Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kisima Kikuu cha Artesia Ni Nini

Kisima Kikuu cha Artesia Ni Nini

Kisima Kikuu cha Artesia Ni Nini

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

TUNAPOSAFIRI kwa ndege kuelekea magharibi na kufika mwisho wa safu ya milima mikubwa ya pwani ya Australia, twaona mandhari yenye kupendeza. Anga lenye rangi ya samawati latanda juu ya mandhari hiyo. Ardhi ni tambarare. Twapita eneo lenye mimea ya rangi ya kijani-kibichi na nyanda za rangi ya dhahabu na kuona eneo lenye udongo mwekundu na nyasi kavu hapa na pale.

Amini usiamini, chini ya ardhi hiyo kuna maji mengi sana. Kiasi cha maji hayo ni theluthi mbili ya yale yanayopatikana katika Bahari ya Mediterania. Bonde hilo kubwa la maji ya chini ya ardhi huitwa Kisima Kikuu cha Artesia.

Kisima hicho ni muhimu kwa watu wanaojiruzuku katika maeneo yenye joto yaliyo mbali na pwani ya Australia. Ili tuelewe kwa nini kisima hicho ni muhimu sana na jinsi kilivyofanyizwa, ni lazima kwanza tuifahamu nchi ya Australia.

Nchi Kavu

Australia ni nchi kavu. Australia ndilo bara dogo zaidi kati ya yale mabara matano ulimwenguni na jangwa la pili kubwa duniani liko huko. Mto Darling, ambao ni mojawapo ya mito mirefu zaidi ulimwenguni, uko huko pia. Hata hivyo, mito ya Australia haina maji mengi. Kiasi cha maji yanayotiririka kila mwaka hadi baharini kutoka kwenye Mto Mississippi huko Marekani, kinazidi kile cha mito yote ya Australia kwa mara 60. Mbona mvua hainyeshi sana huko?

Kwa kuwa bara hilo liko kwenye latitudo ya kusini ya digrii 30, halihewa yake huathiriwa sana na pepo zenye kani-eneo ya juu. Pepo hizo husukuma hewa yenye joto katikati ya nchi hiyo. Kwa kuwa eneo ni tambarare, pepo hizo hazipiti kwenye milima mirefu na hivyo mvuke hubaki hewani. Safu ya milima mirefu huwa tu kwenye pwani ya mashariki ya bara hilo. Mlima mrefu zaidi katika safu hiyo una urefu wa meta 2,228, na hivyo ni mlima mfupi sana ukilinganishwa na milima mingine ulimwenguni. Pepo za mvua zinazoelekea nchi kavu kutoka upande wa mashariki kwenye Bahari ya Pasifiki, huzuiwa na milima hiyo na hivyo mvua hunyesha kwenye eneo dogo tu la pwani. Australia ndilo bara kavu zaidi duniani kwa sababu ni tambarare, lina halijoto za juu, na kwa sababu ya mahala ambapo milima yake ipo.

Maji Mengi Chini ya Ardhi

Chini ya ardhi kavu ya Australia kuna visima 19 vikubwa. Kisima kikubwa zaidi, kinachoitwa Kisima Kikuu cha Artesia, kiko chini ya asilimia 20 ya bara hilo. Kisima hicho kina ukubwa wa kilometa za mraba milioni 1.7, kutoka kwenye Rasi ya York upande wa kaskazini hadi Ziwa Eyre huko Australia Kusini. Kisima hicho kina lita bilioni 8,700 za maji. Maji hayo yakijazwa katika maziwa ya Michigan na Huron huko Amerika Kaskazini, maziwa hayo yatafurika.

Hata hivyo, maji ya Kisima Kikuu cha Artesia hayapatikani kwa urahisi kama yale yanayotoka kwenye Maziwa Makuu ya Amerika Kaskazini. Maji ya mvua huingia katika kisima hicho kupitia udongoni na kufyonzwa na matabaka ya jiwe-mchanga yenye maji. Kila siku, lita milioni 300 hivi za maji huingia katika kisima hicho kwa njia hiyo. Maji yote hayo huenda wapi?

Kulowesha Sifongo Kubwa

Kisima Kikuu cha Artesia ni kama sifongo kubwa. Matabaka ya jiwe-mchanga yaliyo kama sponji, yenye upana wa meta 100 hadi kilometa tatu, huwa katikati ya matabaka ya miamba migumu isiyofyonza maji. Matabaka hayo yaliyopindika yameinama upande wa magharibi, na ukingo wake wa mashariki umetokezea karibu na safu ya milima ya Great Dividing Range. Maji ya mvua hufyonzwa na ukingo huo nayo husonga polepole kuelekea magharibi. Kila mwaka, maji hayo husonga umbali wa meta tano tu.

Kisima kinapochimbwa chini ya mlima hadi kwenye tabaka la jiwe-mchanga, maji husukumwa juu na nguvu za uvutano. Kwa sababu maji husukumwa juu na shinikizo, kisima hicho huitwa kisima cha artesia. Jina hilo lilibuniwa kutokana na jina la mkoa wa zamani wa Artois huko Ufaransa. Kisima cha kwanza cha aina hiyo kilichimbwa katika mkoa huo. Wakati watu walipogundua kwamba kuna maji chini ya ardhi huko Australia, visima vingi sana vilichimbwa.

