiri sana usafiri, na mahangaiko hayo yanapasa kushughulikiwa hatimaye. Bado haijulikani jinsi mambo hayo yatakavyoathiri utalii wakati ujao.

Utakapoamua kwenda likizo ili kupumzika kwenye hoteli fulani katika eneo la mbali, yatumainiwa kwamba utathamini biashara hiyo ya ulimwenguni pote, yaani, utalii wa kitaifa na wa kimataifa.

[Picha katika ukurasa wa 15]