Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mti Mkubwa Unaoitwa Tule

Mti Mkubwa Unaoitwa Tule

Mti Mkubwa Unaoitwa Tule

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

MITI mirefu kushinda miti mingine yote ulimwenguni ni miti aina ya mvinje iitwayo redwood huko California, inayoweza kufikia urefu wa meta 110 au zaidi. Hata hivyo, mti wa mvinje wa Mexico, wa jamii ya sequoia, una mzingo mkubwa kuliko miti mingine yote. Mti maarufu zaidi wa aina hiyo unakua umbali wa kilometa 13 mashariki ya jiji la Oaxaca, Mexico, katika mji uitwao Santa María del Tule. Mti huo unaitwa mti wa Tule. Sehemu ya chini ya shina lake ina mzingo wa meta 46. Angalau watu 30 walionyoosha kabisa mikono yao wangehitajika ili kuzunguka kabisa shina lake, na watu zaidi ya 500 wangeweza kupata kivuli chini ya matawi yake!

Inakadiriwa kwamba mti huo una umri wa zaidi ya miaka 2,000. Matawi makavu ya mti huo yaliyokatwa mwaka wa 1996 yalikuwa na uzito wa kilogramu 10,000. Wenyeji wanauita mti huo El Gigante (Jitu). Nchini Mexico jamii hiyo ya mti inaitwa ahuehuete, maana yake katika Kinahuatl ni “mzee wa maji,” kwa kuwa mara nyingi mti huo hukua karibu na maji au katika vinamasi.