Maji Yapungua Kisimani

Mwishoni mwa miaka ya 1800, watu waliohamia nyanda kubwa za Queensland na New South Wales walichimba visima wakifikiri kwamba maji hayo hayawezi kwisha. Kufikia mwaka wa 1915, visima 1,500 hivi vilikuwa vikivuta lita bilioni 2,000 za maji (kiasi hicho cha maji kinaweza kujaza mabwawa ya kuogelea 1,000 yanayotumiwa kwenye michezo ya Olimpiki) kila siku kutoka kwenye Kisima Kikuu cha Artesia. Maji ya kisima hicho kikubwa yalipungua haraka sana kwa kuwa maji mengi yalivutwa kuliko yale yaliyokuwa yakiingia; hivyo visima vingi vilikauka.

Leo, kati ya visima 4,700 vya artesia ambavyo vimechimbwa, ni visima 3,000 tu vilivyo na maji ya chemchemi. Visima vingine 20,000 huvuta maji kutoka kwenye Kisima Kikuu cha Artesia kwa kutumia pampu zinazoendeshwa na upepo. Serikali fulani zinafanya jitihada ili kuhifadhi kisima hicho kwani kwa sasa, asilimia 95 ya maji yanayobubujika hupotea bure yanapovukizwa.

Ni muhimu kuhifadhi maji ya kisima hicho kwani asilimia 60 ya maeneo ya Australia hutegemea maji ya chini ya ardhi. Miji mingi na viwanda vingi vya bara hutegemea maji ya kisima hicho. Maji hayo yana ladha gani? Jason, aliyelelewa mashambani katika eneo la Queensland linalotegemea maji hayo ya kisimani, anasema hivi: “Maji hayo yana ladha ya chumvi kidogo, na ninapenda kunywa maji ya mvua zaidi wakati yanapopatikana; lakini ng’ombe wanapenda maji hayo ya kisima.” Maji hayo yana ladha ya chumvi kwa sababu yanapata madini wakati yanapofyonzwa na matabaka ya miamba. Maji yanayopatikana kandokando ya kisima hicho hayana chumvi nyingi, lakini maji ya katikati yana chumvi nyingi sana—yanafaa kutumiwa tu na kondoo na ng’ombe. Maji ambayo hayavutwi au kutumiwa na watu huendelea kuteremka kuelekea magharibi kwenye maeneo makavu.

Kisima Kikubwa Kinaathiriwa

Tunapoendelea kusafiri kuelekea magharibi, tunaona chemchemi ndogo za maji zilizotapakaa jangwani. Maji ya mvua yanaposonga kilometa nyingi kwenye matabaka ya chini zaidi ardhini, baada ya maelfu ya miaka, maji hayo hufika kwenye ukingo wa kusini-magharibi wa Kisima Kikuu cha Artesia na kububujika juu ya uso wa ardhi. Hivyo ndivyo chemchemi hizo hufanyizwa. Maji ya chemchemi hizo yanapovukizwa, madini hubaki. Madini hayo huteka mchanga unaopeperushwa na upepo ambao unainua chemchemi hizo pole kwa pole.

Hata chemchemi hizo zinazotegemeza mimea na ndege huharibiwa na watu. Kitabu Discover Australia chasema hivi: ‘Chemchemi nyingi zimeharibiwa na ng’ombe, sungura, na hata hivi majuzi zimeharibiwa na watalii. Huenda kiasi cha maji kinachovutwa kutoka kwenye visima kwa ajili ya mifugo ndicho kimepunguza sana kiwango cha maji katika chemchemi hizo.’

Japo Kisima Kikuu cha Artesia ni kikubwa, kinaathiriwa sana na wanadamu. Usimamizi mzuri unahitajiwa ili kuhifadhi yale maji mengi ya chini ya ardhi ya Kisima Kikuu cha Artesia.

[Ramani katika ukurasa wa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

KISIMA KIKUU CHA ARTESIA

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Pampu zinazoendeshwa na upepo hutumiwa sana kuvuta maji katika maeneo makavu ya mashambani ya Australia

[Picha katika ukurasa wa 26]

Madini yanayorundamana pole kwa pole kandokando ya chemchemi yameziinua hadi kufikia meta 15

[Hisani]

Courtesy of National Parks and Wildlife South Australia

[Picha katika ukurasa wa 26]

Chemchemi zenye maji yaliyohifadhiwa kwa maelfu ya miaka

[Hisani]

Courtesy of National Parks and Wildlife South Australia

[Picha katika ukurasa wa 26]

Asilimia 60 ya maeneo ya Australia hutegemea maji ya chini ya ardhi, kama wakazi wa shamba hili lililoko mbali

[Picha katika ukurasa wa 26]

Ziwa la maji ya chumvi lililoko kwenye ukingo wa kusini-magharibi wa Kisima Kikuu cha Artesia