Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

 Kuutazama Ulimwengu

Uhalifu wa Kiuchumi Unaongezeka Ulaya

Kulingana na ripoti iliyotolewa na Baraza la wabunge wa Ulaya, “uhalifu wa kiuchumi umeongezeka hasa tangu mwaka wa 1998.” Uhalifu wa kiuchumi ni nini? Ripoti ya Kamati ya Mambo ya Kiuchumi na Maendeleo, yaorodhesha uhalifu huo kuwa “biashara ya kuuza watu, matumizi mabaya ya dawa za kulevya na biashara nyinginezo za magendo, utengenezaji wa bidhaa bandia, uhalifu wa kimazingira, uhalifu unaofanywa kupitia Internet, udanganyifu katika kodi, kuhalalisha pesa haramu, ufisadi na biashara haramu zinazofanywa na watu wenye mamlaka.” Kwa kuwa uhalifu wa namna hiyo unahusiana sana na siasa, ripoti hiyo inaonya hivi: “Jitihada za nchi za Ulaya za kuzuia uhalifu huo huenda zikafifia, na hivyo zikashindwa kabisa kukomesha uhalifu wa kiuchumi.” Mwandishi wa ripoti hiyo, Vera Squarcialupi wa Italia asema hivi: “Sheria, ambayo ni muhimu sana katika jamii iliyostaarabika itaathiriwa kwanza.”

Kuokoka Aksidenti za Ndege

Gazeti la National Post la Kanada lasema, “zaidi ya asilimia 95 ya wasafiri huokoka aksidenti za ndege za abiria.” Kulingana na gazeti la Post, uchunguzi uliofanywa na Baraza la Kitaifa la Usalama wa Usafiri wa Ndege la Marekani ulionyesha kwamba wasafiri wengi hata huokoka “aksidenti mbaya sana” ambazo huharibu ndege kabisa. Mkurugenzi-mkuu wa Idara ya Usafiri wa Ndege ya Kanada, Art LaFlamme, aeleza hivi: “Aksidenti nyingi hutokea ndege zinapotua au kupaa. Aksidenti za aina hii hazitangazwi na vyombo vya habari na watu wanaweza kunusurika aksidenti hizi. Ndiyo sababu tunakazia zaidi kwamba maelezo mafupi ya usalama yatolewe kabla ya safari.” Watu wanaosafiri kwa ukawaida huenda wakapuuza maagizo hayo. Lakini ni kama msemaji mmoja mwanamke wa kampuni ya ndege alivyosema, “ni muhimu watu wayatii maagizo hayo. Kuokoka kwao kutategemea kufuata maagizo hayo iwapo hali ya dharura itatokea.”

‘Mikazo ya Kitekinolojia’

Inasemekana kwamba ‘mikazo ya kitekinolojia’—mfadhaiko unaosababishwa na tekinolojia mpya—inaongezeka, laripoti gazeti Maclean la Kanada. Uchunguzi unaonyesha kwamba mikazo hiyo inasababishwa na, ‘kujifunza daima kutumia tekinolojia mpya, kutoweza kutofautisha kazi ya ofisi na maisha ya nyumbani kwa sababu ya uvumbuzi mpya kama vile e-mail, mifumo ya kuwasilisha simu na simu za mkononi.’ Unaweza kuikabilije? Wataalamu wanapendekeza kuweka mipaka. Angalia iwapo kutumia chombo fulani kutafanya maisha yako yawe sahili au yawe tata zaidi. Kumbuka kwamba wakati mwingi unahitajiwa kujifunza tekinolojia mpya ili upate kujua faida yake. ‘Tenga wakati kila siku wa kufanya mambo mengine muhimu badala ya kujishughulisha na vifaa vya kitekinolojia.’ “Badala ya kufanya mambo muhimu kwanza, watu wengi huanza siku kwa kusoma barua zinazotumwa kwa kompyuta,” asema Dan Stamp, mtaalamu wa uzalishaji kutoka Vancouver. “Wakati ulio bora zaidi, yaani saa za asubuhi, hutumiwa kwa mambo yasiyo na maana.”

Wanatunga Vitabu Vyao Wenyewe

Katika jitihada ya kuchochea usomaji huko Zambia, watoto wa shule wametiwa moyo kutunga vitabu vya hadithi fupi zenye picha, laripoti gazeti Zambia Daily Mail. Ripoti moja ya serikali yasema kwamba, “Maktaba nyingi za shule zina vichapo vinavyozungumzia mambo yaliyo mapya na magumu kwa watoto wa Zambia kuelewa. Faida ya watoto kutunga vitabu vyao wenyewe ni kwamba wanaandika mambo wanayoelewa na yanayowapendeza.” Baadhi ya vitabu hivi huenda vikawekwa katika maktaba za shule au za darasani, vikasomwa kwenye redio au hata kuchapishwa. Gazeti la Daily Mail lasema: “Hii ni njia isiyo na gharama ya kuongeza idadi ya vichapo vya kusoma kwani yahitaji kalamu na karatasi tu. Ni njia ya kutumia pia rasilimali inayopatikana kwa wingi yaani, wanafunzi ili kutokeza rasilimali iliyo nadra na iliyo ghali yaani, vitabu.”

Klorokwini Haitibu Tena Malaria

‘Klorokwini, dawa iliyotumiwa sana kuzuia malaria huko Zambia, haitatumiwa tena katika zahanati za serikali na badala yake matibabu yenye matokeo zaidi yatatumiwa, laripoti gazeti Times of Zambia. Uamuzi huo ulifikiwa baada ya uchunguzi kuonyesha kwamba “kushindwa kwa Klorokwini kutibu malaria kunasababisha vifo 12,000 kati  ya vifo 25,000 vya watoto wenye umri usiozidi miaka mitano kila mwaka nchini Zambia.” Mabadiliko hayo yameanzishwa pia katika nchi nyinginezo za mashariki na kusini mwa Afrika. “Ingawa klorokwini imetumiwa kwa zaidi ya miaka 30 nchini humo, haitibu tena malaria, ugonjwa unaoua watu wengi sana katika taifa hili,” lasema Gazeti Times.

