Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Viumbe Waharibifu

Gazeti la International Herald Tribune lasema hivi: “Viumbe ‘wageni’ waharibifu wanasababisha hasara ipatayo mamia ya mabilioni ya dola ulimwenguni pote kila mwaka na wanaeneza magonjwa na kuharibu sana mazingira.” Mimea na wanyama wengi ambao si waharibifu katika mazingira yao ya asili huhamishwa kwenye maeneo mengine makusudi au bila kukusudia. Kwa mfano, nyoka-miti wanaopatikana hasa nchini Australia na Indonesia, wamewaangamiza ndege wa msituni kwenye kisiwa cha Guam na wanaendelea kuongezeka kwenye eneo la Bahari ya Pasifiki—nyakati nyingine kwa kujificha kwenye nafasi za kuwekea magurudumu ya ndege. Viumbe wengi wanaoishi majini wameangamia kwa sababu mwani wa caulerpa na gugumaji la Amerika Kusini lilihamishwa kwenye makao yao. Nyasi zilizopelekwa nchini China kutoka Marekani ili zipandwe kwenye viwanja vya gofu zinasambaa kotekote sasa, huku mbawakawa wa China waliojificha katika mbao za kubebea mizigo, wanaharibu misitu ya Amerika Kaskazini. Viumbe wengine waharibifu wanatia ndani nguchiro wa India, kome aina ya zebra, mti wa Miconia, sangara, kuchakuro wa kijivu wa Amerika Kaskazini, kambare, konokono aina ya Rosy wolf, na chungu wa aina fulani.

Vipodozi vya Watoto

Gazeti la The Japan Times lasema kwamba watengenezaji wa vipodozi huko Japani wanauza vipodozi vilivyoundwa hasa kwa ajili ya watoto. Kufuatia msisimuko uliopo katika nchi hiyo kuhusu vipodozi, wasichana wachanga, hata wale ambao hawajabalehe, wanamiminika madukani kununua bidhaa kama vile rangi ya mdomo inayometameta na wanja ili kuiga wanamuziki wanaowapenda. Hapo zamani, watoto walipaka rangi mdomoni kama mchezo tu. Sasa, watoto wengi zaidi wanatumia vipodozi na wanataka kujua jinsi vinavyoweza kutumiwa kurembesha sura. Mhariri mmoja wa gazeti la watoto alisema hivi: “Siku hizi vijana wengi hawaoni haya. Watoto wa siku hizi wanajua udhaifu wao wanapokuwa wachanga sana kuliko watoto wa zamani.” Hata hivyo, shirika moja lilikataa wazo hilo la kuwatengenezea watoto vipodozi kwa kusema hivi: “Kulingana na utamaduni wa Japani, haifai watoto wa shule za msingi kutumia vipodozi. Hatutawatengenezea (watoto) vipodozi kwa sababu ya maadili ya jamii.”

Ugonjwa wa Vitoto Vilivyotikiswa

Gazeti la El Universal la Mexico City lasema kukitikisa kitoto kwa kukishika mikono, miguu, au mabega kwaweza kukiletea matatizo makubwa ya afya. ‘Madaktari fulani wanaamini kwamba watu wengi wana matatizo ya kujifunza kwa sababu walitikiswa walipokuwa wachanga.’ Juan José Ramos Suárez, mtaalamu wa magonjwa ya watoto, asema kwamba ‘hali hiyo yaweza kusababisha kitoto kivuje damu ubongoni na kupata madhara ya ubongo hata ingawa hakina majeraha yoyote.’ Anasema kwamba hali hiyo inaweza pia kumfanya mtu awe kiziwi, kipofu, aharibike uti wa mgongo, apooze, apapatike mwili, na hata kufa. Hiyo ni kwa sababu kichwa cha kitoto ni kizito, na misuli ya shingo haina nguvu sana na haiwezi kuhimili shinikizo la kutikiswa. Ni kweli kwamba kilio cha kitoto chaweza kuudhi. Lakini ili kuwasaidia watu wanaowatunza watoto, gazeti hilo ladokeza “hatua tatu zinazoweza kuchukuliwa kwa muda mfupi tu: (1) Tua, (2) keti chini, na (3) utulie. Dhibiti hisia zako badala ya kukikasirikia kitoto.” Kisha ushughulikie kile kinachofanya kitoto kilie—labda kwa kukilisha au kukibadilisha nepi—au ufanye mambo yatakayokituliza na kukifurahisha.

Kutoweka kwa Gondola?

Gazeti la The Independent la London lasema kwamba ‘ufundi wa kale wa kujenga mashua za gondola unatoweka pole kwa pole huko Venice. Huenda gondola za wakati ujao zikajengwa na mafundi wasio stadi na hivyo kutoendeleza ustadi, vifaa na utamaduni wa mojawapo ya majiji yenye kupendeza zaidi ulimwenguni.’ Ufundi wa kujenga mashua hizo maarufu, ulioanza katika karne ya 11, unaelekea kutoweka “kwa kuwa ule utaratibu wa zamani wa kupokeza biashara hiyo, kutoka kwa baba hadi mwana au kutoka kwa fundi hadi mwanafunzi, hauendelei.” Utaratibu huo umekoma kwa sababu ya gharama nyingi za kazi na pia vijana wa Venice hawataki kutumia miaka 20 kujifunza ufundi huo. Kwa hiyo, yaonekana kwamba mafundi waliopo sasa wakistaafu, hakuna atakayechukua mahala pao. Gondola moja hujengwa kwa muda wa saa 500. Mashua ya gondola ni tofauti na mashua nyingine kwani upande wa kushoto ni mpana kuliko upande wa kulia. Mashua hiyo husawazishwa na uzito wa mwendesha-gondola na makasia yake. Muundo huo usiolingana unamwezesha mwendesha-gondola kupitia mifereji myembamba ya Venice.

