Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Mungu Hutumia Nguvu kwa Njia ya Haki?

Je, Mungu Hutumia Nguvu kwa Njia ya Haki?

Maoni ya Biblia

Je, Mungu Hutumia Nguvu kwa Njia ya Haki?

SIKUZOTE, wanadamu wametumia nguvu vibaya. Yakadiriwa kwamba, huenda watu 170,000,000 waliuawa na serikali zao za kisiasa katika karne ya 20. Kama Biblia inavyoonyesha kwa usahihi, wanadamu wamewatawala wenzao kwa hasara yao.—Mhubiri 8:9.

Kutokana na jinsi ambavyo wanadamu hutumia nguvu vibaya, huenda wengine wakashutumu jinsi ambavyo Mungu hutumia nguvu kuwaharibu adui zake. Je, Wayahudi hawakuwashambulia na kuwaua wakazi Wakanaani wa Bara Lililoahidiwa kufuatia amri ya Mungu? (Kumbukumbu la Torati 20:16, 17) Je, Mungu mwenyewe hakusema kwamba atavunja na kukomesha serikali zote zinazompinga? (Danieli 2:44) Watu fulani wenye moyo mnyoofu wamejiuliza iwapo sikuzote Mungu hutumia nguvu kwa njia ya haki.

Matumizi Mabaya ya Nguvu

Ni muhimu kufahamu kwamba ni sharti serikali yoyote iwe na uwezo wa kutumia nguvu. Hivyo, serikali isiyoweza kutekeleza sheria zake haina uwezo. Kwa mfano, ingawa visa vya polisi kutumia nguvu vibaya huripotiwa, ni watu wangapi wangependa kuishi bila ulinzi wa polisi? Na ni mtu yupi mwenye akili timamu anayeweza kudai kwamba hakuna haja ya kuwa na mahakama zinazodumisha sheria katika jamii yoyote ile?

Mohandas Gandhi, aliyejulikana sana kwa kuchukia jeuri, alisema hivi wakati mmoja: ‘Tuseme mtu apandwe na hasira kali kisha atoke kwa ghadhabu huku akibeba upanga mkononi, na kuua kila mtu anayekutana naye, na hakuna mtu anayethubutu kumkamata. Mtu yeyote atakayemwua mtu huyo mwenye kichaa atasifiwa na watu, naye ataonwa kuwa mtu mwema.’ Naam, hata Gandhi aliona umuhimu wa kutumia nguvu katika hali fulani.

Ni wazi kwamba uwezo wa kutumia nguvu ni muhimu kwa jamii yoyote thabiti. Kwa ujumla, watu wanaposhutumu matumizi ya nguvu, huwa wanalalamika hasa kuhusu matumizi mabaya ya nguvu.—Mhubiri 4:1-3.

“Njia Zake Zote Ni Haki”

Hakuna uthibitisho wowote katika historia unaoonyesha kwamba Mungu amewahi kutumia mamlaka yake vibaya. Hatawali kimabavu. Yeye anataka tumwabudu kwa kuchochewa na upendo. (1 Yohana 4:18, 19) Kwa hakika, Mungu hatumii nguvu iwapo kuna njia nyingine ifaayo. (Yeremia 18:7, 8; 26:3, 13; Ezekieli 18:32; 33:11) Na anapochagua kutumia nguvu, sikuzote yeye hutoa maonyo mengi ili mtu yeyote anayetaka ajirekebishe. (Amosi 3:7; Mathayo 24:14) Je, Mungu mkatili anayetawala kimabavu angefanya hivyo?

Jinsi Mungu anavyotumia nguvu si sawa na jinsi ambavyo wanadamu hutumia nguvu vibaya. Musa alisema hivi kumhusu Yehova: “Njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu.” (Kumbukumbu la Torati 32:4) Tofauti na serikali za wanadamu wanaotawala kimabavu, serikali ya Mungu haitegemei ni mtu yupi aliye na mamlaka kubwa zaidi. Katika hali zote, ametumia nguvu kupatana na upendo, hekima, na haki yake kamilifu.—Zaburi 111:2, 3, 7; Mathayo 23:37.

Kwa mfano, Mungu aliwaharibu waovu kupitia Furiko baada ya kuwaonya kwa miaka mingi. Mtu yeyote angeingia ndani ya safina na kuokoka. Ni watu wanane tu waliofanya hivyo. (1 Petro 3:19, 20; 2 Petro 2:5) Katika siku za Yoshua, Waisraeli walitekeleza hukumu ya Mungu dhidi ya Wakanaani waovu. Hukumu hiyo ilitangazwa miaka 400 mapema! (Mwanzo 15:13-21) Katika kipindi hicho chote, Wakanaani hawakukosa kuona uthibitisho ulioonyesha wazi kwamba Waisraeli walikuwa watu wa Mungu waliochaguliwa. (Yoshua 2:9-21; 9:24-27) Hata hivyo, mbali na Wagibeoni, hakuna taifa lingine la Kanaani lililotaka kuhurumiwa au kufanya amani. Badala yake, Wakanaani waliamua kufanya mioyo yao kuwa migumu dhidi ya Mungu.—Yoshua 11:19, 20.

Mungu Ana Mamlaka

Tunapojaribu kuelewa jinsi Mungu anavyotumia nguvu, ni lazima kwanza tuelewe kweli ya msingi kuhusu mahala petu mbele za Mungu. Nabii Isaya alikubali hivi kwa unyenyekevu: “Sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu.” (Isaya 64:8) Kwa wazi, akiwa Muumba wa ulimwengu wote mzima, Mungu aweza kutumia nguvu katika njia yoyote anayotaka. Kwa kutambua mamlaka ya Mungu, twaweza kusema hivi kama Solomoni: “Neno la mfalme lina nguvu; naye ni nani awezaye kumwambia huyo, Wafanya nini?”—Mhubiri 8:4; Waroma 9:20, 21.

Kwa sababu ya cheo cha Mungu akiwa Muumba mwenye uwezo wote, yeye ana haki ya kuwapa viumbe wa kidunia uhai na pia kuuondoa. Kwa kweli, wanadamu hawana haki wala ujuzi wa kutosha kushutumu njia ya Mungu ya kutumia nguvu. Ni lazima mwanadamu ajifunze kupatanisha njia yake ya kufikiri na ya Mungu. “Njia zenu sizo zisizo sawa?” akauliza Yehova.—Ezekieli 18:29; Isaya 45:9.

Haki ya Yehova na upendo wake kwa wanadamu ndio utamsukuma kuharibu watu wanaotumia uwezo vibaya na wanaoingilia haki za wengine kikatili. Tendo hilo la kutumia nguvu litaleta hali bora duniani kwa wanadamu wote wanaopenda na wanaotaka amani. (Zaburi 37:10, 11; Nahumu 1:9) Hivyo, serikali ya Mungu itathibitishwa kuwa ya haki na itatetewa daima.—Ufunuo 22:12-15.