Usiendeshe Baiskeli Ukiwa Mlevi

Kuendesha baiskeli baada ya kunywa pombe, kunaweza kuwa hatari kama kuendesha gari baada ya kunywa pombe, laripoti gazeti la New Scientist. ‘Kuendesha baiskeli kunahitaji uwezo wa kiakili na usawaziko wa kimwili wa hali ya juu sana kuliko kuendesha gari. Kwa hiyo pombe huwaathiri sana waendeshaji-baiskeli,’ asema Guohua Li wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, Maryland, Marekani. Walipochunguza waendeshaji-baiskeli 466, Li na wenzake walipata kwamba uwezekano wa kujeruhiwa vibaya au hata kuuawa kwa wale waliokunywa chupa nne au tano za pombe ulikuwa mara 20 zaidi ya wengineo. Hata kunywa chupa moja tu ya pombe, kuliongeza hatari ya mwendeshaji-baiskeli kujeruhiwa kwa mara sita. ‘Isitoshe, pombe yaweza kumfanya mwendeshaji-baiskeli asahau kuvaa kofia ya kujikinga kichwa,’ lasema gazeti New Scientist.

Karatasi za Migomba ya Ndizi

Baada ya ndizi kuvunwa, mara nyingi migomba yake huachwa shambani iwe mbolea. Hata hivyo, Profesa Hiroshi Morishima wa Chuo Kikuu cha Jiji la Nagoya amefaulu kutengeneza karatasi kutoka kwa migomba ya ndizi, laripoti gazeti la Asahi Shimbun la Japani. Nyuzi-nyuzi za mgomba “ni ndefu na ngumu na ni bora kama zile za Mkonge zitumiwazo kutengenezea karatasi. Karatasi ya mgomba wa ndizi inapotengenezwa na mashine, hufanana na karatasi za kawaida, na imethibitika kuwa bora kuliko karatasi ya fotokopi iliyorejelezwa. Gazeti hilo lilisema kwamba, “nchi 123 ulimwenguni hukuza ndizi, na kila mwaka tani 58,000,000 hukuzwa, jambo linalofanya zao hilo liwe rasilimali yenye kutegemeka sana.”

Asali Huponya

Mbali na utamu wake wenye kupendeza, asali imejulikana kwa muda mrefu kwa sababu ya uwezo wake wa kuponya. Kulingana na gazeti The Australian, utafiti kutoka kwa vyuo vikuu vya Queensland na Sydney umeonyesha ni kwa nini asali ina uwezo wa kuua bakteria. Inapochanganywa na maji na kupakwa kwenye jeraha na sehemu zilizoungua, kimeng’enya fulani katika asali humeng’enya sukari ili kutokeza haidrojeni peroksaidi, inayotumiwa sana kwa ung’arishaji wa nyumbani. Kemikali hii haiui tu bakteria kama Staphylococcus aureus bali pia husaidia tishu kujitengeneza upya.

Kutoweka kwa Msumari

“Bila shaka, enzi za matumizi ya msumari wa kawaida zimekwisha,” lasema gazeti The Toronto Star. Gazeti hilo laripoti kwamba biashara ya misumari ya kawaida “imepungua kwa asilimia 50 katika miaka michache iliyopita.” Kubuniwa kwa nyundo inayogongomea misumari ya pekee kumepunguza mahitaji ya misumari ya kawaida huko Amerika Kaskazini. Maduka ya kuuza vifaa vya ujenzi huko Marekani yaripoti kwamba wataalamu wa ujenzi hawanunui sana misumari ya kawaida, badala yake wanapendelea kutumia misumari ya pekee, iliyo myepesi zaidi. Kwa nini watengenezaji wa misumari ya kawaida hawatengenezi misumari hiyo ya pekee? “Kwa sababu ileile inayofanya makampuni ya magari-moshi yasiweze kuingia katika biashara ya mashirika ya ndege,” lajibu gazeti Star. “Bidhaa hizo zinatofautiana kabisa.”

Elimu Kuhusu Adabu

Kwa miaka minane iliyopita, Taasisi ya Tekinolojia ya Massachusetts imetoa mfululizo wa mafunzo kuhusu adabu bila malipo kwa wanafunzi wote. Kwa nini? Travis Merrit, aliyekuwa mshauri wa mambo yanayohusu wanafunzi wa shahada ya kwanza, aliwafafanua wanafunzi kuwa, “wasiovalia kwa adabu, wasiotambua mitindo inayofaa, na wasio na adabu,” laripoti gazeti The Scientist. Masomo hayo ya siku moja yanatia ndani mashauri kuhusu kuwa na adabu mezani, katika mavazi, mahusiano ya kibiashara, kutumia simu za mkononi, na katika mahusiano pamoja na wengine. Wanafunzi wanafunzwa namna ya kutembea na jinsi ya kupiga chafya kwa busara na wanakumbushwa pia, ‘tofauti iliyopo kati ya mazungumzo na mahojiano.’ Mfunzi mmoja, Roseanne Thomas, anakazia umuhimu wa kusema “asante” unapopongezwa. “Haya ni mambo ya msingi maishani,” asema Roseanne Thomas. “Nafikiri inashangaza watu wanapotambua kwamba ili kufanikiwa maishani, ni lazima kuwa na mahusiano mazuri na wengine.”