Uharamia Unaongezeka

Gazeti la Valeurs Actuelles la Kifaransa laripoti kwamba “uharamia unaongezeka.” Mashambulizi ya maharamia yameongezeka zaidi ya maradufu katika miaka miwili iliyopita. Hali hiyo imezidi hasa huko Kusini-Mashariki mwa Asia, ambako matatizo ya kiuchumi yamewafanya maskini kugeukia uhalifu. Lakini uharamia unaongezeka pia katika bahari za Afrika na za Amerika Kusini. Edouard Berlhet, mwakilishi wa Kamati Maalumu ya Wamilikaji wa Meli wa Ufaransa, alisema kwamba “mnamo mwaka wa 1998, kulikuwa na hasara ya dola bilioni 16 za Marekani. Meli nyingine hutoweka kabisa pamoja na mizigo. Meli hizo hutekwa nyara na kubadilishwa, kisha zinatokea tena kwenye bandari zinazoshukiwa huku zikitumia bendera ya nchi nyingine ili kukwepa kodi na malipo mengine.” Maharamia hao wanaotumia meli zinazokwenda kasi na vifaa vya mawasiliano vya hali ya juu, huwa na bunduki kubwakubwa na ni wajeuri sana.

Vijana Walevi

Gazeti la Süddeutsche Zeitung la Ujerumani laripoti kwamba ‘vijana wachanga huko Ulaya hulewa mara nyingi.’ Mawaziri wa afya wa Muungano wa Ulaya walifahamishwa jambo hilo linaloshtua hivi majuzi. Tatizo hilo ni kubwa kadiri gani? Uchunguzi uliofanywa mwaka wa 1998 ulionyesha kwamba katika nchi fulani kati ya asilimia 40 na 50 ya vijana wenye umri wa miaka 15 hunywa pombe kwa ukawaida, huku wasichana wa umri huohuo huko Uingereza, Scotland, na Wales hunywa divai na mivinyo mingine zaidi ya wavulana. Zaidi ya nusu ya wavulana wenye umri wa miaka 15 huko Denmark, Finland, na Uingereza, wamelewa chakari zaidi ya mara moja. Maelfu ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 29 katika Muungano huo hufa kila mwaka kwa sababu ya kileo. Baraza la Mawaziri limependekeza kwamba vijana waelimishwe kuhusu vileo ili wafahamu madhara yake.

Je, Uvutaji wa Sigara Unasaidia Uchumi?

“Maafisa wa Kampuni ya Philip Morris katika Jamhuri ya Cheki wamekuwa wakisambaza ripoti ya kiuchumi inayoonyesha kwamba . . . vifo vya mapema vya wavutaji wa sigara hupunguza gharama za matibabu,” lasema gazeti la The Wall Street Journal. “Ripoti hiyo, iliyoagizwa na kampuni hiyo . . . , inajumlisha ‘faida’ za kuvuta sigara juu ya uchumi wa nchi, kutia ndani mapato yanayopatikana kwa kodi za sigara na jinsi ‘gharama za matibabu hupunguzwa kwa sababu ya kifo cha mapema.’” Makala hiyo yaongeza: ‘Kwa kuhesabu faida na hasara, ripoti hiyo yakata kauli kwamba mnamo mwaka wa 1999 serikali ilipata pato halisi la dola milioni 147.1 za Marekani kutokana na biashara ya sigara.’ Watu walilalamika mara moja kuhusu ripoti hiyo. Mwandishi mmoja wa gazeti alisema hivi: “Hapo zamani, makampuni ya sigara yalikuwa yakisema kwamba sigara haziui watu. Sasa yanajivunia vifo vya wavutaji.” Mtaalamu wa uchumi Kenneth Warner alisema hivi: “Sifikiri kuna kampuni nyingine inayoweza kujivuna kwamba inasaidia serikali kuchuma fedha kwa kuwaua wateja wake.” Juma moja baadaye, Kampuni ya Philip Morris iliomba msamaha. Steven C. Parrish, makamu-msimamizi, alisema hivi: ‘Tunafahamu kwamba tulifanya kosa zito. Lilikuwa jambo baya kabisa.’

Kuwasaidia Watoto Kutopenda Mali Sana

Gazeti la Globe and Mail la Kanada laripoti kwamba “wafanyabiashara huwalenga watoto hasa” huku watoto wachanga wakipenda sana kununuliwa vitu. “Na hakuna jambo lolote ambalo limeweza kukomesha hali hiyo.” Hata hivyo, kundi la maprofesa kwenye Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Stanford wanadhani kwamba wamepata utatuzi. Maprofesa hao walipanga mtaala wa miezi sita ili kuwasaidia watoto kupunguza muda wao wa kutazama televisheni na kuwasaidia kuteua mambo wanayotazama. Baada ya kumaliza mwaka wa shule, watoto waliokuwa katika mpango huo hawakuomba sana wanunuliwe vitu na wazazi wao. Kwa mujibu wa gazeti la Globe, ‘kwa kawaida mtoto hutazama matangazo ya biashara 40,000 kila mwaka. Katika miaka ya 1970, watoto walikuwa wakitazama matangazo ya biashara 20,000 kila mwaka.’